Sunday 30 June 2024

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMATATU JULAI 1, 2024



Share:

YUSUPH MANJI AFARIKI DUNIA



Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Diwani wa Kata ya Mbagala Kuu kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mkurugenzi wa Kampuni ya Qualify Group LTD, Yusuph Manji, amefariki Dunia jana Jumamosi, Juni 29, 2024 huko Florida nchini Marekani alikokuwa akipatiwa matibabu.

Taarifa za kifo cha Manji zimethibitishwa na mtoto wake Mehbub Manji.

Taarifa zaidi kukujia...

CHANZO: MWANANCHI_OFFICIAL

https://ift.tt/9yFWi7c

Share:

THPS YASISITIZA UMUHIMU WA KUWEKEZA KWENYE KINGA NA TIBA DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akisikiliza maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa THPS, Dkt. Redempta Mbatia
kuhusu huduma za Tiba kwa Waraibu (MAT) na huduma za Kinga, Tiba na Matunzo ambazo zinatolewa na THPS katika mikoa ya Tanga, Pwani, Shinyanga na Kigoma alipotembelea Banda la THPS kwenye maonesho ya kilele cha maadhimisho ya kitaifa ya siku ya kupiga vita dawa za kulevya duniani yaliyofanyika kuanzia Juni  30,2024 katika viwanja vya Nyamagana Jijini Mwanza - Picha na Kadama Malunde
Mkurugenzi Mtendaji wa THPS, Dkt. Redempta Mbatia akimwelezea Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa kuhusu huduma za Tiba kwa Waraibu (MAT) na huduma za Kinga, Tiba na Matunzo ambazo zinatolewa na THPS katika mikoa ya Tanga, Pwani, Shinyanga na Kigoma.


Siku ya Kimataifa ya Kupiga Vita Matumizi na Usafirishaji wa Dawa za Kulevya Duniani huadhimishwa tarehe 26 Juni kila mwaka ili kuimarisha hatua na ushirikiano katika kushinda vita dhidi ya dawa za kulevya.

Hata hivyo, maadhimisho ya kitaifa kwa mwaka huu 2024 yamefanyika katika viwanja vya Nyamagana Jijini Mwanza kuanzia tarehe 27 hadi 30 Juni 2024 chini ya kaulimbiu: 'Wekeza kwenye Kinga na Tiba dhidi ya Dawa za Kulevya'.


Tanzania Health Promotion Support (THPS) iliungana na Serikali na wadau wengine katika kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuwekeza katika huduma ya tiba kwa waraibu (MAT) na huduma za kinga, matunzo na matibabu ya maambukizi ya VVU na Kifua kikuu.


Katika hafla hiyo ya siku nne, shughuli mbalimbali ziliandaliwa kwa ajili ya kuelimisha jamii kuhusu madhara ya matumizi ya dawa za kulevya na umuhimu wa kuwekeza katika mikakati ya kujikinga. 

Mradi wa THPS Afya Hatua unaofadhiliwa na Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na Ukimwi (PEPFAR) kupitia Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (U.S. CDC) umekuwa ukishirikiana na wadau mbalimbali katika kutoa huduma za MAT na huduma za Kinga, Tiba na Matunzo katika mikoa ya Pwani na Tanga.

"Tumefanikiwa kuandikisha watumiaji 2,442 wa dawa za kulevya katika mpango wa MAT, na kati yao 1,426 bado wanaendelea na matibabu", amesema Dkt. Redempta Mbatia, Mkurugenzi Mtendaji wa THPS. 


Pamoja na huduma za MAT, waraibu wote waliojiandikisha waliweza kupata ushauri nasaha na upimaji wa VVU. Kati ya hao, watumiaji dawa za kulevya 122 waligundulika kuwa na VVU na mara moja walianza kupata huduma za tiba na matunzo katika kliniki za tiba na matunzo (CTC) zilizopo maeneo yao. Huduma hizi zinasaidia sio tu kuokoa maisha bali pia kuboresha ustawi wa jamii tunazohudumia”, amesema.


Mradi wa Afya Hatua umekuwa ukiziwezesha Asasi za Kiraia (AZAKI) katika mikoa ya Tanga na Pwani katika utambuzi wa waraibu wa dawa za kulevya, kuwapatia elimu na kuwaunganisha na huduma za MAT. 

Dkt. Mbatia amesema kuwa kila mwezi AZAKI hizo zimefanikiwa kuandikisha wastani wa watumiaji wa dawa za kulevya wapya 30 na kuwarudisha tena watumiaji dawa za kulevya 45 ambao awali walikuwa wameacha matibabu. Utaratibu huu umesaidia kupunguza changamoto ya uraibu wa dawa za kulevya na kudhibiti maambukizi ya VVU katika mikoa hiyo. 

Katika hafla hii ya maadhimisho ya kupiga vita dawa za kulevya duniani, wanufaika wa huduma za MAT wameshiriki na kutoa ushuhuda wa jinsi huduma hizi zilivyotumika kama njia ya kuokoa maisha, zikiwasaidia kurejesha udhibiti wa maisha yao kutoka kwenye uraibu. 

Kupitia elimu, uhamasishaji, na ushirikishwaji wa jamii, inawezekana kushishinda vita dhidi ya dawa za kulevya.

Akizungumza wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya kupiga vita dawa za kulevya, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amesema serikali inaendelea na jitihada za kupambana na dawa kulevya hivyo kuwataka wadau kuongeza nguvu za pamoja.


" Dawa za kulevya ni janga,zina madhara makubwa kiafya na kiuchumi ni lazima litokomezwe.

Nitoe wito kwa vijana tuachane na dawa za kulevya, tufanye shughuli zingine za kujenga uchumi..Mamlaka ya kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), mnafanya kazi nzuri, endeleeni kutekeleza majukumu yenu, tunataka dawa za kulevya zipotee kabisa Tanzania", ameongeza Mhe. Majaliwa.


"Katika mapambano haya sisi serikali hatufanyi kazi peke yetu, tunawashukuru sana PEPFAR, ICAP, CDC, THPS hawa ni wadau wetu wakubwa tunafanya kazi nao vizuri katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya. Serikali itaendelea kushirikiana nanyi ili kuhakikisha vijana wetu wanabaki salama", amesema Mhe. Waziri Mkuu.


Kuhusu THPS

Tanzania Health Promotion Support (THPS) ni asasi isiyo ya kiserikali iliyoanzishwa mwaka 2011, chini ya Sheria ya asasi zisizo za kiserikali nambari 24 ya 2002.

THPS inafanya kazi kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara za Afya za Tanzania Bara na Zanzibar; Wizara ya Jinsia, Vijana, Wazee na Makundi Maalum; Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Kwa ufadhili wa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Misaada ya UKIMWI (PEPFAR) kupitia Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (U.S. CDC), THPS inatekeleza afua mbalimbali za VVU/UKIMWI; Kifua kikuu; kuzuia ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto; huduma za afya ya uzazi, uzazi, watoto wachanga, watoto na vijana; mifumo ya habari ya maabara na usimamizi wa afya, na UVIKO-19.

Kuhusu mradi wa CDC/PEPFAR Afya Hatua (Oktoba, 2021- Septemba, 2026)

Mradi huu unalenga kutoa huduma jumuishi katika vituo vya afya (Kigoma, Pwani, Shinyanga na Tanga) na katika jamii (Kigoma, Pwani na Tanga). 

Huduma hizi ni pamoja na matibabu na matunzo ya watu wanaoishi na VVU, huduma za kitabibu za tohara kwa wanaume katika mikoa ya Kigoma na Shinyanga na programu ya DREAMS kwa wanawake katika mkoa wa Shinyanga.

Utafiti wa Ustawi na Afya wa Vijana na Watoto nchini Tanzania (WHYS 2024)

Utafiti huo unalenga kuelewa aina mbalimbali za ukatili, maambukizi ya VVU, na uhusiano wake na ukatili miongoni mwa vijana wenye umri wa miaka 13-24 Tanzania Bara na Zanzibar.

  

Mkurugenzi Mtendaji wa THPS, Dkt. Redempta Mbatia akimwelezea Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa kuhusu huduma za Tiba kwa Waraibu (MAT) na huduma za Kinga, Tiba na Matunzo ambazo zinatolewa na THPS katika mikoa ya Tanga, Pwani, Shinyanga na Kigoma

 Picha na Kadama Malunde
Mkurugenzi Mtendaji wa THPS, Dkt. Redempta Mbatia akimwelezea Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa kuhusu kuhusu huduma za Tiba kwa Waraibu (MAT) na huduma za Kinga, Tiba na Matunzo ambazo zinatolewa na THPS katika mikoa ya Tanga, Pwani, Shinyanga na Kigoma
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (kushoto) akisikiliza maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa THPS, Dkt. Redempta Mbatia 
kuhusu huduma za Tiba kwa Waraibu (MAT) na huduma za Kinga, Tiba na Matunzo ambazo zinatolewa na THPS katika mikoa ya Tanga, Pwani, Shinyanga na Kigoma
alipotembelea Banda la THPS kwenye maonesho ya kilele cha maadhimisho ya kitaifa ya siku ya kupiga vita dawa za kulevya duniani yaliyofanyika kuanzia Juni  30,2024 katika viwanja vya Nyamagana Jijini Mwanza



 

Share:

TANROADS YAMPA TANO RAIS SAMIA KUTOA BIL 101.2 KUANZA UJENZI WA KM 73 ZA LAMI BARABARA YA KAHAMA-BULYANHULU JCT – KAKOLA


Baada ya tarehe 16 Machi 2024 Serikali kusaini Mkataba wa ujenzi wa barabara ya Kahama-Bulyanhulu Jct - Kakola yenye urefu wa Kilomita 73 kwa kiwango cha lami, tayari Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation imeanza utekelezaji wake.

Pamoja na Barabara hiyo kufungua fursa za kiuchumi za madini, kilimo, misitu na utalii katika mikoa ya Shinyanga, Geita, Tabora, Kagera na Kigoma mara baada ya kukamilika pia Barabara hiyo ni muhimu katika shughuli za kiuchumi na kijamii kwa Mkoa wa Shinyanga hususani Manispaa ya Kahama ambako kuna mkusanyiko mkubwa wa Wasafirishaji wa mizigo kutoka bandari kuu ya Tanzania kwenda nchi za jirani za Rwanda na Uganda.

Akizungumza mara baada ya kukagua hatua zilizofikiwa za ujenzi wa barabara hiyo, Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Shinyanga Mhandisi Joel Samwel Mwambungu amesema kuwa barabara hiyo inajengwa na serikali kwa gharama ya Shilingi Bilioni 101.2 kwa ufadhili wa Kampuni ya Madini ya Barrick Tanzania Mining Companies (BTMCs).

Mhandisi Samwel ameeleza kuwa barabara hiyo itajengwa kwa muda wa Miezi 27 kwa kusimamiwa na kitengo maalumu cha ushauri wa Kihandisi ndani ya Wakala ya Barabara Tanzania-TANROADS (Tanroads Engineering Consulting Unit-TECU).

Amesema kuwa Mradi wa ujenzi wa barabara ya Kahama – Bulyanhulu Jct – Kakola (km 73) kwa kiwango cha lami ni moja ya mikakati ya serikali ya kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii Mkoani Shinyanga hususani Manispaa ya Kahama kwa kuboresha mtandao wa barabara ili kuongeza ufanisi katika sekta ya usafiri na usafirishaji.

Mhandisi Samweli amesema kuwa kwa sasa zoezi la kuhamisha miundombinu ya mawasiliano, maji na umeme iliyopo ndani ya eneo la ujenzi vinaendelea wakati mkandarasi anaendelea na zoezi la kuleta mitambo eneo la ujenzi.

Mkandarasi amefanikiwa kupata kambi yake iliyopo kilometa 10 kutoka eneo la Manzese-Kahama na tayari ameanza zoezi la kulisafisha kwaajili ya ujenzi wa kambi hiyo.

Aidha, Mkandarasi amefanikiwa kupata sehemu ya kujenga Ofisi za Mhandisi Mshauri na tararibu za uthaminishaji wa sehemu hiyo unaendelea kwa ajili ya kuidhinisha malipo.
Share:

DC MACHALI AZINDUA JENGO LA DAWATI LA JINSIA NA WATOTO WILAYANI MKALAMA

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Moses Machali amezindua jengo la Dawati la Jinsia na Watoto linalopatikina katika kituo kikuu cha polisi wilayani Mkalama ikiwa ni jihudi ya serikali katika kutokomeza ukatili wa kijinsia nchini Tanzania .

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa jengo hilo Juni 29,2024 amewataka wakazi wilayani Mkalama kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia wilayani Mkalama

“Kila mmoja ahakikishe anapambana kutoa taarifa kuhusu ukatili wa kijinsia kwenye mamlaka zinazohusika, tutumie Jeshi letu la polisi vizuri. Sisi sote tunapaswa kuwa mashujaa katika mapambano haya”, Mhe. Machali

Aidha Mhe. Moses Machali amewasisitiza wazazi Wilayani Mkalama kuwapeleka watoto wao shule ili waweze kutimiza ndoto zao za kimaisha na mzazi atakayekataa kumpeleka mtoto shule serikali itamchukulia hatua kali dhidi yake.

Kwa Mujibu wa taarifa ya Kamishina wa Kamisheni ya Polisi Jamii, CP Faustine Shilogile, amesema vitendo vya ukatili vimeongezeka nchini kwa mwaka 2023 kulinganisha na mwaka 2022 huku moja ya sababu ya kuongezeka kwa vitendo hivyo ni kutokana na uelewa mkubwa wa jamii katika kuripoti matukio ya ukatili kulinganisha na miaka ya nyuma.

“Kwa mwaka 2023 vitendo vya ukatili viongozeka hadi kufikia 22,147 kulinganisha na matukio 18,403 kwa mwaka 2022 kwa watu wazima na kwa upande wa watoto matukio yaliyoriptiwa ni 15,301 kulinganisha na 12,162 kwa mwaka 2022 “CP Faustine Shilogile

Naye Naibu Mwakilishi Mkazi UNWOMEN Ms Katherine Gifford amelipongeza Jeshi la Polisi nchini Tanzania na serikali kwa ujumla kwa kuwa mstari wa mbele katika kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia nchini.

Share:

Saturday 29 June 2024

WILAYA YA CHEMBA YAPATA BARAZA LA ARDHI NA NYUMBA TANGU KUANZISHWA KWAKE


Wananchi wa Wilaya ya Chemba Mkoani Dodoma  wanakwenda kutatuliwa Kero yao ya Muda mrefu ya kukosekana kwa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ambalo hutumika kutatua Migogoro mbalimbali ya Ardhi inayojitokeza.

Hayo yamebainishwa leo Juni 28, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary  Senyamule wakati akiwaapisha wajumbe Wanne wa Baraza hilo, hafla ambayo imefanyika katika ukumbi wa Ofisi yake Jengo la Mkapa Jijini Dodoma.

“Tangu kuanzishwa kwa Wilaya ya Chemba 2012, wananchi wake wamekuwa wakisafiri umbali mrefu kwenda katika Baraza la wilaya ya Kondoa kutafuta haki zao. Sasa wamepata baraza lao na kufanya Dodoma kuwa na jumla ya Mabaraza 6 hivyo, kero ya wananchi wa Chemba kutokua na Baraza la Ardhi na Nyumba inakwenda kutatuliwa” amesema Mhe. Senyamule

Mbali na hilo, Mkuu wa Mkoa amemtaka Katibu Tawala Mkoa pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi Mkoa, kusimamia mchakato wa kuhakikisha Wilaya ya Chamwino nayo inapata baraza la Ardhi na Nyumba hivyo kukamilisha Mabaraza yote saba katika Mkoa wa Dodoma kwani ndiyo pekee imesalia bila kuwa na Baraza hilo.

Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe. Gerald Mongella, ameishukuru Serikali kwa kuifanyia kazi kero hiyo.

 “Tumekua tukipambana na Migogoro mingi ya Ardhi hivyo baraza hili litatusaidia kupunguza kero hizo, Kupitia Baraza hili, haki itapatikana na amani itatamalaki kama ilivyo matamanio ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassani  kumaliza migogoro yote ya Ardhi Nchini”.

Naye, Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya ya Dodoma Bw. Omary Mbega, amesema kuwa jukumu kubwa la wajumbe hao ni kusaidia haki itendeke na kuwasihi kufuata maadili, kanuni na taratibu zinazoliongoza Baraza kwani ukiukwaji wake unaweza kupelekea kutenguliwa kwenye nafasi hiyo inayodumu kwa kipindi cha miaka mitatu tu.
Share:

Friday 28 June 2024

TAMWA ZNZ, IDARA YA MICHEZO WEMA, ZAFELA, GIZ NA CYD KUANDAA MTOTO WA AFRIKA MARATHON

 
Ni katika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika Zanzibar

CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kwa kushirikiana na Idara ya Michezo, Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Taasisi ya Maendeleo ya Mashirikiano ya Ujerumani (GIZ) na Kituo cha Mijadala kwa Vijana (CYD), inatarajia kuadhimisha ya siku ya kimataifa ya Mtoto wa Afrika tarehe 29 Juni 2024 kwa kuandaa mashindano ya riadha kwa wanafunzi wa skuli mbalimbali za Zanzibar.


Maadhimisho hayo yatawahusisha jumla ya washiriki 150 ambapo kati ya hao watakaoshiriki mashindano ni wanafunzi 75 kutoka katika skuli za Unguja ambazo zimeshajiandaa kushiriki mashindano hayo.


Tukio hili muhimu ambalo linalenga kuhamasisha usawa wa kijinsia katika michezo litawaleta pamoja wadau kutoka taasisi za kierikali na zisizokuwa za kiserikali ikiwemo wanafunzi kutoka skuli mbalimbali za Unguja, wanamichezo, walimu wa michezo, na wadau wote wa masuala ya usawa wa kijinsia.


Maadhimisho haya yanatoa fursa kwa wasichana kuonesha vipaji vyao na uwezo wao wa kushiriki katika michezo mbalimbali, pamoja na kujadili changamoto na vikwazo vinavyowazuia kushiriki katika michezo na kuhimiza uanzishwaji wa madawati ya jinsia katika taasisi za michezo.


Mashindano haya ya riadha yataanza saa 12 na nusu asubuhi, yakianzia maeneo ya Forodhani na yataishia katika viwanja vya Mnazi Mmoja Zanzibar yakishirikisha wanafunzi wa jinsia zote  kutoka skuli mbalimbali za Unguja.


Kaulimbiu ya wadau katika maadhimisho ya mwaka huu ni Wakati ni sasa! Wekeza katika elimu na michezo kwa watoto wote”. Tukio hili linatarajiwa kuleta mwamko na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kuwapa nafasi sawa watoto wote kushiriki katika michezo, bila kujali jinsia zao. Mashindano hayo yatatoa washindi watatu zaidi wanawake na watatu wanaume na kutambuliwa rasmi.  


Tunaamini kuwa michezo ni nyenzo muhimu ya kuleta usawa wa kijinsia na kuwawezesha watoto wa kike na wa kiume kujifunza stadi za maisha, kujenga ujasiri, na kushirikiana kwa amani na kuheshimiana.


Tunawaalika wanahabari, wazazi, walezi, na wananchi wote kujitokeza kwa wingi kushuhudia na kuunga mkono tukio hili la kihistoria katika kukuza usawa wa kijinsia na kuwawezesha watoto wote kufikia ndoto zao katika Nyanja mbali mbali bila vizuizi vyovyote.


Imetolewa na Idara ya mawasiliano,

TAMWA ZNZ.

info@tamwaznz.or.tz 

www.tamwaznz.or.tz 


Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger