Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe pamoja na Waziri wa Habari, Utalii na Mambo Kale Zanzibar Mhe. Mahmoud Thabit Kombo na Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi Ally Abeid Karume wamesaini makubaliano ya ushirikiano katika kusimamia na kutekeleza sekta za Habari, Utamaduni,Sanaa na michezo ili kuongeza tija.
Uwekaji wa saini za ushirikiano huo umefanyika jana Jijini Dodoma katika ukumbi wa chuo cha Ufundi Veta, baada ya vikao vya ngazi za wataalam na Makatibu Wakuu wa Wizara husika kuwasilisha taarifa hizo kwa Mawaziri na hatimaye kuridhia tayari kwa ajili ya utekelezaji.
“Hatua hii ni nzuri na muhimu kwetu katika kuhakikisha tunadumisha na kuhifadhi muungano wa kihistoria ambao ulioasisiwa na waasisi wa Taifa hili Mwalimu Julius Kamabarage Nyerere na Shehe Amani Abed Karume” Alisisitiza Dkt. Mwakyembe.
Aidha, Waziri wa Habari, Utalii na Mambo Kale Zanzibar Mhe. Mahmoud Thabit Kombo ameeleza kuwa katika sekta ya habari ni muhimu kwa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kushirikiana na Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) ili kuandaa vipindi mbalimbali ikiwemo kipindi cha utalii Safari chaneli.
“Kwa kutambua umuhimu wa sekta ya utalii nchini , vyombo hivi vya habari TBC na ZBC vinapaswa kushirikiana kuandaa vipindi vya utalii ili kuitangaza sekta hii nje na ndani ya nchi” Alisisitiza Mhe. Mahmoud Thabit Kombo .
Kwa upande wake Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi Ally Abeid Karume amesema kuwa katika kuhakikisha kuwa lugha ya Kiswahili inatangazwa na kuenezwa kuna umuhimu wa kuandaa kanzi data itakayojumuisha wataalam wa Kiswahili ambao watakuwa wakifundisha wageni ndani na nje ya nchi.
“Tanzania imechangia sana katika kukuza lugha ya Kiswahili na watu wengi wanapenda kuja kujifunza kwetu ,hivyo naamini kwa kuwa na kanzi data hii itasaidia sana katika kuwapata watalaam wazuri wa kufundisha lugha hii”. Balozi Ally Abeid Karume.
Vilevile Mawaziri hao wamekubaliana kuimarisha ushirikano katika sekya ya sanaa kwa kuhakikisha kuwa ifikapo desemba 2019 wanakuwa wamesha andaa kanuni zitakazowawezesha watayarisha wa filamu kutoka nje ya nchi ili kuruhusu utumiaji wa maudhui hayo kwa vyombo vya habari vya serikali.
Mawaziri hao walimalizia kwa kueleza kuwa sekta ya michezo ni sekta muhimu sana katika kutambulisha taifa kupitia michezo mbalimbali na hivyo walikubaliana kuandaa kombe la Muungano, namna bora ya kuibua na kukuza vipaji pamoja na kuteua wajumbe wa bodi ya Baraza laTaifa la Michezo (BMT) na Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar.
Vilevile Mawaziri hao walipata wasaa wa kutembelea shule ya Fountain Gate Academy iliyopo maili mbili Jijini Dodoma, ambayo huibua na kuendeleza vipaji vya michezo kwa vijana wenye vipaji hivyo ili kuwaendeleza na kuweza kufikia ndoto zao ikiwa ni moja ya jitihada za kuendeleza sekta ya michezo nchini.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment