Serikali mkoani Shinyanga imekamata pombe kali aina ya Shujaa, ambayo ilikuwa imetelekezwa porini eneo la Lubaga manispaa ya Shinyanga, ikiwa ndani ya gari aina ya Roli lenye namba za usajili T 391 AES, kwa madai ya kukwepa kulipa kodi.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari Novemba 9, 2019 Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack akiwa kwenye kituo cha Polisi wilaya ya Shinyanga, eneo ambalo gari hilo limewekwa chini ya ulinzi, amesema kuwa serikali itawashughulikia wawekezaji wote ambao wanatabia ya kukwepa kulipa kodi ya serikali.
Telack ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na usalama mkoa wa Shinyanga, amesema Serikali inahitaji sana wawekezaji hapa nchini ili kukuza uchumi wa taifa, lakini siyo wawekezaji wa kukwepa kodi na kufanya biashara kiujanja ujanja.
“Pombe hii kali ya Shujaa Katoni 1,490 tumeikamata ikiwa imefichwa porini eneo la Lubaga manispaa ya Shinyanga, ikiwa ndani ya gari hili ambalo mnaliona hapa, na wamiliki wa kiwanda hiki wamekuwa na tabia ya kukwepa kulipa kodi na siyo mara ya kwanza kukamatwa,”amesema Telack.
“Hivyo naagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA Kesho wafike hapa, ili kufanya tathmini ya kujua kiasi gani cha kodi ambacho watu hawa wanapaswa kulipa, ili Serikali iweze kukusanya mapato na kupata fedha za kutekeleza maendeleo kwa wananchi,”ameongeza.
Pia ameonya baadhi ya Askari Polisi kushirikiana na waharifu hao wa kiwanda cha Shujaa, na kuwapa mbinu za kukimbia ili kukwepa mkono wa Serikali, na kumuagiza Kamanda wa Jeshi hilo mkoani Shinyanga, kuwa ndani ya siku nne, wamiliki wa kiwanda hicho wawe wameshakamatwa.
Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Richard Abwao, alithibitisha kukamata Pombe hiyo ya Shujaa, na kuahidi kutekeleza maagizo hayo ya mkuu wa mkoa, huku akitoa wito kwa wamiliki hao wa kiwanda cha Shujaa wajisalimishe wenyewe kwa usalama wao kwani watakamatwa tu popote pale walipo.
Picha na Marco Maduhu- Malunde 1
Picha na Marco Maduhu- Malunde 1
0 comments:
Post a Comment