Monday, 28 April 2025
Sunday, 27 April 2025
ZUHURA: MICHEZO NI MWAROBAINI WA MAGONJWA YASIYO YA KUAMBUKIZA KWA WAFANYAKAZI
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Bi. Zuhura Yunus akikabidhi zawadi ya kombe kwa kiongozi wa timu ya mpira wa pete ya OSHA, Rachel Nkoma. OSHA imetwaa ubingwa katika mpira wa pete baada ya kuifunga timu ya Wizara ya Maji magoli 17 kwa 14 katika mchezo wa fainali.
**********
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Bi. Zuhura Yunus amewasisitiza wafanyakazi wa sekta mbalimbali nchini kujenga tabia ya kushiriki michezo na mazoezi kwa ujumla ili kuimarisha afya zao na kuepuka magonjwa yasiyoyakuambukiza ambayo kwasasa ameeleza ni changamoto inayowakabili watu wengi ulimwenguni.
Bi. Zuhura ametoa wito huo wakati akifunga Bonanza la michezo (OSHA Bonanza) lililoandaliwa na kuratibiwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kama sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi inayoadhimishwa kitaifa Mkoani Singida katika Viwanja vya Mandewa.
Bi. Zuhura ameeleza kuwa Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa ikihamasisha umuhimu wa michezo na mazoezi kwa wananchi katika kujenga afya na kupambana na magonjwa yasiyoyakuambukiza ikiwemo saratani, kisukari, magonjwa ya moyo na shindikizo la damu.
“Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinakadiria asilimia 75 ya vifo vyote vinavyotokea ulimwenguni kila mwaka husababishwa na magonjwa yasiyoyakuambukiza na hata Wizara ya Afya nichini inakadiria kati ya vifo 100 vinavyotokea kila mwaka vifo 33 vinasababishwa na magonjwa hayo, hivyo nawasishi wafanyakazi wote kuepuka mtindo mbaya wa maisha na kujenga tabia ya kufanya mazoezi ili kuepuka magonjwa haya” ameeleza Bi. Zuhura
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda amesema madhumuni makubwa ya Bonanza hilo ni kutoa hamasa kwa wafanyakazi kushiriki michezo ili kujenga afya zao pamoja na kuimarisha uhusiano baina ya wafanyakazi huku akieleza kuwa taasisi yake itaendelea kulinda nguvu kazi kupitia programu mbalimbali ikiwemo kaguzi za usalama na afya ili kuhakikisha wafanyakazi wote wanakua salama na wenye afya njema ili watekeleze majukumu yao vyema.
Bonanza hilo lilijumuisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu,mpira wa pete, mbio za magunia, riadha, mbio za vijiti, kuvuta kamba, kukimbiza kuku,mchezo wa kukimbia na ndimu na katika michezo hiyo OSHA imetwaa ubingwa katika michezo mchezo ya mpira wa pete, riadha kwa wanawake na wanaume huku timu ya mpira wa miguu ya OSHA Sports Club ikiishia hatua ya nusu fainali katika mchezo wa mpira wa miguu.
Aidha, timu zilizoshiriki katika michezo mbalimbali ya Bonanza hilo lililofanyika katika viwanja vya VETA Singida ni timu kutoka OSHA, Wizara ya ujenzi, Mgodi wa Geita (GGM),Wizara ya Uchukuzu, Mahakama, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Maji, Bohari ya Dawa (MSD),TANROADS,Shanta Gold Mine, Wizara ya Afya, Benki ya NMB, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikiali, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) n.k.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda akisisitiza umuhimu wa wafanyakazi kushiriki michezo wakati akizungumza na washiriki wa Bonanza la OSHA lililofanyika Mkoani Singida.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Bi. Zuhura Yunus akigawa zawadi ya vikombe na medali kwa washindi wa michezo mbalimbali katika Bonanza la OSHA lililofanyika katika Viwanja vya VETA Mkoani Singida.
Timu ya mpira wa pete ya OSHA ikicheza mchezo wa fainali dhidi ya timu ya Wizara ya Maji ambapo OSHA ilishinda goli 17 kwa 14 na kutwaa ubingwa wa Bonanza la OSHA kwa upende wa mchezo wa mpira wa pete.
Timu za wafanyakazi kutoka maeneo mbalimbali ya kazi nchini zikishiriki katika michezo tofauti tofauti katika Bonanza la OSHA lililofanyika katika Viwanja vya VETA Mkoani Singida.
WAKULIMA WA KAHAWA MBINGA WAOMBA SERIKALI KUDHIBITI WALANGUZI WA MAZAO
Mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Ushirika Kinjolu kata ya Kikolo Halmashauri ya Mji Mbinga Mkoani Ruvuma Bosco Turuka kushoto,akikagua uzalishaji wa Kahawa katika moja la shamba la mkulima katika kijiji cha Kikolo ,wengine ni baadhi ya Wanachama wa Kinjolu Amcos.
Na Regina Ndumbaro-Mbinga.
Wakulima wa kahawa wanaohudumiwa na Chama cha Msingi cha Ushirika Kinjolu Amcos kata ya Kikolo na Kihungu, Halmashauri ya Mji Mbinga mkoani Ruvuma, wameiomba Serikali kuchukua hatua kali dhidi ya wafanyabiashara wanaonunua kahawa kwa magendo na wengine kununua kahawa ikiwa bado shambani.
Mwenyekiti wa chama hicho, Bosco Turuka, amesema kuwa kila msimu wa mavuno wafanyabiashara hao hupita mashambani na kuwarubuni wakulima kuuza kahawa kwa bei ndogo, huku wakitumia vipimo haramu vya magoma vinavyowanyonya wakulima na kuwakwamisha kiuchumi.
Amesema kuwa iwapo Serikali itadhibiti vitendo hivyo, wakulima wataongeza kipato na uzalishaji, hasa baada ya Serikali ya Awamu ya Sita kuanzisha mpango wa utoaji wa mbolea za ruzuku kwa wakulima wa kahawa.
Kwa mujibu wa Turuka, mpango wa mbolea za ruzuku umeongeza uzalishaji wa kahawa kutoka tani 93 msimu wa 2022/2023 hadi tani 192 msimu wa 2024/2025. Aidha, alisema kuwa ruzuku hiyo imeongeza kipato cha wakulima na kuboresha maisha yao kwa kujenga nyumba bora, kununua vyombo vya usafiri, na kusomesha watoto wao.
Pia, ruzuku hiyo imehamasisha wanachama wapya kujiunga na Ushirika kutoka wanachama 93 hadi 300.
Turuka amesema kuwa kutokana na usimamizi madhubuti wa Serikali kupitia mfumo wa stakabadhi gharani msimu wa 2024/2025, wakulima wameuza kahawa kwa bei nzuri ikilinganishwa na kama wangeruhusiwa kuuza kwa makampuni au watu binafsi, ambapo wangeambulia bei ya chini.
Ametumia nafasi hiyo kuiomba Serikali kufanya matengenezo ya barabara ili kurahisisha usafirishaji wa mazao, kwani ubovu wa miundombinu unatoa mwanya kwa walanguzi kununua mazao moja kwa moja mashambani kwa bei ya chini.
Kwa upande wake, mkulima Gotan Komba ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imefufua na kuimarisha sekta ya ushirika, jambo lililowezesha wakulima kuongeza tija na uzalishaji wa kahawa na mazao mengine.
Amesema kuwa hapo awali walikuwa wakilima bila kupata manufaa makubwa kutokana na gharama kubwa za uzalishaji, lakini mpango wa ruzuku ya mbolea umepunguza gharama hizo na kuhamasisha wakulima kuongeza ukubwa wa mashamba yao.
Ameiomba Serikali kuendeleza mpango huo kwa kutoa pembejeo zaidi, hasa mbolea na dawa za kuua wadudu, ili kuongeza ufanisi katika kilimo cha kahawa ambacho ni uti wa mgongo wa uchumi wa Wilaya ya Mbinga na Mkoa wa Ruvuma.
Hilda Komba, mkulima kutoka kijiji cha Kikolo, naye amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutambua mchango na juhudi za wakulima wa kahawa.
Amesema utoaji wa ruzuku ya mbolea umechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza uzalishaji wa kahawa.
Aidha, amempongeza Waziri wa Kilimo kwa kutoa bure miche bora ya kahawa kwa wakulima, hatua ambayo itasaidia kuongeza uzalishaji, kuboresha maisha ya wakulima, kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika Wilaya ya Mbinga, Mkoa wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla.
Saturday, 26 April 2025
JOWUTA , THRDC WALAANI WANAHABARI KUKAMATWA NA KUPIGWA
CHAMA cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu nchini (THRDC) wamelaani kuanza kuibuka matukio ya waandishi wa habari na watangazaji kukamatwa na baadhi kupigwa na hata kuharibiwa vifaa vyao vya kazi na vyombo vya dola.
Kauli ya kulaani imetolewa Aprili 25 mwaka huu na Mwenyekiti wa JOWUTA Mussa Juma mkoani Mbeya, wakati wa mafunzo kwa wanahabari kuhusu uandishi wa habari za uchaguzi, ulinzi na usalama kazini.
Mafunzo hayo yamehusisha waandishi kutoka mikoa ya Mbeya, Iringa na Njombe, ambapo Juma amesema matukio ya kukamatwa, kupigwa na kuharibiwa vitendea kazi hayakubaliki katika nchi inayojinadi kuwa inazingatia misingi ya kidemokrasia.
Juma amesema katika siku za karibuni, kumeanza kutokea matukio ya baadhi ya wanahabari kukamatwa na vyombo vya dola, kupigwa na wengine kuzuiwa kufanyakazi, jambo ambalo sio sahihi.
Mwenyekiti huyo, amesema mahusiano mazuri baina ya vyombo vya dola na wanahabari, yalikuwa yameimarishwa katika siku za nyuma lakini sasa yanaanza kuharibika jambo ambalo halipaswi kuvumiliwa.
“Kama mwanahabari amekiuka taratibu zozote kuna utaratibu wa kufuata kisheria, badala ya kutumika nguvu kumkamata ama kumzuia kufanyakazi yake”amesema.
Hata hivyo, Juma amewataka wanahabari nchini, kufanyakazi kwa kuzingatia maadili ya uandishi wa Habari, hasa kipindi hiki cha harakati za uchaguzi mkuu, ikiwepo kutoandika habari za upendeleo kwa chama chochote za siasa, kuacha kuwa washabiki wa vyama na watowe fursa sawa kwa vyama vyote.
“Msimamo wa JOWUTA kama mwanahabari unataka kujihusisha na masuala ya siasa ni bora kujiweka kando mapema na tasnia ya habari hadi chaguzi zipite, badala ya kutumia chombo chako cha habari kwa maslahi binafsi ya kisiasa”amesema.
Awali,Wakili Jones Sendodo wa kutoka THRDC, amesema mtandao huo unaungana na wadau wote kulaani matukio yoyote ya kunyanyaswa, kupigwa ama kuharibiwa vitendea kazi mtetezi wa haki za binaadamu, wakiwepo wanahabari.
Wakili Sendodo amesema ni vyema vyombo vya dola kuzingatia sheria za nchi wakati wa kutekeleza wajibu wao.
“Tunapinga matukio ambayo yanaendelea kwa vyombo vya dola kutumia nguvu kubwa kuwanyanyasa watetezi wa haki za binaadamu na sisi kama THRDC kwa kushirikiana na wadau wengine tutaendelea kuwatetea na kuwapa msaada wa kisheria, msaada wa ushauri wa kisaikolojia na hata makazi salama ya muda watetezi wa haki za binaadamu wakiwepo wanahabari wanapokabiliwa na majanga ama vitisho”amesema.
Wakili Sendodo pia akitoa mada katika mafunzo hayo ya uchaguzi kwa wanahabari, aliwataka kujua sheria mbalimbali ambazo zinawahusu ili kujitahidi kutozivunja, ikiwepo Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016, Sheria ya Takwimu, Sheria za Uchaguzi na nyingine.
Hata hivyo, alitaka wanahabari kujali usalama wao wakiwa kazini na kuchukuwa tahadhari mbali mbali ili kuhakikisha wakati wote wanabaki salama, wakati wakitekeleza wajibu wao.
Katibu Mkuu wa JOWUTA, Selemani Msuya aliwataka wanahabari nchini, kuendelea kujiunga na JOWUTA kwani ndio chama pekee kinachotambulika kisheria kutetea maslahi ya wafanyakazi katika vyombo vya habari na mazingira bora ya kazi.
"Tumekuja kuwapa elimu ya uchaguzi, lakini pia nitumie nafasi hii kuwaomba wafanyakazi wa vyombo vya habari mjiunge JOWUTA, ili tuwe na nguvu moja ya kupigania maslahi yetu," amesema.
JOWUTA inaendelea na kutoa mafunzo kwa wanahabari nchini kuhusiana na kuripoti vyema uchaguzi mkuu mwaka huu na kubaki salama, mafunzo hayo yamedhaminiwa na Shirikisho la Kimataifa la Waandishi wa Habari (IFJ), Shirikisho la Waandishi wa Habari Afrika (FAJ),THRDC, Taasisi wa Wanahabari ya Kusaidia Jamii za Pembezoni (MAIPAC) na JOWUTA.



































