Simba
wamepata ushindi wa kihistoria dhidi ya Mbao FC mechi ya ligi kuu
Tanzania bara iliyochezwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba mkoani Mwanza.
Mbao
FC walianza kwa kutangulia kupata magoli mawili kipindi cha kwanza na
kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kuibuka na pointi tatu katika mchezo
huo. Magoli ya Mbao yamefungwa na Bernard dakika ya 18 na dakika ya 33.
Hadi
dakika ya 80 Simba ilikuwa nyuma kwa magoli 2-0 matokeo ambayo kama
yangebaki hivyo dakika 90 zinamalizika basi Wekundu wa Msimbazi
wangekuwa kwenye nafasi finyu ya kutwaa taji la ligi kuu msimu huu.
Mabadiliko
yaliyofanywa na benchi la ufundi la Simba kwa kumtoa Pastory Athanas na
nafasi yake kuchuliwa na Said Ndemla, Blagnon na Mavugo wakaingia
kuchukua nafasi za Liuzio na Hamad ndiyo yaliyo badili mchezo na kuipa
Simba ushindi wa kwanza Kanda ya Ziwa msimu huu baada ya kuchapwa 2-1 na
Kagera Sugar Jumapili iliyopita.
Magoli
ya Simba yamefungwa dakika za lala salama ambapo goli lao la kwanza
limefungwa dakika ya 82 na Frederick Blagnon. Uzembe wa golikipa wa Mbao
Erick Ngwegwe ambaye aliuacha mpira udunde kisha akashindwa kuudaka kwa
usahihi ulitua miguuni mwa Blagnon akafunga goli la pili dakika ya 90+1
na kufanya matokeo kuwa 2-2.
Wakati
kila mmoja akiamini mchezo utamalizika kwa sare ya Mbao 2-2 Simba,
Mzamiru Yassin akaifungia Simba goli la tatu dakika ya 90+7 kwa shuti
kali baada ya beki wa Mbao kupiga kichwa mpira ambao ulitua kwa Mzamiru
kisha kiungo huyo wa Simba kuachia mkwaju uliomshinda mlinda mlango wa
Mbao.
Ushindi
huo unaifanya Simba ifikishe pointi 58 ikiwa imecheza mechi 26 na
kurejea kwenye nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa ligi kwa pointi mbili
zaidi ya Yanga wanaoshuka kwenye nafasi ya pili lakini wakiwa na faida
ya mechi moja mkononi.
Mbao
inaendelea kubaki na pointi zake 27 ikiwa katika nafasi ya 13 kwenye
msimamo wa ligi, pointi nne zaidi ya Toto Africans ambayo ipo katika
timu tatu zitakazoshuka daraja.
Simba
wataendelea kubaki jijini Mwanza wakisubiri kucheza dhidi ya Toto
Africans timu ambayo imekuwa mwiba kwa ‘mnyama’ hususan mechi
inapochezwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba.
Mbao
FC wamefungwa mechi zao zote (mbili) walizokutana na Simba msimu huu.
Kabla ya kuchapwa 3-2 leo April 10, 2017, walifungwa 1-0 kwenye mchezo
wa raundi ya kwanza uliochezwa October 20, 2016 kwenye uwanja wa Uhuru,
Dar.
Swali
ambalo mashabiki wengi wa Simba huenda wakawa hawajalipatia majibu ni
kwanini Ibrahim Ajib, Laudit Mavugo, Said Ndemla na golikipa Daniel
Agyei kuanzia nje wakati wanne hao wamekuwa wakifanya vizuri kwenye
mechi za hivi karibuni?
Kikosi cha Simba kilichoanza kwenye mechi dhidi ya Mbao kiliongozwa na Juuko
Murshid (nahodha), Peter Manyika Jr (GK), Hamadi Juma, Mohamed Hussein,
Bessala Bokungu, James Kotei, Mzamiru Yassin, Juma Liuzio, Mohamed
Ibrahim na Pastory Athanas.
Walionzia benchi ni Daniel Agyei, Mwinyi Kazimoto, Frederick Blagnon, Hija Ugando, Ibrahim Ajib, Said Ndemla na Laudit Mavugo.
Matokeo kutoka uwanja wa Manungu Complex, Turiani, Morogoro
Mtibwa Sugar 0-0 Azam FC
0 comments:
Post a Comment