Monday, 9 February 2026

BALOZI MATINYI AKUTANA NA WAWEKEZAJI WA SWEDEN, AELEZEA FURSA ZA UWEKEZAJI

...




Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Mobhare Matinyi (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyabiashara na wawekezaji wa Sweden na maafisa wa ubalozi mara baada ya kikao kwenye ofisi za ubalozi jijini Stockholm, mnamo tarehe 6 Februari, 2026 (Picha kwa hisani ya Ubalozi).
Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Mobhare Matinyi akiwasilisha mada kuhusu fursa na vivutio vya uwekezaji nchini alipokutana na wafanyabiashara na wawekezaji wa Sweden kwenye ofisi za ubalozi jijini Stockholm, mnamo tarehe 6 Februari, 2026 (Picha kwa hisani ya Ubalozi).

Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Mobhare Matinyi (kushoto), akizungumza na Makamu wa Rais wa kampuni ya Dynamis Investment Partners, Bw. Bo Löfgren, mara baada ya kikao na wafanyabiashara na wawekezaji wa Sweden kwenye ofisi za ubalozi jijini Stockholm, mnamo tarehe 6 Februari, 2026 (Picha kwa hisani ya Ubalozi).
****

Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Mobhare Matinyi, ameongoza ujumbe wa ubalozi na taasisi za Serikali ya Tanzania katika kikao cha kimkakati na wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Chama cha Wafanyabiashara wa Sweden na Afrika, kilichofanyika tarehe 6 Februari, 2026, katika  Ubalozi wa Tanzania jijini Stockholm, Sweden. 

Kikao hicho kiliandaliwa mahsusi kwa ajili ya kuelezea fursa za biashara na uwekezaji zilizopo nchini, pamoja na kufafanua mazingira bora ya uwekezaji yaliyowekwa na Serikali. Ujumbe wa Sweden uliongozwa na rais wa chama hicho, Bi. Åsa Jarskog, ambapo kwa Tanzania mbali ya Ubalozi zilikuwepo pia taasisi za Serikali zilizoshiriki kwa njia ya mtandao kutokea jijini Dar es Salaam. 

Taasisi hizo ambazo zilitumia fursa hiyo kufafanua masuala kadhaa zilikuwa ni Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), pamoja na uongozi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) na Chama cha Taifa cha Wafanyabiashara (TNCC) na wanachama wao.

Mhe. Balozi Matinyi alielezea mwelekeo wa Serikali ya Tanzania kuhusu biashara na uwekezaji kwa mujibu wa Dira ya Maendeleo ya 2050, na mipango ya Serikali  kuendeleza hali ya utulivu nchini. Katika kufafanua zaidi mipango ya nchi, Mhe. Balozi Matinyi alikariri ujumbe uliomo kwenye hotuba tatu za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Hotuba hizo ni ile ya uzinduzi wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano mnamo tarehe 14 Novemba 2025; hotuba kwa mabalozi katika Sherehe ya Mwaka Mpya iliyofanyika Ikulu Chamwino tarehe 15 Januari 2026; na hotuba yake aliyotoa kwenye Mkutano wa Dunia wa Serikali (WGS) katika Uzinduzi wa Jukwaa la Kimataifa la Uwekezaji Afrika (GAIS), uliofanyika tarehe 5 Februari 2026, huko Dubai, Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE).

Katika wasilisho lake, Mhe. Balozi Matinyi alibainisha kuwa sekta muhimu ambazo Tanzania  inaelekeza nguvu ili kuvutia uwekezaji ni pamoja na nishati, viwanda, kilimo-biashara, misitu, uchumi wa buluu, uchumi wa kidijitali, utalii, madini ya kimkakati, miundombinu na usafirishaji. Balozi Matinyi aliakisi hotuba hizo kwa kusema, “Kwa muda mrefu Tanzania imekuwa kivutio cha uwekezaji na inaendelea kufungua milango yake kwa wawekezaji zaidi”.

Kufuatia kikao hicho, kampuni kadhaa za Sweden zilizoshiriki zimeanza majadiliano ya awali na ubalozi ili kuanza mchakato wa kuwekeza nchini katika sekta za uzalishaji wa umeme kwa kutumia taka na utengenezaji wa vifaa vya tiba, maeneo mawili ambayo Sweden  ni mojawapo ya nchi zinazoongoza barani Ulaya.

Kikao hicho kiliazimia kupendekeza kwamba ubalozi kwa kushirikiana na  jumuiya hiyo ya wawekezaji na Shirika la Ndege la Qatar uandae ziara ya ujumbe wa wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Sweden kuja nchini Tanzania mwezi Septemba au Oktoba mwaka huu ili kujionea fursa za uwekezaji zilizopo na vivutio vilivyowekwa na Serikali. 

Imetolewa na:

Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Sweden,

Stockholm, 08 Februari 2026

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger