Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameliagiza jeshi la Polisi Mkoani Arusha kwa kushirikiana na Mkuu wa Upelelezi, na Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) kuwakamata viongozi mbalimbali wa Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo cha Arusha Kurugenzi kutokana na ubadhilifu wa fedha za wanachama.
Waziri Hasunga ametoa maagizo hayo jana tarehe 9 Novemba 2019 mara baada ya kusikiliza malalamiko ya wanachama wa chama hicho wakati wa kikao kazi kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha na kuhudhuriwa pia na Mkuu wa Mkoa huo Mhe Mrisho Gambo.
Amesema kuwa watuhumiwa hao wanapaswa kukamatwa haraka iwezekanavyo kuanzia waliokuwa viongozi mwaka 2004 mpaka 2015 ili kurudisha fedha zote walizozizihujumu za wanachama na walizokopa.
Wengine alioagiza wakamatwe ni pamoja na wajumbe wote wa kamati za mikopo, Kamati ya usimamizi wa SACCOS iliyokuwepo kipindi chote hicho, Wajumbe wote wa Bodi ya SACCOS iliyokuwepo awali kabla ya Bodi iliyopo sasa.
“Tunachotaka sisi fedha zote za wanachama zirudi na hata leo wakirudisha fedha hizo hatutaendelea na kesi” Alisema
Pia ameagiza mwanachama wa SACCOS hiyo Bi Zainab Nassor aliyeanzisha vikundi hewa 14 akamtwe, huku wengine ni aliyekuwa Mwenyekiti wa SACCOS Dkt Freedom Makiago, Makamu Mwenyekiti Gasto Gasper, Meneja Christina Sumaye, na wajumbe Andrea Sekidio, Joseph Kuhamwa na Mwanahamisi Gembe.
Katika hatua nyingine Mhe Hasunga ameagiza kukamatwa kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa kamati ya Usimamizi Bi Mwanahawa Kombo, na wajumbe Samwel Mushy, Estomin Chang’ah. Huku akiagiza pia karani wa SACCOS hiyo Edith Malley kukamatwa.
Katika hatua nyingine ameagiza viongozi wote walioandikwa kwenye vikundi vya mikopo kukamatwa haraka iwezekanavyo na kuchukuliwa hatua za haraka ikiwemo kurudisha fedha za wanachama.
Mhe Hasunga amesema kuwa lengo la kunzishwa vyama vya ushirika ilikuwa ni kuwanufaisha wananchi kupitia umoja huo muhimu kwani mafanikio yanahusisha nguvu ya pamoja.
Hata hivyo ameagiza Bodi iliyopo madarakani kubainisha taarifa za kumbukumbu zote za chama hicho kwa kuonyesha idadi ya wanachama na akiba walizonazo katika chama, idadi ya hisa na kiasi cha fedha zinazodaiwa na kila mwanachama.
Kwa sasa chama kinadaiwa fedha kiasi cha shilingi 2,486,365.68 zilizotokana na mikopo kutoka Taasisi mbalimbali za kifedha, Amana, Akiba na Hisa za wanachama hususani wastaafu ambazo zilichukuliwa kwa kutumiwa na wahusika hao bila utaratibu na kwa malengo yao binafsi.
Wanachama wastaafu wanadai zaidi ya shilingi 831,764,924.87 zitokanazo na fedha za Amana walizoweka katika chama kutumia viinua mgongo vyao baada ya kustaafu utumishi, Akiba na Hisa walizowekeza tangu wajiunge na chama hicho.
Wanachama wanaoendelea na chama na waliojitoa wanadai zaidi ya shilingi 770,181,745.56 zitokanazo na Amana, Akiba na Hisa walizowekeza tangu wajiunge na chama hicho.
Kadhalika, Taasisi za kifedha zinazodai ni pamoja na (CRDB, NSSF na TUMAINI SACCOS) wanaodai zaidi ya shilingi 874,575,517.25 bakaa ya mikopo iliyotolewa bila kuzingatia utaratibu wa kifedha na kwa kutumia taarifa za udanganyifu.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga yupo Mkoani Arusha kwa ziara ya kikazi ya siku 2 kwa mualikowa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe Mrisho Gambo ambapo pamoja na mambo mengine atashuhudia shughuli za sekta ya kilimo.
0 comments:
Post a Comment