Friday, 28 July 2023

NDEGE MPYA YA AIR TANZANIA YA MIZIGO BOEING 767-300 KUWEZESHA HARAKATI ZA UNICEF NCHINI DRC KONGO


*****************

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limeamua kutumia Ndege Mpya ya Kisasa ya Mizigo Boeing 767-300 inayomilikiwa na Kampuni ya Ndege ya Air Tanzania kusafirisha shehena ya chanjo zilizotoka India kwa ajili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Akizungumza na vyombo vya habari wakati wa kupakia shehena hizo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) mmoja kati ya wadau wa Usafirishaji Mizigo wa Anga Bw. John Lupembe amesema sababu ya kutumia ndege hiyo ni kutokana na ubora wa huduma unaotolewa na Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) pamoja na uwezo wa ndege hiyo kuweza kubeba bidhaa zenye mahitaji tofauti tofauti.

Lupembe ameongeza kuwa ndege hii imepunguza adha kubwa ya usafirishaji wa mizigo hapa nchini ikiwemo bidhaa za aina ya chanjo ambazo uhitaji kiwango maalumu cha joto ili kulinda ubora wake.

Kwa upande wa ATCL, Meneja Biashara Edward Nkwabi amesema wanauzoefu wa kutosha katika kusafirisha shehena za madawa na chanjo.

Ameeleza hapo awali, walikuwa wakitumia ndege yao ya masafa ya mbali ya abiria Boeing 787-8 Dreamliner kusafirisha mizigo ya aina hiyo.

Nkwabi amesema ATCL wataendelea kutoa Kipaumbele katika kuwezesha harakati za Mashirika ya Umoja wa Mataifa kama sehemu ya mchango ili kufanikisha huduma za ukozi duniani.

Meneja huyo amesema wasafirishaji wa mizigo hawana budi kutumia fursa hiyo iliyoletwa na Serikali katika kuhakikisha wafanyabiashara wa ndani ya nchi wanaendelea kunufaika.

“Nia ya ndege hii ilikuwa ni kuchochea bidhaa zetu za ndani kusafirishwa kwenda nje, hivyo tunahitaji ushirikiano wa Serikali kuhakikisha wanaongeza thamani ya bidhaa zao kwa kuwa zinaondokea hapa hapa,” amesema Nkwabi.

Amesema licha ya shirika hilo kuanza biashara ya usafirishaji na ushindani uliopo sokoni, bado ndege hiyo ya mizigo inatoa huduma kiasi cha kuendelea kuaminiwa na Mashirika ya Umoja wa Mataifa ikiwemo UNICEF.

Naye, Mbarouk Mbarouk, Rubani Mtanzania anayeongoza ndege hiyo, amesema leo wanakwenda Kinshasa na Tani 26 za mzigo pia watachukua mizigo mingine jijini Nairobi na kurudi Tanzania.


Share:

TAASISI YA BILAL MUSLIM YATUMIA KUMBUKIZI YA KIFO CHA MJUKUU WA MTUME (S.A.W) KUCHANGIA DAMU HOSPITALI YA RUFAA BOMBO

 










Na Oscar Assenga, TANGA.

WANAFUNZI, walimu pamoja na waumini wa dini ya Kiislamu zaidi ya 130 kutoka Taasisi ya Bilal Muslim Mission of Tanzania Tawi la Tanga wametumia maadhimisho ya mwaka mpya wa kiislamu ulioambatana na kukumbukizi ya kifo cha Mjuu wa Mtume (S.A.W) Imam Hussein Ally kuchangia damu salama katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo

Mkuu wa shule ya Wasichana katika taasisi hiyo Sheikh Sajad Hassan akizungumza mara baada ya zoezi hilo alisema kuwa uchangiaji wa damu katika hospitali hiyo kawaida yao ya kila mwaka ikiwa ni ishara ya kuonesha moyo wa kujitolea wahitaji mbalimbali hususani watoto na mama wajawazito waliopo hospital wanaohitaji kuongezewa damu.

Mbali na kuchangia damu lakini pia waliwatembelea kwenye wodi ya wakina mama wajawazito na kugawa zawadi mbalimbali kwa wagonjwa ikiwa ni sehemu ya kuwafariji.

Alisema kusudio la wao kuchangia damuni kujitolea sadaka ambayo wanaifungamanisha na na tukio la kuwawa kwa mjukuu wa bwana mtume (S.A .W) Hussein Bin Ally aliyeuwawa mwaka 61 Hijiria huko Irak aliyekuwa wakiipigania dini kwa lengo la kukemea mabaya na kuamrisha mema, aliyetoka kutetea wanyonge na wale waliodhulumiwa

Aidha alisema wao kama taasisi wamejiwekea utaratibu wa kufanya zoezi hilo kila mwaka katika maeneo tofauti tofauti lengo ni kuonyesha kwamba wamesimama pamoja na mjukuu wa bwana mtume (S.A.W) katika kutetea wanyonge.

“Tunaimani kwamba damu hii itasaidia wanyonge, pia tunasimama na kukemea dhuluma zozote zinazoendelea ulimwenguni" alisema Sheikh Hassan.

Awali akizungumza wakati wa zoezi hilo Mkuu wa Idara ya Maabara katika Hospital ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo Sinde Ntobu ameishukuru Bilal Muslim kwa kuona kuwa wanayo nafasi kubwa kuokoa maisha ya watu wanaofika hospitalini hapo kupatiwa huduma ikiwemo kuongezewa damu.

Alisema uhitaji wa damu kwa mwezi katika hospital hiyo ni mkubwa tofauti na ile inayochangiwa ambapo uhitaji wao unafikia lita 500 hadi 600 wakiwa na upungufu wa damu kwa Unit 250 hadi 300 hivyo kuziomba taasisi na watu binafsi kuona umuhimu wa kuchangia damu ili kuokoa maisha ya watu.

" Sisi kama hospital kwa wastani kwa mwezi tunatumia chupa za damu 500 mpaka 600 lakini uwezo wa kuchangia damu ambayo inapatikana mara nyingi tunapata unit 250 mpaka 300 kwahiyo uhitaji wa damu kwa wagonjwa ni mkubwa "Alisema Mtobu

Hata hivyo aliiasa jamii kuona umuhimu wa kuchangia damu ili kuweza kuokoa maisha ya wengine wahitaji lakini baadae zinaweza kuwasaidia wanapokuwa wahitaji.
Share:

Thursday, 27 July 2023

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO IJUMAA JULAI 28,2023



































Share:

WAZIRI BASHUNGWA AWASILI UTURUKI NA UJUMBE WAKE KWA ZIARA YA KIKAZI

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Innocent Bashungwa (Mb) amewasili mjini Istanbul, Uturuki na ujumbe wake kwa ziara ya kikazi, kufuatia mwaliko wa Waziri wa Ulinzi wa Uturuki, Mhe. Yasar Guler kwa ajili ya kuhudhuria Maonesho ya Kimataifa ya viwanda vya Kijeshi.

Akiwa nchini humo, Mheshimiwa Bashungwa amepata fursa ya kukutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake, kabla ya kutembelea Maonesho hayo ya Kimataifa ya viwanda Kijeshi.

Mazungumzo baina ya Mawaziri hao wa Ulinzi, yanalenga kuendeleza na kuimarisha ushirikiano uliopo baina ya Wizara za Mataifa haya mawili kupitia sekta ya Ulinzi kwa ustawi wa Majeshi yetu pamoja na nchi hizi kwa ujumla. 

Historia ya ushirikiano baina ya Tanzania na Uturuki ilianza tangu mwaka 1979, baada ya Uturuki kufungua Ofisi za Ubalozi wake jijini Dar es Salaam.

Ushirikiano baina ya mataifa haya mawili ni kupitia nyanja mbalimbali zikiwemo za uchumi, ulinzi, elimu, afya, utalii, mawasiliano pamoja na ziara za viongozi wa Kiserikali na Kijeshi wa Mataifa haya mawili kutembeleana.

Share:

WANAFUNZI 640 KUNUFAIKA NA SAMIA SCHOLARSHIP 2023/24


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda,akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 27,2023 jijini Dar es Salaam kuhusu ufadhili kwa wahitimu wa Kidato cha Sita wapatao 640 kwa ajili ya kugharamia elimu ya juu kwa asilimia 100 kupitia mpango wa Samia Skolashipu kwa Mwaka wa masomo 2023/24.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo,akizungumzia ufadhili kwa wahitimu wa Kidato cha Sita wapatao 640
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda,akiwa katika picha ya pmoja mara baada ya kuzungumzia ufadhili kwa wahitimu wa Kidato cha Sita wapatao 640 kupitia mpango wa Samia Skolashipu kwa Mwaka wa masomo 2023/24.

Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM

Serikali inatarajia kutoa ufadhili kwa wahitimu wa Kidato cha Sita wapatao 640 kwa ajili ya kugharamia elimu ya juu kwa asilimia 100 kupitia mpango wa Samia Skolashipu kwa Mwaka wa masomo 2023/24.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesisitiza kuwa ufadhili huo ni kwa masomo ya Shahada ya Kwanza kwa wanafunzi waliopata ufaulu wa juu katika Mitihani ya Kidato cha Sita mwaka 2023 inayoendeshwa na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) katika tahasusi za Sayansi na kuchaguliwa kujiunga na Programu za Sayansi Teknolojia, Elimu Tiba na Hesabu katika Vyuo vikuu nchini.

Ameongeza kuwa kwa mwaka wa masomo 2023/24 Wizara imetenga zaidi ya Shilingi Bilioni 6 kuwezesha utekelezaji wa mpango huo.

Ameeleza kuwa Maombi ya Samia Scholarship yatawasilishwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa njia ya mtandao kupitia mfumo wa https://ift.tt/rMwTV3B kuanzia Jumatatu, Septemba 25, 2023.

Amesisitiza kuwa Skolashipu hizo zitaendelea kutolewa kwa haki na kwa uwazi , kwani vigezo vinafahamika na vitafuatwa na kwamba lengo ni kuongeza chachu ma idadi ya wanasayansi nchini.

“Samia Skolashipu inalenga kuongeza idadi ya wanasayansi nchini ambao watachangia moja kwa moja katika maendeleo ” amesisitiza waziri huyo.

Aidha, Prof. Mkenda amesema kuwa kwa mwaka wa masomo 2022 /23 shilingi bilioni tatu zilitengwa na kunufaisha wanafunzi 636 ambapo Kati ya wanafunzi hao, wa kike walikuwa 261 (41%) na wa kiume 375 (59%) na kwamba wanafunzi hao walidahiliwa na kusajiliwa katika taasisi 18 za Elimu ya Juu kikiwemo Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS),

Amesema Idadi ya wanafunzi watakaokuwa wamefadhiliwa na Scholarship hiyo katika miaka miwili itakuwa imefikia wanafunzi 1276.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema kuwa ufadhili utazingatia viwango na miongozo ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu na utagharamia maeneo ya ada ya mafunzo, posho ya chakula na malazi, Vitabu na Viandikwa, utafiti,Bima ya Afya, mahitaji maalum ya vitivo, mafunzo kwa vitendo na vifaa saidizi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu na kwamba Orodha ya majina ya wanafunzi wenye sifa za kuomba itapatikana kupitia www.moe.go.tz na www.heslb.go.tz kuanzia wiki ya kwanza ya mwezi Agosti, 2023.

Prof. Nombo amesisitiza kuwa Mwanafunzi atakaepata ufadhili wa SAMIA SCHOLARSHIP atapaswa kuzingatia masharti ambayo ni pamoja na Kusoma, kuelewa na kusaini Mkataba wa Makubaliano ya Ufadhili wa Masomo kati yake na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Masharti mingine ni pamoja kuwa mnufaika hataruhusiwa kubadilisha programu ya masomo aliyopatia ufadhili bila barua ya idhini ya maandishi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia; na hataruhusiwa kuahirisha masomo, isipokuwa kwa sababu za kiafya, na kuthibitishwa na chuo husika.

Katibu Mkuu ameongeza kuwa Iwapo kiwango cha ufaulu wa mnufaika kitashuka chini ya GPA 3.8 katika mwaka wa masomo, ufadhili utasitishwa mnufaika ataendelea na masomo kupitia mkopo wa Elimu ya Juu.

Aidha ameongeza kuwa ina mfumo wa kufuatilia maendeo ya wanufaika hao ambapo kila mmoja wao apaswa kujiandikisha katika mfumo kupitia https:schlarshis.moe.go.tz

Mwanafunzi wa Mwaka wa Kwanza katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili Dina Giga ameishukuru Serikali kwa ufadhali huo ambao umeondoa gharama kwa wazazi, lakini pia imeleta hamasa kwa wanufaika kusoma kwa bidii na pia kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha sita kujiunga na programu za Sayansi.
Share:

MSAJILI WA HAZINA APOKEA BILIONI 2.5/- GAWIO KUTOKA KAMPUNI YA TIPER

Msajili wa Hazina Bw.Nehemiah Mchechu (Kulia) akipokea mfano wa hundi ya shilingi Bilioni 2.5 kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa TIPER Tanzania Bw.Mohamed Mohamed kama gawio kwa Serikali ambazo zitasaidia kutekeleza miradi ya Maendeleo. Hafla hiyo imefanyika leo Julai 27,2023 katika hoteli ya Hyatt Regency Jijini Dar es Salaam.

**************

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI imepokea Gawio la sh. bilioni 2.5 kutoka Kampuni ya Kimataifa ya Kuhifadhi Mafuta (TIPER) Tanzania, fedha hizo zitasaidia kutekeleza miradi ya maendeleo.

Akizungumza katika hafla fupi ya kupokea gawio hilo, jijini Dar es Salaam, jana, Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu alisema lengo la uwekezaji wa kampuni hiyo ni kuongeza mchango kwa maendeleo ya taifa.

"Nawapongeza sana TIPER kwani walichofanya ni kiitu kikubwa, tunazihimiza kampuni nyingine kutoa gawio kwani fedha hizo ndizo ambazo zinakwenda kuinua uchumi wa nchi na kutekeleza miradi ya maendeleo," alisema.

Alifafanua kuwa kuna baadhi ya kampuni ambazo mwaka ujao wa fedha zitafutwa kutokana na kupitwa na wakati au huduma zake na nyingine zitaunganishwa kutokana na shughuli zake kushabihiana ambapo zikiunganishwa na kufanya kazi pamoja zitaleta tija zaidi.

"Kuna timu inaendelea kufanya uchambuzi zaidi na mwezi wa nane mwaka huu ripoti itapokelewa na kutangazwa ni kampuni gani zitaunganishwa au kufutwa kwani wakati mwingine kampuni hufanya vibaya sababu ni uongozi hivyo lazima wapewe muda kwa kuwavumilia na kuangalia uongozi wao," alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa TIPER Tanzania, Mohamed Mohamed, alisema kuwa sekta ya mafuta ni moja ya maeneo muhimu kwa maendeleo ya nchi yoyote duniani na ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi.

Alisema sekta hiyo ina mchango mkubwa katika usafirishaji, kilimo na miundombinu kwa sababu mafuta yanatumika kwa matumizi mbalimbali, hivyo imeendelea kuwa mhimili muhimu kwa maendeleo ya uchumi.

"Kuwekeza katika rasilimali watu ni jambo muhimu hususan kwa kampuni ambayo inaendelea kukua na inapenda kujipqmbqnua kuwa kampuni yenye nmchango mkubwa katika jamii," alisema.

Akizungumzia uwekezaji ambao wanataka kuufanya nchini, alisema kuwa uwekezaji umekuwa ukifanyika kipindi cha miaka 10 iliyopita na wamendelea kuwekeza, hivyo ni jambo endelevu.

Alisema TIPER imejipanga kuongeza ufanisi, ,tija na faida, na kwamba wanaimani mwaka unaokuja wanaweza kutoa gawio kubwa zaidi huenda likawa mara mbili ya walilotoa mwaka huu.Msajili wa Hazina Bw.Nehemiah Mchechu (Kulia) akipokea mfano wa hundi ya shilingi Bilioni 2.5 kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa TIPER Tanzania Bw.Mohamed Mohamed kama gawio kwa Serikali ambazo zitasaidia kutekeleza miradi ya Maendeleo. Hafla hiyo imefanyika leo Julai 27,2023 katika hoteli ya Hyatt Regency Jijini Dar es Salaam.Msajili wa Hazina Bw.Nehemiah Mchechu akizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya makabidhiano ya gawio la Serikali kutoka Kampuni ya TIPER Tanzania ambapo TIPER imetoa gawio kwa serikali shilingi Bilioni 2.5 ambazo zitasaidia kutekeleza miradi ya Maendeleo nchini . Hafla hiyo imefanyika leo Julai 27,2023 katika hoteli ya Hyatt Regency Jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa TIPER Tanzania, Mohamed Mohamed akizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya kukabidhi gawio la Serikali ambapo TIPER imetoa gawio kwa serikali shilingi Bilioni 2.5 ambazo zitasaidia kutekeleza miradi ya Maendeleo nchini. Hafla hiyo imefanyika leo Julai 27,2023 katika hoteli ya Hyatt Regency Jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya wadau mbalimbali wakishiriki katika hafla ya makabidhiano ya gawio la Serikali kutoka Kampuni ya TIPER Tanzania ambapo TIPER imetoa gawio kwa serikali shilingi Bilioni 2.5 ambazo zitasaidia kutekeleza miradi ya Maendeleo nchini . Hafla hiyo imefanyika leo Julai 27,2023 katika hoteli ya Hyatt Regency Jijini Dar es Salaam.

Share:

DK. NDUMBARO ATAKA HOSPITALI YA WILAYA SONGEA IKAMILIKE KWA WAKATI, UBORA

Mbunge wa Songea Mjini ambaye pia ni Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dk. Damas Ndumbaro amewataka wataalam wa Halmashauri ya Songea pamoja na mkandarasi anayejenga hospitali ya Wilaya ya Songea kuongeza kasi na ubora wa ujenzi wa hospitali hiyo.

Mhe.Ndumbaro ametoa rai hiyo wakati wa ziara yake pamoja na Kamati ya Siasa ya Mkoa na Wilaya kukagua maendeleo ya ujenzi wa hospitali hiyo inayojengwa katika Mtaa wa Sanangura, Kata ya Tanga wilayani Songea.

“Wananchi hawa wamenipa ridhaa ya kuwatumikia na ni jukumu langu kuhakikisha natafuta fedha kwa ajili ya maendeleo yao na nimekuja leo kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ukiwemo huu wa hospitali.

Kwa wataalamu wetu, rai yangu, muhakikishe mnasimamia ujenzi huu unakamilika kwa wakati na kwa ubora tuliokubaliana ili wananchi hawa waanze kupata huduma haraka kama tulivyo waahidi,” amesema Mhe.Ndumbaro huku akiwataka wananchi kushirikiana na mkandarasi kwa shughuli ndogondogo kama za usafi katika eneo hilo.

Mhe Dk. Ndumbaro pia amemshukuru Mhe.Dk. Samia Suluhu Hassan,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha za miradi mbalimbali inayotekelezwa katika Jimbo lake la Songea Mjini na kuahidi kusimamia miradi hiyo ili thamani ya fedha aliyoitoa Mhe Rais ionekane na ilete tija iliyokusudiwa.

“Mhe.Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan ametuletea Shilingi Bilioni Moja kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hii. Lakini mimi nilimuomba atuongezee fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi na kuifanya kuwa hospitali ya kisasa zaidi na Mhe Rais Dk. Samia akakubali na ametuongezea Shilingi Milioni 800.

Tunataka inapofika tarehe 1, Septemba huduma zianze kutolewa hasa hizo za awali hivyo lazima kasi iongezwe wananchi hawa waanze kupata huduma mapema zaidi,” amesisitiza Mhe Dk. Ndumbaro.

Amesema kuwa hospitali hiyo itakapokamilika kutakuwa na gari la kubebea wagonjwa, kutakuwa na huduma za upasuaji, maabara kubwa, wodi pamoja na mashine za kisasa za kutolea huduma na hivyo kuwaondolea adha wagonjwa waliokuwa wanalazimika kusafirishwa mikoa ya karibu kwa ajili ya matibabu.
Share:

WATOTO WALIOWEKA REKODI GGML KILICHALLENGE, WANG'ARA SIKU YA MASHUJAA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Jenista Mhagama (katikati) akiwa Abeli Mussa (kushoto) na Rebecca Damian (kulia) baada ya kuwapokea wanafunzi hao walioshiriki kupanda Mlima Kilimanjaro kupiti kampeni ya GGML KiliChallenge -2023 inayolenga kuhamasisha uchangishaji wa fedha za mapambano dhidi ya VVU/Ukimwi.


Na Mwandishi wetu

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenista Mhagama amewapongesa watoto Abel Mussa na Rebbeca Damian wenye umri wa miaka 14 waliopanda mlima Kilimanjaro kupitia kampeni ya GGML KiliChallenge- 2023, huku watoto hao wakibainisha kuwa hatua yao hiyo ililennga kuunga mkono jitohada za Rais Samia Suluhu Hassan hususani katika kuwajali watoto nchini.

Watoto hao wanaolelewa na Kituo cha Moyo wa Huruma kilichoazishwa na kufadhiliwa na Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML), walikuwa ni moja ya washiriki 61 waliopanda mlima Kilimanjaro tarehe 14 Julai 2023 na kushuka tarehe 20 Julai mwaka huu.

Washiriki hao walipanda mlima huo kupitia kampeni ya GGML KiliChallenge anayolenga kukusanya fedha za kuendeleza mapambano dhidi ya VVU/ Ukimwi.

Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya mashujaa juzi tarehe 25 Julai 2023 jijini Dodoma, Mhagama alisema watoto hao walimuambia wamepanda mlima huo kwa kuzingatia kazi kubwa anayofanya Rais Samia Suluhu Hassan ya ulinzi wa watoto wa kitanzani, haki zao na ustawi wao.


"Vilevile kwa kazi kubwa iliyofanywa na Serikali katika ujenzi wa miundombinu ya elimu ya msingi na sekondari na vyuo vikuu. Lakini pia wamesema walipanda kwa kuzingatia kazi kubwa unayofanya kwenye miundombinu ya afya haya yote yakiwa na ustawi mkubwa wa watoto wote wa Tanzania," alisema.


Amesema mbali na kushirikiana na serikali kusaidia mapambano dhidi ya tatizo la Ukimwi, pia watoto hao ambao ni wanafunzi wa darasa la saba, walipanda mlima huo kwa lengo la kuanzisha moyo wa uzalendo kwa watoto wengine ili watambue kuwa nchi sasa inaoongozwa na rais ambaye anajali ustawi wa watoto.


Kati ya watoto hao, Rebecca Damiani ambaye ni mwanafunzi katika Shule ya Msingi Kivukoni- Geita, alifika katika kilele cha Uhuru cha mlima huo, huku Abel Mussa ambaye ni mwanafunzi wa shule ya msingi Mbugani pia kutoka mkoani Geita, alirudia njiani baada ya kuugua malaria.


Kampeni hiyo iliyoasisiwa na GGML mwaka 2002 kwa kushirikiana na Tume ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), mwaka huu ilishirikisha wapanda mlima 35 na waendesha baiskeli 26 waliouzunguka mlima Kilimanjaro kwa siku saba.


Akiwapokea washiriki hao, tarehe 20 Julai mwaka huu, Mhagama alimwagiza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuhakikisha wanafunzi hao wanaingizwa kwenye orodha ya miongoni mwa watu watakaohudhuria sikukuu ya mashujaa ambayo imefanyika juzi tarehe 25 Julai 2023.
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger