Thursday, 20 July 2023

SERIKALI HAITOVUMILIA UDANGANYIFU WOWOTE TASNIA YA MBOLEA


Mkurugenzi wa Uhamasishaji Uzalishaji wa Ndani na Ununuzi wa mbolea kwa Pamoja wa TFRA, Josephy Charos akifafanua jambo wakati wa kikao baina ya wajumbe wa Bodi, Menejimenti na Wakulima wa AMCOSS ya Kaloleni tarehe 19 Julai, 2023 kulia kwake ni Mwenyekiti wa AMCOSS hiyo Mohamed Nditi
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Lilian Gabriel akizungumza jambo na wakulima wa AMCOSS ya Kaloleni (hawapo pichani) wakati wa kikao baina ya bodi, menejimenti ya TFRA na wakulima hao tarehe 19 Julai, 2023
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Shimo Peter Shimo akizungumza na wakulima wa AMCOSS ya Kaloleni Mkoani Kilimanjaro walipotembelea ili kujua changamoto wanazokutana nazo katika shughuli za kilimo hususani katika tasnia ya mbolea tarehe 19 Julai, 2023
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa , Thobias Mwesigwa akizungumza na wakulima wa Amcoss ya Kaloleli ya mkoani Kilimanjaro walipowatembelea kusikia changamoto zao pamoja na kuwashauri namna bora ya kuendeleza kilimo ili kupata tija zaidi


Na Mwandishi wetu -Kilimanjaro
Bodi ya Wakurugenzi na menejimenti ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imesema haitavumilia udanganyifu wa aina yeyote kwenye tasnia hiyo iwe unafanywa na watumishi, wafanyabiashara au wakulima.


"Hatutakubali kuvumilia udanganyifu wa aina yeyote iwe ni kwenye vipimo, bei ya mbolea au viwango vya ubora".

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Bodi ya TFRA, Thobias Mwesigwa wakati wa kikao baina ya wajumbe, menejimenti na wanachama wa AMCOSS ya Kaloleni iliyopo katika halmashauri ya Manispaa ya Moshi.

Mwesigwa ameeleza hayo baada ya mkulima Ramadhani Abdalla Mariki kuwasilisha ombi la kuwaagiza mawakala wa pembejeo za mbolea kuwa na mizani kwa ajili ya kupima mbolea ili kujiridhisha na uzito kama ulivyoandikwa kwenye vifungashio.


Aidha, mkulima Reward Shelukindo ameeleza uwepo wa baadhi ya wananchi wasiokuwa waaminifu wanaouza mbolea kinyume na bei elekezi iliyotolewa na serikali ikiuzwa kwa kiasi cha shilingi 75,000 hadi 100,000 jambo ambalo bodi hiyo imeeleza kutokuvumilia jambo hilo na kueleza hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watu hao wenye nia ovu.

"Wale waliobainika wamefanya udanganyifu msimu uliopita tunawafuta kwenye biashara ya mbolea lakini pia hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao na wale waliosafi tutaendelea nao.


Mwesigwa amewataka wakulima na watanzania kwa ujumla kutoa taarifa pindi wanapobaini uwepo wa udanganyifu kwenye kilimo hususan kucheza na ruzuku ya mbolea iliyotolewa na serikali kwa lengo la kuwakwamua wakulima na kuongeza uzalishaji.


"Mzee ukipata taarifa yoyote tupe tutaifanyia kazi. Naomba niwahakikishie wananchi kuwa changamoto hizo zitatatuliwa ili muweze kupata mbolea yenye viwango na kwa bei iliyotolewa na serikali", Mwesigwa alikazia.


Amewaomba wakulima kutoe ushirikiano kwa serikali, na kueleza kuwa, Bodi kwa kushirikiana na TFRA watajitahidi kutatua changamoto za wakulima hususan za kufikisha mbolea kwa wakulima kwa wakati.


Akieleza lengo la ziara hiyo, Mkurugenzi wa Uhamasishaji Uzalishaji wa Ndani na Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja, Josephy Charos amesema imelenga kuwatembelea wazalishaji, wanufaika ambao ni wakulima pamoja na wafanyabiashara ya mbolea ili kusikia changamoto wanazokutana nazo na kuzitafutia ufumbuzi.

Aidha, ameeleza kuwa, kufuatia Bodi kuwa na muda mfupi tangu iteuliwe imeona vyema kujifunza kwa vitendo na kupata uelewa wa kile wanachokisimamia kutokea chini kabisa.


Kwa upande wake Hadija Jabir Mjumbe wa bodi aliwashauri wakulima kuhakikisha wanapima afya ya udongo katika mashamba yao ili kuweza kutumia virutubisho sahihi kutokana na uhitaji uliojidhihirisha baada ya kupima.

Pamoja na hayo alitoa ushauri ka wakulima kutumia visaidizi vya udongo kama vile chokaa ili kuimarisha afya ya udongo na kuongeza mazao na tija kwenye kilimo.
Share:

BARRICK NORTH MARA NA SWALA SOLUTIONS YAFANIKISHA UJENZI WA NYUMBA YA WALIMU YA KISASA KATIKA SEKONDARI YA MATONGO


Viongozi wa kata ya Matongo katika Halmashauri ya wilaya na Tarime wakifurahi pamoja na walimu wa sekondari ya Matongo katika hafla ya kukabidhiwa nyumba ya walimu wa shule hiyo iliyojengwa na kampuni ya ukandarasi katika mgodi wa Barrick North Mara ya Swala Solutions kwa kushirikiana na mgodi huo.wengine pichani ni Kaimu Meneja Uendeshaji wa kampuni ya Swala Sulutions , Roy Kiprono Kimutai (mwenye miwani) na Kaimu Meneja wa Idara ya Mahusiano wa Mgodi wa Barrick North Mara, Hermence Christopher, (wa nne kulia).Hafla hiyo ilifanyika katika Shule ya Sekondari Matongo
Kaimu Meneja Uendeshaji wa kampuni ya Swala Solutions , Roy Kiprono Kimutai (Kushoto) akikabidhi funguo za nyumba ya walimu kwa Diwani wa kata ya Matongo,Godfrey Kegoye na Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Matongo,Daud Itembe (mwenye kofia) katika hafla ya kukabidhi nyumba ya walimu katika shule ya sekondari ya Matongo iliyopo katika halmashauri ya wilaya ya Tarime ambayo imejengwa na kampuni hiyo kwa kushirikiana na mgodi wa Barrick wa North mara.
Walimu na viongozi wa kata ya matongo wakifurahi pamoja na wawakilishi wa makampuni Barrick na Swala Solutions katika hafla hiyo.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Matongo, Mwalimu Zabron Orege akikabidhi cheti cha shukrani kwa wawakilishi wa Barrick North Mara , Hermence Christopher na Alex Maengo katika hafla hiyo.
Wageni waalikwa wakifuatilia matukio wakati wa hafla hiyo

Tarime: Katika jitihada za kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha sekta ya elimu nchini,kampuni ya Swala Solutions ambayo ni mzabuni wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, kushirikiana na mgodi huo imekabidhi msaada wa nyumba pacha ya kisasa (two in one) ya walimu yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 120 katika Shule ya Sekondari Matongo iliyopo Kaskazini Magharibi mwa mgodi huo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.


Hafla ya kukabidhi nyumba hiyo sambamba na uzinduzi wake ilifanyika shuleni hapo jana na kuhudhuriwa na wananchi,Diwani wa kata ya Matongo ,walimu na viongozi wa vitongoji jirani na eneo hilo na Mkurugenzi wa kampuni ya kikandarasi ya Nyamongo Contractors and Mine Company Ltd, Samwel Paul Bageni, ambaye ameipatia shule hiyo msaada wa kompyuta mbili.


Akizungumza katika hafla hiyo, Diwani wa Kata ya Matongo, Godfrey Kegoye, amezishukuru kampuni za Swala Solutions na Barrick, akisema msaada wa nyumba hiyo umeipunguzia shule hiyo changamoto zinazoikabili.


"Tunamshukuru sana wadau wetu wetuwa maendeleo Barrick na Swala. Nyumba hii ni nzuri sana na hata mkandarasi ameitendea haki. Nitoe shukrani nyingi pia kwa mgodi wa Barrick kwa kutusaidia kutatua changamoto na kwenye sekta ya elimu tunaenda vizuri sana," amesema Kegoye ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.

Ameishukuru pia Serikali ya Kijiji cha Matongo na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kwa ushirikiano mkubwa waliouonesha katika kusimamia utekelezaji wa mradi huo wa elimu.


Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Matongo, Daudi Itembe, amesema msaada huo ni ishara ya matunda ya uhusiano mzuri uliopo kati ya Kampuni ya Barrick na jamii inayozunguka mgodi huo.


“Barrick ni mdau mkubwa sana wa maendeleo katika kata ya Matongo, na sioni tabu kusimama na kusema mgodi unafanya vizuri," amesema Itembe huku akitaja miradi mingi ambayo inatekelezwa katika kijiji hicho kwa ufadhili wa mgodi wa Barrick North Mara.


Kwa upande wake Kaimu Meneja Uendeshaji wa Kampuni ya Swala Solutions, Roy Kiprono Kimutai, ameshukuru kwa ushirikiano walioupata kutoka Barrick North Mara, Serikali ya Kijiji, Kata ya Matongo na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime katika utekelezaji wa mradi huo.


Naye Kaimu Meneja wa Idara ya Mahusiano wa Mgodi wa Barrick North Mara, Hermence Christopher, ameipongeza Kampuni ya Swala Solutions, akisema kitendo walichofanya ni mfano wa kuigwa.“Huu ni ushirikiano mzuri na kwenye vikao vyetu tunahamasisha wakandarasi/ wazabuni kutoa kidogo kwenye sehemu ya faida yao kurudisha kwenye maendeleo ya jamii,” amesema Christopher.


Ameongeza kuwa manufaa ya mgodi wa Barrack North Mara kwa jamii inayouzunguka ni makubwa, ikiwemo kugharimia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia mpango wake wa Uwajibikaji kwa Huduma za Kijamii (CSR).


Awali, Mkuu wa Shule ya Sekondari Matongo, Mwalimu Zabron Orege amesema nyumba waliyokabidhiwa imefanya idadi ya nyumba za walimu zilizokamilika shuleni hapo kufikia nne, kila moja ikiwa pacha (two in one).


Mwalimu Orege amesema ujenzi wa nyumba za walimu nyingine mbili unaendelea, na kwamba shule hiyo ina walimu 12 (wanaume tisa na wanawake watatu) na wanafunzi 228.

Share:

BENKI YA CRDB YAZINDUA SIMBANKING APP MPYA INAYOTUMIA TEKNOLOJIA YA KISASA KUTAMBUA MAHITAJI YA WATEJA NA KURAHISISHA MIAMALA


Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo, akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa SimBanking App inayotumia teknolojia ya kisasa zaidi inayowezesha kutambua mahitaji ya wateja na kurahisiha hudumana miamala yenye muunganiko wa teknolojia za kisasa na za hali ya juu ikiwamo akili bandia (Artificial intelligence), iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa makao makuu ya Benki ya CRDB, jijini Dar es salaam leo tarehe 19 Julai 2023.
Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo, akiwa mbele ya kifaa kinachotumia teknolojia ya kisasa zaidi inayowezesha kutambua mahitaji ya wateja na kurahisiha huduma na miamala yenye muunganiko wa teknolojia za kisasa na za hali ya juu ikiwamo akili bandia (Artificial intelligence) ambayo inatumika katika SimBanking App mpya iliyozinduliwa leo katika hafla , iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa makao makuu ya Benki ya CRDB, jijini Dar es salaam leo tarehe 19 Julai 2023.

=========== ========= ==========


Wakati dunia ikishuhudia mabadiliko makubwa ya teknolojia yanayochagiza maendeleo katika nyanja mbalimbali za maisha, leo Benki ya CRDB inayoongoza kwa ubunifu nchini imezindua SimBanking App inayotumia teknolojia ya kisasa zaidi kutambua mahitaji ya wateja.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa programu hiyo, Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo amesema SimBanking App hii mpya imetengenezwa kwa muunganiko wa teknolojia za kisasa na za hali ya juu ikiwamo akili bandia (Artificial intelligence).
“Teknolojia iliyotumika katika SimBanking App hii inampa uwezo mteja kuchagua mpangilio wa huduma kwa namna ambavyo yeye mwenyewe angependelea, teknolojia hiyo pia ina uwezo wa kutambua ni huduma gani mteja anapendelea zaidi na kumrahisishia namna ya kuipata,” alisema.

Nshekanabo alibainisha kuwa teknolojia hiyo mpya ni ya kimapinduzi katika kufikisha huduma za fedha kwa wateja kwani itaongeza wigo wa huduma zinazoweza kutolewa kidijiti huku kasi ya miamala ya wateja ikirahishwa kwa kiasi kikubwa.

“Eneo jingine ambalo tumelipa uzito mkubwa katika SimBanking App hii mpya ni ulinzi na usalama wa taarifa na miamala ya wateja. Tunatumia teknolojia ya biometriki kuhakikisha usalama kwa wateja. Hii inatufanya kuwa Benki pekee nchini na kati ya chache barani Afrika inayotumia teknolojia hii,” aliongezea Nshekanabo.
Akizungumzia huduma mpya ambazo zimeongezwa, Meneja Mwandamizi wa Huduma za Kidijiti na Ubunifu wa Benki ya CRDB, Jacklina Jackson amesema SimBanking App inatoa fursa za uwekezaji kwa wateja kwa kuwawezesha kuwekeza kupitia akaunti za uwekezaji (Fixed Deposit) kidijiti.

“Wateja pia sasa hivi wanaweza kupanga uhamisho wa fedha na malipo yanayojiruida au ya mara kwa mara kwa urahisi. Uhamisho unaweza kupangwa kila siku, kila wiki au kila mwezi. Tumeboresha upande wa kumbukumbu za taarifa ya miamala ambapo wateja wanaweza kupata risiti ya miamala yote wakati wowote kwa urahisi,” alisema Jacklina.

Katika upande wa malipo, alisema SimBanking App imeboresha malipo kupitia watoa huduma za kidijiti kwa kuwezesha ukusanyaji wa malipo kupitia programu hiyo ambapo mteja ana uwezo wa kutoa ruhusa ya malipo kwa kutumia mfumo wa namba ya siri ya mara moja (one time passcode).
“Vilevile tumefanya maboresho katika huduma za bima kwa kuongeza kasi na muda wa upatikanaji wa huduma,” aliongezea Jacklina kuhusu huduma hiyo ya bima za vyombo vya moto ambayo ilizinduliwa kwa mara ya kwanza kupitia SimBanking App mwaka 2020 benki ilipofanya maboresho.

Aidha, SimBanking App mpya inakuja na programu ya uaminifu (loyalty program) inayowawezesha wateja kupata kupata alama wanapotumia application na kisha kujishindia zawadi. Wateja pia aplikesheni hii mpya pia inatoa fursa kwa wateja kutoa maoni yao kila wakati wanapokamilisha miamala mfumo unaohusisha uwasilishaji wa maandishi na matumizi ya emoji kuonyesha hisia juu ya huduma.

Hii ni mara ya pili kwa Benki ya CRDB kufanya maboresho makubwa katika huduma ya SimBanking baada ya maboresho yaliyofanyika mwaka 2020. Tarifa ya Benki hiyo inaonyesha sasa hivi asilimia 96 ya miamala yote inafanyika kidijitali huku SimBanking ikichangia sehemu kubwa.

Huduma ya SimBanking ambayo ilianzishwa mwaka 2022 imekuwa ikitajwa kuwa moja ya huduma bora zaidi za kidijitali ambazo zinatoa mchango mkubwa katika ujumuishi wa kifedha nchini na taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi.

SimBanking imepata tuzo mbalimbali ndani na nje ya nchi ikiwamo tuzo za Consumer Choice Awards, tuzo za za Global Finance zinazotolewa nchini Marekani, na hivi karibuni imepata tuzo ya huduma bora ya kidijitali katika tuzo za Tanzania Digital Awards.



Share:

Wednesday, 19 July 2023

SERIKALI YAAHIDI KUENDELEA KUTATUA CHANGAMOTO SEKTA YA MADINI, WAZIRI BITEKO ATIA NENO

Waziri Dotto Bitteko wa Wizara ya Madini akizungumza jambo kwenye mkutano wa Wizara hiyo (Breakfast Mining Briefing) na Chama Cha wachimbaji wa Madini na Wadau mbalimbali wa sekta hiyo na kujadili Mafanikio na changamoto za wachimbaji wa madini jijni Dar es Es Salaam

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Waziri wa Maji ,Nishati na Madini Zanzibar, Shaibu Kaduwara na Naibu Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Shabani Othman.

***************


Na Mwandishi Wetu,


SERIKALI ya Awamu ya Sita kupitia Wizara ya Madini imesema sekta ya madini imepewa msukumo mkubwa kwenye sekta hiyo sambamba na kuhakikisha inaondoa changamoto ambazo zinawakabili wachimbaji madini.


Akizungumza katika mkutano wa wwchimbaji madini uliofanyika leo jijini Dar es Salaam Waziri wa Madini Dotto Biteko ameeleza wamekutana kwa ajili ya kujadili changamoto lakini wakati huo huo kuelesa Serikali inafanya katika sekta ya uchimbaji madiji ili wachimbaji wafanye shughuli zao kwa ufanisi.


Hivyo kupitia mkutano huo ulioandaliwa na Chama Cha Wachimba Madini Tanzania Biteko miongoni mwa maeneo ambayo yataangaliwa ni miundombinu ya umeme pamoja na barabara kwa kuhakikisha maeneo ya migodi yanaboreshwa.


Pamoja na hayo amesema Serikali imeweka msumkumo mkubwa kwenye miundombinu ya uzalishaji ,hivyo katika fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya umeme vijijini na mahali pengine karibu asilimia 20 ya fedha hizo zimekwenda maeneo ya migodi ya wachimbaji wakubwa,wakati na wadogo


"Wizara ya Madini inatoa shukrani kwa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwani amefanya mambo makubwa katika sekta ya madini na maeneo mengi ya uchimbaji yanapelekewa umeme, " ameseema.


Aidha amesema katika kutatua maeneo ambayo yamekuwa na muingiliano wa migodi na uchimbaji, tayari Rais Dk.Samia ametoa maelekezo Wizara hiyo kukaa na Wizara ya Maliasili na Utalii kupata ufumbuzi wake na hilo litatekelezwa haraka.


"Tunafahamu changamoto wanazokumbana nazo wachimbaji wetu maeneo ya hifadhi lakini lazima tukubali tunaowajibu kulinda na kuhifadhi mazingira lakini eneo lenye leseni lazima uchimbaji ufanyike kwa kufuata sheria na taratibu zilizopo."


Awali Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini Tanzania Mhandisi Filbert Rweyemamu amesema ili wafanye kazi zao ufanisi ni lazima kuwepo kwa mahusiano mazuri kati ya Mkusanyiko wa hiari wa watafiti,wachimbaji na watoa huduma katika sekta ya Madini.


Amesema kupitia mikutano hiyo ukiwemo wa leo wametoa taarifa muhimu za maendeleo ya shughuli zao pamoja na kuieleza Serikali mambo yanaweza kurahisisha shughuli zao.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Tembo Nickel Benedick Masunzu amesema katika Mradi wao wa uchimbaji wa Madini aina ya Nickel fedha ni muhimu zaidi na tayari kampuni hiyo imefanikiwa kupata kiasi cha fedha kitakachosaidia kuanza uzalishaji wa madini hayo ifikapo mwaka 2026.


Wakati huo huo Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Faru Ghraphite inayotarajia kuchimba madini hayo kwenye mgodi wa Mahenge mkoani Morogoro Alimiya Othman amesma Wizara ya Fedha na Benki Kuu ya Tanzania( BOT) wameweza kutafuta suluhisho kutatua changamoto za kifedha kwa kuwa wao ni wadau wakubwa.
Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini Tanzania Mhandisi Filbert Rweyemamu






















Share:

TUME YA MADINI YATOA SIKU SABA KWA WAMILIKI WA LESENI KUTEKELEZA MASHARTI










 Dodoma Julai 19, 2023 

Tume ya Madini imetoa siku saba kwa wamiliki wote wa leseni za madini zikiwemo leseni za utafutaji wa madini, leseni za uchimbaji mdogo, wa kati na mkubwa wa madini, leseni za uchenjuaji wa madini, leseni za uyeyushaji wa madini na leseni za usafishaji wa madini kuhakikisha wanatekeleza masharti  ya leseni zao kwa mujibu wa Sheria.

Agizo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula leo jijini Dodoma kwenye mkutano wake na waandishi wa habari alipokuwa akitoa ufafanuzi wa masuala kadhaa ya Sekta ya Madini.

Amesema kuwa, zipo kampuni za  madini ambazo zimeaminiwa na Serikali kwa kupewa leseni za madini lakini wamekuwa wakikiuka masharti ikiwa ni pamoja na kutoendeleza maeneo ya uchimbaji wa madini hivyo kukosesha fursa kwa waombaji wengine wenye nia ya kuchimba madini na Serikali kupata mapato yake.

“ Tumetoa muda wa siku saba ( kuanzia tarehe 19 hadi 25 Julai, 2023 kwa wamiliki wote kutekeleza masharti ikiwa ni pamoja na wamiliki wote wa leseni za madini ambao leseni zao zimetoka lakini hawajazichukua kuhakikisha wamezichukua, leseni ambazo hazijalipiwa ada ya pango ya mwaka kuhakikisha wamelipia na leseni ambazo hazijaendelezwa kuhakikisha zinaendelezwa ndani ya muda ulioainishwa sambamba na kuwasilisha taarifa ya kuanza kazi na taarifa za kila robo mwaka kuwasilishwa,” amesema Profesa Kikula.

Katika hatua nyingine, Profesa Kikula amewataka waombaji wote wa leseni za madini wenye mapungufu kurekebisha mapungufu hayo ndani ya siku saba ikiwa ni pamoja na maombi ambayo hayajalipiwa ada ya maombi, maombi yaliyokosa viambatisho muhimu kwa mujibu wa sheria na waombaji waliokidhi vigezo vya kupewa leseni lakini hawajalipa ada ya maandalizi  na ada ya pango kwa mwaka.

Akielezea hatua zitakazochukuliwa kwa wamiliki au waombaji wa leseni watakaoshindwa kurekebisha mapungufu ndani ya muda wa siku saba, Profesa Kikula amefafanua hatua hizo kuwa kwa leseni ambazo hazijalipiwa ada ya pango ya mwaka, leseni ambazo haziendelezwi na leseni ambazo  zimeshatolewa lakini hazijachukuliwa zitafutwa kwa mujibu wa sheria na kwa maombi yote ya leseni ambayo hayakidhi vigezo, yataondolewa kwenye mfumo wa utoaji na usimamizi wa leseni ili waombaji wengine wenye sifa waweze kuomba maeneo hayo.

Aidha, Profesa Kikula amesisitiza kuwa dhumuni la Serikali ni kuweka mazingira rahisi na wezeshi kwa wawekezaji wote nchini na kuongeza kuwa Serikali haitamfumbia macho mwekezaji wa ndani au kutoka nje ya nchi ambaye ameshikilia maeneo bila ya kuyaendeleza au kuyatumia maeneo hayo kujipatia fedha kisha kuwekeza nje ya nchi.

Pia, Profesa Kikula ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo katika madini ya kimkakati yanayohusika katika utengenezaji wa vifaa vya kisasa na kieletroniki ikiwemo magari yanayotumia umeme ambayo ni rafiki kwa mazingira.

Wakati huohuo, Profesa Kikula ameongeza kuwa Serikali imekamilisha kanuni za wajibu wa wamiliki wa leseni za madini kwa jamii za mwaka 2023 ambazo zitasaidia wamiliki wa leseni kuwa na mwongozo wa namna bora ya kutoa huduma kwa jamii zinazozunguka migodi yao.

Share:

TANZANIA YABAINISHA HATUA INAZOCHUKUA KUELEKEA USAWA WA KIJINSIA


Na WMJJWM, Kigali, Rwanda

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameshiriki mdahalo wa hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa Ahadi za Nchi kwenye Jukwaa la kizazi chenye usawa.

Katika Mjadala uliofanyika Julai 18, 2023 jijini Kigali, ikiwa ni sehemu ya Mkutano wa Women Deliver, Mhe. Dkt. Gwajima amebainisha maeneo makuu ya vipaumbele, ili kutekeleza ahadi hizo ikiwa ni pamoja na kutokomeza Ukatili wa Kijinsia, uwezeshaji wa Wanawake Kiuchumi, Ushiriki wa Wanawake katika kufanya maamuzi, na uingizaji wa Jinsia katika Sera za Kisekta.

Aidha, ameelezea jinsi gani Tanzania inaendelea kuhakikisha wanawake wanainuliwa kiuchumi ambapo, imehamasisha na kuratibu kuundwa kwa Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake kiuchumi kuanzia ngazi ya taifa, mikoa, wilaya na hadi kata na vijiji.

Ameelezea pia jinsi gani Tanzania iko mstari wa mbele kuhakikisha wanawake wanawezeshwa kwenye kushika nafasi za uongozi wa juu akitoa mifano kadhaa ya viongozi wa kitaifa kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi Zanzbar na Tanzania Bara.

Katika hatua nyingine, Waziri Dkt. Gwajima ameeleza jinsi Tanzania inavyoendelea kutumia mabaraza ya watoto kama mojawapo ya chombo cha kufanya sauti za watoto wa shule za msingi na sekondari kusikika na kusikilizwa.

Akiwasilisha mada kwenye mjadala uliohusu umuhimu wa wasichana kushiriki kwenye mijadala ya maamuzi ya kisera, Mhe. Dkt. Gwajima amebainisha kuwa, matokeo ya sauti hizo ni kuanzishwa kwa Madawati ya ulinzi wa watoto katika Shule za msingi na sekondari nchini.

Aidha, ametoa wito kwa Wadau mbalimbali kuja kushirikiana na Tanzania kwenye mipango hii. Ameishukuru taasisi ya BRAC kwa ushirikiano wao kwenye mpango wa kufikia vijana takribani 500000 (laki tano) kupitia mkataba wa mashirikiano na Wizara.

Katika Mijadala hiyo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Riziki Pembe, ameshiriki pamoja na viongozi wengine kutoka Tanzania akiwemo Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Mgeni Hassan Juma na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii Mhe. Fatma Toufic.

Viongozi wengine ni Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar Abeida Rashid Abdallah pamoja Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju.

Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger