Profesa wa Mikrobiolojia na Immunolojia MUHAS, Eligius Lyamuya akiwasilisha matokeo ya utafiti wa Chanjo dhidi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) iliyofanyiwa majaribio katika maeneo mbali mbali ya nchini Tanzania na Msumbiji wakati wa kongamano la Kisanyansi la Kitafiti lililofanyika jijini Dar es Salaam. Picha zote na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.
Wageni waalikwa na wafunzi wa Chuo Kikuu MUHAS wakifuatilia.
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Prof Andrea Barnabas Pembe akitoa neno la ufunguzi wakati wa kongamano la Kisanyansi la Kitafiti lililofanyika jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Muhadhara huo, Prof. Kisali Pallangyo akiendesha muhadhara wakati wa kongamano la Kisanyansi la Kitafiti lililokuwa na lengo la kuwasilisha matokeo ya utafiti wa Chanjo dhidi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).
Profesa wa Mikrobiolojia na Immunolojia wa Chuo cha Afya St. Joseph, Fred Mhalu akichangia mada wakati wa kongamano la Kisanyansi la Kitafiti lililofanyika jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kulia ni Prof. Said Aboud na Dkt Edith Tarimo.
Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Mohamed Kambi akitoa ufafanuzi wa jambo.
Kamishna Msaidizi wa Polisi na Maganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Polisi iliyopo Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam ACP Dkt Charles Msenga akitoa mchango wake katika kongamano la Kisanyansi la Kitafiti lililokuwa na lengo la kuwasilisha matokeo ya utafiti wa Chanjo dhidi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Prof. Appolinary Kamuhabwa akifunga kongamano la Kisanyansi la Kitafiti lililofanyika jijini Dar es Salaam lililokuwa na lengo la kuwasilisha matokeo ya utafiti wa Chanjo dhidi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).
Kamishna msaidizi wa Polisi na Maganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Polisi iliyopo Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam ACP Dkt Charles Msenga (kulia) akiteta jambo na Dkt Patricia Munseri wa MUHAS.
Na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.
Chanjo dhidi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) inayofanyiwa majaribio nchini Tanzania ni salama na ina uwezo wa kuufanya mwili kutengeneza viashiria vya kinga.
Hata hivyo hiyo haimaanishi chanjo hiyo ni kinga dhidi ya Maambukizi ya Virusi (VVU) hivyo, matokeo ya utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), yamebainisha.
Akiwasilisha matokeo hayo, Profesa wa Mikrobiolojia na Immunolojia MUHAS, Eligius Lyamuya, amesema chanjo hiyo iliyofanyiwa majaribio imetengenezwa nchini Sweden na wataalam wenzao ambao wanashirikiana nao katika masuala ya tafiti.
"Tumeifanyia utafiti chanjo hii tuliangalia iwapo ni salama na iwapo ina uwezo wa kuchangamsha ile kinga ya mwili kutengeneza viashiria vya kinga na iwapo ina uwezo wa kutengeneza chembe chembe hai za mwili.
"Au uwezo wa kutengeneza molecular mbalimbali ambazo zinaashiria hii inaweza kuwa zinahusika katika kinga dhidi ya chanjo ambayo imetolewa.
" Hivyo, tumebaini chanjo hii ni salama na wote waliochanjwa hakuna ambaye amepata madhara yoyote hadi sasa wako vizuri," alisema.
Aliongeza "Jambo la pili ni kwamba tuna ushahidi kulingana na tafiti yetu chanjo hii inachangamsha ile kinga ya mwili kutengeneza viashiria vya kinga.
"Lakini hivi viashiria vya kinga vinavyotengenezwa haina maana kwamba ndiyo kinga yenyewe dhidi ya maambukizi ya VVU, hapana hivi ni viashiria tu vitahitaji kitu kingine zaidi kuona kama vina uwezo wa kupigana na vile virusi au la!," alisema.
Amesema katika kutengeneza chanjo hiyo wataalam wenzao wa Sweden waliangalia pia iwapo itafaa kutumika katika mazingira yetu au la!
"Tulikubaliana lazima ifae katika mazingira yetu kwa maana kwamba itakapotengenezwa huko siku zijazo kuwe na uwezekano wa kukinga dhidi ya virusi vya ukimwi ambavyo vipo katika mazingira yetu maana kuna aina nyingi ya virusi," amesema.
Amesema matokeo hayo yana maana kubwa kwamba bado wanaweza kuendeleza tafiti hizo kwa kushirikisha wahusika (sampuli) wengi zaidi.
"Katika hatua ya kwanza tulihusisha watu, wahusika walikuwa 60, lakini walioweza kupata chanjo zote tatu walikuwa 56 na walioweza kupata chanjo zote tatu na nyingine mbili za ziada walikuwa 42.
"Hii ina maana kuna ambao waliachia kwa sababu zao binafsi lakini kwa sababu ushiriki ni wa hiari hatuwezi kuuliza mtu kwa nini hakushiriki kupata chanjo mwanzo hadi mwisho," alisema.
Akizungumza, Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Mohamed Kambi amesema matokeo ya utafiti huo yameonesha wazi namna MUHAS ilivyofanya kazi kubwa kuunga mkono jitihada za kidunia katika kutafuta chanjo dhidi ya Ukimwi.
"Wizara tunaunga mkono juhudi hizi kwa sababu dunia inamaanisha tunaweza kufikia hatua ya kupata chanjo itakayofanya kazi vizuri, iliyo salama na kwa bei nafuu ambayo itasaidia mno katika kudhibiti maambukizi ya Ukimwi," alisema.
Ameongeza "Kimsingi, yamefanyika majaribio mengi, kizuri katika yote haya chanjo zimeonekana ni salama na zina uwezo wa kufanya mwili kutengeneza vichocheo vya kinga.
"Sasa chuo kitajikita kutafiti iwapo itakuwa na uwezo wa kukinga watu kutopata maambukizi ya ukimwi," amesisitiza Profesa Kambi.
0 comments:
Post a Comment