Monday, 9 December 2019

SERIKALI YAITAKA TAASISI YA UHASIBU TANZANIA (TIA) KUBORESHA ZAIDI MITAALA YAKE

...
Mgeni Rasmi Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk Rehema Nchimbi ( kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango) akimkabidhi mmoja wa Wahitimu Shahada yake. 

Na Abby Nkungu, Singida

SERIKALI imeitaka Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) kuboresha zaidi mitaala yake ili iweze kuzalisha wataalamu mahiri wenye ujuzi na weledi kwa ajili ya kujibu changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa Sera ya uchumi wa Viwanda  hivyo kuwezesha Tanzania kufikia uchumi wa kipato cha kati kabla ya mwaka 2025.


Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk Rehema Nchimbi  kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango mjini Singida wakati wa Mahafali ya 17 ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) kwa Wahitimu 1,688 wa kozi za Cheti cha Awali, Astashahada, Stashahada na Shahada kutoka Kampasi za Mwanza, Kigoma na Singida.

Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk Rehema Nchimbi, Waziri Mpango alisema fani za Uhasibu, Ununuzi na Ugavi, Usimamizi wa biashara na Uongozi wa raslimali watu ambako Kampasi za Kigoma, Mwanza na Singida  zimejikita, ni muhimu katika kuendesha uchumi wa Taifa; hususan katika kusimamia mapato na matumizi ya fedha za umma. 

Alisisitiza kuwa Sera ya nchi kwa sasa ni Uchumi wa Viwanda, hivyo umahiri wa Wataalamu wanaozalishwa na Taasisi hiyo lazima uonekane dhahiri ili kufanikisha azma ya Serikali ya Tanzania ya Viwanda. 

"Ili kukabiliana na changamoto za Usimamizi wa mapato na matumizi ya fedha za umma, mahitaji ya soko, ushindani na utandawazi mnapaswa kuboresha mitaala yenu kukidhi viwango vya Kimataifa katika umahiri badala ya maarifa tu ili kukabiliana na changamoto za utekelezaji wa Sera ya viwanda. Tunahitaji wataalamu wenye weledi, maarifa na umahiri wa kutatua changamoto na si kuongeza changamoto", alifafanua.

Aidha, aliwasihi wahitimu hao kuweka mbele suala la uaminifu na uadilifu kwa kuwa hiyo ndiyo silaha na dira sahihi ya maisha yao ya kila siku. “Uhasibu ni taaluma iliyotukuka; hivyo ni vyema ninyi mliosomea mkazingatia kwa kiwango cha juu miiko, kanuni na taratibu zinazotawala fani hiyo”.

Alieleza  kuwa kashfa mbalimbali zinazosikika nchini na kwingineko duniani ni matokeo ya  watu kukosa uaminifu na uadilifu.  “Mtakapotoka hapa baada ya kuhitimu masomo yenu, mtakutana na changamoto mbalimbali, ila mkumbuke ni uadilifu na uaminfu pekee ndio utakaowaongoza katika maisha yenu yote” ,aliwaasa.


Dk Mpango aliwataka wahitimu hao kutumia vyema elimu waliyoipata katika kubuni, kuanzisha na kusimamia shughuli mbali mbali za kibiashara zitakazowasaidia wao na jamii yote ya Watanzania katika kujiletea maendeleo.


“Hatua mliyofikia iwe chachu ya kujiimarisha zaidi kitaaluma ili kuweza kushindana katika soko la ajira na kujiajiri. Msipojiimarisha, mtajikuta kazi zenu zinachukuliwa na watu wa nje" alisema na kutoa angalizo; 

"Soko letu la ajira rasmi ni dogo na kwa kweli halikidhi mahitaji ya wahitimu wote nchini. Ili kukabiliana na changamoto ya soko la ajira, ni vyema mkaelekeza mawazo yenu kwenye kujiajiri badala ya kuajiriwa".

Ofisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Bi Luciana Hembe alitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili Taasisi hiyo kuwa ni pamoja na gharama kubwa za pango katika Kampasi za Kigoma na Mwanza kutokana na kukosa majengo yao wenyewe na uhaba wa miundombinu ya majengo Kampasi ya Singida kutokana na ongezeko kubwa la wanafunzi. 

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TIA, Saidi Chiguma aliwataka wahitimu hao kuzingatia uadilifu, nidhamu na uzalendo wakati wote ili kujipambanua na wahitimu wa vyuo vingine. 
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger