Monday, 11 November 2019

MIKOPO YA ELIMU YA JUU YAFIKIA SH. BILIONI 162.8 .....NI KWA WANAFUNZI 46,838 WA MWAKA WA KWANZA KWA MWAKA 2019/2020

...
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hadi kufikia Novemba 3, mwaka huu, Serikali imekwishatoa mikopo ya sh. bilioni 162.8 kwa wanafunzi 46,838 wa mwaka wa kwanza nchini kote.


“Kwa mwaka 2019/2020, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 450 kwa ajili ya mikopo kwa wanafunzi walengwa 128,285. Na hadi tarehe 3 Novemba, 2019 wanafunzi 46,838 wa mwaka wa kwanza kwa mwaka 2019/2020, walikuwa wamepewa mikopo inayofikia shilingi bilioni 162.8,” amesema.

Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumapili, Novemba 10, 2019) wakati akizungumza na maelfu ya waumini waliohudhuria Baraza la Maulid kitaifa katika viwanja vya Benki Kuu (BoT) Capripoint, jijini Mwanza.

Waziri Mkuu ambaye alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli, amesema Serikali inatambua kuwa utoaji wa huduma ya elimu ni gharama na kuwa baadhi ya wananchi hawawezi kumudu gharama hizo, hivyo ikaamua kuanzisha utaratibu wa kutoa mikopo ya elimu ya juu kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu.

“Mikopo inayotolewa na Serikali, huongozwa na Sheria ya Bodi ya Mikopo (Sura 178) inayotaja vigezo vya wahitaji na wenye udahili lakini wasio na uwezo wa kumudu gharama zote au sehemu ya gharama za mafunzo au kwenye maeneo ya kipaumbele ikiwemo yatima na wanaotoka familia zenye kipato duni.”

“Hata, hivyo Serikali inaendelea kufanyia kazi maoni na mapendekezo ya wadau mbalimbali ili kuboresha mfumo wa utoaji mikopo ya elimu ya juu. Nitumie nafasi hii kuwapongeza sana BAKWATA kwa kuweka mkakati wa kuunga mkono jitihada za Serikali katika eneo hili.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka viongozi mbalimbali watumie maadhimisho ya mazazi ya Mtume Muhammad (S.A.W) kama chachu ya kujiuliza juu ya uongozi wao, na kwa kiasi gani uongozi wao unaacha alama kwa wale wanaowaongoza.

“Kipindi hiki tunachoadhimisha mazazi ya Mtume huyu mbora wa darja, hebu nasi kama viongozi wa waumini tujiulize na tujitathmini, je, ni kwa kiasi gani tunamuenzi kwa kufuata mwenendo mzima wa Mtume Muhammad Swalla Allahu Alayh Wasallam. Je, ni kwa kiasi gani uongozi wetu umekuwa ni wenye kuacha athari njema kwenye nyoyo na fikra za waumini?”

Amesema wataalamu, waandishi na watafiti wa masuala ya uongozi walitumia muda mwingi kumsoma Mtume Muhammad (S.A.W). “Sababu kubwa iliyowavutia kumtafiti, kumsoma na hata kumuandikia makala na vitabu mbalimbali ni mafanikio makubwa aliyoyapata katika uongozi wake. Itoshe tu kusema kwamba Mtume Muhammad Swalla Allahu Alayh Wasallam alikuwa ni mtu wa familia na kiongozi makini kabisa.”

Aliwataka watambue kwamba mtu anaweza kuteuliwa kuwa sheikh au imamu lakini hawezi kuwa kiongozi bora mpaka pale uteuzi au kuchaguliwa kwake utakapothibiti katika nyoyo na fikra za wale anaowaongoza.

“Nitoe rai kwamba wakati tunapoelekea kwenye uchaguzi wa viongozi wa BAKWATA kwa ngazi mbalimbali baadaye mwaka huu, suala la kumuogopa Allah mtukufu na kufuata mwenendo wa bwana Mtume Muhammad Swalla Allahu Alayh Wasallam uwe ndiyo mwongozo wetu wa kuwapata viongozi,” alisisitiza.

Mapema, akitoa salamu za BAKWATA Taifa, Katibu Mkuu wa BAKWATA, Ustaadh Nuhu Jabir Mruma alisema Baraza hilo limeanzisha vikundi 82 vya uzalishaji vinavyojishughulisha na kazi za bustani na shamba darasa.

Kuhusu masuala ya utoaji wa haki na sheria, Katibu Mkuu huyo alisema watu 59,824 walipatiwa msaada wa kisheria na wataalamu wasaidizi wa sheria (paralegals) 79 katika maeneo mbalimbali nchini.

Alisema Desemba mwaka huu, BAKWATA itafanya uchaguzi katika ngazi mbalimbali. “Kupitia chaguzi hizo, tunatarajia kupata viongozi wabunifu, waadilifu na wachapakazi. Ninawasihi Waislamu wenye sifa wajitokeze kugombea nafasi husika.”

Pia alitumia fursa hiyo kuwaomba Waislamu wote wajitokeze kwa wingi kushiriki uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 24, mwaka huu ili watumie haki yao ya kuchagua viongozi wanaofaa. “Kuacha kupiga kura ni kuwapa wengine fursa wakuchagulie viongozi wanaowataka. Tuepuke kuchaguliwa viongozi tusiowataka,” alisema.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger