Tuesday, 18 November 2025
TIRDO YATOA MAFUNZO KWA WAJASIRIAMALI WA MKA MBADALA, YALENGA UBORA NA UHIFADHI WA MAZINGIRA
DAR ES SALAAM, Novemba 17, 2025 — Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) limetoa mafunzo maalum kwa wajasiriamali wanaojihusisha na utengenezaji wa mkaa mbadala unaotokana na mabaki ya misitu, yakiwa na lengo la kuongeza ujuzi na kuboresha ubora wa bidhaa hiyo kufikia viwango vinavyotakiwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TIRDO, Mhandisi Ramson Mwilangali, amesema mafunzo hayo yanajumuisha nadharia, vitendo na elimu ya uhifadhi wa mazingira pamoja na namna sahihi ya kuhifadhi bidhaa za nishati mbadala.
Wajasiriamali Kujengewa Mtandao na Kupimwa Bidhaa Bure
Mhandisi Mwilangali amesema kupitia mkutano na mafunzo hayo, TIRDO imelenga kujenga mtandao wa wajasiriamali utakaowawezesha kubadilishana ujuzi kati yao na wataalamu wa shirika hilo.
Aidha, alibainisha kuwa mara baada ya mafunzo, wajasiriamali watakaonza uzalishaji wa bidhaa hizo watapatiwa huduma ya kupimwa bure sampuli za mkaa kupitia maabara za TIRDO ili kuhakikisha bidhaa zinazoingia sokoni zina ubora unaohitajika.
“Pale tutakapobaini kuna upungufu, kama taasisi tutatoa maelekezo ya nini kifanyike ili kufikia kiwango kinachotakiwa. Baada ya marekebisho, sampuli inaweza kupimwa tena na kuingia sokoni ikiwa safi na kwa gharama nafuu kwa watumiaji,” amesema.
Wadau Wapongeza Mafunzo
Kwa upande wake, mwakilishi wa kikundi cha Fahari Kijani Group kutoka Tabora, Bw. Amiri Kassanga, amesema walipoanza kutengeneza mkaa mbadala hawakuzingatia matakwa ya viwango, lakini sasa wana matumaini makubwa ya kukuza uzalishaji kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi.
Naye Mkurugenzi wa kampuni ya Blamo Tech Engineering Limited, Bi. Modesta Lukosya, alisema taasisi yake imejikita katika uzalishaji wa nishati safi ili kuwaokoa wanawake na watoto ambao wamekuwa wahanga wa nishati chafu inayozalisha gesi ukaa.
“Tumejikita kwenye kuzalisha nishati safi ili kuokoa wanawake na watoto wanaoathirika na matumizi ya nishati chafu,” amesema.
Wito Kwa Serikali na Wadau
Mkazi wa Mbagala, Bi. Hadija Said, ameishukuru TIRDO kwa mafunzo hayo akisema yatamsaidia kujikimu kiuchumi kama mwanamke mjasiriamali. Ameomba serikali na wadau kujitokeza kutoa mikopo yenye masharti nafuu ili kuwawezesha wahitimu kuanzisha viwanda na kuendeleza uzalishaji wa mkaa mbadala.
WATATU MBARONI TABORA KWA KUJITEKA ILI KUJIPATIA FEDHA KWA NJIA YA UDANGANYIFU
Na mwandishi wetu, Tabora
Jeshi la Polisi Mkoani Tabora limetangaza kuwashikilia watu watatu kwa tuhuma za kutoa Taarifa za Uongo kuwa wametekwa ili kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa ndugu na wana familia wao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, CP Richard Abwao amewaambia waandishi wa habari kuwa watuhumiwa wanaoshikiliwa ni Khadija Jimmy Murijo (39), Kabila Mpare ambaye pia ni mke wa Bw. Emmanuel Peter Mchali, Ashura Swalehe (48) na Vitus Joseph (34) ambapo wote wanadaiwa kushirikiana kutengeneza taarifa ya uongo kwamba Khadija Jimmy ametekwa na watu wasiojulikana.
Watuhumiwa hao inaelezwa kuwa walitengeneza uongo huo ili kujipatia fedha kwa mume wa Khadija Murijo, ambapo walijipatia kiasi cha shilingi 1, 385, 800 kati ya Shilingi Milioni 2 walizoziamrisha kuzipata kutoka kwa Bw. Emmanuel.
Awali walieleza kuwa Khadija alikuwa ametekwa huko Ulyankulu na katika uchunguzi uliofanyika ulibaini kuwa Mtuhumiwa huyu alikuwa ameenda Wilaya ya Urambo, Kijiji cha Vumilia na baada ya uchunguzi inaonekana fedha hizi zote walizitolea kwenye Wilaya ya Kaliua. Uchunguzi utakapokamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani." Amesema Kamanda Abwao.
Kwa upande wake Mume wa Khadija, Bwana Emmanuel Peter Mchali amesema siku hiyo alipigiwa simu na Mke wake na kumueleza kuwa ametekwa na kupata vitisho kutoka kwa mwanaume mmoja kupitia simu ya mkewe, wakimtaka atoe Milioni mbili ili kuweza kuachiwa kwa mkewe, suala ambalo lilimlazimu kukopa fedha ili kwenda kulipa kwa watuhumiwa hao.
Aidha kwa Upande wake Mtuhumiwa mwingine Ashura Swalehe ameeleza namna ambavyo alirubuniwa na Wifi yake ili kudanganya na kubeba fedha kwa mumewe akidai kuwa Mume wake ambaye ni mstaafu wa Jeshi la wananchi wa Tanzania, amekuwa amuhudumii yeye na mtoto wake licha ya kuwa na kipato kikubwa, suala ambalo limekuwa likimfanya kukosa huduma muhimu za kila siku.





















