Halmashauri ya jiji la Dodoma imeichukua na kuanza kuimiliki rasmi timu ya Dodoma Football Club ambayo ilikuwa inamilikiwa na wananchi hapo awali.
Akizungumza na waandishi wa Habari jana Julai 9,2019 katika hafla fupi ya kumtambulisha kocha mpya atakayekinoa kikosi hicho,mkurugenzi wa jiji hilo Godwin Kunambi amesema timu Dodoma FC itakuwa na umuhimu mkubwa katika jiji hilo ambapo jiji la Dodoma lipo tayari kuihudumua na kuigharamikia timu hiyo.
Kunambi amesema”lengo kubwa ni kuwatanabaisha WanaDodoma na Watanzania kwa ujumla kuwa jiji la Dodoma limeichukua rasmi na kuimiliki timu ya Dodoma FC ili iweze kupaa kimataifa zaidi,Mpira ni taaluma kama taaluma zingine na hatutaingilia masuala ya ufundi katika timu itakuwa na bodi yake ya wataalam na washauri kuhusu Masuala ya Soka”
Aidha ,Kunambi ameongeza”Kuhusu kuimarishwa na kuanza kusimamiwa timu ya Dodoma FC kufika hadi ligi kuu na si ligi kuu tu mpaka Simba na Yanga wataisoma Namba tayari tumeshampata kocha Mbwana Makata kwa mkataba wa mwaka mmoja “Alisema.
Naye Kocha atakayekinoa kikosi hicho Mbwana Makata amesema atajitahidi katika kuhakikisha Dodoma FC inasonga mbele katika Mafanikio ya Soka.
“Nina imani kubwa tutakuwa na ushirikiano katika kukuza vipaji vya soka jiji la Dodoma,Bajeti ipo ,nimefundisha zaidi ya timu 20 nimepandisha vilabu vinne Twiga Sports,Mji Mpwapwa,Alliance na JKT Oljoro kikubwa ni Ushirikiano”alisema.
Katibu wa timu ya Dodoma FC Fourtnastus Johson amesema watahakikisha wanaisimamia vyema timu hiyo huku Bakari Fundikila Diwani wa Chang’ombe akizungumza kwa niaba ya Madiwani wa jiji hilo akisema uzalendo na ushirikiano ni nguzo muhimu katika kutekeleza majukumu.
Mbunge wa viti Maalum mkoa wa Dodoma Ester Bula amesema mchezo wa mpira wa Miguu unahitaji kuwa na kocha bora na wachezaji bora na ana mkakati wa kuanzisha timu ya mpira wa Mguu ya wanawake kwani kufanya hivyo inaweza kupatikana vipaji ambao pia wanaweza kuchezea timu ya Taifa.
Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Prof.Davis Mwamfupe amesema jiji la Dodoma litakuwa kitovu cha wachezaji hivyo ni jambo la kila mwanadodoma kuhakikisha anatoa Support katika timu hiyo.
0 comments:
Post a Comment