WAZIRI
wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba amewasimamisha kazi
wakurugenzi watano wa idara tofauti katika wizara hiyo kutokana na
kuonesha udhaifu mbalimbali katika utendaji wao na wengine kusababisha
hasara katika usalama wa chakula.
Waliosimamishwa
kazi ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Chakula nchini, Ombaeli
Lemweli kutokana na kutoa vibali vya ununuzi wa mazao na kuuzwa nje ya
nchi ilhali tathmini ikiwa haijafanyika. Nafasi yake kuchukuliwa na
Elimpaa Kiranga aliyekuwa Mkurugenzi wa Bodi ya Mazao Mchanganyiko.
Aidha,
ameagiza kusimamishwa kazi kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa
Hifadhi ya Chakula (NFRA), Charles Walwa na nafasi yake kushikwa na
Deusdedit Mpazi aliyekuwa Meneja wa NFRA kanda ya Dodoma, kutokana na
kuharibu ghala la chakula na kusababisha hasara.
Viongozi
wengine wa NFRA waliosimamishwa ni Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Huduma,
Anna Ngoo, Mkurugenzi wa Masoko, Mikalu Mapunda na Meneja wa NFRA,
Songea Jeremia Mtafya ambao wametakiwa kupisha na uchunguzi kufanyika
mara moja dhidi yao.
Kadhalika,
Dk Tizeba amemsimamisha kazi aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya
Bahari Kuu, Rashid Hoza na nafasi yake kushikwa na Hosea Mbilinyi
aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi, lengo likiwa ni kuimarisha
ulinzi wa Bahari Kuu.
Mbali
na nafasi hizo, pia Mkuu wa Kituo cha Utafiti cha Uyole mkoani Mbeya,
Dk Zakaria Maly amevuliwa madaraka na kuhamishiwa katika Kituo cha
Utafiti Seliani mkoani Arusha kuendelea na utafiti na badala yake nafasi
yake itachukuliwa na Arnold Msongi anayetoka Kituo cha Utafiti Ilonga,
Kilosa mkoani Morogoro.
Dk
Tizeba alitoa maamuzi hayo jana Dar es Salaam wakati akizungumzia
masuala mbalimbali, ikiwa ni mwezi mmoja baada yakuteuliwa na Rais John
Magufuli kushika wadhifa huo katika mabadiliko madogo ya Baraza la
Mawaziri yaliyompeleka aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Mwigulu Nchemba
kuongoza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri
Tizeba alisema wakati ambapo tathmini ya chakula nchini ikiwa
haijakamilika, Kurugenzi ya Usalama wa Chakula imekuwa ikitoa vibali vya
chakula kusafirishwa nje ya nchi, huku ikiwa haijulikani kama chakula
kilicho kinatosha au hakitoshi na ili ziada ilindwe.
“Mbali
ya kwamba hali ya chakula nchini ni nzuri lakini kumekuwepo na wimbi la
wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi wakipewa vibali na kununua
mazao ndani ya nchi na kuyauza nje ilhali tathmini ikiwa haijakamilika,”
alisema Tizeba.
Alitoa
wiki mbili kuanzia sasa ukaguzi wa chakula nchini uwe umefanyika ili
kupatikana kwa tathmini halisi katika kipindi cha mwaka 2015/2016 kwani
ununuzi wa mazao hayo umeonekana mkubwa na hali hiyo isipodhibitiwa hali
itakuwa mbaya zaidi.
Alisema
vibali hivyo vimekuwa vikitolewa kinyume cha utaratibu kwa kuwa
tathimini ilitakiwa kufanyika kwanza, hivyo Katibu Mkuu amsimamishe kazi
mkurugenzi huyo na uchunguzi ufanyike dhidi yake pamoja na vibali
ambavyo vimekuwa vikitolewa tangu mwaka jana kwani havina harufu nzuri.
“Hata
hivi karibuni nimepata taarifa kuna mfanyabiashara kapewa kibali cha
kusafirisha tani laki tatu kupeleka nchini Malawi, mfanye uchunguzi wa
vibali vyote alivyovitoa,” alisema Tizeba.
Kuhusu
NFRA, Dk Tizeba alisema umekuwepo udhaifu mkubwa katika ghala la
Songea, Dodoma na Sumbawanga ambako mazao yameharibika na kusababisha
hasara huku uongozi wa wakala licha ya kuombwa vibali vya kununuliwa kwa
mazao hayo kama chakula cha mifugo havikutolewa.
Akizungumzia
uvuvi bahari kuu, ameiagiza Kurugenzi wa Uvuvi kubadilisha masharti ya
leseni ya uvuvi katika bahari kuu ili kuangalia uwezekano wa kufanya
ubia na wavuvi hao ili Watanzania nao waweze kunufaika na mavuno ya
mazao hayo.
Alisema kwa wale ambao wana leseni hazitofanyiwa mabadiliko lakini kwa zile mpya na sheria haizuii kufanya hivyo.
Alisema
hivi sasa zipo meli 105 zote zikitoka nje ya nchi zikiwa zinaendelea na
uvuvi na kuchota chochote na kuondoka, huku mamlaka ya bahari wakiwa
wanayajua hayo, wakidai kuwa Tanzania haina mahali pa kushushia.
Alisema
kuanzia sasa meli zote ziambiwe mazao yote watakayovuna ambayo ni
tofauti na leseni zao zinavyotaka yaletwe Dar es Salaam, yagawiwe kama
itakavyohitajika kwani Tanzania imeendelea kuwa shamba la bibi kutokana
na kukosa uwezo wa kuvua katika bahari kuu.
0 comments:
Post a Comment