Wednesday, 20 November 2019

Benki ya Maendeleo ya Afrika – AfDB Yaridhishwa Na Ujenzi Wa Mradi Wa Kituo Cha Kupoza Umeme Cha Zuzu Mkoani Dodoma

...
Na Peter Haule, WFN, Dodoma
Benki ya Maendeleo ya Afrika – AfDB imeridhishwa na kasi ya maendeleo ya mradi wa Kituo cha kupoza umeme cha Zuzu kinachofadhiliwa na Benki hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan- JICA.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya AfDB, Bw. Amos Cheptoo, alipofanya ziara ya  kukagua maendeleo ya Kituo hicho kilichopo katika eneo la Zuzu Mkoani Dodoma.

Bw. Cheptoo alisema kuwa amejionea kazi nzuri inayofanywa na Mkandarasi ya  kuhakikisha mradi huo unakamilika Februari, 2020 na kutumika kikamilifu katika kupoza na kusambaza umeme kwa manufaa ya Tanzania na nchi jirani.

Alisema kuwa mradi huo utakua na tija zaidi baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa umeme wa Julius Nyerere unaotarajia kuzalisha zaidi ya Megawati 2000, hivyo kuifanya miundombinu ya kupoza umeme kutumika kimailifu.

Mkurugenzi huyo wa  AfDB  alisema  umeme ndio nyenzo muhimu katika  ukuzaji wa uchumi na uendelezaji wa viwanda katika nchi za Afrika, kukamilika kwa miradi ya umeme kutasaidia uwepo wa umeme wa kutosha hasa katika nchi za Afrika mashariki na kusini mwa Afrika.

Serikali ya Tanzania imechukua hatua nzuri za kuboresha miundombinu wezeshi ya uzalishaji hasa Dodoma ambapo ndio Makao Makuu ya nchi.

Kwa upande wake mratibu wa mradi huo Mhandisi Peter Kigandye alisema kuwa, mradi huo utakuwa na uwezo wa kushusha umeme kwa Kilovoti 400 na kupoza umeme wenye uwezo wa takribani megawati 400 kisha kusambaza umeme katika maeneo mbalimbali mkoani Dodoma.

Gharama ya mradi huo unajumuisha mradi mwingine uliopo Singida na gharama zake ni dola za Marekani milioni 53 ambazo zimetolewa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania, Benki ya AfDB na Shirika la JICA ambapo Kituo cha Kupozea Umeme cha Zuzu kinagharimu takribani dola za Marekani milioni 22.

Aidha Kamishna Msaidizi wa masuala ya Nishati ya Umeme kutoka Wizara ya Nishati Mhandisi Innocent Luoga, ameishukuru Benki ya AfDB kwa kusaidia uboreshaji wa miundombinu hasa ya umeme kwa kuwa miradi hiyo itakapokamilika, utazinufaisha pia nchi za Zambia, Botswana na hata Afrika ya Kusini, kupitia mtandao wa umeme wa kusini

Amewataka wawekezaji walio na nia ya kuwekeza Dodoma kutumia fursa ya upatikanaji wa umeme wa uhakika kuwekeza hasa katika viwanda vikubwa na vidogo kwa kuwa mazingira ya uwekezaji yapo vizuri.

Mhandisi Luoga ameiomba Benki ya AfDB kusaidia upatikanaji wa fedha kwa ajili ya usambazaji zaidi wa umeme katika Mkoa wa Dodoma na viunga vyake ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kulifanya jiji kuwa na hadhi stahiki.

Mwisho



Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger