Sunday, 16 June 2024
WALIOVAMIA ENEO LA NSSF KUANZA KUONDOLEWA
Na MWANDISHI WETU
Dar es Salaam. Hatimaye waliovamia ardhi ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na kuanza kujenga makazi katika Mtaa wa Malela Kata ya Toangoma, Temeke Dar es Salaam wataanza kuondolewa rasmi katika maeneo hayo kuanzia tarehe 18 Juni 2024.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Jerry Silaa aliyoyatoa Juni 5, mwaka huu, wakati alipofika eneo hilo na kuwakamata watuhumiwa wanne wanaodaiwa kuwatapeli wananchi kwa kuwauzia maeneo yanayomilikiwa kihalali na NSSF, ambapo aliagiza wavamizi wote wa ardhi kuondolewa.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Sixtus Mapunda tarehe 15 Juni 2024 amefika eneo hilo kuendelea kutilia msisitizo wa namna ambavyo NSSF itatekeleza maelekezo yake ya kuwaondoa waliovamia maeneo ya miundo mbinu ya barabara na maji.
Mhe. Mapunda amesema eneo la Malela historia inaonesha kuwa kati ya mwaka 2000 na 2002 Serikali ilichukua eneo hilo kupitia Wizara ya Ardhi na ikawalipa fidia wakazi wote wa asili na kuwa mwaka 2005 mpaka 2008 Wizara ya Ardhi ilikuwa inayagawa kwa kuyauza maeneo hayo kwa watu binafsi na Mashirika ikiwemo NSSF ambayo iliuziwa eneo hilo na walipewa hatimiliki.
Amebainisha kuwa kati ya mwaka 2012 na 2017 kwa nyakati tofauti, wananchi walianza kuvamia eneo hilo na kuwa kati ya mwaka 2020 na 2022 uliitishwa mkutano wa wavamizi baina ya NSSF na uongozi wa Serikali ambapo katika kueleweshana ikaonekana si busara waliovamia kipindi hicho kuondolewa hivyo wakakubaliana kuwa waliovamia waingizwe kwenye mpango wa matumizi ya ardhi na NSSF.
"Baada ya hapo yakawekwa makubaliano kuwa walioingizwa kwenye mpango na NSSF washirikiane na Mfuko wasiwepo watu wengine watakaovamia, lakini kilichotokea kati ya mwaka 2002, 2003 na 2004 waliovamia walikuwa wengi kuliko wale waliokuwepo mwanzoni," amesema Mhe. Mapunda.
Amesisitiza kuwa, waliokuwepo kwenye mpango wa matumizi ya ardhi ambao ni takribani 145 walishaongea na NSSF na tayari walishakubaliana.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, Meneja Milki wa NSSF, Bw. Geofrey Timoth amesema katika kutekeleza maelekezo hayo ya Waziri wa Ardhi, NSSF inatarajia kuondoa nyumba zote ambazo zipo kwenye barabara na miundo mbinu ya maji pamoja na kuhakiki watu wachache ambao wanadai walikuwepo tokea mwaka 2021/22.
Bw. Timoth amesema zoezi hilo ni muendelezo wa utekelezaji wa maelekezo ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, aliyotoa wiki iliyopita.
Amebainisha namna ambavyo NSSF wanaenda kutekeleza maelekezo ya Waziri wa Ardhi ni kuwa bà adhi ya maendelezo yaliyofanywa ambayo waliyabaini mwaka 2021 na 2022 wamekubaliana kuwa watakaa na wahusika kwa sababu yapo kwenye mpango wa ardhi.
"Kwa hiyo tutakaa na wahusika na tutawaambia ni nini cha kufanya ili waendelee kuwa na amani kwenye maeneo husika," amebainisha Timoth.
Saturday, 15 June 2024
BODI YA TAWA KUJA NA MIKAKATI KABAMBE YA KUIBORESHA HIFADHI YA PANDE
Na Beatus Maganja, Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA Mej. Jen. (Mstaafu) Hamis Semfuko amesema Bodi anayooingoza imejipanga kuja na mipango madhubuti ya kuifanya Hifadhi ya Pande iliyopo Jijini Dar es Salaam kuwa kivutio kikubwa kwa watu waishio ndani na nje ya Jiji hilo.
Katika hatua nyingine amebainisha mikakati ya kuendelea kuboresha miundombinu ya hifadhi hiyo sambamba na kuongeza aina mbalimbali za vivutio vya utalii ikiwemo wanyamapori aina ya twiga na faru lakini pia kuongeza kasi ya kuitangaza hifadhi hiyo ambapo amesema hivi karibuni TAWA imekuwa ikiwatumia wasanii wa "Bongo Movie" katika kusaidia kutangaza hifadhi ya Pande.
Aidha ametoa wito kwa wawekezaji wote nchini kuchangamkia fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo hifadhini humo kama vile ujenzi wa kumbi za mikutano, sehemu za kuchezea watoto na "eco lodge" huku akisisitiza fursa bado zipo.
Naye Prof. Suzanne Augustino mjumbe wa Bodi ya TAWA amesema kwa kuhifadhi Pori la Akiba Pande TAWA inaunga mkono juhudi za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye amekuwa akihamasisha utalii nchini na amewataka watanzania wote wanaoshindwa kwenda kutalii katika hifadhi zingine kutokana na umbali watembelee hifadhi ya Pande ili kujionea vivutio vilivyopo.
Awali akitoa taarifa ya utendaji wa Kanda, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ya TAWA Sylvester Mushi amesema kutokana na umakini wa kikosi cha Askari wa mbwa na kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, wamefanikiwa kudhibiti utoroshaji wa nyara za Serikali uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere ( JNIA ).
Aidha nyara nyingine ni wadudu aina ya nge 383, wadudu aina ya "Beatle" 261, Kobe hai 7, vichwa vya fisi 10, vichwa vya pimbi 3 na vichwa vya ndege aina ya Korongo 3 na bunduki 2 ambazo zilikamatwa Pori la Akiba Wami Mbiki
Kwa upande wake Kamanda wa Pori la Akiba Pande Dorothy Massawe ameishukuru Mamlaka kwa kuboresha miundombinu ya utalii ambapo amekiri kuwa imekuwa chachu ya ongezeko la mapato na idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi hiyo
MAJALIWA AMKARIBISHA ZUHURA YUNUS OFISI YA WAZIRI MKUU
Friday, 14 June 2024
WANAHARAKATI WA JINSIA NA MAENDELEO WAICHAMBUA BAJETI YA MWAKA 2024/2025 KWENYE MLENGO WA JINSIA
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
WANAHARAKATI wa Jinsia na Maendeleo kupitia Mtandao wa Jinsia Tanzania- TGNP, wameishukuru Serikali kulifanyia kazi suala la kikokotoo ambacho kimeongezwa kutoka asilimia 33 hadi asilimia 40 ambapo kinatarajiwa kurejesha ahueni kwa wastaafu.
Akizungumza leo Juni 13,2024 Jijini Dar es salaam katika kijiwe cha kahawa kilichoandaliwa na TGNP -Mtandao kwa lengo la kufatilia bajeti iliyopitishwa ya mwaka 2024/2025, Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi amesema licha ya serikali kuyafanyia kazi baadhi ya maeneo ambayo yamekuwa yakionekana yanachangamoto, kuna maeneo mengine bado hayafanyiwa kazi.
Amesema wanatamani kuona mradi wa SGR pamoja na mradi wa bwawa la kuzalisha umeme ikisaidia watu wote katika kujiendeleza kiuchumi yakiwemo makundi ya pembezoni kufaidika kwa kusafirisha mazao yao na kupata usafiri kwa urahisi ili waweze kujiendeleza kiuchumi.
"Tunavyozungumzia mageuzi ya kiuchumi,tuone sasa yale makundi ya pembezoni wale watu ambao hawana uwezo wanawake,wanaume maskini na vijana wakiweza kufaidika kusafirisha mazao yao kupata usafiri kwa urahisi ili waweze kujiendeleza kiuchumi" amesema Lilian.
Aidha ameonesha shahuku yake kuhusiana na kuimarika kwa umeme nchini ambapo anatarajia kuona wanawake na vijana wakikuza uchumi wao kwani umeme ni kichocheo cha ukuaji wa uchumi.
"Uchambuzi unahitajika kwa hii rasilimali iliyo wekezwa ambayo tunajua ndio maana deni letu la taifa linakua tuone sasa ina tija katika taifa letu" amesema.
Kwa Upande wake, Afisa wa Shirika la Wanawake katika Jitihada za Kimendeleo (WAJIK) Janeth Mawinza amedai kuwa bajeti hiyo imewarudisha nyuma kama wanaharakati kwenda kujiandaa tena kwa sababu walivyoshauri havikubebwa kama walivyopendekeza hasa kuhusiana na suala la mlengo wa kijinsia pamoja na kulenga makundi maalumu.
"Tunatamani kama vyombo vyenye mamlaka vinaweza kufikiria na kujadili zaidi suala zima la elimu, tulitegemea tuone bajeti inasema elimu bure inaenda kupata nafasi ,watoto hawatakuwa na michango shuleni" amesema
Naye,Mdau wa masuala ya kijinsia, Mophat Mapunda amepongeza kurudishwa kodi za ardhi na majengo katika mamlaka za halmashauri ambapo itazisaidia kujitanua kimapato katika vyanzo vya ndani na kuchochea maendeleo.
Thursday, 13 June 2024
SHULE YA SEKONDARI YA UFUNDI MTWARA YAOKOA MAMILIONI YA FEDHA, MATUMIZI YA GESI ASILIA
BILIONI 136.2 ZIMETUMIKA UREJESHAJI WA MIUNDOMBINU BARABARA NA MADARAJA
Na Mwandishi wetu,Dodoma
Serikali imetoa jumla ya Shilingi Bilioni 136.2 kupitia Wakala ya Barabara (TANROADS) na Wakala ya Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA), kwa ajili ya kurejesha hali ya awali ya miundombinu ya barabara na madaraja yaliyoharibiwa kwa kiasi kikubwa na janga la mvua za El Nino.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba Bungeni jijini Dodoma Mei 13, 2024 wakati akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali 2024/2025.
Dkt. Mwigulu amewahakikishia Watanzania kuwa Serikali itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya kugharamia ukarabati wa miundombinu iliyoharibiwa.
Dkt. Mwigulu amezielekeza Taasisi zote zinazohusika na ujenzi wa miundombinu kuhakikisha zinafanya usanifu wa miradi kwa kuzingatia mabadiliko ya tabianchi.
Ameeleza kufuatia mvua za El-Nino zilizonyesha nchini kuanzia Septemba, 2023 pamoja na kimbunga Hidaya, barabara mbalimbali za kitaifa katika mikoa 26 zimeathirika ambapo barabara 68 zilikuwa zimejifunga, barabara 106 zilikuwa zinapitika kwa shida na barabara 168 ziliathirika lakini zinaendelea kupitika kwa shida baada ya kufanyiwa matengenezo ya dharura.
“Maeneo yaliyoathirika katika barabara hizo yanakadiriwa kufikia kilometa 520 na kwa upande wa madaraja na makalavati yapatayo 189 yalikuwa yamekatika na mengine kuharibika vibaya”, ameeleza Dkt. Mwigulu.
Aidha, Dkt. Mwigulu ameongeza kuwa tathmini iliyofanyika inaonesha gharama za kurejesha miundombinu hiyo ni shilingi trilioni 1.07 ambapo kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 728 ni kwa ajili ya kufanya matengenezo ya kurejesha miundombinu ya barabara ili zirudi katika hali yake ya awali na shilingi bilioni 158 ni kwa ajili ya matengenezo ya dharura ili barabara hizo ziweze kupitika.
Amefafanua kuwa shilingi bilioni 184.14 ni kwa ajili kurejesha miundombinu iliyoathiriwa na kimbunga Hidaya.