Saturday, 23 November 2024
RAIS SAMIA AWASILI MKOANI MOROGORO KWA KUTUMIA USAFIRI WA TRENI YA SGR
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwasili katika Stesheni ya Jakaya Kikwete Mkoani Morogoro ambapo amesafiri kwa Treni ya SGR kutokea Jijini Dar es Salaam tarehe 23 Novemba, 2024.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwasili katika Stesheni ya Jakaya Kikwete Mkoani Morogoro ambapo amesafiri kwa Treni ya SGR kutokea Jijini Dar es Salaam tarehe 23 Novemba, 2024.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima mara baada ya kuwasili katika Stesheni ya Jakaya Kikwete Mkoani Morogoro tarehe 23 Novemba, 2024.
MATI FOUNDATION YAZINDULIWA RASMI

Mwandishi Wetu ,Manyara.
Taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Mati Foundation yenye lengo la kusaidia jamii ,wahitaji na makundi maalumu ikiwemo wenye ulemavu iliyoko chini ya kampuni ya Mati Super Brands Limited imezinduliwa rasmi leo na Mkuu wa Wilaya ya Babati Emmanuela Kaganda katika makao makuu ya kampuni hiyo Mjini Babati mkoani Manyara.
Akizungumza mara baada ya kuzindua Taasisi ya Mati Foundation , Mkuu wa Wilaya ya Babati amempongeza Mwenyekiti wa Taasisi hiyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Mati Super Brands Ltd David Mulokozi kwa kuwa mstari wa mbele kusaidia jamii inayomzunguka katika Wilaya ya Babati na Tanzania kwa ujumla kwa kutoa sehemu ya faida anayoipata kusaidia jamii.

Emmanuela amesema kuwa kampuni hiyo imekuwa ikiunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwahudumia wananchi kupitia misaada mbali mbali wanayoitoa kwa jamii ya Watanzania.
"Nipende kuipongeza Bodi ya Mati Super Brand Limited kwa kuja na wazo la kusaidia jamii kupitia Taasisi ya Mati Foundation na kuifikiria zaidi jamii ya Wananchi wa Babati na Tanzania kwa ujumla", ameeleza Mkuu wa Wilaya ya Babati.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Mati Foundation ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mati Super Brands Limited David Mulokozi amesema kuwa ndoto yake ni kunyanyua jamii inayomzunguka kwa kurudisha sehemu ya faida anayoipata mwa jamii jambo ambalo limekua ni utamaduni wao na ibada pia.
"Tunapowasaidia watu tunafanya kwa Moyo na Upendo mkubwa na tunajitagidi mengi tunayafanya na hatuyasemi hadharani ,tumekua tukigusa watu mbalimbali na makundi mbali mbali" Anaeleza Mulokozi.
Mwenyekiti Msaidizi wa Mati Foundation Gwandumi Mpoma amesema kuwa tayari wametumia kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 1.5 kusaidia jamii inayozunguka kama mchango wao kwa jamii tangu kiwanda hicho kilipoanzishwa mwaka 2017.
Mpoma amesema kuwa wamekua wakitoa misaada sehemu mbali mbali ikiwemo kwenye maaafa ya Mafuriko hanang,kusaidia fimbo nyeupe kwa wenye ulemavu wa macho pamoja na kutoa misaada kwa yatima,wajane na wazee.


TOTALERNEGIES MARKETING TANZANIA LTD KUPITIA MFUKO WA ELIMU WA TAIFA YATOA KATONI 360 ZA TAULO ZA KIKE KWA SHULE NNE ZA SEKONDARI.
Kaimu Mkurugenzi Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi Bw. Masozi Nyirenda akiongea katika hafla ya kukabidhi katoni 360 za taulo za kike zilizotolewa na TotalEnergies Marketing Tanzania.
Dodoma
Kampuni ya TotalEnergies Marketing Tanzania Ltd leo tarehe 22 Novemba 2024 imekabidhi katoni 360 za taulo za kike zenye thamani ya takribani Sh. Milioni 25.5 ikiwa ni sehemu ya kuchangia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwa lengo la kuwasaidia watoto wa kike kuendelea kufurahia masomo hata wanapokuwa katika siku za hedhi.
Kukabidhiwa kwa taulo hizo za kike katoni 360 hii leo kunaifanya kampuni hiyo ndani ya mwaka 2024 kuwa imetoa jumla ya katoni 500 zenye thamani ya Sh milioni 35.4 ambazo zimesambazwa katika shule saba zikijumuisha za msingi na sekondari.
Hafla fupi ya kukabidhi taulo hizo za kike imefanyika Makao Makuu ya TEA yaliyoko Ilazo Extension Jijini Dodoma ambapo pia imehudhuriwa na wawakilishi wa shule nne za sekondari zitakazonufaika ambazo ni; Lemira iliyoko Hai Kilimanjaro, Sitalike ya Mkoani Katavi, Manunus Mkombozi ya Same Kilimanjaro na Isack Kamwelwe ya Mkoani Katavi.
Shule nyingine zilizonufaika na taulo hizi za kike ni pamoja na Shule ya Sekondari Songwe ya Mkoani Songwe, Kilombero na Njiwa zote za Mkoani Morogoro pamoja na Sisters of Mary iliyoko Kisarawe Mkoani Pwani.
Kwa upande wa TEA hafla hiyo imeongozwa na Kaimu Mkurugenzi Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi Bw. Masozi Nyirenda ambapo upande wa TotalEnergies Marketing Tanzania Ltd imewakilishwa na Mkurugenzi wa Sheria na Mahusiano ya Kampuni, Bi Getrude Mpangile.
Mbali na kuchangia taulo za kike, Kampuni ya TotalErnegies Marketing Tanzania Ltd mwaka huu imetoa msaada wa madawati 200 katika shule tatu katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam yakiwa na thamani ya Sh. milioni 25. 9 kutokana na kuingia makubaliano ya kushirikiana na TEA katika kutoa misaada ya kuboresha mazingira ya kujifunza na kufundishia nchini.
Mamlaka ya Elimu Tanzania inalo jukumu la kuhamasisha wadau mbalimbali wa Elimu ikiwemo mashirika ya umma, mashirika binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali, asasi mbalimbali na watu binafsi kuchangia maendeleo ya elimu kwa kuchangia rasilimali fedha katika Mfuko wa Elimu wa Taifa. Mchangiaji katika Mfuko wa Elimu ananufaika kwa njia zifuatazo;
Kupata Hati ya Utambuzi wa Uchangiaji wa Elimu (Certificate of Educational Appreciation) kwa mujibu wa Kifungu cha 12 cha Sheria ya Mfuko wa Elimu ya mwaka 2001.
Kupata nafuu ya kodi kutoka kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa mujibu wa Kifungu cha 16 (1) cha Sheria ya Kodi ya Mapato Sura 332 marejeo ya mwaka 2019.
Kutangazwa na kutambuliwa kitaifa, ambapo mchangiaji huandikwa katika rejesta ya kudumu ya wachangiaji wa elimu.
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ni Taasisi ya Umma inayofanya kazi chini ya usimamizi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. TEA inaratibu Mfuko wa Elimu wa Taifa ambao unasaidia jitihada za Serikali katika kuboresha miundombinu ya elimu kwa lengo la kuongeza ubora wa elimu na upatikanaji wake kwa usawa.
Mkurugenzi wa Sheria na Mahusiano ya Kampuni wa TotalEnergies Marketing Tanzania Ltd Bi Getrude Mpangile akielezea dhamira yao ya kuchangia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia katika hafla ya kukabidhi katoni 360 za taulo za kike. 
Kaimu Mkurugenzi Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi Bw. Masozi Nyirenda (kulia) akipokea taulo za kike kutoka kwa Mkurugenzi wa Sheria na Mahusiano ya Kampuni wa TotalEnergies Marketing Tanzania Ltd Bi Getrude Mpangile tayari kwa ajili ya kuzipatia shule nne zitakazonufaika. 

Walimu kutoka shule nne ambazo ni wanufaika wa taulo za kike wakikabidhiwa taulo hizo kwa ajili ya kuwapelekea wanafunzi wa kike kwenye shule zao.
Baadhi ya watumishi wa Mamlaka ya Elimu Tanzania, TotalEnergies Marketing Tanzania na walimu kutoka shule nne nufaika wakiwa katika picha ya Pamoja mara baada ya hafla ya kukabidhiwa jumla ya katoni 360 za taulo za kike kwa lengo la kuwasaidia wanafunzi wa kike kusoma katika hali ya usafi muda wote.
Friday, 22 November 2024
MCHAKA MCHAKA KAMPENI ZA UCHAGUZI CCM KAMBARAGE.. ODILIA ASEMA MAKUBWA YAMEFANYIKA
Na Suzy Butondo,Shinyanga press Blog
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi CCM mkoa wa Shinyanga Odilia Batimayo amewataka wananchi wote wa kata ya Kambarage kuendelea kukiamini Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwa viongozi wake wamefanya maendeleo makubwa katika sekta mbalimbali za kijamii zikiwemo barabara na vituo vya afya.
Hayo ameyasema leo wakati akizindua kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika leo Novemba 21,2024 katika mtaa wa Majengo kata ya Kambarage manispaa ya Shinyanga
Batimayo amesema Chama Cha Mapinduzi CCM kwa usimamizi mkubwa wa Rais Samia Suluhu Hassan kimefanya maendeleo makubwa katika Taifa la Tanzania na kwa kata ya Kambarage, barabara zilikuwa mbovu lakini kwa sasa zinapitika vizuri,kulikuwa hakuna kituo cha afya lakini kwa sasa kipo na wananchi wanapata huduma vizuri, wanawake wana uhakika wa kujifungua salama, hivyo tuendelee kuzaa tu kwa sababu usalama upo.
"Kinachotakiwa tutembee kifua mbele na tukawe mabalozi wa kuzungumzia maendeleo makubwa yaliyofanyika katika awamu ya sita,hivyo tupo katika kukumbushana na kuwaomba wananchi waendelee kutuamini kwani mama yetu mama Samia amefanya maendeleo makubwa na kama kuna mtu ambaye hayaoni maendeleo haya atakuwa na matatizo", amesema Batimayo.
"Na leo kazi kubwa ni kufanya uzinduzi kwa kuwaomba wananchi wachague wenyeviti na wajumbe wa kutoka CCM na si kwingine kwa sababu maendeleo tunayaona ambayo yalisimamiwa na wenyeviti wa CCM , hivyo tunaomba kura zenu zote kwa wenyeviti wetu na tunaamini watashinda kwa asilimia 100 , wapinzani waache kufanya majaribio kwenye maendeleo ya watu cha msingi tuchagueni mwenyekiti wa CCM", ameongeza
Kwa upande wake diwani wa kata ya Kambarage Hassan Mwendapole amesema toka mwaka 2000 walikuwa na shida ya ufaulu wa watoto lakini matokeo ya sasa wanafaulu vizuri na madarasa yapo ya kutosha, wote wataingia darasani hakuna atakayebaki.
Diwani viti maalumu Sheila Mshandete amesema katika kata ya Kambarage wamejipanga vizuri kuhakikisha wanapata ushindi kwa kwa kishindo, walikuwa na kero ya maji kuingia kwenye makazi ya wa watu lakini kwa sasa hayaingii tena, viongozi wa CCM wamelishughulikia.
















