Friday, 19 January 2024

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA MABORESHO YA KANUNI ZA MADALALI

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda akizungumza wakati wizara yake ilipowasilisha Taarifa ya Marekebisho ya Kanuni za Madalali mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo tarehe 19 Januari 2024 jijini Dodoma.

**********************

Na Munir Shemweta, WANMM

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo imeipongeza Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika Marekebisho ya Kanuni za Uteuzi, Malipo na Nidhamu kwa Madalali wa Baraza na Wasambaza Nyaraka za mwaka 2023 katika Sheria ya Mahakama za Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi Sura ya 216.

Akizungumza wakati wa wasilisho la Taarifa ya marekebisho hayo tarehe 19 Januari 2024 jijini Dodoma, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Ramadhani Suleiman Ramadhani amesema, wizara hiyo imezingatia mapendekezo ya Kamati katika kufanya maboresho na kamati yake haina budi kuipongeza Wizara ya Ardhi kwa kazi nzuri.

‘’Wizara imezingatia mapendekezo ya Kamati hivyo niwapongeze kwa kazi nzuri ya kufanya marekebisho yaliyozingatia maoni ya Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo ‘’ alisema Mhe. Ramadhani.

Mjumbe wa Kamati hiyo ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu mkoani Mtwara Yahya Mhata amesema, maboresho yaliyofanyika yanonesha jinsi gani Wizara ya Ardhi ilivyo jipanga na kutoa pongeza kwa wizara hasa Katibu Mkuu wa wizara hiyo aliyemueleza kuwa ndiye Mtendaji Mkuu.

‘’Wizara iko ‘smart’ napenda niishukuru na kuipa pongezi kwa maboresho ya Kanuni za Madalali na zaidi nimpongeze Mtendaji Mkuu wa wizara’’ alisema Yahya.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sheria Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Method Msokele aliwaeleza wajumbe wa kamati kuwa, Kanuni zilizofanyiwa marekebisho zitajulikana kama Kanuni za Marekebisho ya Kanuni za Uteuzi, Malipo na Nidhamu kwa Madalali wa Baraza na Wasambaza Nyaraka za mwaka 2023.

‘’Kanuni hizi zitasomwa pamoja na Kanuni za Uteuzi, Malipo na Nidhamu kwa Madalali wa Baraza na Wasambaza Nyaraka za mwaka 2023 ambapo hapa zitarejewa kama Kanuni Kuu’’. Alisema Msokele.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda aliishukuru Kamati kwa ushauri wake wakati wa kufanya marekebisho ya kanuni za Madalali na kuahidi wizara kusimama katika mhimili wakati wa kutekeleza majukumu yake.

‘’Niwashukuru sana wajumbe wa Kamati hii, mmetupa ushirikiano wakati wote wa maboresho ya Kanuni za Madalali na niwaahidi Wizara yangu itasimama katika mhimili wakati wote wa kutekeleza majukumu yake’’ alisema Mhe. Pinda
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sheria Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Method Msokele akiwasilisha taarifa ya Marekebisho ya Kanuni za Madalali mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo tarehe 19 Januari 2024 jijini Dodoma.
Sehemu ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo wakifuatilia uwasilishaji Taarifa ya Marekebisho ya Kanuni za Madalali tarehe 19 Jnuari 2024 jijini Dodoma.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo Mhe. Ramadhani Suleiman Ramadhani (Kushoto) akizungumza wakati wa wasilisho la Taarifa ya Marekebisho ya Kanuni za Madalali tarehe 19 Jnuari 2024 jijini Dodoma. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
Share:

TANESCO DODOMA YATOA SEMINA KWA MADIWANI HALMASHAURI YA JIJI LA DODOMA


Madiwani wa kata zote 41 za jijini Dodoma wakifatilia Mkutano ulioandaliwa na Shirika la Umeme (TANESCO) Mkoa wa Dodoma.

Na.Mwandishi Wetu-DODOMA

SHIRIKA la Umeme (TANESCO) Mkoa wa Dodoma limetoa semina kwa madiwani wa kata zote 41 za jiji la Dodoma lengo likiwa ni kueleza mikakati ya shirika hilo pamoja na miradi inayotekelezwa katika mkoa wa Dodoma.

Akitoa elimu leo Januari 18, 2024 jijini Dodoma, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Dodoma Mhandisi Donasiano Shamba amesema kikao hicho kimejumuisha Madiwani, kamati ya ulinzi na Usalama Wilaya na Polisi kata wa halmashauri ya jiji la Dodoma.

“Kikao hiki kimehusisha madiwani kutoka kata zote 41 za jiji la Dodoma pamoja na Polisi kata lengo ni kueleza mikakati yetu lakini pia kueleza changamoto zinazotukabili sisi kama shirika hasa suala la uharibifu wa miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme”amesema Mhandisi Shamba

Aidha Mhandisi Shamba amesema kwa kuwashirikisha madiwani hao kwenye kikao hicho watakuwa wamewafikia watu zaidi ya 700,000 wa halmashauri ya jiji la Dodoma.

Mhandisi Shamba ameeleza kuwa Dodoma hakuna uhaba wa umeme bali shida iliyopo ni ubovu wa miundombinu ambayo inachangia kukatika kwa umeme mara kwa mara.

Ameelezea kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/24 Shirika la Umeme (TANESCO) mkoa wa Dodoma, limetengewa kiasi cha Sh. bilioni 14, kwa ajili ya kupeleka nishati hiyo kwa wananchi na kukarabati miundombinu ili kumaliza tatizo la kukatika kwa umeme.

“Katika mwaka huu wa fedha tumepatiwa kiasi cha Sh. bilioni 14 na kati ya hizo bilioni sita ni kwa ajili ya kuboresha miundombinu yetu na kiasi kingine ni kwa ajili ya kupeleka umeme maeneo ya karibu na wananchi.” Amesema Mhandisi Shamba

Awali Afisa Usalama wa TANESCO mkoa wa Dodoma Bw. Madega Dudu, amesema shida inayowakabili hivi sasa ni pamoja na uharibifu wa miundombinu ya kusafirishia na kusambazia umeme.

"Hivi sasa kumekuwepo na shida ya wizi wa vyuma kwenye miundombinu ya kusafirishia (Grid) umeme, mafuta ya transfoma, nyaya za kopa pamoja na miundombinu ya usalama kwenye mashine umba (Transfoma).

“Tunaomba wananchi kutoa taarifa dhidi ya watu hawa ambao wanajihusisha na uharibifu wa miundombinu hii, tafiti zinaonyesha mafuta ya transfoma wanayoiba kwa kiasi yanachanganywa na mafuta ya kukaangia chipsi lakini pia mikoa ya kanda ya ziwa na bahari yanatumika kukaangia samaki.

“Na wengine wanayatumia kwa ajili ya vipodozi na kiasi kikubwa yanatumika kutengenezea vilainishi vya mitambo.” Amesema Dudu.

Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Prof. Davis Mwamfupe ,ameipongeza TANESCO Mkoa wa Dodoma kwa kuboresha huduma ya nishati katika mkoa huo na kuendelea kuwafikia wateja kwa wakati pindi inapotokea changamoto yoyote.

"Sisi kama Madiwani tunawapongeza TANESCO Mkoa wa Dodoma kwa kuendelea kutoa huduma bora ya nishati Mkoa wa Dodoma hakuna changamoto kubwa ya umeme hata inapotokea mnatatua kwa wakati na kuwafikia wateja wenu kwa wakati kwa hilo tunawapongeza sana." Amesema Prof.Mwamfupe.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Dodoma Ndugu Charles Mamba aliyekuwa mgeni rasmi akifunga semina hiyo amewataka madiwani kwenda kuwa mabalozi wazuri katika kusimamia miundombimu ya umeme kwa kutoa Elimu kwa wananchi wa maeneo Yao.

"Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ikiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania DKt.Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwajali wananchi wake kwa kuwaletea huduma Bora za Nishati na kwa mikakati ya TANESCO hapa Makao Makuu ya nchi, shida ya umeme inaenda kuwa historia." Amesema Ndg Mamba


Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Dodoma Mjini Ndugu Charles Mamba,akizungumza wakati akifungua Mkutano wa Madiwani, kamati ya ulinzi na Usalama Wilaya na Polisi kata wa halmashauri ya jiji la Dodoma ulioandaliwa na Shirika la Umeme (TANESCO) Mkoa wa Dodoma leo Januari 18,2024 jijini Dodoma.


Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Prof. Davis Mwamfupe,akizungumza wakati wa Mkutano wa Madiwani, kamati ya ulinzi na Usalama Wilaya na Polisi kata wa halmashauri ya jiji la Dodoma ulioandaliwa na Shirika la Umeme (TANESCO) Mkoa wa Dodoma leo Januari 18,2024 jijini Dodoma.


Meneja wa Shirika la Umeme (TANESCO) Mkoa wa Dodoma Mhandisi Donasiano Shamba,akiwasilisha taarifa ya TANESCO halmashauri ya jiji la Dodoma wakati wa Mkutano wa Madiwani, kamati ya ulinzi na Usalama Wilaya na Polisi kata wa halmashauri ya jiji la Dodoma leo Januari 18,2024 jijini Dodoma.



Meneja wa Shirika la Umeme (TANESCO) Mkoa wa Dodoma Mhandisi Donasiano Shamba,akisisitiza jambo zaidi wakati akiwasilisha taarifa ya TANESCO halmashauri ya jiji la Dodoma wakati wa Mkutano wa Madiwani, kamati ya ulinzi na Usalama Wilaya na Polisi kata wa halmashauri ya jiji la Dodoma leo Januari 18,2024 jijini Dodoma.



Madiwani wa kata zote 41 za jijini Dodoma wakifatilia Mkutano ulioandaliwa na Shirika la Umeme (TANESCO) Mkoa wa Dodoma.



Sehemu ya kamati ya ulinzi na Usalama Wilaya na Polisi kata wa halmashauri ya jiji la Dodoma wakifatilia Mkutano ulioandaliwa na Shirika la Umeme (TANESCO) Mkoa wa Dodoma.


Afisa Uhusiano na Huduma kwa wateja TANESCO Mkoa wa Dodoma Sarah Libogoma,akitoa elimu wakati wa Mkutano wa Madiwani, kamati ya ulinzi na Usalama Wilaya na Polisi kata wa halmashauri ya jiji la Dodoma leo Januari 18,2024 jijini Dodoma.


Afisa Usalama wa TANESCO mkoa wa Dodoma Bw. Madega Dudu,akitoa elimu kuhusu uharibifu wa miundombinu ya kusafirishia na kusambazia umeme wakati wa Mkutano wa Madiwani, kamati ya ulinzi na Usalama Wilaya na Polisi kata wa halmashauri ya jiji la Dodoma leo Januari 18,2024 jijini Dodoma.


Baadhi ya Waheshimiwa Madiwani wakitoa maoni yao wakati wa Mkutano wa Madiwani, kamati ya ulinzi na Usalama Wilaya na Polisi kata wa halmashauri ya jiji la Dodoma ulioandaliwa na Shirika la Umeme (TANESCO) Mkoa wa Dodoma leo Januari 18,2024 jijini Dodoma.


Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Dodoma Mjini Ndugu Charles Mamba,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua Mkutano wa Madiwani, kamati ya ulinzi na Usalama Wilaya na Polisi kata wa halmashauri ya jiji la Dodoma ulioandaliwa na Shirika la Umeme (TANESCO) Mkoa wa Dodoma leo Januari 18,2024 jijini Dodoma.
Share:

Thursday, 18 January 2024

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO IJUMAA JANUARI 19,2024




Share:

JINSI RAIS SAMIA ANAVYOIPAISHA TANZANIA KIUCHUMI...IMF YAITAJA TZ MIONGONI MWA MATAIFA 10 YENYE MADENI MADOGO ZAIDI BARANI AFRIKA


# IMF yaitaja Tanzania miongoni mwa mataifa 10 yenye madeni madogo zaidi barani Afrika

#Sera za uchumi za Rais Samia zaleta matunda makubwa nchini


Januari 18, 2024

Na Mwandishi Wetu Zanzibar

Hatua ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kuitaja Tanzania miongoni mwa mataifa 10 ya Afrika yenye deni dogo la taifa imedhihirisha mafanikio ya mageuzi ya kiuchumi yanayoendelea nchini tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani karibu miaka mitatu iliyopita.

Chini ya utawala wake, Rais Samia ameongeza maradufu uwekezaji wa serikali kwenye miundombinu na huduma za jamii, ikiwemo sekta za elimu, maji, afya, umeme na kilimo.

Uwekezaji wa serikali, hususan kwenye ujenzi wa miundombinu, umechochea ukuaji wa uchumi nchini.

Kupitia mkakati wa Royal Tour, Rais Samia pia ameongeza kwa kiasi kikubwa sana idadi ya watalii wanaokuja nchini.

Ongezeko la watalii limeleta pesa za kigeni nchini na kuongeza ajira.

Vilevile, Serikali yake imeongeza bajeti kwenye sekta ya kilimo kwa kiwango ambacho hakijawahi kuonekana tangu nchi ipate uhuru na hivyo kuongeza tija kwa wakulima nchini.

Sera rafiki za Serikali ya Samia kwa sekta binafsi zimesaidia kuongeza kasi na ukubwa wa uwekezaji wa makampuni ya nje na ya ndani.

Rais Samia pia ameweza kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia wa Tanzania na taasisi za kimataifa na nchi za nje ambazo zimeongeza utoaji wa misaada na mikopo yenye masharti nafuu kwa Tanzania.

Mikopo nafuu yenye riba ndogo na muda mrefu wa marejesho imepunguza mzigo wa deni la taifa.

Pamoja na kwamba Tanzania imeendelea kukopa nje ili kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo, ukopaji makini wa Serikali ya Rais Samia wa kutumia mikopo nafuu badala ya mikopo yenye masharti ya kibiashara na ukuaji wa kasi kubwa wa Pato la Taifa (GDP), vimepunguza mzigo wa deni la taifa.

Uwiano wa Deni la Taifa kulinganisha na GDP ambao hutumiwa na IMF na wachumi wengine duniani kupima uhimilivu wa deni la taifa, uko chini Tanzania kulinganisha na wastani wa dunia.

Takwimu za kimataifa zinaonesha kuwa jumla ya deni duniani sasa hivi ni Dola za Marekani trilioni 307, ambayo ni sawa na asilimia 336 ya GDP ya dunia.

Zifuatazo ni nchi 10 za Afrika zenye uwiano wa Deni la Taifa mdogo kabisa kwenye bara hilo kuilinganisha na pato la taifa (GDP), kwa mujibu wa IMF:

🇨🇩 DRC 11.1%

🇧🇼 Botswana 18.1%

🇪🇹 Ethiopia 31.2%

🇬🇼 Guinea Bissau 31.5%

🇬🇶 Equatorial Guinea 33.7%

🇰🇲 Comoros 36.9%

🇹🇩 Chad 38.7%

🇨🇲 Cameroon 39.6%

🇳🇬 Nigeria 41.3%

🇹🇿 Tanzania 41.8%


Nchi 10 duniani zenye kiwango kikubwa cha deni (uwiano wa Deni la Taifa kulinganisha na GDP) hizi hapa:


Japan🇯🇵 264%

Singapore 🇸🇬 160%

Italia 🇮🇹 145%

Marekani 🇺🇸 129%

Hispania 🇪🇸 113%

Canada 🇨🇦 113%

Ufaransa 🇫🇷 112%

Uingereza 🇬🇧 101%

India 🇮🇳 89%

Argentina 🇦🇷 85%
Share:

Video : NG'WANA KANG'WA - HARUSI YA VICTOR

Share:

Video Mpya : MINZI GANHWANI - BHANANZENGO

 

Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger