Sunday, 27 September 2026

BARRICK BULYANHULU YAFANIKISHA UJENZI WA KITUO CHA POLISI NYANG’HWALE


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, SACP Safia Jongo, akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Kituo Kidogo cha Polisi katika Stendi ya Mabasi ya Ikangala, Halmashauri ya Nyang’hwale mkoani Geita. Kituo hicho kimejengwa kwa ufadhili wa fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kutoka Barrick Bulyanhulu, kwa lengo la kuimarisha usalama katika eneo hilo. Wengine pichani ni maofisa waandamizi kutoka Halmashauri ya Nyang’hwale na Barrick Bulyanhulu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, SACP Safia Jongo, akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Kituo Kidogo cha Polisi katika Stendi ya Mabasi ya Ikangala, Halmashauri ya Nyang’hwale mkoani Geita. Kituo hicho kimejengwa kwa ufadhili wa fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kutoka Barrick Bulyanhulu.
Muonekano wa sehemu ya Kituo Kidogo cha Polisi katika Stendi ya Mabasi ya Ikangala, Halmashauri ya Nyang’hwale mkoani Geita. Kituo hicho kimejengwa kwa ufadhili wa fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kutoka Barrick Bulyanhulu.
Muonekano wa sehemu ya Kituo Kidogo cha Polisi katika Stendi ya Mabasi ya Ikangala, Halmashauri ya Nyang’hwale mkoani Geita. Kituo hicho kimejengwa kwa ufadhili wa fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kutoka Barrick Bulyanhulu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, SACP Safia Jongo, akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kituo Kidogo cha Polisi katika Stendi ya Mabasi ya Ikangala, Halmashauri ya Nyang’hwale mkoani Geita. Kituo hicho kimejengwa kwa fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kutoka Barrick Bulyanhulu, kwa lengo la kuimarisha usalama katika eneo hilo.
Afisa Mahusiano ya Jamii wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Bw. William Chungu akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kituo Kidogo cha Polisi katika Stendi ya Mabasi ya Ikangala, Halmashauri ya Nyang’hwale mkoani Geita.
Picha ya pamoja ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, SACP Safia Jongo, viongozi wa Halmashauri ya Nyang’hwale na Barrick Bulyanhulu, wakati wa uzinduzi wa Kituo Kidogo cha Polisi katika Stendi ya Mabasi ya Ikangala, Halmashauri ya Nyang’hwale mkoani Geita. Kituo hicho kimejengwa kwa fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kutoka Barrick Bulyanhulu, kwa lengo la kuimarisha usalama katika eneo hilo. Wengine pichani ni maofisa waandamizi wa Halmashauri ya Nyang’hwale na Barrick Bulyanhulu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, SACP Safia Jongo, akibadilishana mawazo na Afisa Mahusiano ya Jamii wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Bw. William Chungu, wakati wa uzinduzi wa Kituo Kidogo cha Polisi katika Stendi ya Mabasi ya Ikangala, Halmashauri ya Nyang’hwale mkoani Geita. Kituo hicho kimejengwa kwa fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kutoka Barrick Bulyanhulu.

***

Katika mwendelezo wa kuunga mkono jitihada za Serikali za kuleta maendeleo na kulinda usalama wa raia,mgodi wa Barrick Bulyanhulu uliopo Halmashauri ya Msalala wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga kupitia fedha za uwajibikaji kwa jamii (CSR) umefanikisha ujenzi wa kituo cha polisi kidogo cha polisi katika stendi ya mabasi ya Ikangala wilayani Nyang'hwale mkoani Geita.

Akiongea wakati wa uzinduzi wa kituo hicho Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Nyang’hwale Ntiriyo Ezekiel, alisema jengo la kituo hicho ambalo linajumuisha sehemu ya mahabusu na ofisi ya Meneja wa kituo tayari limekamilika kwa asilimia 100.

 “Halmashauri ilipokea fedha za CSR shilingi milioni 36.6 kutoka Barrick Bulyanhulu ambapo kwa kushirikiana na ofisi Kamanda wa Polisi wa wilaya ilianza utekelezaji wa ujenzi”, alisema.

Ezekiel alisema mbali na ujenzi wa kituo cha polisi Barrick Bulyanhulu pia imefanikisha ujenzi wa stendi ya mabasi ya kisasa ya Ikangala ambapo uwepo wa kituo hicho utaimarisha zaidi ulinzi na usalama wa abiria pamoja na mali zao ikiwemo kuwahudumia wananchi wanaoishi maeneo ya jirani na kituo hicho.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita  SACP Safia  Jongo ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo, alitoa shukrani kwa kampuni ya Barrick kwa kuwa mstari wa mbele kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuimarisha usalama wa raia na kuongeza kuwa kituo hicho kitaweza kusaidia kuimarisha ulinzi katika kituo hicho na kuwa msaada kwa abiria, wamiliki wa vyombo vya usafiri na kuwezesha askari polisi kufanya kazi ya kuwahudumia wananchi katika mazingira rafiki.

SACP Jongo ameongeza kuwa katika Kituo hicho Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita litaweka Dawati la masuala ya kijinsia  na ustawi wa jamii kwa ajili ya kushugulikia kesi za  unyanyasaji wowote wa kijinsia na alimtaka Mkurugenzi wa Halmshauri hiyo kuweka utaratibu mzuri kwa mawakala na wapiga debe ndani ya stendi kwa kuwapa sare  na vitambulisho ili kuepuka Abiria kuibiwa mali zao wakiwa ndani ya stendi.

Mwakilishi wa mgodi wa Barrick Bulyanhulu katika hafla hiyo Bw. William Chungu ambaye ini Afisa Mahusiano ya Jamii, alisema  Barrick kupitia migodi yake nchini  itaendelea kushirikiana na Serikali katika masuala mbalimbali ikiwemo kutekeleza miradi ya kimkakati ambayo itanufaisha wananchi  hususani wanaoishi maeneo ya jirani.

Chungu aliongeza kuwa kukamilika kwa mradi huu ni hatua muhimu katika kuboresha huduma za usafiri, kuimarisha usalama wa abiria na mali zao pamoja na kuweka mazingira bora kwa shughuli za kiuchumi katika eneo la stendi.

Alieleza kuwa kukamilika kwa mradi huu ni hatua muhimu katika kuboresha Huduma za usafiri, kuimarisha usalama wa abiria na mali zao pamoja na kuweka mazingira bora kwa shughuli za kiuchumi katika eneo la stendi.

Barrick ambayo inaendesha shughuli zake nchini kwa ubia na serikali kupitia kampuni ya Twiga imekuwa ikishirikiana na serikali kupitia jeshi la polisi kufanikisha usalama kwa raia ambapo mwaka juzi  ilikabidhi msaada wa vifaa vya kisasa vya kupima ulevi vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 100 za Kitanzania kwa Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani ikiwa ni mwendelezo wa kampeni ya Barrick ya ‘Journey to zero’ ambayo inalenga kuhamasisha afya na usalama kwa wafanyakazi wake na wadau wengine wote kwenye jamii.

Pia Barrick imekuwa mstari wa mbele kushirikiana na wadau mbalimbali wanaotoa elimu ya ukiukaji wa haki za Binadamu ikiwemo ukatili wa kijinsia ambapo imekuwa ikishirikiana  na Jeshi la Polisi kufikisha elimu ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia kwenye jamii.






Share:

MAGAZETI YA LEO JUMAPILI SEPTEMBA 27,2026



Magazetini Leo












Share:

Saturday, 26 September 2026

TANESCO YATOA ELIMU YA USALAMA WA UMEME KABLA YA MVUA KUBWA LIULA

Afisa msaidizi wa mahusiano TANESCO Mkoa wa Ruvuma bi Emma Ulendo akiwa katika kijiji cha Liula kata ya Matimila wakati walipotembelea kijiji hicho kutoa elimu kuhusu utunzaji wa miundombinu ya umeme na kujikinga na mvua kubwa ya El Niño 
Diwani wa Kata ya Matimila iliyopo katika Halmashauri ya Songea Vijijini Mkoani Ruvuma Menace Cosmas Komba akizungumza na wananchi wa kijiji cha Liula namna ya kutunza miundombinu ya umeme kijijini hapo 

Na Regina Ndumbaro, Songea-Ruvuma

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Ruvuma limeendelea kutoa elimu kwa wananchi wa Kijiji cha Liula, Kata ya Matimila, Halmashauri ya Songea Vijijini, kuhusu namna ya kujikinga na madhara yanayoweza kujitokeza wakati wa mvua kubwa za El Niño, utunzaji wa miundombinu ya umeme, namna ya kulipia huduma hiyo, kupambana na wizi wa vifaa vya umeme pamoja na kuepuka uchomaji moto holela katika maeneo yenye nguzo za umeme. 

Share:

Friday, 25 September 2026

LOWASSA APENDEKEZA MAMA TESHA KUTUNUKIWA TUZO YA HESHIMA YA RAIS




Na mwandishi wetu,Arusha

Mbunge Mstaafu wa Monduli, Mheshimiwa Fredric Lowassa, ametoa wito kwa Tume inayomshauri Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuzingatia mchango mkubwa wa Mwalimu Mama Tesha katika jamii na elimu, na kupendekeza jina lake kwa ajili ya kutunukiwa Tuzo ya Heshima ya Rais.

Mheshimiwa Lowassa ametoa kauli hiyo wakati akizungumza katika Mahafali ya 27 ya Shule ya St. Margarets, mkoani Arusha, akieleza kuwa mchango wa Mama Tesha unapaswa kutambuliwa si katika sekta ya elimu pekee, bali pia kama mchango wenye umuhimu kwa taifa.

Amesema nchi nyingine, ikiwemo Uingereza, zina utaratibu wa kutambua watu waliofanya mchango mkubwa katika jamii kupitia tuzo za heshima, akitumia uzoefu wake akiwa Mbunge wa Monduli kueleza namna alivyowahi kusaidia mgeni mmoja aliyekuwa ametoa mchango katika mradi wa maendeleo Meserani kupata tuzo kama hiyo.

“Nikiwa Mbunge wa Monduli, alikuja Mzungu mmoja alitusaidia mradi pale Meserani. Akaniambia nimwandikie barua kwenda kwa Malkia wakati ule, ili nimwombe apate tuzo ya heshima. Na nilimwandikia kutoka Monduli kwa sababu mchango huo alitusaidia Monduli, alipata ile tuzo ya heshima,” amesema Lowassa.

Akihusisha uzoefu huo na mchango wa Mama Tesha, Mheshimiwa Lowassa amesema sasa ni wakati muafaka kwa Tanzania kuwa na utaratibu wa kutambua watu walioleta mafanikio makubwa katika jamii, akisisitiza kuwa Mama Tesha anastahili kupewa heshima hiyo kutokana na mchango wake.

“Ninasema na nitatoa wito leo kwa Tume ambayo inamshauri Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Sasa ni wakati muafaka na sisi kama taifa tukaweza kutambua mafanikio makubwa kama ya Mwalimu Mama Tesha, akatambuliwa akapokea tuzo ya heshima ya Mheshimiwa Rais kwa mchango wake huo,” amesema.

Mheshimiwa Lowassa ameongeza kuwa suala la kutambua watu wenye mchango mkubwa linapaswa kuwa la kitaifa na kugusa sekta mbalimbali, akisema pendekezo la Mama Tesha ni hatua ya kuanzia katika kutambua mchango wa watu waliotoa huduma kubwa kwa jamii.


“Ni wakati sasa wote tukumbushane, wote ni jambo la kitaifa, sisemi sekta ya elimu pekee lakini kila sekta. Lakini sisi tunaanza kwa kupendekeza jina la Mama Tesha litambuliwe, lipate tuzo ya heshima ya elimu ya taifa kwa ujumla,” amesema.

Kauli hiyo imekuja ikiwa sehemu ya hotuba yake katika Mahafali ya 27 ya Shule ya St. Margarets, ambapo amesisitiza umuhimu wa jamii na taifa kutambua mchango wa watu wanaojitoa katika kujenga na kuendeleza jamii.

Mheshimiwa Lowassa amehitimisha kwa kuwashukuru wahudhuriaji wa mahafali hayo na kuwatakia baraka pamoja na siku njema.












Share:

MFUGALE: WANAHABARI MNA NGUVU YA KUOKOA JAMII DHIDI YA MABADILIKO YA TABIANCHI


Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Waandishi wa habari za mazingira nchini wametakiwa kuandika kwa kina habari za uchunguzi kuhusu shughuli na matukio mbalimbali yanayochangia kuongezeka kwa athari za mabadiliko ya tabianchi, kwa lengo la kuisaidia jamii kuchukua hatua na kulinda mazingira.

Wito huo umetolewa na Mhariri Mwandamizi wa Habari za Mazingira, Deodatus Mfugale, wakati akitoa mada kuhusu uandishi wa habari za uchunguzi wa mazingira katika mafunzo ya wanahabari 35 kutoka mikoa ya Kanda ya Kati yaliyofanyika jijini Dodoma.

Mfugale amesema maeneo mbalimbali nchini yanaendelea kukabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi, ambazo zinachangiwa kwa kiasi kikubwa na shughuli za kibinadamu ikiwemo ukataji miti, upanuzi wa mashamba katika maeneo yaliyohifadhiwa, uvamizi wa vyanzo vya maji, uchafuzi wa mazingira, uvamizi wa maeneo ya malisho pamoja na shughuli za uchimbaji madini zisizozingatia kikamilifu masuala ya mazingira.

Amesema waandishi wa habari wana nafasi muhimu katika kuibua changamoto hizo na kusaidia jamii kuelewa madhara yake, huku akiwataka kutumia takwimu sahihi, sheria na vyanzo vya kuaminika ili kuibua masuala ya uwajibikaji.

“Waandishi, nendeni mkaandike habari za uchunguzi kusaidia jamii ili kuifanya dunia kuendelea kuwa salama. Lakini muandike kwa usahihi na mjumuisha sauti za wananchi wanaoathirika,” amesema Mfugale.

Amesema uandishi wa habari za mazingira haupaswi kuishia katika kuripoti matukio pekee, bali unapaswa kwenda hatua zaidi kwa kuchunguza chanzo cha tatizo, wahusika, madhara yanayotokea na hatua zinazochukuliwa kukabiliana na changamoto hizo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Wanahabari ya Usaidizi wa Jamii za Pembezoni (MAIPAC), Mussa Juma, amesema mwandishi wa habari za mazingira anapaswa kuandika kwa usahihi na uhuru, kuelewa kwa kina jambo analolifanyia kazi na kuhakikisha anashirikisha sauti za makundi mbalimbali katika jamii.

Juma amesema makundi hayo yanapaswa kujumuisha wanawake, vijana na jamii zinazoathirika moja kwa moja na changamoto za kimazingira, huku akisisitiza umuhimu wa uandishi unaochochea uwajibikaji na kulinda maslahi ya umma.

Amesema wanahabari wanapaswa kuongeza utafiti kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi katika maeneo mbalimbali nchini, zikiwemo athari zinazohusiana na ongezeko la joto duniani, ukame, mafuriko, kupungua kwa uzalishaji wa chakula na uharibifu wa mifumo ya ikolojia.

Naye Mkurugenzi wa Miradi na Uendeshaji wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Wakili Halima Sonda, ametoa wito wa kuhakikisha wanahabari wanawake wanapewa fursa sawa na wenzao wanaume katika kufanya na kuchapisha habari za uchunguzi, hususan zinazohusu mazingira.

Wakili Sonda amesema bado kuna changamoto ya udhalilishaji wa wanawake kwenye mitandao ya kijamii pamoja na mifumo dume katika jamii, hali ambayo inaweza kuwazuia wanawake kushiriki kikamilifu katika uandishi wa habari za uchunguzi.

Amesema changamoto hizo zinapaswa kupingwa huku wanahabari wanawake wakitakiwa kufahamu sheria na taratibu zinazolinda haki zao dhidi ya ukatili na udhalilishaji.

Mafunzo hayo yameandaliwa na THRDC kwa kushirikiana na MAIPAC, kwa ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), kwa lengo la kuwawezesha wanahabari kuimarisha ujuzi wa kuandika habari za mazingira, kuibua changamoto na kuchangia uwajibikaji katika usimamizi wa mazingira.

Mafunzo hayo yamewakutanisha wanahabari kutoka Dodoma, Singida, Mbeya, Iringa na Morogoro, na ni sehemu ya mfululizo wa mafunzo yanayotolewa kwa wanahabari nchini kupitia mradi unaolenga kuwawezesha waandishi wa habari za mazingira kuimarisha uwezo wao na kukuza uelewa wa jamii kuhusu masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

Kabla ya mafunzo ya Kanda ya Kati, mafunzo kama hayo tayari yametolewa katika Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Ziwa.


Share:

RC MHITA AAGIZA USAFI KILA JUMAMOSI SHINYANGA, ATOA TAHADHARI YA MVUA ZA EL NIÑO

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita

Na Stela Paul , Shinyanga

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amesisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kutekeleza zoezi la usafi wa mazingira kila Jumamosi, akieleza kuwa usafi si jukumu la siku moja bali ni sehemu ya nidhamu na maisha ya kila siku.

Mhe. Mhita ameyasema hayo leo, Septemba 25, 2026, wakati akiongoza viongozi mbalimbali wa mkoa na wilaya pamoja na wananchi katika zoezi la usafi wa mazingira lililofanyika katika Soko la Ujasiriamali la Ibinzamata, mjini Shinyanga.

Zoezi hilo limefanyika ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa kampeni ya usafi wa mazingira inayolenga kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika kutunza mazingira na kuyafanya kuwa safi na salama.

Akizungumza baada ya zoezi hilo, Mhe. Mhita amesema siku ya Jumamosi imeelekezwa kuwa siku maalumu ya usafi wa mazingira kuanzia ngazi ya kaya, huku akiwataka viongozi wa serikali za mitaa na vijiji kuweka utaratibu utakaowezesha zoezi hilo kutekelezwa kwa ufanisi.

“Kila Jumamosi kazi ya kwanza ni kuhakikisha unaangalia usafi wa eneo lako. Haimaanishi kwamba siku nyingine usafi usizingatiwe. Usafi ni jukumu la kila siku na usafi ni nidhamu,” amesema Mhe. Mhita.

Ameagiza pia Wakurugenzi wa Halmashauri zote mkoani Shinyanga kuhakikisha wanawasilisha tathmini za kila mwezi kuhusu mwenendo wa usafi katika kata na maeneo mbalimbali, ili kubaini changamoto na kuchukua hatua stahiki.

“Wakurugenzi wote wanatakiwa kuleta tathmini ya kila mwezi ya taarifa ya mwenendo wa usafi kwa kata na maeneo yote, maana ni lazima tuchukue hatua kwenye maeneo yote machafu, ikiwemo kuchukua hatua za kisheria na kutoza faini pale inapobidi. Usalama wetu sote ni kuzingatia usafi,” ameongeza.

Katika hatua nyingine, Mhe. Mhita amewataka wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi, ikiwemo mabondeni na maeneo yanayoweza kuathiriwa na mvua, kuchukua tahadhari mapema ili kujikinga dhidi ya madhara yanayoweza kujitokeza wakati wa msimu wa mvua.

Amesema wananchi wanapaswa kuzingatia tahadhari zinazotolewa na mamlaka husika, ikiwa ni pamoja na kuondoka katika maeneo hatarishi endapo wataelekezwa kufanya hivyo.

“Kwa wenzetu wote ambao mnakaa kwenye mabonde, majarubuni na maeneo yote hatarishi, tunawasihi kuchukua hatua mapema. Tunatarajia kuwa na mvua za El Niño, hivyo kuchukua tahadhari mapema ni muhimu ili kuhakikisha uhai haupotei, madhara hayajitokezi kwenye miundombinu na wananchi kwa ujumla,” amesisitiza.

Mhe. Mhita amesema Serikali imeendelea kujiandaa kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua, ikiwemo changamoto za kiafya na magonjwa ya mlipuko, akisisitiza kuwa afya na usalama wa wananchi ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, amesema suala la usafi wa mazingira limeendelea kusimamiwa na kutekelezwa katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanaishi katika mazingira safi na salama.

Amesema ushiriki wa wananchi, viongozi na wadau mbalimbali ni muhimu katika kuhakikisha kampeni hiyo inaleta matokeo yanayotarajiwa.

Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger