Na Munir Shemweta, WANMM KILOMBERO
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameiagiza halmashauri ya wilaya ya Kilombero mkoa wa Morogoro kuzifuatilia taasisi za serikali zinazodaiwa kodi ya pango la ardhi kwenye halmashauri hiyo zaidi ya bilioni 1.9 ili ziweze kulipa deni hilo.
Dkt Mabula alitoa agizo hilo jana alipokutana na uongozi wa wilaya ya Kilombero pamoja na watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri za wilaya ya Kilombero na ile ya Mji wa Ifakara wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Morogoro.
Agizo hilo la Dkt Mabula linafuatia kuelezwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kilombero Injinia Stephano Kaliwa kuwa miongoni mwa wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi katika halmashauri yake ni taasisi za serikali zinazodaiwa zaidi ya bilioni 1.9.
Alizitaja taasisi hizo kuwa ni Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linalodaiwa zaidi ya bilioni 1.7 katika maeneo yake inayomiliki ya Kidatu shilingi 1,007,452.00, Kihansi 996,957,750.00 pamoja na Mlimba 29,826,650.00. Pia taasisi ya The Trustees of TANAPA nayo inadaiwa jumla ya shilingi milioni 12,819,550.00.
Hata hivyo, Afisa Mipango Miji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero Remigi Lipiki alimueleza Naibu Waziri Mabula kuwa, TANESCO imetaka kufanyika uhakiki kwanza wa deni lake kwa madai kuwa baadhi ya maeneo inayomiliki yalishachukuliwa na taasisi nyingine na kutolea mfano wa eneo la Kidatu.
Dkt Mabula alisema, halmashauri ya wilaya ya Kilombero lazima ihakikishe inazifuatilia taasisi hizo ili ziweze kulipa madeni ya kodi ya ardhi kwa kuwa taasisi hizo zimekuwa zikitenga fedha kwa ajili ya malipo ya huduma mbalimbali ikiwemo kodi hiyo ya pango la ardhi.
‘’Taasisi zinashindwa kulipa madeni na hazijachukuliwa hatua, haiwezekani deni lifikie zaidi ya bilioni moja, fuatilieni suala hili na mchukue hatua za kisheria.’’ alisema Dkt Mabula
Hata hivyo, Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kilombero alieleza changamoto kubwa inayoikabili halmashauri yake kuwa ni ukusanyaji kodi ya pango la ardhi kwa baadhi ya wawekezaji wa Mashamba kutokana na kutokamilika taratibu za uhaulishaji mashamba hayo ambayo wamiliki wake hawana nyaraka.
Aliataja baadhi ya wamiliki wa mashamba hayo kuwa, ni Kampuni ya Mufindi Paper Mills yenye hekta 10,000 , Green Resource Limited hekta 25,000, Hiragro Ltd hekta 1500 na Sygen yenye ekari 30,000.
Kwa mujibu wa Kaliwa, kutokana na kutokamilika mchakato wa uhaulishaji wa mashamba hayo kumekuwa na upotevu wa makusanyo ya kodi ya jumla ya shilingi 132,865,031.00 kila mwaka.
0 comments:
Post a Comment