Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya wamenusurika kwenda gerezani baada ya mahakama kuridhia ombi la kutowafutia dhamana zao.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba leo Jumatano Novemba 20, saa saba mchana imetoa uamuzi kuhusu maombi ya Jamhuri ya kutaka washtakiwa hao wafutiwe dhamana kwa kushindwa kufika Mahakamani Novemba 15 mwaka huu.
“Baada ya kupitia hoja za pande zote mbili na hoja za washtakiwa mahakama inaona kwamba maelezo yao hayana mashiko na kuwafutia dhamana ni hatua kali sana badala yake mahakama inawapa onyo kali wasirudie tena,” amesema Hakimu Simba.
Hakimu Simba amesema walifanya makusudi na kwamba hatua ya kujisalimisha polisi ni uoga wa jambo ambalo lingewatokea.
Kutokana na hali hiyo, amesema mahakama imewaachia kwa dhamana zao za awali na kuwataka wafuate masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Februari Mosi na Februari 16, mwaka huu Mbowe na wenzake wakiwa Kinondoni, Dar es Salaam kwa pamoja walikula njama na wengine ambao hawapo mahakamani ya kutenda kosa la jinai ikiwamo kuendelea na mkusanyiko isivyo halali na kusababisha chuki na uchochezi wa uasi.
0 comments:
Post a Comment