Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini [TAKUKURU] mkoa wa Dodoma inamshikilia Bw.David Daud Tengeneza mwenye umri wa miaka 50 ambaye ni afisa mtendaji katika kijiji cha Mapanga kata ya Itiso wilaya ya Chamwino kwa kosa la kushawishi na kujaribu kupokea rushwa kinyume na kifungu cha sheria Na.15[1]a cha sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa Sura ya 329 marejeo ya mwaka 2018.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Ofisini Kwake jijini Dodoma Nov.5,2019,Mkuu wa TAKUKURU mkoani hapa Bw.Sosthenes Kibwengo amesemaTAKUKURU imekuwa ikipokea tuhuma kadhaa juu ya afisa mtendaji huyo kujihusisha na vitendo vya rushwa .
“Mtendaji huyu amekuwa na tuhuma mbalimbali za rushwa ambapo TAKUKURU Mkoa wa Dodoma imekuwa ikifuatilia kwa kina na safari hii arobaini yake imewadia”amesema.
Bw.Kibwengo amefafanua kuwa “,baada ya kupokea taarifa mbili tofauti dhidi ya mtuhumiwa wiki iliyopita tuliamua kufuatilia mojawapo ambapo uchunguzi ulithibitisha kwamba ameomba rushwa ya shilingi laki tatu[300,000/=]kutoka kwa mtoa taarifa wetu ambaye ni mfugaji.
Tarehe 30 Oktoba ,2019 afisa wetu aliambatana na mtoa taarifa hadi ofisini kwamtuhumiwa ambapo alielekeza apelekewe fedha hizo ndipo ampatie barua ya kumruhusu kuingiza kijijini Mapanga ng’ombe arobaini na nane[48] aliowatoa kijiji jirani cha Segala la sivyo angemchukulia hatua za kisheria kwa kutokuwa na kibali.”
Mkuu huyo wa TAKUKURU ameendelea kusema kuwa,kutokana na uzoefu wa Mtuhumiwa katika vitendo vya rushwa ,mtuhumiwa alipomwona mtoa taarifa akiwa na mtu mwingine alianza kumhoji huku akisisitiza kuwa yeye ni mzoefu na mara kadhaa amekoswa na TAKUKURU,hivyo kumtaka akaweke fedha hizo nje ya chooni lakini hakuacha fedha hiyo ya Rushwa na walipoondoka ,mtuhumiwa akaenda chooni kuangalia na akagundua kuwa hongo yake haipo.
Mtuhumiwa aliamua kumfuata mtoa taarifa na kumtaka arudi na akahojiiweje hongo haipo naye akamweleza hawezi kuacha fedha bila kupewa barua,ndipo akaelekezwa aiweke chini ya jiwe lililo chini ya mti nje ya Ofisi ya mtuhumiwa na aingie ndani kuandikiwa barua.
Bw.Kibwengo ameendelea kusema,baada ya kuweka fedha hiyo chini ya jiwe,mtoa taarifa aliingia ndani ya ofisi lakini mtuhumiwa hakumwandikia barua kwa kisingizio cha kuisahau mihuri nyumbani na TAKUKURU imemkamata na atafikishwa mahakamani.
Hivyo ,Bw.Kibwengo amewakumbusha wananchi wote kuwa ni kosa la jinai kushawishi na kujaribu kuchukua rushwa na wananchi wanapokutana na hali hizo watoe taarifa mapema kwa TAKUKURU.
Pia,Bw.Kibwengo amewakumbusha watumishi wa Umma kwamba mkono wa sheria ni Mrefu hivyo ukijihusisha na uhalifu ipo siku ya arobaini itafika na fedheha itakuja ni vyema kuzingatia Maadili ya kazi kwani Rushwa hailipi.
0 comments:
Post a Comment