Friday 25 September 2020

WADAU WAJADILI UTEKELEZAJI WA MKAKATI WA KITAIFA KUTOKOMEZA MAUAJI DHIDI YA WAZEE

Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Naftali Ngóndi akitoa salamu kwa washiriki wa mkutano wa kujadili utekelezaji wa mkakati wa kutokomeza mauaji ya wazee uliofanyika jijini Dodoma. Kushoto ni Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya – Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii ambaye pia ni Mkurugenzi wa Sera na Mipango Sayi Magesa na kulia ni Mwakilishi kutoka TAMISEMI Mariam Mkumbwa.
Picha ya Pamoja ya washiriki wa mkutano wa kujadili utekelezaji wa mkakati wa kutokomeza mauaji ya wazee uliofanyika Jijini Dodom.Waliokaa kutoka kulia ni Mwenyekiti wa Wazee Mkoa wa Shinyanga Mzee Sengerema ,Kamisha wa Ustwu wa Jamii Dkt Naftali Ng'ondi,Mwenyekiti wa Mtandao wa mashirika yanayotetea wazee nchini Cotilda Isidory,Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya-Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Sayi Magesa na Mwakilishi kutoka Idara ya Operesheni na mafunzo Jeshi la Polisi Boniphace Isaack
Kamishna Msaidizi wa Ustawi wa Jamii kutoka Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Mwanaisha Moyo akichangia jambo katika mkutano wa wadau kujadili utekelezaji wa mkakati wa kutokomeza mauaji ya Wazee

Washiriki wa mkutano wa kujadili utekelezaji wa mkakati wa kutokomeza mauaji ya wazee uliofanyika jijini Dodoma wakiwa katika majadiliano hayo

Picha na WAMJW




Wadau mbalimbali wanaoshughulika na masuala ya wazee nchini wamekutana kujadili hatua iliyofikiwa ya utekelezaji wa mkakati wa Kitaifa wa kutokomeza mauaji dhidi ya Wazee leo jijini Dodoma.

Akifungua mkutano huo kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya - Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu, Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Sayi Magessa .

Amesema tangu mkakati huo wa miaka 5 uzinduliwe mapema mwaka jana, idadi ya mauaji ya wazee imepungua kutoka 557 mwaka 2014 hadi wazee 74 mwaka 2019 na kueleza kuwa hadi mwaka huu idadi ya wanaouliwa kwa sababu mbalimbali ni chini ya wazee 10 kwa mwaka.

“Mkakati huu umesaidia sana kupunguza kutoka 557 mwaka 2014 hadi 74 mwaka 2019 lakini hadi sasa idadi inazidi kupungua hadi kufikia mmoja hadi tisa, kipindi kama hiki cha uchaguzi hali ilikuwa mbaya pia hata kwa walemavu kutokana na Imani potofu tu”

Ameongeza pia mkutano huu unalenga kuangalia mafanikio, changamoto na malengo zaidi ya baadaye ili kufanikisha kutokomeza kabisa mauaji ya wazee.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi kufungua mkutano huo, Kamishna wa Ustawi wa Jamii nchini Dkt. Naftali Ngóndi ametoa rai kwa vyombo vinavyohusika na upelelezi pamoja na hukumu kuhusu mauaji ya wazee kusaidia ili jamii itambue kuwa jambo hili ni kosa kwani wazee wana haki ya kuishi na kufurahia maisha.

“Mwisho wa siku tutatoka na maazimio ambayo kwa miaka iliyobaki historia ya kuua wazee iwe tumeisahau katika nchi yetu, nitoe rai kwa wenzetu wanaoshughulikia mifumo ya jinai kusaidia mchakato wa kupeleleza mauaji ya wazee pamoja na kuwahukumu wote wanaohusika, hii itatoa ujumbe kwa jamii kuwa hii siyo sahihi” alisema Ngóndi.

Naye Meneja wa Programu Haki kwa Wazee na ushirikiano wa Wadau kutoka Shirika la HelpAge InternationalJoseph Mbasha amesema kwa ushirikiano na jitihada za wadau, nchi inakwenda vizuri katika kutokomeza mauaji ya wazee kwani takwimu zimepungua sana pamoja na kuwa barani Afrika nchi nyingi zilikumbwa na janga hilo kutokana na Imani potofu.

Mmoja wa Wazee walioshiriki mkutano huo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mtandao wa mashirika yanayotetea Wazee nchini Bi. Cotilda Isidory amesema tangu Serikali kupitia vyombo vyake mbalimbali iingilie kati suala la mauaji ya wazee, hivi sasa yamepungua kwa kiasi kikubwa kwani hapo kabla wameuawa wengi hali iliyokuwa inawatisha wazee hao.

Katika mkutano huo, washiriki walibainisha kuwa Serikali katika ngazi zote ikishirikiana na wadau ikiwemo vyombo vya Habari, kwa Pamoja walifanya jitihada kubwa kuhakikisha mauaji ya wazee yanakwisha.

Share:

Mwanafunzi Atiwa Mbaroni Kwa Kumkata Mapanga Mwalimu Wake

Mwanafunzi  wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Kiaga wilayani Butiama, mkoani Mara, anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumkata mapanga na kumsababishia majeraha mwalimu.
Inadaiwa kuwa chanzo ni utoro shuleni na kuamriwa kuita wazazi shuleni.

Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Daniel Shillah, alisema tukio hilo limetokea shuleni majira ya asubuhi wakati mwalimu akiwa anakagua wanafunzi watoro ndipo mwanafunzi huyo alimkata panga mwalimu wake wakiwa darasani.

Alisema mwanafunzi huyo amekuwa na tabia ya kutodhuria shuleni mara kwa mara, jambo ambalo liliwalazimu walimu kumuandikia barua ya kuita wazazi ili wajue sababu za kutohudhuria mara kwa mara.

Shillah aliongeza kuwa wakati mwalimu huyo akikagua wanafunzi watoro darasani, alimuuliza mwanafunzi huyo (jina limehifadhiwa) sababu ya kutokuja na wazazi wake, ndipo alipochomoa panga alilokuwa amelificha ndani ya nguo zake za shule na kuanza kumkatakata mwalimu sehemu ya bega la kulia na kiganja cha mkono wa kushoto.

Kamanda huyo alisema walifanikiwa kumtia mbaroni mwanafunzi huyo, na kuwa yupo mahabusu akisubiri uchunguzi kukamilika ili afikishwe mkortini.


Mwalimu huyo, Majogoro John, alisema wakati anaita majina ya wanafunzi watoro darasani hapo alimuona mwanafunzi huyo na kumuuliza kwanini hakuchukua barua ya kupeleka kwa wazazi wake, lakini mwanafunzi huyo hakumjibu kitu, badala yake akasubiria wakati anatoka darasani ndipo akachomoa panga alilokuwa na kuanza kumkatakata.

Alisema alipoona mwanafunzi huyo anamsogelea akamgeukia na kukatwa panga la begani upande wa kulia na kwamba wakati anajiandaa kukabiliana nae, akamkata tena kwenye kiganja cha mkono wa kushoto ukawa unaning’inia kisha mtuhumiwa alikimbia kutoka eneo la tukio.


Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Mara, Dk. Joachim Iyembe, amesema walimpokea majeruhi huyo na kumfanyia uchunguzi wa awali na kubaini kuwa sehemu iliyojeruhiwa zaidi ni mkono wa kushoto ambapo mifupa miwili imekatika na kusababisha mishipa ya fahamu kutokufanya kazi .

Iyembe alisema kuwa kutokana na kuhitaji huduma za matibabu zaidi hospitali ya mkoa imeamua kumpa rufani ya kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Nayo ofisi ya mkuu wa mkoa imetoa tiketi ya ndege kwa ajili ya mwalimu huyo kupelekwa Muhimbili jijini Dar es Salaam haraka, huku hospitali ya mkoa ikitoa gari kwa ajili ya kumfikisha mgonjwa huyo jijini Mwanza kwa ajili ya kupanda ndege.
 
Credit:Nipashe




Share:

MAKALA: Mambo 500 ya Kujivunia Chini ya Uongozi wa Rais Magufuli


Na Mwamba wa Kaskazini
Mpaka leo tafiti mbalimbali zinampa Rais Dkt John Pombe Magufuli ushindi wa zaidi ya asilimia 85 katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 mwaka huu dhidi ya wagombea wengine.


Bila shaka, hili linatokana na uchapakazi wake pamoja na uzalendo wake kwa taifa hili.


YAPO MENGI YA KUJIVUNIA  CHINI YA RAIS MAGUFULI
Kwa miaka Mitano iliyopita Tumeshuhudia  Rais John Pombe Magufuli akiendelea Kuwa Mfuasi Mzuri wa  Falsafa za Mwalimu Julius Nyerere ambaye Kupitia Dira ya Uongozi wake,  alisisitiza sana Kujenga Taifa la Kijamaa na Kujitegemea.


 Niendelee Kwa Kusema Kuwa  Rais Magufuli Mara baada ya kuingia tu Madarakani ili Kujenga Taifa la Kujitegemea Kiuchumi alifanya yafuatayo na kuendelea kuyasimamia Kikamilifu; Ameboresha Ukusanyaji  Mapato ya serikali yatokanayo na Kodi  Kutoka Bilioni 850 Mwaka 2015  hadi  Kufikia Trilioni 1.3 ( Disemba 2019 )  Fedha za Kitanzania na Kwa Mapato yasiyo ya Kodi Rais Magufuli amefanikiwa kwa Kiasi Kikubwa Kuboresha Ukusanyaji wake  na Kuongezeka Kutoka Chini ya Bilioni 688 mwaka 2014/2015 hadi Kufikia Trilioni 2.4  Fedha za Kitanzania Mwaka 2018/2019


 Aidha Rais Magufuli pia amefanikiwa sana Katika  kudhibiti Matumizi yake na  Kwa Kiasi kikubwa   ameelekeza fedha  hizo kuwahudumia Watanzania Kwa kuwaletea Maendeleo Katika Sekta zote. Rais Magufuli amefanikiwa Kwa Kiasi Kikubwa Kuimarisha Utendaji Kazi Serikalini, Maadili na Nidhamu Kwa Watumishi wote wa Serikali ( UMMA ) na Katika hili hakusita Kuchukua hatua za kinidhamu hadharani  Kwa Watumishi Walioshindwa Kufanya Kazi kwa Weledi, Nidhamu, Maarifa na Uadilifu.


Rais Magufuli toka ameingia madarakani mwaka 2015 alituahidi Kulinda Raslimali za Taifa letu ili kuhakikisha Urithi wa Raslimali tulizojaaliwa na Mwenyezi Mungu zinabaki Kuwanufaisha Watanzania wote na hapa ningependa kuwakumbusha Watanzania Kwa kurejea  katika lile Sakata la makinikia na Madini yetu kama mfano mmoja wapo.


Mosi kabisa, Mageuzi Makubwa sana yamefanyika  Ikiwa ni pamoja na Kuanzisha Wizara Mahsusi ya Madini, Kudhibiti Utoroshaji  na Usafirishaji wa Madini ghafi nje ya Nchi, Rais Magufuli ameanzisha Masoko ya Madini Kila Mkoa ambapo Kupitia hili Mapato  yatokanayo na Madini sasa yamekuwa na yanaonekana wazi. Serikali ya Rais Magufuli kupitia Bunge la JMT ilitunga na kupitisha Sheria ya Kulinda Rasilimali za Taifa ya Mwaka 2017 (  The Natural Wealth and Resources Permanent Sovereignty Act, 2017 ) Ikiwemo Madini.


 Kupitia Sheria hii, tumeshuhudiwa Kwa mara ya Kwanza  Watanzania wanamiliki Rasilimali zao kwa Nguvu za Kisheria Kama akina Saniniu Laizer😅 Mzee wa Tanzanite.


Ni kupitia Sheria hiyo pamoja na Jitihada za Rais  Magufuli na Serikali yake, wale Waliokuwa wanatunyonya “Mabeberu"  Walisalimu Amri na Kukubali Kutulipa Watanzania Malipo ya Fidia ya *Dola za Kimarekani Milioni Mia Tatu ( us-dollars 300 Millions ) ambazo Kampuni ya Barrick  ilikubali Kutulipa Kufuatia Majadiliano na Makubaliano na Tayari Dola za Kimarekani Milioni Mia Moja ( us –dollars 100 Millions ) tumekwisha lipwa.


 Mafanikio mengine Kupitia Makubaliano ya Serikali ya Rais Magufuli na Kampuni ya Barrick*  ni pamoja na Kuanzishwa  kwa Kampuni ya Twiga Minerals Company  ambayo Serikali yetu inamiliki 16%  na Kampuni ya Barick 84% .


Watanzania tunayo mengi sana  ya Kujivunia Kama Taifa linalohitaji Kusonga Mbele  Kimaendeleo, Kiuchumi na Kidemokrasia pia.


Kwa Uchache tu, nakukumbushia Machache Miongoni Mwa Mengi aliyoyafanya:
• Arusha amepeleka Miradi Mkubwa wa Maji: Bilioni 520 Arusha Jiji, Mradi wa Maji Chanzo toka Mto Simba Kilimanjaro Bilioni 16, Ujenzi na Upanuzi wa Barabara  Kuwa njia nne Kutoa  Ngaramtoni hadi USA River  ikiwemo zile za Mchepuko / Mzunguko ( By-Pass ) ambazo zimekamilika zaidi ya Bilioni 164, Tumejengewa Hospitali  Mpya  za Wilaya  ya Longido ( Bilioni 2 ), H/Wilaya Karatu Bilioni 1.5, H/ Wilaya Ngorongoro ( Bilioni 1.8 )  na H/Wilaya Arusha ( Bilioni 1.5 ) Pamoja na Kuboresha Hospitali za zamani.


• Ununuzi wa Ndege Mpya 11 Kwa fedha zetu za ndani sio mkopo, yaani CASH PAYMENTS ( Boeing 787-8 Dreamliners ziko 2, Airbus 220-300 ziko 2, Bombadier Dash 8  Q-400 ziko 4 na  nyingine Tatu kuja Miezi michache ijayo. Hapa Serikali ya Dkt. Magufuli imeboresha huduma ya Usafili wa Anga kupitia  Shirika  la  Huduma  ya  Usafirishaji Kwa  njia ya  Anga Tanzania      ( ATCL )ambapo Mapato yameongezeka na Utalii umeongezeka zaidi na Kuongeza Pato la Taifa.


• Ujenzi Mradi Mkubwa wa Uzalishaji  Umeme wa Mwl. Nyerere - Megawati 2115 ( Stieglers Gorge ) utakaogharimu  Pesa zetu za ndani Trilioni 6.5 ( Dola za Kimarekani Bilioni 2.9 ) hadi kukamilika Kwake na Kazi inaendelea vizuri sana.


• Mradi Mkubwa wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa  ya Treni ya Umeme ( SGR ) Kutoka  Dar es salaam hadi Mwanza. Maendeleo ya Mradi wa Kipande cha Kutoka  DSM-Morogoro na Kutoka Morogoro hadi Makutupora  Dodoma utagharimu Trilioni 7.062  fedha zetu wenyewe kwa kodi zetu.  Kipande cha Mwanza –Isaka-Dodoma Maandalizi yanaendelea vizuri. .
• Rais Magufuli hakuwasahau wana Dar es salama. Kawapelekea Miradi ya Kutosha;


 Miradi Mikubwa ya Ujenzi wa Madaraja na  Barabara za Juu  kama: Mradi wa Ujenzi wa Barabara za Juu Ubungo ( Ubungo Interchange Flyover (  zaidi ya Bilioni 200 zimetumika ), Mradi wa Ujenzi wa Barabara za Juu - Mfugale flyover  ( zaidi ya Bilioni 247  ), Mradi wa Salender Brigde  na Daraja la Majini Ziwa Viktoria  Busisi – Kigongo urefu wa Km 3.2 litakalo gharimu Bilioni 699 pesa za Kitanzania hadi kukamilika kwake, ujenzi unaendelea vizuri sana.


• Mpango wa Elimu Bila Malipo Kuanzia Shule Msingi hadi Sekondari ambapo Serikali ya JPM inatenga zaidi ya Bilioni 23 Kila mwezi ili kugharamia Elimu Msingi hadi Sekondari.


• Rais Magufuli ametimiza ndoto  ya  Baba wa Taifa Hayati  Mwl. JK Nyerere ya Mpango wa Kuhamishia  Serikali Dodoma. Dodoma sasa inapendeza, vijana wamepata ajira na Maendeleo Mkoa wa Dodoma sio suala la kuuliza Mwenye Majicho atizame mwenyewe.


• Mpango wa Kujenga Vituo vya Afya Kila Kata Nchini Kote Kwa Maeneo yasiyokuwa na Vituo vya Afya.


• Rais Magufuli pia ameweza Kujenga Hospitali  Mpya za Wilaya  Katika Halmashauri 67 Nchini Kote.


• Uboreshaji wa Viwanja vya Ndege ikiwemo Jengo Jipya la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ( JNI ), Mradi uliogharimu Bilioni 722 Fedha zetu za ndani. Sambamba na hili tunakumbuka pia Ununuzi na Ujenzi wa Mifumo ya Kuongozea Ndege Katika Viwanja vya Ndege vya JNIA Dar es salaam, Mwanza, Kilimanjaro na  Songwe Kwa gharama ya Bilioni 67.3 Fedha zilizotolewa na Serikali ya Rais Magufuli.


Ndugu zangu ni Mengi ya Kujivunia Kutokana na Uongozi wa Rais Magufuli. Nimeshindwa Kuyaandika yote maana ni Mengi sana.  


Lakini hawa wengine , tujiulize wamefanya nini  kwa taifa hili walipokuwa watumishi, au wabunge  kumzidi   JPM??


1. Wengine walipokuwa  wabunge hawawezi kukuonesha hata mtaro wa maji waliosaidia kuujenga jimboni;


2. Wakiwa wabunge walisifika kwa kuzuia wananchi kushiriki maendeleo;


3. Wakiwa wabunge hawakuwahi kupitisha bajeti yoyote kwa maendeleo ya wananchi zaidi ya kuzikataa zote;


5. Kiongozi sahihi ni lazima Asisitize amani, Lakini wapo wagombea  wengine hakuna mahali popote wamesisitiza amani zaidi ya vurugu.


6. Kiongozi Bora ni lazima awe mzalendo wa taifa lake...Lakini wapo wengine Wanaonekana kuamini katika mataifa ya nje kuja kuwasaidia kwa kufikiri na kutekeleza.


7. Wapo waonaponda kila kitu cha nchi wakiwemo Waasisi wa Taifa


8. Wapo waonaponda kila maendeleo yaliyopo nchini ikiwemo barabara wanazopita, maji wanayokunywa, umeme wanaoutumia kila siku n.k



Share:

Paulina Gekul aahidi kuzibeba Kero za Wananchi na kuzitafutia Ufumbuzi.

Na John Walter-Babati                                    
Mbunge mteule wa Jimbo la Babati Mjini (CCM) Paulina Gekul ameahidi kuzibeba kero za wananchi wa jimbo hilo na kuwasilisha serikalini kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi wa haraka.


Ametoa ahadi hiyo alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kiongozi kata ya Maisaka, Kijiji cha Chemchem kata ya Mutuka pamoja na Balowa Kata  Nangara kwenye mikutano ya kampeni za Chama cha Mapinduzi kuelekea uchaguzi mkuu  wa Madiwani, Wabunge na Rais Oktoba 28 mwaka huu.


Amewaomba Wananchi  katika Jimbo la Babati Mjini,  wajitokeze  kukipigia  kura Chama cha Mapinduzi kumchagua Rais Magufuli na Madiwani wanaotokana na chama hicho ili  kuendelea  kuwahudumia wananchi katika kipindi Kingine cha Miaka Mitano.


Mbunge huyo anaesubiri kuapishwa,  akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kiongozi kata ya Maisaka, ameahidi kutafuta Suluhu ya mgogoro uliopo kati ya wananchi wa Kijiji hicho  na wamiliki wa shamba la Tinna Estate.


Aidha ameahidi kuendelea kushirikiana na Viongozi wa chama na  serikali katika kushughulikia kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wa Jimbo hilo.


Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Elizabeth Malle  amesema kwa mambo mengi ya maendeleo aliyoyafanya Rais Magufuli na kuwasikiliza wanyonge, anastahili kupewa kura nyingi katika uchaguzi huo  ili aendelee kuongoza Watanzania.


Mgombea Udiwani kata ya Mutuka Yona Wawo amesema katika kipindi cha Miaka Mitano ijayo atahahakikisha anashirikiana na Mbunge ili shule shikizi  iliyopo katika kijiji cha Chemchem inapata usajili na kuwa shule inayojitegemea ili wanafunzi wasiende Umbali Mrefu.



Share:

Takukuru Hanang yaondoa milango 83 iliyowekwa kwenye Kituo cha Afya Chini ya Kiwango

 Na John Walter-Manyara
Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa wilayani Hanang mkoa wa Manyara imemuamuru Mzabuni Ayubu Iyaka  aliyepewa kazi ya kutengeneza na kupachika milango kwenye jengo la kituo cha Afya cha Hirbadaw, kuondoa milango yote 83 aliyoweka kwenye kituo hicho baada ya kubainika haina Ubora.


Takukuru imebaini hayo baada ya maafisa wake kufanya ukaguzi kwenye kituo hicho ambapo aliingia mkataba na Halmashauri hiyo kutengeneza na kupachika milango 83 yenye ubora iliyotengenezwa kwa kutumia mbao ngumu kwa gharama ya shilingi Milioni 28,000,000.


Mkuu wa Takukuru mkoa wa Manyara Holle Makungu  Septemba 24,2020, amesema wamejiridhisha kuwa kwa makusudi Mzabuni huyo aliamua kukiuka mkataba akatengeneza na kuweka kwenye jengo hilo la Kituo cha Afya milango hiyo isiyokuwa na ubora.


Pamoja na hayo  amesema Halmashauri ilishamlipa shilingi Milioni 14,000,000 ambazo ni nusu ya  fedha walizoingia mkataba.


Makungu amesema milango hiyo ambayo inadaiwa kuwa ni mipya, imeonekana ikiwa  imepasuka,mingine imepinda na kuvunjika kabla ya kituo kuanza kutumika.


Amesema kufuatia hayo Takukuru wilayani Hanang,  imemuamuru Mzabuni huyo kuondoa milango yote 83 na kutengeneza mingine yenye ubora unaokubalika katika majengo ya serikali na kwa mujibu wa mkataba alioingia na Halmashauri, na kwamba ataruhusiwa kuweka milango hiyo baada ya kukaguliwa na kujiridhisha kama ubora wake umekidhi vigezo.


Takukuru imewaasa  Wazabuni wanaopenda kufanya kazi na serikali kuwa waadilifu na kuzingatia mikataba ya kazi, huku ikitoa rai kwa watumishi wa Umma waliopewa dhamana ya kusimamia miradi ya Umma kutimiza wajibu wao kwa kuhakikisha miradi inatekelezwa katika ubora unaokubalika.



Share:

TAMWA YATOA MAFUNZO KWA WANAJAMII 66O KUPAMBANA NA UDHALILISHAJI WA KIJINSIA UNGUJA


Baadhi ya wananchi wa shehia ya Bumbwini wilaya ya kaskazini B Unguja waliohudhuria katika mkutano maalumu wa utowaji wa elimu dhidi ya matendo ya udhalilishaji yaliotolewa na TAMWA-Zanzibar kwa kuhirikiana na Action Aid.
Wasanii kutoa taasisi ya Thesode wakionesha igizo ambalo linaashirikia kukamatwa na mhusika wa matukio ya udhalilishaji kwa wanawake huku lengo kuu likiwa ni kutoa elimu kwa jamii kutoyafumbia macho matendo hayo.

Na Muhammed Khamis,Tamwa-Zanzibar
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tamwa Zanzibar kwa kushirikiana na shirika la Action Aid kwa lengo la kupambana na udhalilishaji wa kijinsia wamewapatia mafunzo wanajamii 660 kutoka shehia 22 Wilaya ya Kaskazini B Unguja.

Afisa wa maswala ya udhalilishaji kutoka TAMWA-Zanzibar Zaina Salum Abdaala alisema lengo kuu la mafunzo hayo kwa wanajamii hususani wanawake ni kujengewa ufahamu zaidi juu ya dhana nzima ya udhalilishaji na madhara yake kwa kuwa bila ya kuwa na elimu sahihi dhidi ya matendo hayo hayataweza kumalizika.

Alieleza kuwa anaamini elimu hiyo ilitolewa kwa muda wa wiki mbili kwa wanajamii italeta mabadiliko makubwa ikiwemo wanajamii kufahamu viashiria vya udhalilishaji sambamba na umuhimu wa kutoa taarifa mara pale matukio hayo yanapojitokeza kwenye jamii.

Alisema kuwa katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar hadi sasa baadhi ya wanajamii wamekuwa wakiyafumbia macho matendo hayo kwa wanawake na watoto kutokana kuhofia sababu mbali mbali ikiwemo kuvunjika kwa ndoa zao.

"Kuna matukio mbali mbali ya udhalilishaji yanafanyika lakini watu wapo tayari kuona yanaendela lakini hushindwa kusema kwa kuhofia kupewa talaka na waume zao’’aliongeza.

Hata hivyo Afisa huyo aliasa jamii kubadilika na kutokuwa na muhali badala yake watoke na kutoa taarifa dhidi ya matendo hayo kwa lengo la kuchukuliwa hatua kali zaidi kwa watendaji wote watakaobainika kutenda unyama huo.

Akizungumza kwa niaba ya Masheha wenzake sheha wa shehia ya Kitope Khamis Ndende Juma alisema ni kweli kuwa wamekua wakikabiliwa na matukio mbali mbali ya udhalilishaji kwenye jamii zao kiasi cha kwamba walio wengi wameanza kushtuka na kuhofia madhara zaidi.

Alisema suala la muhali bado ni tatizo ambalo wanaendelea kukabiliana nalo ndani ya jamii zao kwa kuwa wapo baadhi ya watu wanatendewa matendo hayo na kisha kuamua kunyamaza kimya.

Hata hivyo Sheha huyo alisema kupitia elimu hio ilitolewa na TAMWA-Zanzibar anaamini kwa kiasi kikubwa itakwenda kubadili jamii na hatimae watu kuwa tayari kutoa ushirikiano wa kina dhidi ya matendo hayo kwa lengo la kuyamaliza kabisa.


Mzee Ali Makame kutoka shehia ya Kitope alisema ili jamii iweze kumaliza tatizo hilo ipo haja kuhakikisha wazazi na walezi wanakua karibu zaidi na watoto wao kila wakati.

Alisema baadhi ya matukio mengi yanayotokea yanaonesha wazi kuwa baadhi ya wazazi ama walenzi wamekosa umakini katika suala zima la uangalifu kwa watoto na wakati mwengine hua sababu ya kufanyiwa unyama huo.

Kwa upade wake Afisa Dawati la Jinsia Mkoa wa kaskazini Unguja Salum Khamis Machano alisema jeshi la polisi kupitia dawati la jinsia wanajitahidi kwa kiasi kikubwa kupambana na matukio hayo ikiwemo kuwachukulia hatua wale wote wanaofikishwa katika dawati hilo.

Hata hivyo Afisa huyo alisema bado kuna tatizo ndani ya jamii ikiwemo la kukosa utayari wa kuendelea na baadhi ya kesi ambazo huwa tayari zimeshafikishwa katika vituo mbalimbali vya polisi.

Aliomba jamii kubadilika na kuyachukuliwa matendo hayo kuwa ni ya kinyama na yasiopaswa kuvumiliwa kwa mtu yoyote yule awe mzee,mtoto ndugu au jirani.

Share:

TARI YATOA MAFUNZO YA AGRONOMIA YA KOROSHO KWA MAAFISA UGANI NA WAKULIMA KONGWA


Mtafiti  kutoka Tari- Naliendele Programu ya Zao la Korosho, Kasiga Ngiha, akitoa mafunzo ya jinsi ya kuandaa shamba, kulipima na upandaji wa zao la korosho kwa Maafisa Ugani na Wakulima wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa katika shamba la Shule ya Sekondari ya Mnyakongo.
Mtafiti  kutoka Tari- Naliendele Programu ya Zao la Korosho, Kasiga Ngiha, akitoa mafunzo ya jinsi ya upimaji wa shamba kabla ya kupanda korosho.
Afisa Kilimo kutoka Kata ya Songambele, Asha Malekela wa Wilaya ya Kongwa akipima shamba kwa kamba katika mafunzo hayo kwa vitendo. 

Maafisa Ugani na Wakulima wakijifunza kwa vitendo namna ya upimaji wa shamba la korosho kabla ya kupanda.
Mkulima Gasper Rupia kutoka Kijiji cha Ibwaga,  akijifunza namna ya kupima shamba wakati wa mafunzo kwa vitendo. Kulia ni Mkulima Raheli Esau kutoka kijiji hicho.

Afisa Kilimo, Said Kajagale  kutoka Kata ya Ngomai akijifunza kunyoosha mstari kwa kuelekeza kwa mkono katika mafunzo hayo ya vitendo. 
Afisa Kilimo kutoka Kata ya Mkoka, Marcelin Chingilile (kushoto) na wenzake wakiwa kwenye mafunzo hayo
Afisa Kilimo kutoka Wilaya ya Kongwa, Elias Chilemue (kushoto) na wenzake, wakijifunza kutoka TARI namna ya kuweka alama wakati wa mafunzo kwa vitendo ya upimaji wa shamba la korosho.
Afisa Kilimo kutoka Wilaya ya Kongwa, Dominica Swai (kushoto) akijifunza namna ya kuweka mambo wakati wa mafunzo kwa vitendo ya upimaji wa shamba la korosho.
Mratibu wa Kitaifa wa Zao la Korosho kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI Naliendele Mtwara, Dkt.Geradina Mzena (kulia), akielekeza namna ya kunyosha mstari kwa kamba katika mafunzo hayo. 

Mkulima  Richard Sanyaji kutoka Kata ya Songambele ,  akishiriki mafunzo kwa vitendo kwa kuchimba mashimo katika shamba hilo la mfano la korosho la Shule ya Sekondari Mnyakongo.

Mkulima Gasper Rupia kutoka Kijiji cha Ibwaga,  akijifunza namna ya kuchanganya udongo na samadi kabla ya kupanda korosho.
Afisa Kilimo kutoka Kata ya Chitego, Michael Edward,  akishiriki mafunzo kwa vitendo kwa kuchimba mashimo katika shamba la mfano la korosho la Shule ya Sekondari Mnyakongo.

Mtafiti wa Kilimo kutoka  Tari Naliendele, Selemani Libaburu,  akitoa mafunzo ya jinsi ya kupanda korosho katika  shamba la mfano la korosho la Shule ya Sekondari Mnyakongo.


Share:

DKT JESCAR LEBA: MAZIWA YA NG’OMBE NI KWAAJILI YA MTOTO WA NG’OMBE


Mmoja wa akina mama waliohudhuria kongamano la onyonyeshaji linalojulikana kama Mother Meet Up event lililoandaliwa na USAID TULONGE AFYA mjini Iringa Pendo Muhongole akifuatilia kwa makini maelezo ya mgeni rasimi kwenye kongamano hilo.
Mgeni rasmi wa kongamano la unyonyeshaji linalojulikana kama Mother Meer Up event lililoandaliwa na USAID TULONGE AFYA mjini Iringa Dkt Jescar Leba (mganga mkuu wa halmashauri ya manispaa ya Iringa) akiongea na akinamama wakati wa kongamano hilo.

**
Mganga mkuu wa halmashauri ya manispaa ya Iringa Dokta Jescar Leba amewataka wakinamama wanaojifungua kufuata maelekezo ya wataalamu ikiwemo kutowaongezea chakula chochote watoto pindi wanapozaliwa hadi kufikia umri wa miezi sita kwa lengo la kulinda afya zao.

Dokta Leba ametoa rai hiyo kwenye shughuli ya wakina mama wenye watoto chini ya miezi 6 ijulikanayo kama “Mother Meetup” iliyoandaliwa na na mradi wa USAID TULONGE AFYA kupitia jukwaa la NAWEZA kwa lengo la kuwakumbusha wakinamama hao juu ya malezi bora ya watoto ambapo amesema watoto wanaozaliwa hawapaswi kuongezewa chakula chochote kwakuwa nyongeza hiyo ya chakula inaweza kuathiri afya na ukuaji wao kimwili na kiakili.

Aidha Dokta leba ameongeza kuwa zipo mila na desturi mbaya zilikuwa zinaathiri kampeni hiyo lakini kwa juhudi za serikali na wadau wa maendeleo, jamii imeelewa umuhimu wa unyonyeshaji maziwa ya mama pekee na kuanza kufuata utaratibu huo na kuongeza kuwa kwa mujibu wa takwimu walizonazo kwasasa unyonyeshaji bila nyongeza ya chakula kwa miezi sita ni karibu asilimia mia moja.

“Tulikuwa na changamoto ya mila na desturi katika eneo hili ambapo wazazi walikuwa wakishinikizwa na wanafamilia mfanobibi au majirani kwamba mtoto akilia anapaswa kupewa uji au hata maji kwa madai kuwa maziwa ya mama pekee hayatoshi lakini kwa sasa wengi wamekwishaelewa na utekelezaji ni karibu asilimia mia moja”,aliongeza Dokta Leba

Baadhi ya wakinamama hao wametoa ushuhuda na kueleza kuwa changamoto ya mila na desturi ilikuwa kikwazo kutokana na jamii inayowazunguka kulazimisha watoto kupewa nyongeza ya chakula ndani ya muda mfupi wa kuzaliwa kwa madai kuwa maziwa yam am hayawezi kumtosheleza.

“Mimi nilipojifungua ndani ya kipindi cha wiki mbili mtoto wangu wa kwanza alikuwa analia sana ndipo nikaambiwa nimuongezee chakula kwa madai kuwa maziwa yangu yalikuwa hayatoshi. Lakini nilikataa na kuendelea kumnyonyesha mwanagu mpaka alipofikisha miezi sita ndipo nikaanza kumuongezea vyakula na mpaka sasa ana afya njema”. alisema bi. Theresia Joseph ambaye ni mama wa watoto wawili.

Sezaria Andrew ni yeye ni mratibu wa afya ya uzazi na mtoto wa manispaa ya Iringa alisema pamoja na hamasa iliyofanywa na serikali katika kuhakikisha unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee kwa kipindi cha miezi sita unazingatiwa, mchango wa wadau wa maendeleo kupitia miradi mbalimbali kama mradi wa USAID Tulonge Afya si wakubezwa katika mafanikio yaliyofikiwa kwenye kampeni hiyo.

“Tunawashukuru wadau wetu USAID TULONGE AFYA kwani wamekuwa kiungo cha mabadiliko ya tabia ndani ya jamii, ,tunawaomba waendelee kutuunga mkono ili tuendelee kumpambania mtoto wa kitanzania. Watoto wanaoanzishiwa chakula kabla ya miezi sita ya kuzaliwa wengi husumbuliwa na magonjwa mbalimbali ikiwemo magonjwa ya tumbo kutokana na utumbo kutokuwa na uwezo wa kuchakata chakula” alisema dokta Sezarina Andrew.

Mradi wa USAID Tulonge Afya ni mradi miaka mitano unatekelezwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na shirika la FHI360 na wadau wengine wakiwamo mashirika ya TCDC na TMARC chini ya ufadhili wa shirika la kimarekani lijulikanalo kama USAID. Mradi huu unatekelezwa hapa nchini katika Wilaya 29 kwenye mikoa 12. Kwa upande wa mkoa wa Iringa mradi unatekelezwa katika wilaya tattu ambazo ni Iringa Manispaa, Mufindi DC na Kilolo DC.
Share:

MUST, WADAU WAKUTANA KUJADILI MITAALA MITATU NISHATI JADILIFU


Mhadhiri Msaidizi wa Chuo hicho Philemon Mutabilwa akiwasilisha mada katika majadiliano jana Dar es Salaam
**

CHUO Kikuu  cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) kimekutana na wadau wa Nishati Jadilifu lengo likiwa  kujadili mitaala ya nishati hiyo inayotarajiwa kuanzishwa mwaka wa masomo 2021/22.

Katika majadiliano hayo chuo hicho kimebainisha mitaala hiyo ni Shahada ya kwanza ya nishati hiyo , Astashahada ya uhandishi mitambo na Nishati Jadilifu pamoja na Astashahada ya uhandishi umeme na nishati.

Akizungumza katika mjadala huo Dar es Salaam jana Mhadhiri Msaidizi wa Chuo hicho Philemon Mutabilwa alisema  nishati hiyo ni muhimu ila haijawekewa mkazo hivyo endapo malengo yatatimia yatachochea kupata wahitimu wenye ujuzi wa kutosha watakaonufaisha taifa. 

"Mitaala itajikita katika namna ya kutumia nishati jadilifu kabla haijaanzishwa walimu watajengewa uwezo ili wakafundishe kuzalisha wahitimu wenye sifa stahiki kwenye soko la ajira," alisema Mutabilwa.

Alibainisha kuwa MUST haitaishia kwenye  kujikita katika mitaala hiyo badala yake miaka ijayo wataangalia uanzishwaji wa mitaala ya nishati ya upepo pamoja na masalia ya chakula.

Alifafanua kuwa Serikali ya Uholanzi ndio wafadhili wa mradi wa mkakati wa uanzishaji mitaala hiyo ambapo Sh.bilioni 1 zimetolewa kugharamia huku walengwa wakiwa MUST na Chuo cha Teknolojia Arusha (ATC).

Alisisitiza kuwa mradi wa mitaala hiyo imejikita kuwajengea uwezo walimu watakaofundisha pamoja na kujenga miundo mbinu hivyo aliishauri serikali kujiandaa endapo kutatokea ukosefu wa vifaa baada ya mradi kukamilika.

Alimshukuru Rais Dkt.John Magufuli kwa kukamilisha na kufanikisha  ujenzi wa Jengo kubwa la Maktaba .

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Wadau wa Nishati hiyo Mhandisi Dkt . Mathew Matimbwi alizishsuri taasisi za elimu ya juu zinazotoa mitaala hiyo kujenga miundombinu bora ya utendaji kwa vitendo ikiwemo maabara za kisasa ili kuwapa wahitmu ujuzi utakaowasaidia wanapokwenda sehemu za kazi.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Profesa Nkotage Hamisi alisema walimu wa kozi za uhandisi wawekewe  utaratibu wa kwenda kushiriki mafunzo kwa vitendo ili kuwasaidia kuwajengea uwezo.

Wakati huo huo Mtafiti kutoka UDSM Brenda Kazimili alishauri kuwa MUST kujenga utamaduni wa kutembelea shule za sekondari za wasichana ili kuwajengea hamasa na kuwahimiza kuyapenda masomo ya sayansi na uhandisi.

Katika hatua nyingine Mdau kutoka Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF) Sylivester Mwambije alishauri kuwepo utaratibu wa kuwapeleka wanafunzi wa mitaala hiyo kwenye taasisi binafsi wapatiwe mafunzo ili kuwapa ujuzi utakaosaidia kuendana na solo la ajira.

Vile vile imeelezwa na Rehema Mbugi ambaye ameshiriki  kama wadau kutoka baraza la ujuzi la Nishati kutoka TPSF   kwa ajili ya kusapoti MUST kuja na mitaala huo mpya alisema itachochea ajira kwa wahitimu kupata nafasi nzuri katika kuajirika.
Bi . Rehema Mbugi (katikati) ambaye ameshiriki kama wadau kutoka baraza la ujuzi la Nishati kutoka TPSF .

Share:

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Ijumaa Septemba 25



















Share:

PROF. MSANJILA ASHUHUDIA KILO 2,271 YA MADINI YA BATI IKIUZWA

 

Katibu Mkuu Wizara Madini Prof. Simon Msanjila akisaini Kitabu katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Rashidi Mwaimu.
Katibu Mkuu Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila akieleza jambo kwenye Mkutano uliofanyka katika Soko la Madini ya Bati la Wilaya ya Kyerwa Mkoani Kagera.
Baadhi ya washiriki walioshiriki Mkutano wa Katibu Mkuu Wizara Madini Prof. Simon Msanjila katika Soko la Madini ya Bati la Wilaya ya Kyerwa Mkoani Kagera.


Katibu Mkuu Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali katika Soko la Madini ya Bati la Wilaya ya Kyerwa Mkoani Kagera.


Katibu Mkuu Wizara ya Madini Prof.Simon Msanjila ameshuhudia biashara ya Madini ya Bati (Tin) ikifanyika ambapo Shirika la Taifa la Uchimbaji Madini (STAMICO) likifanya manunuzi Kilo 2,271 ya Madini ya Bati yenye thamani ya shilingi Milioni 34 kutoka kwa Wachimbaji Wadogo.

Katika ziara yake hiyo, Prof. Msanjila alitembelea Soko la Madini la Wilaya ya Kyerwa Mkoani Kagera na kuzungumza na Wachimbaji Wadogo pamoja na Wafanyabiashara wa Madini hayo.

Aidha Prof. Msanjila amewataka wachimbaji Wadogo na Wafanyabiashara wa Madini ya Tin kulitumia Soko la Kyerwa kuuzia Madini yao ili wanapotaka mkopo kutoka benki inakuwa rahisi kwa Wizara kudhibitisha mauzo yao kwa kuwa yatatambuliwa kwenye mfumo wa Wizara.  

Pia Prof. Msanjila amewasihi Wachimbaji Wadogo na wafanyabishara wa Madini ya Bati kufungamanisha biashara ya madini na chumi zingine kama kilimo, ufugaji n.k. ili kujiongezea wigo wa fursa zitokanazo na Sekta ya Madini.

Katika ziara hiyo yenye lengo la kuhakikisha Soko la Madini ya Bati la Wilaya ya Kyerwa Mkoani Kagera limeanza kufanya kazi, Prof. Msanjila aliambatana na viongozi Mbalimbali wa Serikali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Rashidi Mwaimu.

Vile vile, Prof. Msanjila amewasisitiza wachimbaji Wadogo na Wafanyabiashara wa Madini ya Bati kuongeza juhudi za uzalisha wa madini hayo kwani Soko la uhakika kwa sasa linapatikana na kuwataka kuepuka utoroshaji wa madini hayo.

Pia, Prof. Msanjila maipongeza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kyerwa kwa ushirikiano na uzalendo waliouonesha katika kulinda Rasilimali Madini kwa manufaa ya Nchi.

“Mwaka jana mwezi wa pili Tanzania tulifanikiwa kupata Cheti cha Uhalisia wa Madini ya Bati ambapo Waziri Mkuu Kassim Mjaliwa alikizindua cheti hicho hivyo, tuongeze juhudi kuzalisha Madini kwa wingi na kuyaongezea thamani na hatimaye tuyapeleke nje ya nchi tukawauzie”, alisema Prof Msanjila.

Wakati huo huo, Prof Msanjila alisikiliza kero na changamoto za Wachimbaji Wadogo wa Madini ya Bati pamoja na Wafanyabiashara wa madini hayo na kuyatolea majibu papo hapo.

Pamoja na mambo mengine Prof. Msanjila alitembelea Viwanda vya kuchakata Madini ya Bati kikiwemo Kiwanda cha African Top Mineral Limited pamoja na Tanzplus ili kujionea shughuli za uongezaji thamani katika viwanda hivyo zinavyo fanyika.

Prof. Msanjila amewataka wanunuzi wa Madini ya Bati kuwalipa fedha zao Wachimbaji Wadogo kwa wakati na kuepuka usumbufu wa kuwacheleweshea malipo yao.

Aidha, Prof. Msanjila amewataka Wachimbaji Wadogo na Wafanyabiashara ya Madini ya Bati kupendana, kuthaminiana na kuachana na mambo ya majungu ili waongeze tija kwenye shughuli yao ya uchimbaji madini.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Rashidi Mwaimu alimpongeza Katibu Mkuu kwa ziara yake hiyo ambayo imesaidia kuondo changamoto za Wachimbaji Wadogo na Wafanyabiasha wa Madini ya Bati ambayo yalidumu kwa muda mrefu.

Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger