Thursday, 20 March 2025

SOUWASA YAPITA NYUMBA KWA NYUMBA KUHAMASISHA WATEJA KUREJESHA HUDUMA ZA MAJI


Wafanyakazi wa SOUWASA wakitoa elimu kwa mwananchi na mkazi wa Ruhuwiko Shuleni kuhusu umuhimu wa matumizi ya maji na kutumia fursa iliyotolewa bure ya kurejeshewa maji.
Wafanyakazi wa SOUWASA Songea wakizungumza na wananchi kuhusu huduma hiyo ya maji kwa kurejeshewa bila fidia yoyote

Na Regina Ndumbaro, Ruvuma

Katika kuelekea kilele cha Wiki ya Maji, Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Songea (SOUWASA) imezindua kampeni maalumu ya kuhamasisha wateja waliositishiwa huduma kurejesha maji yao kwa kulipa nusu ya deni lao. 

Kampeni hii inalenga kuwapa fursa wakazi wa Manispaa ya Songea kurejesha huduma zao kwa urahisi, huku ikihamasisha jamii kuhusu umuhimu wa maji safi na salama.

Timu maalumu ya SOUWASA, ikiongozwa na Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja, Bi Baby Biko, imetembelea maeneo ya Ruhuwiko Kanisani na Ruhuwiko Shuleni ili kutoa elimu na kuwaeleza wananchi kuhusu ofa hii maalumu. 

Timu hiyo imepita nyumba kwa nyumba kuhakikisha kila mkazi anayehitaji kurejesha huduma za maji anapata taarifa sahihi na fursa ya kufanikisha hilo kwa urahisi.

Ofa hii maalumu inatoa nafasi kwa wateja waliositishiwa huduma kurejeshewa maji bila fidia yoyote, endapo watalipa nusu ya deni lao ndani ya muda uliopangwa. 

Kampeni hii itadumu kwa wiki moja, kuanzia tarehe 16 hadi 22 Machi 2025, na imelenga kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Songea wanaokabiliwa na deni la maji.

SOUWASA inawataka wakazi wa Manispaa ya Songea kuchangamkia fursa hii kwa haraka ili kuepuka usumbufu wa ukosefu wa maji katika makazi yao. 

Huduma ya maji ni hitaji la msingi kwa kila kaya, hivyo mamlaka hiyo imeamua kuweka mazingira wezeshi kwa wateja wake ili waendelee kupata huduma bora kwa gharama nafuu.

Kampeni hii ni sehemu ya juhudi za SOUWASA kuhakikisha kila mkazi wa Songea anapata maji safi na salama kwa matumizi ya kila siku. 

Mamlaka hiyo inaendelea kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa kulipa bili zao kwa wakati ili kuepusha usitishaji wa huduma na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji kwa wote.
Share:

Wednesday, 19 March 2025

MFUMO WA RUZUKU YA MBOLEA UMEONGEZA MATUMIZI YA MBOLEA KUTOKA TANI 363,599 HADI 840,714


Na Dotto Kwilasa,Dodoma

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Kupitia mfumo wake wa ruzuku ya mbolea,imesaidia ongezeko la matumizi ya mbolea kutoka tani 363,599 mwaka 2020/2021 hadi tani 840,714 mwaka 2023/2024.

Ongezeko hilo limewezesha kuongezeka kwa matumizi ya mbolea kutoka kilo 19 za virutubisho kwa hekta mwaka 2020/2021 hadi kilo 24 za virutubisho kwa hekta mwaka 2024/2025.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo (TFRA), Joel Laurent ameeleza hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 19, 2025, katika Ofisi za jijini Dodoma.

Amesema lengo ni kufikia kilo 50 za virutubisho kwa hekta ifikapo mwaka 2033 kwa kuzingatia makubaliano ya Wakuu wa Nchi za Afrika yaliyofanyika Nairobi 2024.

Amesema kuongezeka kwa matumizi ya mbolea nchini kumechangia kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya chakula kutoka tani 19,980,718 mwaka 2020/2021 hadi tani 22,803,316 mwaka 2023/2024 sawa na ongezeko la asilimia 14 na kufanya utoshelevu wa chakula nchini kufikia asilimia 128.

"Katika miaka minne ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan, sekta ya mbolea nchini imepiga hatua kubwa za maendeleo, ikiwa na mafanikio makubwa ambayo yamechangia kuimarika kwa kilimo, biashara ya mbolea, na uwekezaji katika viwanda vya mbolea, " ameeleza.

Amefafanua kuwa Mpango huo maalumu wa ruzuku ya mbolea umewezesha kupunguza gharama ya mbolea na kufanya wakulima kununua mbolea kwa bei ya shilingi 40,000/= hadi 80,000/= kwa kutegemea aina ya mbolea na umbali sawa na punguzo la takribani asilimia 50 ya bei.

Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka minne,biashara ya mbolea nchini imekua kwa kiasi kikubwa ambapo wafanyabiashara wa mbolea waliopewa leseni wameongezeka kutoka 3,069 mwaka 2020/21 hadi 7,302 Februari, 2025.

Aidha upatikanaji wa mbolea umeongezeka kutoka tani 766,024 mwaka 2020/2021 hadi tani 1,213,729 mwaka 2023/2024, uingizaji wa mbolea umeongezeka kutoka tani 504,122 mwaka 2020/2021 hadi tani 728,758 mwaka 2023/2024 na uzalishaji wa ndani umeongezeka kutoka tani 42,695 mwaka 2020/2021 hadi tani 158,628 mwaka 2023/2024.

"Ili kusogeza huduma kwa wakulima, Mamlaka imeanzisha Maabara ya kisasa ya mbolea ambapo Tanzania inakuwa Nchi ya kwanza katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa na Maabara mahususi ya mbolea yenye uwezo wa kupima sampuli za mbolea, udongo na tishu za mimea,

Hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha udhibiti wa ubora wa mbolea nchini.
Aidha, maabara hiyo inatarajiwa kutoa huduma kwa nchi jirani zinazotumia bandari za Tanzania, kama vile Malawi, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi, na Rwanda, "amefafanua

Katika kusogeza huduma kwa jamii, Mkurugenzi huyo amesema Mamlaka imeongeza Ofisi za Kanda kutoka kanda tatu (3) 2020/2021 ambazo ni Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Ziwa na Kanda ya Kaskazini hadi kufikia Kanda tano (5) mwaka 2023/24 ambapo Kanda ya Kati na Kanda ya Mashariki zimeongezeka.

Aidha amesema , Mamlaka imeajiri Wawakilishi katika Mikoa yote 26 ili kusogeza huduma katika ngazi ya Mkoa.
Share:

BODI YA USIMAMIZI WAPIMA ARDHI YAKUTANA DODOMA

Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi na Utoaji wa Leseni kwa Wapima Ardhi (BCLS) ambaye ni Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Hamdouny Mansour akizungumza wakati wa kikao cha Bodi kinachofanyika jijini Dodoma kuanzia tarehe 18 hadi 19 Machi 2025.

**********************

Na Munir Shemweta, WANMM

Bodi ya Usimamizi na Utoaji wa Leseni kwa Wapima Ardhi (Board of Control and Licensing of Surveyors-BCLS) imeanza kikao chake cha siku mbili jijini Dodoma ambapo katika kikao hicho inajadili na kupitia masuala mbalimbali ikiwemo mashauri ya kinidhamu kwa makampuni yaliyokiuka maadili, Kanuni na taratibu za upimaji.

Moja ya jukumu la Bodi ya Usimamizi na Utoaji Leseni kwa Wapima Ardhi ni kusimamia utendaji wa wapima ardhi kwa lengo la kuongeza tija katika kazi za kitaalamu zisizohusiana na upimaji ardhi.

Aidha, katika kikao hicho kilichofunguliwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo Bw. Hamdouny Mansour tarehe 18 Machi 2025, mbali na kupitia mashauri ya makampuni ya upimaji yaliyokiuka taratibu, kikao pia kitapitia mitaala ya shahada ya GEOMATICS inayotolewa na Chuo Kikuu cha Ardhi.

Bodi ya Usimamizi na Utoaji wa Leseni kwa Wapima Ardhi (Board of Control and Licensing of Surveyors-CLS) imeanzishwa kwa sheria ya upimaji ardhi Sura ya 324 chini ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Baadhi ya majukumu ya bodi hiyo ni kusajili na kutoa leseni kwa wapima ardhi wenye sifa, kutunza rejista kwa wapima ardhi waliosajiliwa, kufanya mapitio na kutoa mapendekezo ya mitaala mipya na inayohusishwa na stashahada na shahada mbalimbali za vyuo vya kati na vya juu pamoja na kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya wataalamu waakaobainika kukiuka sheria, kanuni na miongozo mbalimbali ya upimaji.
Sehemu ya wajumbe wa Bodi ya Usimamizi na Utoaji Leseni kwa Wapima Ardhi wakiwa katika kikao cha bodi hiyo kinachofanyika jijini Dodoma kuanzia tarehe 18 hadi 19 Machi 2025 .
Wajumbe wa Bodi ya Usimamizi na Utoaji wa Leseni kwa Wapima Ardhi wakifurahia jambo wakati wa kikao cha Bodi ya hiyo kinachofanyika jijini Dodoma kuanzia tarehe 18 hadi 19 Machi 2025 .
Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi na Utoaji wa Leseni kwa Wapima Ardhi ambaye ni Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Hamdouny Mansour akisisitiza jambo wakati wa kikao cha Bodi kinachofanyika jijini Dodoma kuanzia tarege 18 hadi 19 Machi 2025.
Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi na Utoaji wa Leseni kwa Wapima Ardhi (BCLS) ambaye ni Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Hamdouny Mansour akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa bodi wanaoshiriki kikao kinachofanyika jijini Dodoma kuanzia tarege 18 hadi 19 Machi 2025. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
Share:

CWT PWANI YASIFU UCHAGUZI WA VIONGOZI BAGAMOYO

Wageni waalikwa na kamati ya utendaji iliyochaguliwa
Mwenyekiti wa uchaguzi, mwalimu Leonard Gange
Katibu wa Chama cha walimu mkoa wa Pwani Mwalimu Suzan Shesha
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo , Shaibu Ndemanga (kulia) na Mwenyekiti wa CWT Wilaya ya Bagamoyo, Hamisi Kimeza(kushoto)
Katibu wa CWT wilaya ya Bagamoyo, Mwalimu Joyce Maisa akisoma risala


NA. ELISANTE KINDULU, BAGAMOYO

CHAMA cha walimu mkoa wa Pwani kimesifu uchaguzi wa viongozi wa CWT Wilaya ya Bagamoyo uliofanyika mwanzoni mwa wiki hii katika ukumbi wa Stella Maris mjini hapa.

Sifa hizo zimetolewa na katibu wa CWT mkoa wa Pwani Bi. Suzan Shesha mara baada ya kumalizika kwa zoezi la upigaji kura.

"Niwashukuru kwa kufanya uchaguzi kwa utulivu mkubwa. Niwashukuru pia viongozi waliochaguliwa kwa kipindi cha 2025-2030. Na bila kuwasahau waliothubutu kugombea japo kura hazikutosha", alisema katibu huyo.

Nafasi ya mwenyekiti wa Chama cha walimu wilaya ya Bagamoyo na idadi ya kura kwenye mabano ni Hamisi Juma Kimeza (100), Alfred Peter Ringi(52), Bilali Mkeha (25), Nyamba Johanes(9) na Linus Aidan (7).

Kwa upande wa mweka hazina ,Mwalimu Siza Mnjokava (188) na Mwalimu Samwel Mbwasi (6).

Wanaounda kamati ya utendaji kwa kushirikiana na mwenyekiti na mweka hazina ni pamoja na Mwalilishi wa walimu vijana, David Phares(111) na Bakari Kibangu (79).

Mwakilishi shule za awali walikuwa Stella Mwihambi (93) na Asha Mohamed (88).

Wawakilishi wa shule za msingi zinatakiwa nafasi nne kwa walioongoza kwa kura. Matokeo ni kama ifuatavyo, Elisante Kindulu (51), Msafiri Innocent (38), Bahati Mohamed (32), Mohamed Kiparai (16), Hamisi Tuwaqal(15) na Ali Makame (1).

Nafasi mbili za wawakilishi wa shule za sekondari zilichukuliwa na Bernad Kapera na William Mrope.

Wagombea waliopigiwa kura za ndio na hapana na kushinda ni Anna Choaji(mwakilishi wa kitengo cha walimu wanawake), Phinus Tuarila(Mwakilishi wa walimu wenye ulemavu), Mzee Kihaku (Taasisi) na Beginus Mbiro (Vyuo).

Kwa upande wa kitengo cha walimu wanawake waliochaguliwa ni Veronica Kirumbi (Mwenyekiti), Anna Choaji(katibu), Theresia Kilimo(mweka hazina), Hawa Magulumali(mjumbe), Pili Mrope (mjumbe), Teddy Setebe (mjumbe) na Saida Msosa(mjumbe).

Wapiga kura katika mkutano huo ni mwalimu mmoja mmoja kutoka kila shule , chuo na ofisi ya elimu wilaya ambapo inafahamika kama tawi la chama mahala pa kazi.

Wilaya ya Bagamoyo ina jumla ya walimu 2189, Kati Yao wanachama wa CWT ni 2154 na matawi ya wawakilishi mahala pa lazi ni 195.

Share:

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMATANO MACHI 19,2025

Magazeti

Magazeti  
Share:

Tuesday, 18 March 2025

Ngoma Mpya : INAGA MLYAMBELELE - SAFARI YA INDIA


Inaga Mlyambelele anasimulia safari yake ya India
Share:

Ngoma Mpya : INAGA MLYAMBELELE - MJA NA NDEGE, BAADA YA KUPONA!

Hii hapa ngoma ya Inaga Mlyambelele baada ya kupona!
Share:

MTENDAJI MKUU WA BENKI YA NMB ATEMBELEA OFISI YA WAKILI MKUU WA SERIKALI


Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi akizungumza na Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi. Ruth Zaipuna (hayupo pichani) alipomtembelea Wakili Mkuu wa Serikali kwa lengo la kujitambulisha Ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi. Ruth Zaipuna akizungumza na Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Ally Possi (hayupo pichani) alipomtembelea kwa lengo la kujitambulisha Ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

Maafisa waandamizi wa Benki ya NMB wakimsikiliza Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi (hayupo pichani) akizungumza na Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo,
Bi. Ruth Zaipuna (hayupo pichani) walipomtembelea Wakili Mkuu wa Serikali kwa lengo la kujitambulisha ofisi kwake jijini Dar es Salaam.
Share:

Monday, 17 March 2025

Video : INAGA AMEPONA, MTAZAME HAPA AKIFUNGUKA BAADA YA KURUDI KUTOKA INDIA

 

Share:

WADAU WAIANGUKIA SERIKALI KURIDHIA MKATABA WA MASUALA YA WATU WENYE ULEMAVU AFRIKA




Mkurugenzi wa Shirika lisilokuwa la kiserikali linalojihusisha na masuala ya watu wenye ulemavu,Wakili Gideon Mandes, alizungumza na waandishi wa habari mara baada ya semina ya Waandishi wa habari na wadau kutoka vyama vya watu wenye ulemavu yaliyoandaliwa na Shirika la Sightsavers yaliyolenga kuwajengea uelewa kuhusu umuhimu wa itifaki hiyo.

Na.Mwandishi Wetu

KATIKA kukabiliana na mila, imani potofu na ushirikina unaodhuru watu wenye ulemavu, wadau wameiangukia serikali kukamilisha mchakato wa kuridhia Itifaki ya masuala ya watu wenye ulemavu Afrika kabla ya kuvunjwa kwa Bunge la 12 ili kulinda haki zao.

Itifaki hiyo inatokana na Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu uliopitishwa na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali za Umoja wa Afrika katika Mkutano wa 30 wa kawaida wa Bunge mnamo Januari 2018 na hadi sasa Tanzania bado haijaridhia.

Rai hiyo ilitolewa jana jijini Dodoma na wadau kutoka vyama vya watu wenye ulemavu na waandishi wa habari katika mafunzo yaliyoandaliwa na Shirika la Sightsavers yaliyolenga kuwajengea uelewa kuhusu umuhimu wa itifaki hiyo.

Akizungumza kuhusu faida za itifaki hiyo, Mkurugenzi wa Shirika lisilokuwa la kiserikali linalojihusisha na masuala ya watu wenye ulemavu,Wakili Gideon Mandes, alisema katika mkataba huo kuna haki za watu wenye ulemavu katika masuala ya elimu, ajira, afya, fursa za kiuchumi na miundombinu inayofikika.

Pia, alisema mkataba huo unaongelea masuala ya uwakilishi wa watu wenye ulemavu katika shughuli za kisiasa na umma, haki za wanawake, wasichana na watoto.

“Tanzania bado hatujaridhia kwasababu moja kwanza ilitakiwa mchakato upitie serikalini na serikali zote mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar tupate maoni ili kwenda kwenye hatua nyingine za michakato ya itifaki,”alisema.

Naye, Mjumbe wa Shirikisho la Vyama Vya Watu Wenye Ulemavu (Shivyawata) Dodoma, Sophia Mhando, alisema wanawake wenye ulemavu wanaomba serikali iridhie mkataba huo ili kuweka uchechemzi wa haki zao za kiafya kwenye sera na sheria zinazotungwa.

Mratibu wa mradi wa macho wa Shirika la Sightsavers, Upendo Minja, alisema shirika hilo limetambua mchango wa vyombo vya habari katika kutoa hamasa kuhakikisha haki za watu wenye ulemavu zinalindwa na mkataba huo kuridhiwa.

Alisema hadi sasa nchi 16 zimeridhia na kwa kupitia vyombo vya habari wananchi watajua umuhimu wa mkataba huo kwa Tanzania na kuhamasisha serikali kuridhia mkataba huo.

Awali, Ofisa wa Sera, uchechemuzi na ushawishi Kanda ya Afrika Mashariki Kati na Kusini wa Sightsavers, Neema Kalole, alisema ni muhimu kwa Tanzania kuridhia mkataba huo ambao unakwenda kuhakikisha haki za watu wenye ulemavu kwa Afrika zinalindwa kwa kuwa kuna mambo hayafanani na nchi zingine zilizoendelea.

“Mfano mauaji ya watu wenye ulemavu wa Ngozi (albino) ni kitu ambacho kinatokea kwenye nchi zetu za Afrika na mkataba huu utaenda kuongelea kinagaubaga mazingira yaliyopo kwenye nchi zetu yatatuliwe, mkataba huu una manufaa mengi sana,”alisema.

Alisema mkataba huo unaendana na jitihada zinazofanywa na serikali za kuweka kipaumbele kutetea haki za watu wenye ulemavu na kwamba tayari kuna mapitio ya Sera ya Mwaka 2004 ambayo yanachochea utetezi huo na mkataba huo ukiridhiwa utaongeza nguvu na Tanzania itaonesha namna ilivyojizatiti kukomesha vitendo vya ukiukwaji wa haki za watu wenye ulemavu.
Share:

DIWANI WA KATA YA MSHANGANO AJIUZULU







Diwani wa Kata ya Mshangano ,Samuel Mbano akionesha barua ya kujiuzulu
Diwani wa Kata ya Mshangano ,Samuel Mbano aliyejiuzulu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Ruvuma.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya James Danny Mgego akithibitisha kupokea barua ya kujiuzulu kwa diwani wa Kata ya Mshangano Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma

Na Regina Ndumbaro Ruvuma. 

Diwani wa Kata ya Mshangano katika Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma, Samuel Mbano, ametangaza kujiuzulu nafasi yake ya udiwani. 

Uamuzi huu umechukuliwa kutokana na kile alichokitaja kama kufanya kikao bila ya  idhini ya  chama na kujadili maendeleo ya kata yake bila kuwashirikisha viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na kutozingatia ilani ya chama.

Mbano amesema kuwa amejiuzulu kwa hiari yake ili kulinda heshima ya chama na maslahi ya serikali yake kwa ujumla. 

Aidha, amesisitiza kuwa licha ya kuachia ngazi, bado ataendelea kuwa mwanachama mwaminifu wa CCM na kuendelea kukipigania chama chake kwa namna yoyote 

Kwa upande wake, Katibu wa CCM Wilaya ya Songea, James Danny Mgego, amethibitisha kupokea barua rasmi ya kujiuzulu kwa diwani huyo. 

Mgego amesema kuwa katika barua hiyo, Mbano hajatoa sababu nyingine zaidi ya kutaja kuwa amejiuzulu kwa lengo la kulinda heshima ya chama na serikali.

Mgego ameongeza kuwa ndani ya CCM, mtu anapojiona amefikia ukomo wa nafasi yake anaweza kujiuzulu kwa hiari yake. 

Ameeleza kuwa kwa sasa chama hakijatoa tamko rasmi kuhusu suala hilo, lakini barua ya diwani huyo tayari imepelekwa kwa ngazi za juu za chama kwa hatua zaidi.

Hadi sasa, hakuna maelezo zaidi kutoka kwa uongozi wa CCM kuhusu hatua itakayofuata baada ya kujiuzulu kwa Mbano. 

Wananchi wa Kata ya Mshangano wanasubiri maamuzi ya chama kuhusu nafasi hiyo na hatma ya uongozi wa kata yao.

Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger