Mbunge wa Kigoma Kusini (CCM), Husna Mwilima, ameomba radhi kufuatia kauli yake ya kudai idadi kubwa ya watumishi wa kike katika Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) hawana mvuto, na kudai lengo la kauli yake ilikuwa ni kushinikiza maboresho kwenye shirika hilo.
Mwilima ametoa kauli hiyo Bungeni jijini Dodoma, leo Novemba 14, 2019, wakati wa kipindi cha maswali na majibu kwenda kwa Wizara ya TAMISEMI, ambapo kabla ya kuuliza swali lake aliomba radhi kwa Watanzania.
Mbunge Mwilima amesema kuwa "nilitoa ile kauli lengo lilikuwa ni kuboresha Shirika letu la Ndege la ATCL, kwa kuwa ile kauli yangu iliwaboa sana Watanzania hasa wanawake nitumie nafasi hii kuomba radhi Watanzania hasa wanawake wenzangu"
Mara baada ya kutoa kauli hiyo, Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai alimpongeza na kusema msamaha wake umepokelewa.
Novemba 7, 2019 wakati akichangia kwenye mpango wa maendeleo ya Taifa Bungeni jijini Dodoma, Mbunge Mwilima alidai kuwa watumishi wanawake kwenye Shirika la Ndege la ATCL, hawana mvuto na kupelekea kutokuwa na hamasa kwa wateja.
Chanzo - EATV
0 comments:
Post a Comment