Na Lydia Lugakila -Bukoba.
Mwassa ametoa Kauli hiyo Desemba 22, 2024 katika kikao na waandishi wa habari kilichofanyika katika Ofisi za Mkoa huo.
Amesema kuwa ulevi kwa asilimia kubwa unasababusha ajali hivyo watumiaji wa vyombo vya moto wahakikishe waendeshe kwa umakini ili waepuke ajali zinazoweza kujitokeza.
"Tunaposherehekea siku kuu hizi za Christmas na Mwaka mpya tujiepushe na yote yanayoweza kutugharimu pia wazazi tuwaangalie watoto wasitembee wenyewe barabarani kwani ajali ni nyingi lakini msiwaruhusu kwenda fukwe za bahari bila uangalifu" alisema Mwassa.
Alisema kuwa Mkoa ulimpoteza mtoto hivi karibuni baada ya kuzama ziwani hivyo sehemu zote za hatari wasipelekwe watoto kucheza.
Aidha aliongeza kuwa katika siku kuu hizo ni vyema watoto wakapelekwa katika maeneo yanayotambuliwa kwa michezo yao.
Mwassa pia alitumia fursa hiyo kuwaomba wazazi kutowapeleka watoto katika maeneo ya baa ili kulinda ustawi na makuzi.
Hata hivyo alieleza kusikitishwa na ajali iliyotokea Wilayani Biharamulo Mkoani humo iliyosababisha watu 11 kufariki dunia na wengine 16 kujeruhiwa ikiwa siku za hivi karibuni pia kumetokea ajali mbaya katika Wilaya ya Karagwe na kusababisha vifo na majeruhi ambapo pia aliwapa pole Watanzania na wanakagera kutokana na majonzi hayo.