Monday, 11 November 2019

Waziri Wa Kilimo Aagiza Viongozi Wa Chama cha Akiba na mikopo na Chama cha Ushirika wa Ayalabe Dairy Wakamatwe

...
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Arusha
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameliagiza jeshi la Polisi Mkoani Arusha kwa kushirikiana na Mkuu wa Upelelezi, na Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) kuwakamata viongozi mbalimbali wa Chama cha Akiba na mikopo cha Ayalabe na na Chama cha Ushirika wa Ayalabe Dairy kutokana na ubadhilifu wa fedha za wanachama wa vyama hivyo.
 
Waziri Hasunga ametoa maagizo hayo jana tarehe 10 Novemba 2019 wakati mara baada ya kusikiliza malalamiko ya wanachama wa vyama hivyo wakati wa kikao kazi kilichofanyika katika eneo la uwanja wa vyama hivyo Wilayani Karatu ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani Arusha.
 
Waziri Hasunga ameagiza viongozi hao kukamatwa haraka iwezekanavyo kwani dhamira ya serikali ya awamu ya tano ya kuanzisha vyama vya ushrika ni kuwanufaisha wananchi kupitia umoja huo.
 
Viongozi hao ni Wajumbe wa Bodi ya AYALABE SACCOS ambao ni aliyekuwa Mwenyekiti Ndg Christopher Kastuli, Aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Ndg Yuda Moratha, Waliokuwa makatibu Bi Maria Lohay na Anastazia Evodi pamoja na wajumbe Eustela Kastuli, Faustini Tekko, Ludovick Marmo, Tarsila Visent na Costantine Matle.
 
Wengine ni waliokuwa wajumbe wa Chama cha Ushirika wa Ayalabe Dairy ambao ni aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho Yuda Moratha, aliyekuwa Makamu mwenyekiti Faustine Tekko, aliyekuwa katibu wa chama hicho Ndg Yasinta Faustin, na wajumbe ambao ni EufrasiaAntony, Israel Sarwat, Evarist Sulle, Florance Neston na Eustela Kastuli.
 
Waziri Hasunga ameagiza pia kukamatwa viongozi wote wa makampuni yaliyochukua hela kinyume na taratibu za ushirika, kampuni hizo ambazo ni Shimaswa na Teddy Agrovet.
 
Katika hatua nyingine ameagiza Ndg Blanka Michael akamatwe kutokana na kukodisha eneo la Chama cha Ushirika wa Ayalabe Dairy pasipo kufuata utaratibu wa kisheria.
 
Katika mkutano huo pia Mhe Hasunga ameagiza kuwekwa kizuizini viongozi na wajumbe wa kamati ya usimamizi wa Chama cha Akiba na mikopo cha Ayalabe ambao ni aliyekuwa Mwenyekiti Ndg Lazaro Titus Lazaro  na wajumbe Joseph Bayo na Eudesi Jonas.
 
Waziri Hasunga ameuagiza uongozi uliopo wa Chama cha Ushirika cha akiba na mikopo cha Ayalabe kusitisha mara moja kulipa deni la mkopo waliochukua wa shilingi 500,00,000 kutoka Benki ya TIB kwa kutumia hati za majengo ya Ayalabe Dairy mpaka serikali itakapojiridhisha kama mkopo huo ni halali.
 
Ameagiza watuhumiwa hao wote wafunguliwe kesi ya uhujumu uchumi na watakaoweza kurudisha fedha za wanachama waweze kusamehewa. Pia ameuagiza uongozi wa wilaya ya Karatu na Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuhakikisha kuwa wanasimamia ukarabati wa kiwanda cha Ayalabe Diary na kufikia mwezi Januari 2020 kianze kufanya kazi.
 
Chama cha Ushirika wa maziwa cha Ayalabe kilipokea kiasi cha shilingi 513,407,077 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Karatu kupitia miradi ya ASDP na DADPS tangu mwaka 2009 hadi 2013 kwa ajili ya ujenzi wa kuboresha kiwanda cha maziwa ambapo hata hivyo baada ya kufanyiwa uchunguzi na ukaguzi kilibainika kuwa na ubadhilifu wa Tshs 147,126,000 huku chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) chenyewe kilikuwa na akiba za wanachama ambazo ni shilingi 11,015,000 na hisa zao zilikuwa Tshs 2,830,000, huku kikiwa kimechukua mkopo wa Tshs 500,000,000 kutoka Benki ya TIB.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger