Monday, 18 November 2019

WANAFUNZI CHUO KIKUU WATOA WARAKA BAADA YA KUKERWA BEI YA VYAKULA KUPANDA CHUONI

...
Na Said Mwishehe,Globu ya jamii 

BAADA ya kupanda kwa bei ya vyakula na hasa vilivyozoeleka vikiwemo vya Wali maharage na chipsi kuku katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), Serikali ya Wanafunzi Chuo hicho(DARUSO) imeamua kufanya mazungumzo na watoa huduma ya vyakula ili kuangalia uwezekano wa kupunguza bei ya vyakula ambayo wamedai iko juu.

Hata hivyo tayari Serikali hiyo ya wanafunzi imetoa waraka unaoeleza kwa kina kuhusu kupanda kwa bei ya vyakula na kusababisha athari za kisaikolojia kwa wanafunzi kwa kile walichoeleza hali ya maisha si rafiki kwao kumudu gharamu hizo.

Sehemu ya waraka huo wa Serikali ya Wanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam uliosainiwa na Katibu Mkuu Ofisi ya DARUSO Mliman Hamis Hamis umesema kupitia ofisi ya Rais imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya mfumo wa bei za vyakula kiholela kwa baadhi ya vyakula pendwa.

Hivyo Ofisi ya Rais DARUSO inawapa pole wanafunzi wote walioathirika na changamoto hizo kwa namna moja au nyingine.

Pia waraka huo umesema Serikali ya wanafunzi inatambua kuwepo kwa changamoto hiyo kubwa japo hatua za mazungumzo zimekwishafanyika mara kadhaa na imeonekana kutozaa matunda kutokana na wawekezaji kusimamia mikataba yao waliyoingia na Chuo kama inavyowaelekeza bila kujali uwezo wa wanafunzi kumudu bei elekezi katika mikataba hiyo.

Akizungumza na Michuzi Globu ya jamii jijini Dar es Salaam leo Novemba 18,2019, Katibu Mkuu DARUSO Hamis Hamis amesema kwa sasa wanaendelea na mazungumzo kati yao na watoa huduma ya vyakula.

"Tunaendelea na mazungumzo kati yetu na watoa huduma ya vyakula hapa chuoni.Mazungumzo yanakwenda vizuri na tutafikia pazuri.Mfuko wa bei ya vyakula hapa chuoni umekuwa mkubwa sana na maisha yetu yanafahamika,"amesema Hamis.

Ameongeza wanafunzi walio wengi hawana fedha mfukoni na hata wale ambao wamepata mkopo wa Serikali fedha bado hazijaingia katika akaunti zao , na hivyo kuongeza kwa bei ya vyakula kumesababisha changamoto za kimaisha.

Hata hivyo ametoa ombi kwa wanafunzi kuendelea kuwa na subira wakati mazungumzo yakiendelea na wawe na imani na Serikali yao ya wanafunzi ambayo inashughulikia malalamiko hayo.

Hata hivyo wakati DARUSO wakitafuta ufumbuzi wa kushuka kwa bei ya vyakula chuoni hapo, mwishoni mwa wiki Waziri wa Kilimo na Chakula Japhet Hasunga amenukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akieleza amesikia kuna watu wanalalamika kuhusu kupanda kwa bei ya vyakula ambapo amewataka wafahamu Serikali haiwezi kumpangia bei mkulima.

Wakati anafafanua kupanda kwa bei ya vyakula Waziri Hasunga alieleza kwamba mkulima anapokuwa katika shughuli zake za kilimo hadi anavuna hakuna mtu anayejua gharama anazotumia mkulima katika kuandaa shamba , kupanda, kupalilia hadi kuvuna mazao yake , sasa iweje Serikali iwapangie bei.

Katika hilo Katibu huyo wa DARUSO amesema ni kweli Waziri alichoongea mkulima anapata changamoto nyingi wakati analima lakini hiyo haina maana aachwe apange bei anavyotoka.

"Ifahamike mkulima hapeleki sokoni, hivyo kuna mtu anakwenda kununua na kuleta mazao sokoni na hapo ndipo yanakutana na wanunuzi au walaji ambao itabidi wabebeshwe mzigo wote na kufanya maisha kuwa magumu.Tunaomba hili la bei ya vyakula liangaliwe vizuri na sisi tunaimani na Serikali pamoja na watoa huduma,"amesema Hamis.

Hata hivyo DARUSO kupitia Katibu Mkuu huyo amesema Serikali yao imeapa kuwatumikia na kuyatetea maslahi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa namna yoyote ile.

"Rais wa DARUSO 2019/2020 Hamis Mussa ametoa amri kwa watoa huduma ya vyakula wote hapa chuoni kurudisha haraka bei za awali kama ilivyozoeleka,"amesema Katibu Mkuu kupitia waraka wao na kuongeza iwapo amri hiyo haitatekelezwa watatumia ustaarabu mwingine.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger