Friday, 7 February 2025

MAFUNZO YA URAIA, UTAWALA BORA YAHITIMISHWA KILIMANJARO




Na Dotto Kwilasa, KILIMANJARO

Hatimaye timu ya wataalam wa mafunzo ya Uraia na utawala bora imehitimisha ziara yake mkoani Kilimanjaro safari iliyoanzia mkoani Mtwara.

Wakili wa Serikali Mkuu na Mratibu wa Mafunzo ya Elimu ya Uraia na Utawala Bora kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Prosper Alexander Kisinini,amesema mafunzo hayo yamekuwa na tija kwa walengwa.

Amesema washiriki wote wameonesha kwamba walikuwa na kiu ya mafunzo na wamevutiwa na ufanisi wa mafunzo yaliyofundishwa.

Kisinini amesema lengo kuu la mafunzo haya ni kuhakikisha kila raia anapata elimu kuhusu haki zake, wajibu wake, na namna ya kushiriki kikamilifu katika ulinzi na usalama.

Akieleza tathmini ya jumla kuhusu mafunzo hayo, Kisinini amesema yataenda kuwajengea uwezo washiriki kwa kujituma na kuwa na ari ya kufanya kazi kwa bidii.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuelimisha wananchi kuhusu misingi ya utawala bora na umuhimu wa uwazi na uwajibikaji katika utendaji wa Serikali.

"Washiriki wa mafunzo wametuahidi kuibadilisha jamii kupitia mafunzo haya,hii ni ishara ya kwamba walengwa watatekeleza mafunzo hayo kwa vitendo na hivyo kukuza utamaduni wa utawala bora miongoni mwa jamii, " amefafanua

Halikadhalika amesema washiriki hao wameonesha kuwa na kiu ya mafunzo na wameishauri Wizara hiyo kuwa mafunzo hayo yawe endelevu kwa kutanua wigo wa mafunzo kwa viongozi wengi zaidi wakiwemo madiwani, watendaji wa vijiji na Wenyeviti wa Vijiji.

"Tumewasisitiza kwamba maoni yao tumeyapokea na tutayawasilisha ili kuhakikisha mafunzo haya yanaendelea kuwafaidisha watu wengi ziaidi, " ameongeza Kisinini.

Pia amewashukuru wadau ambao wameshirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria kuanzia Mkoani Mtwara hadi kuhitimishwa kwake mkoani Kilimanjaro wakiwemo Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia Jeshi la Polisi, Ofisi ya Rais TAMISEMI na Tume ya Haki za Binadamu, kwa kuunga mkono juhudi za kuhamasisha ujenzi wa utawala bora na uwajibikaji.

Miongoni mwa watoa Mada katika mafunzo hayo, Wakili wa Serikali ASP Nicholas Mhagama amesema kwa tathmini kabla ya mafunzo, wengi wa Watendaji hawakuwa wanafahamu wajibu wao wa kisheria kwenye suala la ulinzi na usalama.

"Ni wacheche waliokuwa na uelewa na baada ya mafunzo kila mtu ana uelewa wa ulinzi na usalama na wote kwa pamoja wameahidi kushirikisha jamii na kuwa na jamii salama," ameeleza Mhagama.

Naye Afisa Utumishi kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Agness Mabago, ameeleza kuwa Watendaji wa Serikali wanatakiwa kufahamu kuwa waajiri wao ni wananchi, kwa kuwa ndiyo walioiweka Serikali madarakani, hivyo wanayo haki ya kupata huduma nzuri.

"Na sasa tunaimani na Watendaji hawa kwa kuwa wamestawi na watashuka chini kuwahudumia Wananchi kwa haki, kwa kufuata kanuni, sheria na miongozo yao," amesema Mabago.

Kwa upande wake Afisa Uchunguzi Mkuu kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Julina Laurent, ameeleza kuwa kwa mikoa yote miwili, yaani Mtwara na Kilimanjaro, mafunzo hayo yamefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Amesema, "Ni matumaini yetu kwamba viongozi waliopata mafunzo haya wataenda kutenda haki katika kutekeleza majukumu yao ikiwa ni pamoja na kuelimisha jamii namna ya kujitoa kulinda usalama na hatimaye kuwa jamii inayojali na kutii usawa wa haki za binadamu."

Pamoja na Mambo mengine,mafunzo haya ya Uraia na Utawala Bora ni muhimu kwa kuboresha ushiriki wa wananchi katika utawala wa nchi, huku wakisisitiza misingi ya uwajibikaji, usawa, na haki za binadamu.

Ifahamike wakakati wa mafunzo washiriki walijidhatiti kuwa sehemu ya mabadiliko chanya katika jamii zao, huku wakitambua kwamba ni jukumu lao kuhakikisha kuwa wanashiriki kikamilifu katika kudumisha utawala bora na ulinzi wa haki za kila mmoja.





Share:

RUWASA YATEKELEZA MRADI WA VISIMA KIJIJI CHA ANGALIA, TUNDURU


Afisa Mahusiano wa Ruwasa Mkoa wa Ruvuma Geddy Ndimbo kushoto akiangalia sehemu ya kisima cha maji kitakachotumika kuwahudumia wakazi zaidi ya 6,332 wa kijiji cha Angalia kata ya Mtina

Na Regina Ndumbaro Tunduru.

Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Tunduru, Mkoa wa Ruvuma, umeanza kutekeleza programu ya uchimbaji wa visima 900 nchini, ambapo kila jimbo linapata visima vitano. 


Katika Wilaya ya Tunduru, yenye majimbo mawili ya Uchaguzi—Tunduru Kusini na Kaskazini—jumla ya visima 10 vinachimbwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 600.

Afisa Maendeleo ya Jamii wa RUWASA Wilaya ya Tunduru, Leticia Mwageni, amesema mradi huo unalenga vijiji ambavyo havina miradi ya maji ya bomba ili kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi. 

Miongoni mwa vijiji vinavyonufaika ni kijiji cha Angalia, kata ya Mtina, ambacho kinapata kisima kinachojengwa kwa gharama ya shilingi milioni 60 kwa kutumia mafundi wa ndani.


Mwageni ameeleza kuwa RUWASA imenunua vifaa vyote vinavyohitajika ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati. 


Tayari ujenzi wa kituo cha kuchotea maji (kioski) umeanza, na matarajio ni kwamba ndani ya mwezi mmoja wananchi wataanza kupata maji safi na salama.


“Wilaya ya Tunduru ina majimbo mawili—Tunduru Kusini na Kaskazini—ambapo Jimbo la Tunduru Kusini limepata visima vitano kwa gharama ya shilingi milioni 300, huku Jimbo la Tunduru Kaskazini likipata visima vitano pia,” 

Kaimu Mtendaji wa Kijiji cha Angalia, Ramadhan Nyenje, ameishukuru serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka mradi huo wa maji katika kijiji hicho ambacho hakijawahi kuwa na maji ya bomba tangu Uhuru mwaka 1961. 

Amesema kijiji hicho chenye wakazi zaidi ya 6,332 kilikuwa kinategemea vyanzo vya asili kama mito na mabonde, ambavyo havitoshelezi mahitaji yao.


Ameongeza kuwa mradi huo utasaidia kupunguza muda wa kusubiri maji kwenye mabomba machache, na kwa kuwa ujenzi wake uko karibu na Shule ya Msingi ya kijiji hicho, wanafunzi watafaidika kwa kupata maji safi ya kunywa, kupikia na kusafisha mazingira yao.


Mkazi wa kijiji cha Angalia Zena Ismail, ameiomba RUWASA kuharakisha ujenzi wa mradi huo na kuweka mabomba kwenye makazi yao ili maji yaweze kufika majumbani, badala ya kutegemea vituo vya kuchotea maji. 


Amesema kwa sasa wanategemea vyanzo vya maji vya asili ambavyo siyo salama, lakini hawana mbadala, hivyo mradi huo utawapunguzia adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji.


Mkazi mwingine wa kijiji hicho Rashid Zuber amesema  kuwa tangu mwaka 1994 walipopata visima vya pampu ya mkono, baadhi yake vimeharibika, hivyo ujio wa mradi huu utakuwa mkombozi mkubwa kwa maendeleo ya kijiji.


RUWASA imewahimiza wananchi kushirikiana katika kutunza miundombinu ya mradi huo ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kusaidia kizazi cha sasa na kijacho kupata huduma ya maji safi na salama.
Share:

TUME YA TEHAMA YASISITIZA UMUHIMU WA ANUANI ZA MAKAZI



Na Mwandishi Wetu, Dodoma

TUME ya TEHAMA, imeelezea kufurahishwa na uamuzi wa Serikali wa kuanzisha Maonesho ya Anuani za Makazi ikisema ni jukwaa muhimu la kufikisha elimu juu ya mchango wa anuani katika uchumi wa kidigitali.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Maonesho ya kwanza ya Anuani ya Makazi, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga alisema Mfumo wa Anwani za Makazi ni nyenzo ya utambuzi ambayo inarahisisha utoaji na upokeaji wa huduma mbalimbali ili kuchochea maendeleo ya Kiuchumi na kijamii.

Alisema katika zama zama hizi ambazo Mapinduzi ya 4,5 na 6 ya viwanda yanategemea matumizi ya TEHAMA, ushiriki wa Tume ya Tehama katika kutoa elimu kwa Watanzania ni muhimu kwani wao ni sehemu ya kusaidia uwapo wa mifumo thabiti ya utambuzi.

“Katika maonesho haya, ni muhimu sana kwetu sisi kama Tume, lakini kwa taifa kwa ujumla kuweza kuendelea kuwafikia Watanzania wa mijini na vijijini waweze kufahamu umuhimu wa anuani za makazi kidigitali ili kila mmoja ashiriki katika kuujenga uchumi wa kidigitali.

“Kote duniani inafahamika kuwa uchumi wa kidigitali ni uchumi wa watu. Watu ili waweze kutumia mifumo kufanya shughuli zao kidigitali, wanahitaji kupata uhakika wa kufikishiwa huduma katika maeneo yao, iwe ofisini na nyumbani. Kwa hiyo katika utambuzi wa kidigitali, anuani ni ya msingi sana,” alisema Dkt. Mwasaga huku akisisitiza wabunifu kuelekeza nguvu katika ubunifu ili kuwafikia Watanzania.

Maonesho hayo ya anuani za makazi yaliyozinduliwa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa jijini Dodoma, yakiwa na kauli mbiu ya: “Tambua na Tumia Anwani ya Makazi Kurahisisha Utoaji na Upokeaji wa Huduma” yameshirikisha pia ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Mbali ya Tume ya TEHAMA, taasisi nyingine zinazoshiriki maonesho hayo ni Posta, NIDA, UCSAF, TTCL, TCRA, TCRA CCC, NEMC, Tume ya Taarifa Binafsi, Makampuni ya Mawasiliano kama “YAS”, NMB na TANAPA.

Serikali kupitia Tume ya TEHAMA, iko katika juhudi kubwa za uwekezaji na uendelezaji wa Sekta ya TEHAMA, ikielekeza nguvu katika uanzishwaji wa vituo vya kikanda vya kukuza bunifu za sekta hiyo nchini. Kwa kuanzia, vinaelekezwa Arusha, Dar es Salaam, Lindi, Mwanza, Mbeya, Dodoma, Tanga na Zanzibar.

Aidha, juhudi zinaendelea kuanzisha vituo vya kukarabati na kutengeneza vifaa vya TEHAMA kwenye mikoa ya Arusha na Dar es Salaam.

Ili kuwafikia wananchi, Serikali pia inaelekeza nguvu katika ngazi za wilaya ili nako kujengwe vituo vya kukuza bunifu za TEHAMA. Baadhi ya wilaya zitakaanza kunufaika ni Masasi, Kibaha, Rufiji, Tanganyika, Bukoba na Butiama.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, DKt. Nkundwe Mwasaga akifafanua jambo mbele ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia na Habari, Jerry Silaa jana katika Viwanja vya Maonesho ya Anuani za Makazi jijini Dodoma. Kushoto kwa Waziri ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa (Katikati walioketi) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa wizara na taasisi zinazoshiriki katika Maadhimisho ya Wiki ya Maonesho ya Anuani za Makazi yanayoendelea jijini Dodoma. Wa kwanza kushoto waliosimama na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga.
Share:

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO IJUMAA FABRUARI 7,2025


Magazeti ya leo


 

Share:

Thursday, 6 February 2025

MALUNDE BLOG YATUNUKIWA CHETI CHA SHUKRANI NA MAHAKAMA KUU YA TANZANIA KANDA YA SHINYANGA


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga Frank Mahimbali akimtunuku cheti cha shukrani, Mkurugenzi na Mmiliki wa Mtandao wa Malunde 1 blog kama ishara ya kuthamini mchango wa mtandao huo maarufu wa habari katika kufanikisha Maadhimisho ya Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria ya Mwaka 2025.

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga imeadhimisha Siku ya Sheria nchini Februari 3, 2025 ambapo maadhimisho hayo yalitanguliwa na Wiki ya Sheria iliyofanyika Januari 25,2025 hadi Februari 1,2025 katika viwanja vya Zimamoto Mjini Shinyanga.


"Cheti hiki kimetolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga kwa chombo hiki cha habari kutokana na ushirikiano wa karibu na juhudi za Malunde 1 Blog katika kuhamasisha na kuendeleza mahusiano mazuri kati ya Mahakama na jamii. Ushiriki wa Malunde Blog umeleta manufaa makubwa kwa jamii ya Shinyanga na kuimarisha utawala wa sheria katika mkoa wa Shinyanga",amesema Jaji Mahimbali leo Februari 6,2025 wakati wa kikao cha Tathmini ya maadhimisho kilichohudhuriwa na wadau mbalimbali.


Malunde 1 Blog inashukuru kwa kutambuliwa na kuahidi kuendelea kutoa mchango wake katika kukuza elimu ya sheria na haki kwa wananchi.







Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger