Thursday, 30 November 2023
WENYE MAHITAJI MAALUM WAKUMBUKWA UDOM
Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM)kimezindua Harambee ya kuwachangia wanafunzi wenye mahitaji maalum wanaosoma chuoni hapo ili kuchochea ari ya mafanikio yao ikiwa ni pamoja na kuongeza ushawishi kwa wanafunzi wengine wa kundi hilo kutokata tamaa ya kusoma.
Hayo yamejiri November 29,2023 Jijini hapa kwenye Mkutano wa 14 wa Baraza la wahitimu wa Chuo hicho (UDOM) ambapo fedha zitazopatikana kupitia Harambee hiyo zitasaidia kukidhi mahitaji ya ada, magongo,vifaa wezeshi na mengineyo.
Akizungumza kwenye Baraza hilo, Waziri wa Madini nchini Peter Mavunde ameipongeza hatua hiyo huku akitoa maelekezo kwa Uongozi wa UDOM kuandaa orodha ya wadau wa Chuo hicho na kuwaomba kuchangia ili kufikia malengo kwa kuwa kila mwenye ulemavu ana haki ya kuishi maisha mazuri.
Kwa kutambua umuhimu wa wenye mahitaji maalum Mavunde kwa upande wake amechangia shilingi milioni tano za kitanzania ambazo zitasaidia kuboresha baadhi ya mahitaji kwa wanafunzi hao.
"Mnatambua hapa nimemwakilisha Naibu Waziri Mkuu ambaye hajaweza kufika hapa kutokana na kuwa na majukumu mengine, yeye kwa upande wake ameahidi kutoa shilingi milioni kumi,na mimi binafsi natoa milioni tano naamini kabisa hii itaweza kusaidia kwa kiasi fulani," amesema
Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa UDOM anayeshughulikia Mipango,Fedha na Utawala Prof.Winesta Anderson ameeleza kuwa Chuo hicho kina jumla ya wanafunzi 160 wenye mahitaji maalumu .
Amefafanua kuwa kati yao wenye uoni hafifu ni 12,walemavu wa ngozi 28,wenye ulemavu wa kutosikia ni 70 na wengine 46 waliosalia wapo kwenye kundi la ulemavu mwingine.
"Amesema msingi wa jumuiya ya Tanzania unamtaka kila mwananchi kupata elimu bila kujali hali yake na kwamba kwa kulitambua hilo wao kama wadau wana mpango mkakati wake ambao utakamilika 2026 ukiwa umezingatia kwa undani mahitaji ya wanafunzi hao" amesema na kuongeza;
"UDOM kupitia convocation hii tumesema tulilete hili kama kampeni ya kuwasaidia wenye uhitaji kusoma na kufika chuo Kikuu,Wizara yetu mama ya elimu imeendelea kitusapoti kwa kutupatia bajaji nane,laptop 26, mafuta na bado tunaendelea kunapambana kuhakikisha kila sehemu inapitika ili wanafunzi wetu wawe salama,"amesema
Naye Mlezi wa wanafunzi wenye mahitaji maalum chuoni hapo kupitia Kurugenzi ya huduma za wanafunzi Florida Chambi ameeleza kuwa ili kufanikiwa katika kampeni hiyo,kiasi cha shilingi milioni 300 kinahitajika ambacho kitakusanywa kwa kipindi cha miezi 12 kuanzia sasa.
Amesema fedha hizo zitasaidia pia kuboresha hali ya miundombinu ya wanafunzi hao ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya vyumba wanavyolala kuendana na hali yao.
"Tunaishukuru Serikaki na Chuo hiki kwa jitihada zake mfano, Chuo kimeendelea kuwajali wanafunzi hawa kwa kuajiri madereva maalum wanaweza kuendesha bajaji na kuwarahisishia usafiri, Chuo pia kimetoa motisha kwa wanafunzi wanaowasaidia wenye mahitaji maalum kama Shukrani kwa kuwawekea mazingir wezeshi, "amesema
Chambi amesema Chuo hicho kinajali kuwatengea wanafunzi wenye mahitaji maalumu chumba cha mtihani na kueleza kuwa kupitia kurugenzi hiyo wanaendelea kuboresha zaidi kila eneo ili kuwawezesha wanafunzi hao kusoma kwa bidii kufikia malengo yao.
Pamoja na hayo baadhi ya wadau wa UDOM wameweza kuchangia harambee hiyo akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ambaye amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule ambaye ameahidi milioni mbili,Ridhiwan Kikwete milioni mbili,Kituo cha uwekezaji million mbili huku Makamu mkuu wa Chuo hicho Prof.Lughano Kusiluka akiahidi kuchangia shilingi milioni mbili.
Wednesday, 29 November 2023
WATALAAMU WA UHIFADHI WA MALIASILI NA UTALII WAPIGWA MSASA KUFANYA TAFITI ZA KISAYANSI
Na. John Bera
Wizara ya Maliasili na Utalii imeendesha mafunzo kwa watumishi wa Wizara, taasisi mbalimbali za serikali na vyuo vikuu kuhusu namna bora ya kufanya tafiti zitakazosaidia kuondoa changamoto na kuimarisha uwekezaji katika maeneo ya uhifadhi nchini.
Akizungumza leo Jijini Dodoma wakati wa mafunzo ya namna ya kufanya tafiti kuhusu uhusiano wa watu na uhifadhi yaliyoendeshwa na wataalamu wabobezi kutoka Chuo Kikuu cha Bangor cha nchini Uingereza, Mkurugenzi wa Mafunzo na Utafiti kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Edward Kohi amesema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka na kwamba mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo watumishi wa Wizara, vyuo na taasisi zake njia sahihi za kufanya tafiti zinazohusisha watu haswa kama ni suala lenye utata.
Aidha, Dkt. Kohi amesema mafunzo hayo yatakuwa endelevu katika kuhakikisha kazi nzuri inafanyika katika kutambua changamoto za uhifadhi kwa kutumia nyenzo sahihi katika kukabiliana na changamoto hizo. Alifafanua Zaidi kwa kusema katika mafunzo hayo washiriki wanajifunza uandaaji mzuri wa dodoso kwa kuandaa na kuuliza maswali na namna ya kuchakata maswali na takwimu zinazopatikana wakati wa kufanya tafiti.
"Mafunzo haya yanaleta nyongeza ya eneo la saikolojia kwenye tafiti zinazohusisha watu na uhifadhi, na njia mbali mbali za kuandaa maswali ambayo watu wengi huwa na mashaka kuyajibu kiurahisi kama vile ‘umetumia kiasi gani ukiwa hifadhini, umeshawahi winda hifadhini? n.k."
"Mafunzo haya yamekuja wakati sahihi ambapo mkakati wa kutekeleza Sera ya Wanyamapori ya mwaka 2007 inafanyiwa maboresho hivyo mafunzo yatachangia watafiti kupata matokeo na taarifa sahihi za utafiti zitakazoongoza na kusaidia kuboresha sera mbalimbali za uhifadhi, kutatua changamoto na pia yatasaidia katika kufanya uwekezaji na taarifa zinazotuongoza katika kutoa maamuzi makubwa katika sekta ya uhifadhi na utalii."
Kwa upande wake, Mshiriki kutoka Idara ya Misitu na Nyuki, Dkt. Siima Salome Bakengesa amesema kupitia mafunzo hayo wanajifunza namna ya kutumia taarifa sahihi kutoka kwa watu wanaoishi maeneo yanayopakana na hifadhi.
"Tunaamani baada ya mafunzo haya tutakuwa na uwezo wa kufanya tafiti ambazo zitaendelea kutusaidia katika uhifadhi maeneo yetu ambayo tunahifadhi kwa misitu na wanyama."
Naye Dkt. Agnes Carol Kisanga kutoka Idara ya Baiolojia Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) amesema kupitia mafunzo hayo wanajifunza njia tofauti tofauti ya kufanya tafiti wa kujua namna ya kuendelea kuhifadhi.
“Hii ina maana kwa sasa tunakwenda kuhamia kufanya tafiti kwa kutumia sayansi ya saikolojia na sayansi ya jamii kwa kupeana maoni ya watu tofauti na inayofanyika sasa.”
Mafunzo hayo yamehudhuriwa na Washiriki 25 kutoka Wizara ya Maliasili na utalii (TAFORI, TAWIRI, Idara ya wanyamapori, Idara ya Sera na Mipango, Kitengo cha Utafiti na Mafunzo na Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) ikiwemo washiriki kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na taasisi ya COLBAT Ltd.