Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa(NARCO), Profesa Philemon Wambura ambaye uteuzi wake umetenguliwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ametengua uteuzi wa Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Profesa Philemon Nyagi Wambura aliyefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa makosa ya rushwa, matumizi mabaya ya madaraka, uhujumu uchumi na ubadhirifu wa mali za umma.
Kwa Mujibu wa Taarifa kwa Umma iliyotolewa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Edward Kondela imesema Waziri Mpina amefikia uamuzi huo kwa mamlaka aliyopewa kwa mujibu wa Sheria ya Makampuni Sura 212 na Sheria ya Mashirika ya Umma Na. 2 ya mwaka 1992.
Pia taarifa hiyo imebainisha kuwa uteuzi huo umetenguliwa kuanzia 08, Novemba 2019 na kwamba kuwa taratibu za kumpata Meneja Mkuu mpya wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) zinaendelea.
Wiki iliyopita Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kagera, John Joseph aliwaambia waandishi wa habari mjini Bukoba kuwa Prof. Wambura aliomba na kupokea rushwa kiasi cha shilingi milioni 12 kutoka kwa mtu ambaye aliomba kupatiwa kitalu kwenye moja ya Ranchi za Taifa zilizopo Missenyi Mkoani Kagera.
Alisema mnamo tarehe 23.09.2019 Takukuru ilipokea taarifa kwamba Profesa Wambura ambaye ni Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni za Ranchi za Taifa anajihusisha na vitendo dhidi ya rushwa ambapo walianzisha uchunguzi mara moja.
Mkuu huyo wa Takukuru alisema kwenye uchunguzi huo walibaini kwamba mnamo Tarehe 3.1.2018, Profesa Wambura aliomba na kupokea rushwa ya shilingi milioni 12 kwa mtu ambaye aliomba kupewa kitalu lakini hakukubali kumpatia hadi apatiwe milioni 12 na mtu huyo ambaye kwa mujibu wa TAKUKURU jina lake limehifadhiwa aliweza kumpatia kiasi hicho cha fedha na ndipo alipofanikiwa kumpatia kitalu hicho.
Joseph alisema ni makosa kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kwa mtu yoyote kujihusisha na vitendo vya rushwa ambapo tayari TAKUKURU imetoa onyo kali kwa watu wote kutojihusisha na vitendo vya rushwa kwani TAKUKURU iko macho wakati wote na itanawasa na kuwafikisha kwenye vyombo vya dola.
0 comments:
Post a Comment