Monday, 25 November 2024

WAANDISHI WA HABARI MANYARA NA UTPC WAANDAMANA UZINDUZI WA KAMPENI YA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI

WAANDISHI wa habari wa Mkoa wa Manyara na wafanyakazi wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) wameongoza maandamano ya uzinduzi wa kampeni maalum ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Katika maandamano hayo yaliyoanza saa 2 asubuhi Novemba 25 mwaka 2024 katika kituo cha magari cha zamani Babati na kupita mitaa mbalimbali yalishirikisha pia makundi mbalimbali ikiwemo madereva wa bodaboda, wakulima, wafugaji, wanafunzi wa chuo cha Veta Manyara.

Katibu wa Klabu ya Waandishi wa habari wa mkoa wa Manyara (NRPC) Jaliwason Jasson amesema maandamano hayo yakiongozwa na waandishi wa habari yamepitia maeneo ya barabara ya Arusha, Oysterbay, Ngarenaro na kumalizikia White Rose hoteli ili kusikiliza mada mbalimbali zitakazotolewa.

"Nawashukuru waandishi wa habari na wadau mbalimbali waliotuunga mkono katika kushiriki wakiwemo askari polisi wa kikosi cha usalama barabara waliosimamia ulinzi na usalama ili kusitokee ajali," amesema

Share:

TANI 2.2 ZA DAWA ZA KULEVYA ZAKAMATWA TANGA, DAR ES SALAAM

Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo
Dawa za kulevya aina ya Skanka
Dawa za kulevya aina ya Heroin na Methamphetamine



***
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola, imefanikiwa kukamata jumla ya kilogramu 2,207.56 za dawa za kulevya na dawa tiba zenye asili ya kulevya katika mikoa ya Tanga na Dar es Salaam. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo, Novemba 25, 2024, na Kamishina Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, miongoni mwa dawa zilizokamatwa ni skanka, methamphetamine, heroin, na dawa tiba aina ya Fentanyl. 

Amesema Dawa hizo zilipatikana katika operesheni maalum zilizofanyika katika maeneo tofauti na kwamba Watuhumiwa saba wanashikiliwa kuhusiana na dawa hizo.


 Ameongeza kuwa , Kati ya dawa zilizokamatwa, skanka ni kilogramu 1,500.6, methamphetamine kilogramu 687.76, heroin kilogramu 19.20, na chupa 10 za dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Fentanyl. 

"Tarehe 14 Novemba, 2024, jijini Dar es Salaam, katika wilaya ya Kigamboni, mtaa wa Nyangwale, watuhumiwa Mohamed Suleiman Bakar (40) na Sullesh Said Mhailoh (36), wote wakazi wa Mabibo, Dar es Salaam, walikamatwa wakiwa na kilogramu 1,350.4 za dawa za kulevya aina ya skanka. 

Dawa hizo zilikuwa zimefichwa ndani ya nyumba aliyopanga mtuhumiwa Mohamed, ambayo aliitumia kama ghala la kuhifadhi dawa hizo. Aidha, dawa nyingine zilipatikana ndani ya gari aina ya Nissan Juke yenye namba za usajili T 534 EJC, zikiwa tayari kwa kusambazwa",ameeleza.

" Tarehe hiyo hiyo, katika mtaa wa Pweza Sinza E, wilaya ya Ubungo, jijini Dar es Salaam, mtuhumiwa Iddy Mohamed Iddy (46), mkazi wa Chanika Buyuni, alikamatwa akiwa na kilogramu 150.2 za skanka, zilizokuwa zimefichwa katika maboksi ya sabuni na baadhi ya dawa hizo zikiwa zimefichwa kwenye boksi lililotengenezwa kwa bati ngumu na kupachikwa kwenye chassis ya gari aina ya Scania lenye namba za usajili wa Afrika Kusini LN87XJGP, ambalo limekuwa likitumika kusafirisha bidhaa mbalimbali kutoka nje ya nchi",ameongeza. 

Ameeleza kuwa vilevile, tarehe 17 Novemba, 2024, katika jiji la Tanga, watuhumiwa Ally Kassim Ally (52) na Fahadi Ally Kassim (36) walikamatwa mtaa wa Mwakibila wakiwa na kilogramu 706.96 za dawa aina ya heroin na methamphetamine. 

Baadhi ya dawa hizo zilipatikana ndani ya gari aina ya Toyota Noah yenye namba za usajili T 714 EGX, huku nyingine zikibainika kufichwa kwenye nyumba aliyopanga mtuhumiwa. 

  Tarehe 19 Novemba, 2024, katika mtaa wa Kipata na Nyamwezi Kariakoo jijini Dar es Salaam, watuhumiwa Michael Dona Mziwanda (28) mkazi wa Tabata Segerea, na Tumpale Benard Mwasakila (32) mkazi wa Temeke Mikoroshini, walikamatwa wakiwa na chupa kumi za dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Fentanyl wakiwa nazo katika duka la M-PESA. 

Aidha, katika operesheni hizi zilizofanyika, jumla ya magari matatu na boti moja vilivyohusika katika uhalifu huo vinashikiliwa.

 Dawa zilizokamatwa ni nyingi na zingeweza kuwa na madhara makubwa kwa jamii na taifa ikiwa zingeingia mitaani. 

Dawa hizi haziathiri tu wale waliokwisha anza matumizi ya dawa za kulevya, bali pia wafanyabiashara hawa hulenga watu wengine ambao hawajaanza matumizi ili kutanua masoko yao. Walengwa wapya wanaweza kuwa mtu yeyote katika jamii au familia za Kitanzania. 

Hivyo, ni dhahiri kuwa jamii nzima inakabiliwa na hatari ya dawa za kulevya. Kadhalika, Mamlaka imebaini kuwa wahusika wa biashara haramu ya dawa za kulevya hutumia mbinu ya kupanga nyumba ambazo zinageuzwa kuwa maghala ya kuhifadhi dawa za kulevya, huku wao wakiishi katika maeneo mengine. 

Mamlaka inatoa rai kwa wamiliki wa nyumba kuwa makini wanapopangisha nyumba zao, kwani nyumba inayotumika kwa shughuli za dawa za kulevya ni kinyume cha sheria na inaweza kutaifishwa.

 Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Sura ya 95, imeweka katazo kwa mmiliki au msimamizi wa nyumba, msimamizi wa eneo au chombo cha usafirishaji kuruhusu vitumike kwa lengo la kutengeneza, kuvuta, kujidunga, kuuza au kununua dawa za kulevya. 

Aidha, mmiliki anapojua kuwa kosa linatendeka kwenye eneo lake, anajukumu la kutoa taarifa kwa Mamlaka. 

Kushindwa kufanya hivyo ni kosa la jinai, na akitiwa hatiani, adhabu yake inaweza kuwa faini kuanzia shilingi milioni tano hadi milioni hamsini, au kifungo cha miaka mitano hadi miaka thelathini jela, au vyote kwa pamoja. Mamlakaya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inatoa shukrani kwa wananchi wanaotoa ushirikiano kwa kuwafichua watu wanaojihusisha na dawa za kulevya na tunawahimiza wananchi wote kuendelea kutoa taarifa pale wanapobaini matukio yanayohusiana na biashara haramu ya dawa za kulevya. 






Share:

NAIBU KATIBU MKUU MONGELLA KUFUNGA KAMPENI ZA CCM UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA MKOA WA SHINYANGA

 


Naibu Katibu Mkuu CCM Bara Ndugu John V. K. Mongella anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano wa kufunga kampeni za CCM kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2024 Mkoa wa Shinyanga, utakaofanyika tarehe 26 Novemba 2024, Kata ya Kitangiri, mkoani humo.

Share:

WALIMU ZANZIBAR WAPIGWA MSASA UMAHIRI WA UFUNDISHAJI


Taasisi ya Mwanyanya Green Society imeanza kutekeleza mradi mkubwa wa kuboresha ubora wa elimu katika shule za msingi za Wilaya ya Kaskazini B, Zanzibar.

 Mradi huu, unaofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi, na Utamaduni (UNESCO) kwa kushirikiana na Alwaleed Philanthropies, unalenga kuwajengea walimu uwezo kupitia mafunzo ya mbinu za kisasa za ufundishaji na matumizi ya teknolojia ya kidijitali.

Shule zinazofaidika na mradi huu ni pamoja na Kiongwe, Pangatupu, Fujon, Mahonda, Mgambo, Kilombaro, Mgonjon, Hamid Ameir, na Mwanda. Mafunzo haya yanajumuisha walimu, wajumbe wa kamati za shule, na wazazi, yakilenga kuimarisha ushirikiano katika kukuza ubora wa elimu.

Uzinduzi rasmi wa mafunzo haya ulifanyika Novemba 23, 2024, katika Skuli ya Sekondari ya Mahonda, ambapo kituo cha ubunifu wa kisayansi, Mahonda HUB, kinatumika kama eneo la mafunzo. Hafla ya uzinduzi ilihudhuriwa na Mkurugenzi wa Idara ya Elimu ya Mandalizi, Msingi na Kati, Bi. Fatma Ramadhan Mode, ambaye alikuwa mgeni rasmi.

Mafunzo hayo pia yamefanyika katika ukumbi wa walimu wa TC Mkwajuni, ambapo walimu wanajifunza mbinu za kisasa za ufundishaji pamoja na matumizi ya teknolojia ili kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.

Kupitia mradi huu, Mwanyanya Green Society inadhihirisha dhamira yake ya kuboresha sekta ya elimu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Mradi huu unatarajiwa kuleta athari kubwa kwa kuinua uwezo wa walimu na kuboresha kiwango cha elimu ya msingi katika Wilaya ya Kaskazini B, Zanzibar.
Share:

Sunday, 24 November 2024

ELIMU ZAIDI YAHITAJIKA KATIKA MATUMIZI YA KEMIKALI

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi mwandamizi wa Polisi (SACP) George Katabazi, akizungumza katika kikao cha kuhitimisha Kampeni ya utoaji elimu kwa Umma juu ya Usafirishaji salama wa kemikali ya Sodium Cyanide kilichofanyika jijini Dodoma Novemba 23,2024.


*********************


Na Rosemary Celu

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), George Katabazi, amezitaka Taasisi za Serikali na Binafsi kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na matumizi sahihi na salama ya Kemikali.

Kamanda Katabazi amesema hayo leo wakati akihitimisha kikao cha kuhitimisha awamu ya kwanza ya kampeni ya utoaji elimu kwa umma juu ya usafirishaji salama wa kemikali ya Sodium Cyanide kilichofanyika katika ukumbi wa Dkt. Mafumiko jijini Dodoma.

“Kwa upande wa Serikali Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imekua ikitoa elimu na mafunzo kwa makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na wajasiliamali wadogo, wachimbaji dhahabu, wasimamizi wa kemikali mahala pa kazi, Madereva wanaosafirisha kemikali na jamii kwa ujumla, hivyo niziombe taasisi nyingine za Serikali na Binafsi ziige mfano huo wa GCLA” alisema Kamanda Katabazi.

Akizungumzia lengo la kufanyika kwa Kampeni hiyo ya utoaji elimu kwa umma juu ya usafirishaji salama wa kemikali ya Sodium Cyanide ambayo hutumika zaidi kwenye migodi kuchenjua dhahabu, Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Daniel Ndiyo, amesema kwa kuwa kemikali hiyo inaingia kwa wingi nchini na ni hatarishi hivyo ni vema elimu ikatolewa kwa jamii.

“Tupo hapa kwa kazi maalumu ambayo wadau wanatakiwa kuzingatia kusimamia usafirishaji salama wa kemikali ya Sodium Cyanide, tunafanya hivi cha kwanza kemikali inaingia kwa wingi nchini, cha pili kemikali ni hatarishi kwa maana kwamba ni sumu, na cha tatu kemikali hii inahitajika na ina matumizi makubwa kwenye machimbo ya dhahabu ili tupate dhahabu hivyo ni vema jamii ikaelimishwa” alisema Mkurugenzi Ndiyo.

Naye Msimamizi wa Usafirishaji wa Kampuni ya Uchimbaji wa dhahabu ya Barrick, Joseph Mbanya, amewashukuru wadau wote walioratibu zoezi la kampeni hiyo na kwamba ana imani elimu imeweza kufika kwa wadau na wao kwenda kuelimisha jamii kwa ujumla.

Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti, Daniel Ndiyo, akizungumza wakati akimkaribisha mgeni rasmi katika kikao cha kuhitimisha Kampeni ya utoaji elimu kwa Umma juu ya Usafirishaji salama wa kemikali ya Sodium Cyanide kilichofanyika jijini Dodoma Novemba 23,2024.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) George Katabazi (kushoto), akimkabidhi tuzo Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti Daniel Ndiyo (kulia), iliyotolewa na wadau wa usafirishaji wa kemikali ya Sodium Cyanide katika kikao cha kuhitimisha Kampeni ya utoaji elimu kwa Umma juu ya Usafirishaji salama wa kemikali hiyo kilichofanyika jijini Dodoma Novemba 23,2024.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), George Katabazi (kulia), akipokea tuzo kwa niaba ya Jeshi la Polisi Tanzania kutoka kwa Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti, Daniel Ndiyo,(wa pili kushoto), pamoja na Meneja Mkuu wa Kampuni ya Swala Logistics Fardeen Rattansi (kushoto), katika kikao cha kuhitimisha Kampeni ya utoaji elimu kwa Umma juu ya Usafirishaji salama wa kemikali ya Sodium Cyanide kilichofanyika jijini Dodoma Novemba 23,2024.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) George Katabazi (aliyevaa miwani), akipokea zawadi kwa niaba ya Jeshi la Polisi Tanzania zilizotolewa na wadau wa usafirishaji wa kemikali katika kikao cha kuhitimisha Kampeni ya utoaji elimu kwa Umma juu ya Usafirishaji salama wa kemikali ya Sodium Cyanide kilichofanyika jijini Dodoma Novemba 23,2024.


.

Mtumishi wa Mamlaka Revocatus Mwamba,akiwasilisha mada kuhusu Kanuni na Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali katika kikao cha kuhitimisha Kampeni ya utoaji elimu kwa Umma juu ya Usafirishaji salama wa kemikali ya Sodium Cyanide kilichofanyika katika ukumbi wa Dkt Mafumiko jijini Dodoma Novemba 23,2024.

Meneja kutoka Kampuni ya Freight Forwarders, Sadiki Yusuph, akiwasilisha mada kuhusu usafirishaji salama wa kemikali ya Sodium Cyanide katika kikao cha kuhitimisha Kampeni ya utoaji elimu kwa Umma juu ya Usafirishaji salama wa kemikali ya Sodium Cyanide kilichofanyika jijini Dodoma Novemba 23,2024.

Mkaguzi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Stephen Katte,akiwasilisha mada kuhusu Majukumu ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika kikao cha kuhitimisha Kampeni ya utoaji elimu kwa Umma juu ya Usafirishaji salama wa kemikali ya Sodium Cyanide kilichofanyika jijini Dodoma Novemba 23,2024.

Washiriki wakifuatilia mada mbalimbali zilizowasilishwa katika kikao cha kuhitimisha Kampeni ya utoaji elimu kwa Umma juu ya Usafirishaji salama wa kemikali ya Sodium Cyanide kilichofanyika jijini Dodoma Novemba 23,2024.

Wadau wakiuliza maswali mbalimbali katika kikao cha kuhitimisha Kampeni ya utoaji elimu kwa Umma juu ya Usafirishaji salama wa kemikali ya Sodium Cyanide kilichofanyika jijini Dodoma Novemba 23,2024.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) George Katabazi aliyekaa (katikati), akiwa pamoja na Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti, Daniel Ndiyo (wa pili kushoto, waliokaa), Meneja wa Ofisi ya Kanda ya Kati, Gerald Meliyo (wa pili kulia, waliokaa), Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Boniphace Mbao (aliyekaa kushoto), Mwakilishi wa Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji Dodoma, Mkaguzi wa Polisi, Hamadi Dadi (aliyekaa kulia), pamoja na wadau wa usafirishaji wa kemikali na watumishi wa GCLA mara baada ya kuhitimisha kikao cha Kampeni ya utoaji elimu kwa Umma juu ya Usafirishaji salama wa kemikali ya Sodium Cyanide kilichofanyika jijini Dodoma Novemba 23,2024.
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger