SHIRIKA la Grumeti Fund kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii imewaleta pamoja Wanafunzi wa kike 704 na wakiume 634 kutoka katika shule za Tirina,Chamriho na Hunyari Wilayani Bunda, kwa lengo la kutoa Elimu sambamba na kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili watoto wa kike na kiume ili kujenga jamii yenye usawa na yenye kujitambua kwa vijana wa jinsia zote.
"Kutokana na utafiti tulioufanya juu ya uchache wa watoto wa kike katika kuchangamkia fursa za kimasomo zinazotolewa na Grumeti Fund, moja ya njia za kutatua changamoto hii ni kufanya makongamano kwa nia ya kutoa elimu kwa mabinti, kwanza wafahamu thamani yao na pili wafahamu kwamba wanaweza kuwa mtu yeyote watakae katika maisha yao na kukataa kukatishwa tamaa na mtu yeyote. Nataka mfahamu kwamba mnaweza"
Aidha, Bi. Frida amewataka wasichana hao kutokata tamaa kwa changamoto mbalimbali zinazowakabili bali watumia elimu wanayoipata ili iweze kuleta tija na mabadiliko chanya katika jamii na kusisitiza kuwa elimu ndio dira na njia ya kufikia ndoto za vijana hao.
Katika kongamano hilo shirika la Grumeti Fund imetoa msaada wa taulo za kike zinazoweza kutumika kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu (reusable pads) kwa wanafunzi wa kike 704 zenye thamani ya Shilingi Milioni tisa laki nane na elfu hamsini na sita (9,856,000) katika shule za sekondari Tirina,Chamriho na Hunyari
Naye mgeni rasmi katika katika kongamano hilo, Neema Paul ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya wilaya ya Serengeti amewataka wasichana kuzingatia nidhamu sambamba na kuweka malengo katika masomo yao ili waweze kufanikiwa huku akiwataka kutokata tamaa katika masomo yao
"Mwanafunzi yeyote yule unatakiwa kuwa na malengo,hujaja shuleni kutembea Wala kukua weka malengo kuwa unataka kuwa nani na hakikisha unapambania malengo yako kwa kuweka mikakati sahihi", alisema Bi. Neema.
Kwa upande wake mkufunzi kutoka chuo cha Afya Kisare Mwl. Restuda Murutta amewaasa wanafunzi hao kuzingatia elimu ya afya ya uzazi sambamba na kuepuka vishawishi vitakavyo waingiza katika kufanya mapenzi katika umri mdogo na mwisho kupelekea ndoa za utotoni.
“Inasikitisha binti ana umri chini ya miaka 18 ameshaanza kujiingiza kwenye mahusiano ya ngono kitu ambacho sio salama, kabla ya kuingia kwenye mambo hayo kwanza jiulize je ni umri sahihi wa kuingia kwenye Mambo hayo ukishapata jibu acha" alisema Bi. Restuda.
Nao miongoni mwa wanafunzi waliopata mafunzo hayo ameishukuru kampuni ya Grumeti Fund kwa namna wanavyowajali na kuwathamini mabinti na kuahidi kuyaweka katika vitendo mafunzo hayo na kusambaza elimu kwa wengine.
Awali kongamano hili lilitanguliwa na kongamano la vijana wa kiume takribani 634 kutoka shule za Sekondari Tirina,Chamriho na Hunyari ambapo Bi. Frida Mollel Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya jamii kutoka Grumeti Fund amesema baada ya jamii kuwekeza nguvu kubwa katika kutoa Elimu kwa watoto wa kike imefanya watoto wa kiume kusahaulika ndipo Grumeti Fund katika kuleta usawa katika hilo ikaamua kuanzisha makongamano kwa watoto wa kiume ili kujenga jamii shirikishi na yenye usawa na kawaasa vijana kutokuiga tabia na tamaduni za kigeni zinazoweza kuharibu kabisa thamani yao na maisha yao kwa ujumla sambamba na kushiriki katika kutokomeza Mila na desturi kandamizi kwa watoto wa kike.
Naye aliyekuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo Ndg. January Kizumba ambaye ni Afisa Elimu Sekondari kwa upande wa taaluma kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bunda akawataka vijana wa kiume kusisitiza usawa katika jamii sambamba na kuwekeza nguvu katika masomo yao ili kuleta mapinduzi katika jamii.
"Nyie ndio kizazi cha kesho hivyo tunatarajia,ili tuwe na jamii yenye usawa ni lazima tuwaelimishe pande zote mbili ili muwe na uelewa juu ya Mambo yakijisia maana yake tutajenga jamii endelevu na yenye usawa" ,alisema Kizumba.