Friday, 23 May 2025
WANANCHI 1,640 WAPATIWA ELIMU YA KUJIKINGA NA WANYAMA WAKALI NA WAHARIBIFU
Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kujikinga na wanyama wakali na waharibifu, ambapo jumla ya wananchi 1,640 kutoka vijiji vya Engikaret na Kiserian, Wilaya ya Longido mkoani Arusha, wamefikiwa kati ya Julai 2024 hadi Aprili 2025.
Hayo yameelezwa leo Mei 23, 2025 Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Zaytun Seif Swai, kuhusu mikakati ya Serikali katika kukabiliana na uvamizi wa tembo katika Kata ya Engikaret.
Akifafanua, Mhe. Kitandula amesema kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kudhibiti changamoto hiyo ikiwa ni pamoja na kufanya doria za mwitikio wa haraka. Amesema kuwa kati ya Julai 2024 na Machi 2025, jumla ya doria 34 zimefanyika katika Kata ya Engikaret kwa lengo la kukabiliana na matukio ya wanyamapori wakali.
Aidha, Naibu Waziri huyo amebainisha kuwa Serikali ilianzisha kituo maalum cha askari mwaka 2021 katika Wilaya ya Longido ili kuimarisha ulinzi dhidi ya wanyamapori hao. Kituo hicho kina jumla ya askari 18 wakiwemo wahifadhi 8 na askari wa wanyamapori wa vijiji (VGS) 10.
Vituo hivyo vimewezeshwa kwa vitendea kazi ikiwemo gari moja na pikipiki nne ili kufanikisha shughuli za ulinzi.
Katika hatua nyingine, Kitandula amesema Serikali inaendelea kushirikiana na wananchi kwa kuwajengea uelewa juu ya namna bora ya kuripoti matukio ya wanyama wakali kwa wakati, ili hatua za haraka zichukuliwe. Amesisitiza kuwa elimu hiyo inatolewa kwa njia ya mikutano ya hadhara, vipeperushi, na kupitia vyombo vya habari vya jamii.
Vilevile, Serikali inaendelea na jitihada za kuongeza idadi ya askari wa wanyamapori na kuwawezesha vifaa vya kisasa zaidi ili kuongeza ufanisi wa operesheni za kuwalinda wananchi, mali zao pamoja na uhifadhi endelevu wa wanyamapori nchini.
WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI YAOMBA KUIDHINISHWA BAJETI YA BIL. 476.7 KWA KWAKA 2025/2026
Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Bunge la bajeti likiwa linaendelea Jijini hapa,Wizara ya Mifugo na Uvuvi imewasilisha ombi la bajeti ya shilingi bilioni 476.7 kwa ajili ya mwaka wa fedha 2025/2026, lengo likiwa ni kuendeleza shughuli za sekta hizo muhimu nchini.
Akiwasilisha makadirio hayo bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Wizara hiyo Dkt. Ashatu Kijaji amesema kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 101.5 zimetengwa kwa matumizi ya kawaida huku shilingi bilioni 375.1 zikiwa ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Kwa mujibu wa Waziri huyo,Matumizi ya kawaida yanahusisha mishahara ya wafanyakazi (PE) ambayo ni shilingi bilioni 47.3 na matumizi mengineyo (OC) yenye jumla ya shilingi bilioni 54.3.
Katika fedha za maendeleo, Dkt. Kijaji amesema shilingi bilioni 228 zinatarajiwa kutoka ndani ya nchi, huku shilingi bilioni 147.1 zikitarajiwa kutoka kwa wahisani wa nje.
Wizara imesisitiza kuwa fedha hizo zitalenga kuboresha mifumo ya uzalishaji na usindikaji wa mazao ya mifugo na uvuvi, sambamba na kuimarisha upatikanaji wa masoko kwa wafugaji na wavuvi nchini.
Thursday, 22 May 2025
MAKAMU WA RAIS DKT. MPANGO ASHIRIKI MKUTANO WA PILI WA BRAZIL NA AFRIKA KUHUSU USALAMA WA CHAKULA NA MAENDELEO VIJIJINI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameshiriki Ufunguzi wa Mkutano wa pili wa Brazil na Afrika kuhusu Usalama wa Chakula, Mapambano dhidi ya Njaa na Maendeleo Vijijini unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Brazil (Itamaraty Palace) Jijini Brasilia . Tarehe 22 Mei 2025.

“NILIWANASA PALE KWENYE KITANDA CHETU CHA NDOA,” MWAMBA ASIMULIA

“Si uliniambia umeenda Dar?”. Ndivyo alivyoniuliza mke wangu, sauti yake ilisikika usiku wa manane wenye kimya kingi. Mimi, Eric, nilikuwa nikishuku uaminifu wa mke wangu katika ndoa yetu kwa muda mrefu.
Nakumbuka tulikuwa tumefunga ndoa ya kanisani, tumefungwa na viapo vitakatifu, lakini sikuweza kuondoa shaka kwamba alikuwa akiwatamani wanaume wengine huko nje.
DKT.SERERA: SEKTA BINAFSI TUMIENI FURSA ZA AFREXIM BANK KANDA YA AFRIKA

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Suleiman Serera,akizungumza wakati akifungua Kongamano la Afreximbank Roadshow lililoandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania lililofanyika jijini Dar es Salaam.
.....
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt Suleiman Serera ameishauri sekta binafsi ya Tanzania kuhakikisha inatumia fursa ya uwepo wa Benki ya Kanda ya Afrika ya Afrexim kupata mitaji itakayowezesha kuongeza thamani mazao na bidhaa za viwandani kwa kiwango cha kimataifa ili kuiwezesha nchi kushindana ndani ya soko la Afrika.
Dkt. Serera ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati akiongea na Waandishi wa Habari baada ya kufungua Kongamano la Afreximbank Roadshow lililoandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania pamoja na Benki hiyo likilenga kutambua changamoto za wafanyabiashara ili benki hiyo iweze kuzitatua kupitia fursa za mitaji, fursa za masoko na teknolojia
Aidha, Dkt. Serera aliwahimiza Wajasiliamali wa Tanzania, Wawekezaji wa viwanda, na biashara zinazoongozwa na vijana kushirikiana na Afreximbank na kutumia fedha zinazopatikana kwa usindikaji wa kilimo, maendeleo ya mauzo ya nje, ujenzi wa viwanda vya kijani, na biashara ya kikanda.
"Tuwekeze Dodoma, Mbeya, na Kigoma," alihimiza. "Tujenge Maeneo ya Usindikaji wa Mauzo ya Nje, tuimarishe korido za vifaa, na tujenge miundombinu ya kidijitali kwa mfumo wa biashara unaostawi."
Kwa upande wake Rais wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) Bw. Vincent Minja amesema jukwaa hilo ni muhimu katika uwezeshaji wa biashara barani Afrika akiweka bayana kuwa biashara kati ya nchi za Afrika bado ni kidogo ikilinganishwa na biashara kati ya nchi za Bara hilo na mabara mengine duniani
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Uhusiano wa Wateja wa benki hiyo Bw. Eric Monchu ameihakikishia sekta binafsi ya Tanzania kuwa wako tayari kukuza uchumi endelevu wa Tanzania
Aidha Bw Monchu amebainisha kuwa hadi sasa, Benki hiyo imetoa takriban dola bilioni 2 kuwezesha utekelezaji wa Miradi ya Kimkakati nchini ikiwemo Dola milioni 800 kwa kwa ajili ya Mradi wa Umeme wa Maji wa Julius Nyerere, Dola milioni 290 kwa Reli ya Kati (SGR), Dola milioni 200 kwa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) pamoja na Nyongeza ya fedha kwa benki za ndani na wadau wa sekta binafsi
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) Bi Lulu Mkude amewaalika wadau na mabenki mbalimbali waliohudhuria kongamano hilo kushiriki Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es salaam yatakayoanza tarehe 28 Juni hadi 13 Julai 2025 kwani ni jukwaa zuri la kutangaza biashara na huduma wanazotoa.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Suleiman Serera,akizungumza wakati akifungua Kongamano la Afreximbank Roadshow lililoandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania lililofanyika jijini Dar es Salaam.




Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Suleiman Serera (katikati ) akizungumza na Viongozi mbalimbali wakiwemo Kaimu Mkurugenzi wa Uhusiano wa wa Wawateja wa Areximbank Bw. Eric Monchu Intong, Rais wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) Bw. Vincent Minja na Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Bi lulu Mkude kabla ya ufunguzi wa Kowngamano la Afreximbank Roadshow lililofanyika Mei 2025 jijini Dar es Salaam

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Suleiman Serera,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua Kongamano la Afreximbank Roadshow lililoandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania lililofanyika jijini Dar es Salaam.
MHE. MBEKI ASHIRIKI MHADHARA WA SIKU YA AFRIKA UDSM
Rais wa zamani wa Jamhuri ya Afrika Kusini Mheshimiwa Thabo Mbeki ameshiriki mhadhara wa Siku ya Afrika uliofanyika katika Ukumbi wa Nkrumah wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Akizungumza katika mjadala huo Mhe.Thabo Mbeki amesema mjadala huo umewakutanisha wasomi, vijana na Taasisi ya Thabo Mbeki ili kuangalia kwa pamoja juu ya nini kifanyike ili kuiletea maendeleo Afrika.
Mhe. Mbeki alielezea hali ya sasa ya Afrika kwa kutumia muktadha wa kihistoria wa ukoloni, udhaifu wa taasisi za ndani, utegemezi mkubwa wa mataifa ya nje na haja ya Umoja wa Afrika na Taasisi zake kufikia malengo ya kuanzishwa kwake..
“Kesho ya bara la Afrika haiwezi kuendelea kuamuliwa na watu wengine bali utatokana na uamuzi, juhudi na mshikamano wa Waafrika wenyewe na sio watu wengine”, alisema.
Alisema kuwa licha ya mafanikio ya kisiasa yaliyopatikana baada ya uhuru, bado Afrika inakumbwa na changamoto za kiuchumi, usalama, na ukosefu wa mshikamano
Ametoa wito kwa Nchi za Afrika kuhakikisha umoja na mshikamano unaendelea kuwepo na kuongeza kuwa taasisi za Umoja wa Afrika na Tume ya AU lazima zihakikishe zinasimamia misingi ya kuanzishwa kwao na kutimiza malengo yao
Ameongeza kuwa vyama vya siasa katika bara la Afrika vinahitaji viongozi kama Mwalimu Nyerere watakao iwezesha Afrika kufikia matarajio yake ya kiuchumi na kisiasa.
Ametoa rai kwa vijana wa vyuo vikuu kushirikiana na vijana wenzao barani Afrika na kutumia nafasi zao kutoa muelekeo wa nini kifanyike ili kufufua matumaini na mwelekeo wa bara la Afrika.
Nao Wasomi wa UDSM wakichangia mjadala huo, wamesema ni wakati wa kuchukua hatua na kuacha kulalamika na kushirikiana kwa ajili ya kuleta maendeleo ya kweli kwa bara la Afrika
Akitoa salamu za shukurani baada ya mhadhara huo Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Rais wa Awamu ya Nne Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete ameishukuru Taasisi ya Thabo Mbeki kwa kukichagua Chuo hicho kuwa mwenyeji wa mhadhara wa Siku ya Afrika kwani unaonesha imani ya Taasisi hiyo kwa Chuo hicho.
Amesema kauli mbiu ya mhadhara wa Siku ya Afrika usemao “Hali ya Bara la Afrika:Ufufuo mpya wa Mwamko wa Kiafrika“ unaakisi mahitaji ya kweli ili kuifanya Afrika iendelee.
Mhadhara huo uliwakutanisha wasomi kutoka UDSM na Taasisi ya Thabo Mbeki kwa lengo la kujadili na kujenga uelewa wa pamoja, huku wakitafakari makosa yaliyopita na kutathmini hatua stahiki zinazopaswa kuchukuliwa ili kuleta maendeleo ya kweli barani Afrika.
Mhadhara huo uliwaleta pamoja wasomi, wanafunzi, viongozi wa serikali, na wanadiplomasia ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Afrika ambayo huadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 25 Mei.
Washiriki wa mhadhara kwa pamoja walitafakari hatma ya bara la Afrika katika muktadha wa changamoto na fursa zinazolikabili bara la Afrika.






















