Bunge la Tanzania linatarajia kuwa mwenyeji wa vikao vya Kamati ya Uongozi na ya Bajeti za Chama cha Wabunge wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola–Kanda ya Afrika (CPA-AFRICA REGION) vitakavyofanyika tarehe 9 hadi 14, Julai, 2019 katika Ofisi Ndogo za Bunge la Tanzania, Jijini Dar es Salaam.
Kamati hizo zitakutanisha Wajumbe kutoka Mabunge zaidi ya Kumi (10) ya nchi za Afrika ambapo mbali na Wajumbe hao vikao hivyo pia vinatarajiwa kuhudhuriwa na Spika wa Bunge la Kenya Mhe. Justin Muturi, Spika wa Bunge la Sierra Leone Mhe. Dkt. Abbas Bundu, Spika wa Bunge la Uganda Mhe. Rebbeca Kadaga na Spika wa Bunge la Tanzania Mhe. Job Y. Ndugai ambaye ndiye mwenyeji wao.
Aidha, mbali na Maspika hao, vikao hivyo vitahudhuriwa na Naibu Spika wa Bunge la Cameroon Mhe. Emilia Lifaka, Naibu Spika wa Bunge la Namibia, Mhe. Bernard Sibalatani na pia Mnadhimu Mkuu wa Bunge la Ghana Mhe. Dkt. Osei Mensah Bonsu.
Mbali na vikao vya Kamati, kutakuwa pia na kikao cha Bodi ya Chama cha Wabunge wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola-Kanda ya Afrika ambacho kitafanyika tarehe 11 Julai, 2019.
Spika wa Bunge la Tanzania Mhe. Job Y. Ndugai anatarajiwa kuhudhuria na kuongoza kikao cha Bodi ya Chama cha Wabunge wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola–Kanda ya Afrika na pia kutoa hotuba ya ufunguzi wa kikao cha Kamati ya Uongozi wa chama hicho.
Wajumbe wengine ambao ni Waheshimiwa Wabunge wanaotarajiwa kuhudhuria katika vikao hivyo wanatoka katika Mabunge ya nchi za Malawi, Kenya, Nigeria, Ghana, Sierra Leone, Afrika kusini, Uganda, Namibia, Zambia, Lesotho, Mauritius na wenyeji Tanzania. Kwa hivi sasa Bunge la Tanzania ndiyo Sekretarieti ya Chama Chama cha Wabunge wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola–Kanda ya Afrika.
Imetolewa na;
KATIBU WA CPA-KANDA YA AFRIKA
8 Julai, 2019
0 comments:
Post a Comment