Sunday, 7 December 2025

MAHAFALI YA TANO LITTLE TREASURES SECONDARY YANG’ARA, WAZAZI WAHIMIZWA KUWEKEZA KWENYE ELIMU

Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog

Mahafali ya Tano ya Shule ya Sekondari Little Treasures iliyopo Mjini Shinyanga yamefanyika kwa uzito mkubwa na hamasa ya kipekee, yakikutanisha wazazi, walimu, viongozi na wadau mbalimbali wa elimu katika Mkoa wa Shinyanga.

Hafla hiyo iliyofanyika Desemba 5,2025 imeonesha ukubwa wa uwekezaji wa shule hiyo katika kuinua kiwango cha elimu na kujenga kizazi chenye maadili, maarifa na uwezo wa kutimiza ndoto zao.

Akiwasilisha risala ya mahafali hayo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Little Treasures, Alfred Mathias, alisema jumla ya wanafunzi 61 wamehitimu masomo yao, wakiwemo wavulana 36 na wasichana 25, huku akisisitiza kuwa shule hiyo itaendelea kujenga misingi imara ya nidhamu na ufaulu.

Mkurugenzi wa Shule za Msingi na Sekondari Little Treasures, Lucy Mwita, alisema wamejidhatiti kuendelea kuwa hazina ya watoto na daraja la mafanikio kwa kuwajengea uwezo, maadili na uelewa mpana wa masomo yao.
Aliwataka wazazi kuendelea kuiamini na kuiunga mkono shule kwa kupeleka watoto wao ili waendelee kupata elimu bora.

Kwa upande wake, Meneja wa shule hiyo, Wilfred Mwita, alisema Little Treasures itaendelea kujituma kwa bidii kuhakikisha wanafunzi wanafundishwa kwa weledi na kuandaliwa kufikia malengo yao ya kitaaluma na maisha, huku akiomba mashirikiano zaidi kutoka kwa wazazi.

Mgeni rasmi kwenye mahafali hayo, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Bakari Ally, aliwataka wazazi kubadili mtindo wa maisha na kuacha kuendekeza starehe zinazopoteza fedha, badala yake wawekeze kwenye elimu ya watoto wao.
Bakari alisema wazazi wengi wamekuwa wakitumia fedha nyingi kwenye sherehe za ubatizo hadi shilingi milioni 3 au sherehe za siku ya kuzaliwa kwa zaidi ya laki 8, lakini wanapofika Januari wakitakiwa kulipia ada za watoto wao, huanza kuomba muda na kusisitiza kuwa hawana fedha.

“Wazazi wekeni vipaumbele vyenu kwenye mambo muhimu na kuacha kupoteza pesa hovyo. Sasa hivi ni mwezi Desemba lakini mtu anafanya sherehe ya ubatizo shilingi milioni 3, au sherehe ya kuzaliwa shilingi laki 8. Ikifika Januari unadaiwa ada unasema huna hela, hivi unadhani walimu watakuelewa kweli?” alisema.
Alisisitiza kuwa elimu ni uwekezaji na wazazi hawapaswi kuchelewesha ada za watoto wao.

“Maji ukiyavulia nguo lazima uyaoge, lipeni ada kwa wakati. Ukweli mchungu, lakini wazazi badilini mtindo wa maisha ,kusomesha mtoto ni kufanya uwekezaji,” aliongeza.

Katika hatua nyingine, Bakari aliitaka Shule ya Sekondari Little Treasures kuanzisha Club ya Sheria, ambayo itakuwa ikipokea wataalamu wa sheria kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga kwa ajili ya kutoa elimu ya sheria shuleni hapo na kuwajengea wanafunzi uelewa mpana wa masuala ya kisheria.

Aliwataka wahitimu kuendelea kudumisha nidhamu, kuwa mabalozi wazuri wa shule hiyo na kuitangaza vyema popote watakapokwenda.
Sehemu ya wahitumu wakicheza muziki

Mtendaji wa Mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga Bakari Ally akizungumza.
Mkurugenzi wa Shule za Msingi na Sekondari Little Treasures Lucy akizungumza.
Meneja wa shule za Little Treasures Wilfred Mwita.
Mkuu wa shule ya Sekondari Little Treasures Alfred Mathias akisoma Risala ya shule.
Mwakilishi wa wazazi aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akizungumza.

Aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, akimpongeza mtoto wake Cedric kwa kuhitimu kidato cha Nne shule ya Sekondari Little Treasures.
Share:

Saturday, 6 December 2025

“MAWAKILI MNA NAFASI KUBWA YA KUONDOA CHANGAMOTO MBALIMBALI ZA KISHERIA KATIKA TAIFA HILI” – NAIBU MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI


Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Samwel M. Maneno amemuwakilisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza S. Johari katika sherehe za kupokelewa na kukubaliwa Mawakili wapya wa Kujitegemea zilizofanyika tarehe 5 Desemba, 2025 Jijini Dodoma.

Akizungumza katika sherehe hizo za kuwapokea na kuwakubali Mawakili wapya wa Kujitegemea, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amewakumbusha Mawakili hao kuwa wana nafasi kubwa katika kuondoa changamoto za Kisheria zinazowakabili wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.

“Naomba nitumie siku hii adhimu kuwaelezea Mawakili wapya kuwa, mna nafasi kubwa sana ya kuondoa changamoto mbalimbali za kisheria katika Taifa hili." Amesema Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali

Aidha, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amewakumbusha Mawakili wa Serikali juu ya umuhimu wa kuzingatia weledi katika utendaji wa haki kwa wananchi, ambapo ameeleza kuwa Mawakili ni kiungo muhimu sana baina ya wananchi na Mahakama katika kuichambua na kuitafsiri haki na sheria.

“Nitumie nafasi hii kuwaeleza Mawakili mliokubaliwa leo kuwa, mna nafasi kubwa katika kuhakikisha jukumu la utoaji haki linatekelezwa kwa ufanisi na Mahakama. Mnapaswa kuisaidia Mahakama itende haki na kuhakikisha wananchi wanapatiwa haki zao wanapokwenda Mahakamani au kwenye vyombo vingine vya kisheria”. Amesema Mhe. Maneno.

Katika hatua nyingine, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itaendelea kuunga mkono Serikali na taasisi mbalimbali zinazotoa huduma za msaada wa kisheria nchini ambapo Ofisi imeanzisha Kamati za Ushauri wa Kisheria katika ngazi ya Mikoa na Wilaya pamoja na kuendesha Kliniki za msaada wa kisheria katika maeneo mbalimbali nchini.

“Napenda kuwasisitizia pia Mawakili wote ikiwa ni pamoja na Mawakili mlioapishwa siku ya leo kuwa mnapaswa kushiriki katika Wiki ya Sheria na Kampeni mbalimbali za kutoa misaada ya kisheria na kutoa elimu ya sheria kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.” Amesema Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Vilevile Mhe. Maneno amewasihi Mawakili wapya kuwa nidhamu na kuzingatia Kanuni za Maadili ya taaluma ya sheria, huku akiwakumbusha kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ataendelea kudhibiti nidhamu ya Mawakili wa Kujitegemea kwa kuzingatia mamlaka aliyopewa kupitia Sheria ya Mawakili, Sura ya 341.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Jaji George M. Masaju amewataka Mawakili hao wapya waliopokelewa na kukubaliwa kufanya kazi kwa kuzingatia uadilifu kwa kufuata Katiba na Sheria za Tanzania ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa

.“Mnapokwenda kutekeleza majukumu yenu ni muhimu mkafanye kazi kwa uadilifu mkubwa na kuzingatia miongozo mbalimbali ikiwemo Katiba, Sheria na Kanuni mbalimbali.” Amesema Jaji Mkuu.

Sambamba na hilo, Jaji Mkuu wa Tanzania amewaeleza Mawakili hao kuhakikisha wanatenda haki kwa wananchi, kwa kusimamia misingi ya sheria , kanuni na taratibu, huku wakiwa sehemu ya kuendelea kulinda amani ya Taifa.

“Niwaombe Mawakili mliokubaliwa na kupokelewa leo mkatende haki kwa wananchi, mkazingatie utawala wa sheria unafuatwa, pia ninyi ni sehemu ya kuilinda na kuitetea Amani ya Taifa hili.” Amesema Jaji Mkuu.

Sherehe hizo za 73 za kuwapokea na kuwakubaki Mawakili wapya Kujitegemea zimehusisha jumla ya wahitimu 774.
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger