Monday, 4 July 2016

Siku 72 za Vita ya UKAWA na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson

...

Kukamilika kwa siku 72 za mkutano wa Bunge la Bajeti kumeacha rekodi mpya ya wabunge wa upinzani kususia vikao vya Bunge kwa muda mrefu zaidi kutokana na madai ya kutoridhishwa na utendaji wa Naibu Spika, Dk Tulia Ackson katika chombo hicho cha uwakilishi nchini.

Wapinzani chini ya mwavuli wao wa Ukawa, wamejikuta kwa mara ya kwanza, 12 kati yao wakisimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge kwa nyakati tofauti baada ya kutiwa hatiani na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge inayoongozwa na Mbunge wa Newala (CCM), George Mkuchika kwa kukiuka maadili. Wachambuzi wa siasa wameeleza kuwa hali hiyo imefanya Bunge kuongozwa kwa mgogoro ulioathiri mijadala na mikakati ya ndani na nje ya bajeti hiyo.

Hata hivyo, uamuzi wa Ukawa kususia vikao vinavyoongozwa na Dk Tulia kuliwafanya wabunge wa CCM kupoteza wastani wa dakika tatu kati ya 10 ambazo hupatiwa kujadili hoja, kwani walikuta wakitumia dakika za mwanzo kwenye mizaha, kebehi na vioja dhidi ya wapinzani badala ya mijadala.

Baadhi ya wabunge ambao walioongoza kumwaga vijembe ni Livingstone Lusinde (Mtera), Goodluck Mlinga (Ulanga Mashariki), Juliana Shonza (Viti Maalumu) na Abdallah Ulega (Mkuranga).

Ulega katika moja ya michango yake alifikia uamuzi wa kumpatia mtoto wake mchanga jina la Tulia kama ishara ya “kumuenzi Dk Tulia kwa uendeshaji wa Bunge unaofuata kanuni.”

“Dk Tulia umekuwa mvumilivu licha ya wabunge wa upinzani kususia vikao vinavyoendeshwa na wewe. Mke wangu naye amekuwa mvumilivu kama wewe na nitampatia mtoto wangu jina la Tulia,”alisema Ulega kabla ya siku chache Dk Tulia kutembela Hospitali ya Taifa Muhimbili kumuona mtoto huyo.

Mlinga alijikuta akiingia kwenye orodha ya wabunge waliotoa vioja bungeni wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria aliposema wanawake wa vyama vya upinzani ni lazima waitwe ‘baby’ ili wapate ubunge wa viti maalumu.

Kauli nyingine iliyoibua mjadala ni ile aliyoitoa kwenye mjadala wa bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kutaka Sanamu ya Askari iliyopo Mtaa wa Samora Jijini Dar es Salaam ibadilishwe na kuwekwa ya mwanamuziki wa kizazi kipya, Diamond Platinumz kutokana na kuipaisha nchi kimataifa.

Wabunge 12 wasimamishwa 
Katika adhabu za awali, kambi ya upinzani ilishuhudia wabunge saba wakisimamishwa kushiriki vikao vya Bunge baada ya kutiwa hatiani na Kamati ya Maadili kuhusika na vurugu zilizotokea bungeni Januari 27, mwaka huu wakati wakipinga kusitisha matangazo ya moja kwa moja ya Bunge.

Wabunge wawili wa Chadema Esther Bulaya (Bunda Mjini) na Tundu Lissu wa Singida Mashariki, walisimamishwa kuhudhuria vikao vyote vya Bunge la Bajeti lililomalizika wiki iliyopita na mkutano utakaoanza Septemba.

Wengine wa Chadema Pauline Gekul (Babati Mjini), Godbless Lema (Arusha Mjini), Halima Mdee (Kawe) na Kabwe Zitto, Mbunge wa Kigoma Mjini kupitia ACT–Wazalendo walisimamishwa kuhudhuria vikao vyote vya bajeti.

Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (Chadema) alipigwa marufuku kuhudhuria vikao 10 mfululizo. Juni 17 mwaka huu wabunge wawili wa viti maalumu pia kutoka Chadema, Suzan Lyimo na Anatropia Theonest walisimamishwa kwa kudaiwa kusema uongo bungeni.

Suzan alisimamishwa vikao vitano wakati Anatropia alisimamishwa vikao vitatu na kukatwa nusu mshahara na posho.

Kama hiyo haitoshi, wabunge wengine watatu, Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini), James Ole Millya (Simanjiro) na Saed Kubenea wa Ubungo walisimamishwa vikao vya Bunge kuanzia siku hiyo na kumalizia adhabu vikao vya Septemba.

Mbilinyi alisimamishwa vikao 10 kwa kudharau mamlaka ya spika kwa kuonyesha kidole cha kati juu cha mkono wa kulia, ishara ambayo inatafsiriwa ni matusi.

Kubenea na Ole Millya walisimamishwa vikao vitano kwa kudaiwa kusema uongo baada ya kushindwa kuthibitisha madai yao. 

Upinzani wasusa 
Ukilinganisha na mabunge yaliyopita, ukiacha Bunge la Katiba, wabunge wa upinzani walikuwa wakipinga jambo bungeni bila kutoka katika mkutano, lakini safari hii walikuja na staili mpya ya kususia vikao vyote vinavyoendeshwa na Dk Tulia na kusababisha kutochangia bajeti kuu.

Wabunge hao walisusa pia kushirikiana na wabunge wa CCM katika kutumia kantini ya Bunge, michezo na mitandao ya kijamii, mbaya zaidi wamekuwa hawawasalimu.

“Wao wameamua kuanza kututenga wenyewe, Dk Tulia anaona kiongozi wa upinzani anatukanwa, anacheza tu, lakini mbunge wa upinzani anapelekwa kwenye Kamati ya Maadili. Ngoja na sisi tujitenge,” alisema Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia.

Ingawa kuna wenyeviti wanne ambao kwa kawaida Spika hupokezana nao, katika mikutano yote iliyotangulia kiongozi huyo aliacha kiti mara moja tu kwa Andrew Chenge, lakini siku nyingine alikaa mwenyewe na kufanya wabunge wa Ukawa kuondoka ukumbini kila anapoongoza. 

Mbunge CCM akerwa
Hata hivyo, Mbunge wa Kasulu Mjini, Daniel Nsanzugwako (CCM), ingawa alipingwa na wabunge wengi wa CCM, alisema bado anaamini katika kukaa kwa pamoja kati ya wabunge wa upinzani na Dk Tulia ili kumaliza tofauti zao.

Dk Tulia aliwataka wabunge hao kufuata utaratibu wa kikanuni wa kufikisha malalamiko yao kuhusu kiti cha Spika, licha ya kwamba hata yale yaliyofikishwa dhidi yake hayakutolewa maamuzi yoyote. 
Hoja zilizosisimua 
Unapozungumza hoja zilizosisimua katika mkutano huo wa tatu, huwezi kuacha suala la kiinua mgongo cha wabunge kukatwa kodi kwani wabunge karibu wote waliopata nafasi ya kuchangia bajeti kuu waliibuka na hoja hiyo kuipinga, lakini waliambulia patupu.

Hoja hiyo ilihitimishwa baada ya Rais Dk John Magufuli kukubali kukatwa kodi katika kiinua mgongo chake pamoja na Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya.

Wabunge wa CCM walimshukia Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango wakidai kuwa kitendo cha kukata kodi za kiinua mgongo cha wabunge ni mtego wa kuwachonganisha na wananchi.

“Kwanini muwaache Rais, mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na majaji?” alihoji mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe wakati akichangia mjadala huo kabla ya viongozi hao kujumuishwa.

Mbunge wa viti maalumu (CCM), Jacqueline Msongozi alisema Dk Mpango amegusa pabaya kwa kukata kiinua mgongo kwa kuwa tayari kila mwezi hukatwa Sh1.3 milioni ya kodi na kwa miaka mitano watakayokaa bungeni watakuwa wamekatwa Sh50 milioni.

Hoja nyingine iliyojadiliwa kwa kila wizara ni bajeti iliyopitishwa na Bunge kutopelekwa yote ambapo Mbunge wa Tarime Mjini, Easter Matiko (Chadema), alisema katika miaka yote aliyokuwa bungeni hajawahi kuona Serikali ikileta bajeti bungeni inayotekelezeka.

Hata hivyo, Mbunge wa Lulindi Jerome Bwanausi (CCM) alisema usimamizi wa karibu wa Bunge katika kuhakikisha wanachopanga Serikali inatekeleza unaanza mwaka huu kwa kamati ya Bajeti kukutana kila baada ya miezi mitatu ili kujadili utekelezaji wa bajeti na kutoa ushauri.

Kubana matumizi 
Miongoni mwa mambo yalitajwa sana ni kubana matumizi kukidhi sera ya Rais Magufuli, ambapo Mbunge wa Sengerema-CCM, William Ngeleja alisema ni moja ya mambo mema yaliyo kwenye mkutano huo.

“Uchungu wa bajeti hii ni mafisadi na wala rushwa. Walizoea kufanya kazi kwa mazoea wataumia sana. Fedha za matumizi ya kawaida zimepunguzwa kwa kiasi kikubwa, uadilifu ndio utatawala matendo ya watumishi,” alisema Ngeleja.

Katika wizara mbalimbali matumizi ya kawaida ikiwemo bajeti zilizokuwa zikitolewa kwa ajili ya viburudisho imepunguzwa kwa kiasi kikubwa huku ofisi na wizara zikiagizwa kutumia kumbi za Serikali wakati wanapofanya mikutano, makongamano na warsha.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger