Monday, 24 June 2024
Sunday, 23 June 2024
WATOTO NANE WABAKWA NA KULAWITIWA KWENYE KIBANDA CHA MIHOGO, RC TANGA ATOA KAULI NZITO
Na Hadija Bagasha Tanga
Watoto wanane wamebakwa na kulawitiwa baada ya kurubuniwa kwenye kibanda cha mihogo kilichopo karibu na shule yao katika Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga.
Mkuu wa Mkoa Tanga Balozi Dkt Batilda Burian amelaani kitendo hicho na kuagiza kufanyika kwa kura za siri ili kubaini watu wote wanaounga mkono vitendo hivyo wilayani humo.
Balozi Dkt. Burian amesema kitendo cha aina hiyo pia kimeripotiwa katika Wilaya ya Mkinga na kuitaka jamii kufunga kibwebwe kupambana na vitendo hivyo ambavyo vikiachwa vinaweza kuathiri viazazi vya sasa na vijacho.
Mkuu wa Mkoa ametoa maagizo hayo akiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Handeni na Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Mji Mkoani Tanga wakati wa kikao maalumu cha baraza la madiwani la kupokea taarifa za mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali CAG kwa mwaka wa fedha 2022/23 ambapo Halmashauri hizo zilipata hati safi.
Balozi Dkt. Burian amesema kuwa iwapo uchunguzi utafanyika na akapatikana mtu yeyote awe mwalimu au kiongozi wa dini yeyote hawatamuacha mtu kwani vitendo hivyo vimekuwa vikidhoofisha nguvu kazi ya Taifa.
"Watoto wadogo wanane wamebakwa na kulawitiwa watu wazima wameanzisha kigenge kumbe kile kigenge ni cha makusudi cha danganya toto, kumbe wana shughuli zao nyingine watoto wakienda wanadanganywa na mihogo ya kukaanga wanaenda wanawadhulumu watoto wadogo wa kike wa miaka 8, 9 mpaka 10 huyo wa mwisho alienda akapatwa na changamoto ya kutokwa na damu nyingi kwa kuwa alikuwa ni mdogo ndio watu wakajua, "alisema Balozi Dkt Burian.
"Nauliza jamani Handeni hili suala halijawachukiza mmekaa kimya nilifikiri mtaenda pale kwa hasira mkiwa mmefunga vibwebwe watoto wamefanyiwa ukatili au mnataka watu wa Mwanza ndio waje na vibwebwe na maandamano kuwasemea nyinyi watu wa Handeni?sisi tunakiona ni kitu poa na sio kwenu tu Handeni Mkinga pia nimekuta kadhia hii mtoto wa miaka mitatu wa kike amebakwa na kulawitiwa hivi huyo mtoto amekosa nini na ana dhambi gani? , Alihoji RC Batilda.
"Kwa kweli mimi nimesema hili jambo tutahangaika nalo na hawa watu tutahangaika nao na wanasheria wanaisimamia hiyo kesi lazima hukumu ipatikane na iwe fundisho na tutaanza kura za siri kutaja walawiti, wabakaji wa watoto wa kike na wakiume mashuleni huko ipite kura ya siri na wataalamu wanajua nani anaonewa na anayefanya kweli tushirikiane tukikaa kimya hata sisi tutakuwa hatujawatendea haki wanahandeni, "alisisitiza Balozi Dkt Batilda.
"Niwaombe sana sana hili jambo lituume na tulichukie sana hata iwe ni baba mzazi, iwe ni mlezi, kaka au mjomba tulichukie hilo jambo mjmi nasema kuna watu wana agenda yao mataifa ya nje wameshahalisha hilo jambo kwao wanajaribu sasa kutafuta kwa njia ya nyuma kuwafundisha watu na kuwalipa wakiwa wanalenga kizazi kijacho, "alisema Balozi Burian.
Aidha Balozi Dkt Batilda amefafanua kwamba endapo mtoto ataingiliwa kinyume na maumbile atakuwa amepoteza sifa ya kujiunga na majeshi yote nchini jambo ambalo linapaswa kupigwa vita ili kuweza kupata makomando watakaokwenda kupigana maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Sambamba na hayo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Handeni Mji Mussa Mkombati amekiri kweli kuwepo kwa suala hilo na kueleza kuwa suala hilo wanalishughulikia ipasavyo hadi kufikia kutoa ahadi ya zawadi kwa atakayefanikisha kukamatwa kwa mtu anayehusika na ubakaji na ulawiti.
"Tunapofanikiwa kumkamata mbakaji au mlawiti tunakosa ushirikiano kutoka kwa jamii kwa maana suala likishakuwa polisi na kutakiwa kwenda mahakamani jamii husika wanalitoa suala hilo nje ya sheria na kulipeleka nyumbani jambo ambalo linatukwamisha katik mapambano yetu, "alisisitiza Mwenyekiti Mkombati.
"Bado hayujakata tamaa tunaendelea kupambana kuhakikisha waliohusika na matukio haya sheria inachukua mkondo wake na wanapata adhabu stahiki ikiwa ni pamoja na kuendelea kupambana na wabakaji na walawiti kwa kujnda kamati za kuchunguza wanaotekeleza vitendo hivyo nje na ndani katika shule zote za wilaya hiyo, "alisema Mkombati.
Tukio la wanafunzi wanane kubakwa na kulawitiwa Wilayani Handeni Mkoani Tanga lilifanyika mwanzoni mwa mwezi june mwaka huu ambapo walibaini matendo hayo baada ya binti wa miaka 8 aliyebakwa kwa mara ya mwisho kupata changamoto ya damu na kuwataja wenzake waliokuwa wakifanyiwa vitendo hivyo.
DC MKUDE AHAMASISHA WANANCHI KISHAPU KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Joseph Modest Mkude amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi la undikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura pamoja na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024,
Mhe. Mkude ameyasema hayo leo Tarehe 21 Juni 2024 alipokuwa akifunga Mashindano ya Mpira ligi ya kata ya Ukenyenge.
"Ninashukuru sana kwa kunialika kuja kufunga Mashindano haya ya ligi ya Kata ya Kunyenge kwa kuwa mimi ni Mwanamichezo ninayofuraha sana kuzipongeza timu zilizoingia Fainali timu ya Bulimba na Timu ya Wila ninawatakia Mchezo Mwema wenye ushindani mzuri, Pia nitumie fursa hii Kuwahimiza wananchi kujitokeza kwa Wingi pindi utakapoanza Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura na kushiriki kimalifu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 kwani ni haki ya kila mtu kumchagua kiongozi anayeona anafaa. Alisema Mkude.
Kwa Upande wake Diwani wa Kata ya Ukenyenge Mhe. Underson Mandia amezipongeza timu zote zilizofika fainaili kwani mashindano hayo waliyaanzisha kwa lengo la kuhamasisha Wananchi kuutambua Mchakato wa Uchaguzi ili waweze kushiriki kikamilifu katika zoezi Uchaguzi 2024.
Naye Katibu Tarafa wa Kata ya Negezi Bw, Omary Mwenda amesema mashindano hayo yana tija kubwa Sana katika kuhamasisha wanachi kushiriki kikamilifu katika uandikishaji wa Daftari la kudumu la wapiga kura na kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na kuahidi kufanya mashindano hayo kila kata ndani ya Tarafa ya Negezi
Aidha katika Mashindano hayo timu ya Wila iliibuka Mshindi kwa kuiadhibu timu ya Bulimba gori moja ambalo lilifungwa na Mshambuliaji Anthony Masunga.
Saturday, 22 June 2024
TUONE UMUHIMU WA KUCHANGIA DAMU HAKUNA MBADALA WAKE
John Francis Haule
Kila ifikapo Juni 14 dunia huadhimisha siku ya mchangia damu. Katika siku hii hamasa huwa kubwa zaidi lakini ukweli ni kwamba suala la uchangiaji wa damu halina siku maalumu kutokana na umuhimu wake.
Nasema hivi kwa sababu hakuna mbadala wa damu inahitajika kila siku.Damu ni tiba muhimu kwa afya ya mwanadamu na ni damu ya binadamu pekee ndio inayotumika.
Kutokana na umuhimu huo, tuna kila sababu kuhakikisha wakati wote inapatikana na upatikanaji wake ni lazima tujitoe kwa kuwa damu hainunuliwi wala haitengenezwi maabara kama ilivyo dawa nyingine.
Damu mahitaji yake ni makubwa sana na upatikanaji wake ni waasili maana kwamba hakuna kiwanda kinacho chakata damu, ni sisi binadamu tunapaswa kushiriki tendo hili la huruma la kuchangia damu kwa hiari.
Matumizi ya damu nchini ni makubwa kwa akina mama wajawazito wanaopoteza damu wakati wa kujifungua, watoto wenye umri chini ya miaka 5, wahanga wa ajali za barabarani na wagonjwa wa saratani.
Tunafahamu kila uchao zinatokea ajali za barabarani ambazo zinaacha majeruhi wanaohitaji damu, ili kuokoa maisha yao ni lazima tuwe na akiba ya kutosha kwenye benki za damu katika hospitali zetu.
Tunaambiwa kuwa upungufu wa damu unaweza pia kugharimu maisha ya mjamzito na kiumbe kilichopo tumboni mwake. Hii ina maana kuwa mchakato wa kuleta uhai wa mtu mwingine damu ina umuhimu mkubwa.
Takwimu zinaonesha takribani asilimia 19 ya wanawake wajawazito wanapoteza maisha wakati wa kujifungua kutokana na kuvuja damu nyingi.
Hivyo kila mwananchi mwenye afya njema ni muhimu akajitolea kuchangia damu ili kuhakikisha akiba ya damu inadumishwa ili kuokoa maisha ya watu wenye uhitaji hasa katika kuunga mkono ajenda ya kupunguza vifo vya wajawazito nchini Tanzania.
Kutokana na changamoto hiyo ni muhimu benki za damu katika hospitali zote nchini kuwa na damu ya kutosha ili kukabiliana na dharura za aina hiyo zinapojitokeza.
Swali linakuja benki za damu zinatoa wapi ilhali tumekubaliana kuwa hakuna kiwanda wala mtambo wa kuzalisha damu, jibu ni kwamba ni lazima tuwe na utaratibu wa kudumu wa kujitolea damu.
Usilazimike kuchangia damu kwa sababu kuna ndugu yako au mtu wako wa karibu amelazwa hospitali, jenga utamaduni huu kwa kuwa damu yako inaweza kuokoa maisha ya mtu mwingine kabisa.
Kwa umuhimu huo nimeona kuna haja ya kutumia ushawishi wangu na watu wanaonizunguka katika mazingira yangu ya kazi kuhamasisha uchangiaji damu wa hiari na kuwajengea Watanzania desturi hii ambayo ina maana kubwa kwa Mungu.
Pia nishauri wale tuliopewa dhamana ya kuongoza ama kusimamia maeneo yenye mkusanyiko wa watu wengi tutumie hio fursa kuhamasisha jamii kuwa na desturi ya kuchangia damu, mfano vyuoni,kwenye makongamano ya dini.
Kila mchango wa damu ni zawadi ya thamani inayookoa uhai na uchangiaji wa kurudia ndio ufunguo wa kujenga usambazaji wa damu salama na endelevu.
Mwandishi wa Makala hii John Francis Haule (Mkuu wa soko kuu la Arusha anapatikana kwa simu namba 0711 993 907 au 0756717987
DAWASA YASHINDA TUZO KINARA UTOAJI TAARIFA KWA UMMA
Afisa Mawasiliano wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) Ndugu Nelson Shoo (wa pili kulia) akipokea tuzo kutoka kwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye Waziri baada ya Mamlaka kuibuka kinara katika utoaji wa taarifa kwa umma miongoni Mwa Mamlaka za Maji Nchini.
Tuzo hii imetolewa na Mhe. Waziri Nape wakati wa kikao kazi cha Maafisa Habari Serikalini kilichokuwa na kauli mbiu "Jenga Mustakabali endelevu kwenye Sekta ya Habari katika zama za kidijitali".
Friday, 21 June 2024
NSSF YAANZA KUWAONDOA WADAIWA SUGU KATIKA NYUMBA ZAKE
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeanza zoezi la kuwaondoa wadaiwa sugu walioshindwa kutekeleza matakwa ya mkataba wa ununuzi wa nyumba katika miradi yake ya Dar es Salaam. Zoezi la kuwaondoa wadaiwa sugu hao lilifanyika tarehe 18 Juni 2024 katika mradi wa nyumba za Kijichi, Temeke.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Meneja Miliki wa NSSF, Geofrey Timoth amesema zoezi la kuwaondoa wadaiwa sugu walioshindwa kulipa madeni yao ya muda mrefu katika nyumba za NSSF ni endelevu katika miradi yote.
Timoth amesema kuwa NSSF ilitoa notisi ya siku 30 na baadaye ilitoa siku 14 ya kuwataka wadaiwa hao kulipa madeni yao lakini hawakulipa, hivyo baada ya kujiridhisha na kufanya tathimini, NSSF ilifanya maamuzi ya kuwatoa wadaiwa sugu katika nyumba zake ili kutoa fursa kwa wananchi wengine kununua nyumba hizo kwa utaratibu wa mpangaji mnunuzi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Changanyikeni, Dionisia Kamugisha, ametoa wito kwa wananchi wa mtaa huo walionunua nyumba za NSSF kulipa madeni yao wanayodaiwa ili kuepuka adha ya kuondolewa katika nyumba hizo.