Tuesday, 18 July 2023
Monday, 17 July 2023
CCM: UWEKEZAJI BANDARI DAR HATUTARUDI NYUMA, SERIKALI ONGEZENI KASI KUKAMILISHA MCHAKATO
Na Mwandishi Wetu-Michuzi TV- Mtwara
CHAMA Cha Mapinduzi( CCM) kimeitaka na kuisisitiza Serikali kuhakikisha inaharakisha mchakato wa uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam na kwenye hilo Chama hicho hakitarudi nyuma na wala hakitayumbishwa na wanaopinga uwekezaji huo.
Akizungumza katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara kwenye mkutano mkubwa wa hadhara, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi( CCM) Daniel Chongolo amesema wanaohoji kuhusu uwekezaji huo wanajua wakiacha ikatekeleza yote kwa ufanisi kazi yao ni ngumu huko mbele ndio maana wanahaingika kukwamisha
"Sasa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ukiangalia ibara ya 22 inaeleza namna mipango ya uwekezaji ikiwemo bandari ilivyondikwa na kuainishwa wazi lakini ukienda kwenye ibara ya 59 ukurasa wa 92 wa Ilani yetu imeweka wazi kwa kuanisha namna mipango ya uwekezaji ilivyo kwenye bandari nchini.
"Leo wanaamisha ajenda hawataki kujadili Ilani ya uchaguzi na kwamba huu ni utekelezaji wa Ilani ili ninyi mbakie mkifikiri linalotekelezwa sio la kwenu , hili linalotekelezwa ni la CCM, ni ahadi ya CCM na tunatekeleza wana CCM...
"Kwasababu ndio tumepewa dhamana ya kuongoza nchi na hatuna mahali pengine , hatuna msalia mtume , hatuna hofu , hatuna mashaka hili jambo tutalitekeleza kwasababu ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi. Wanaohangaika kuibadilisha na kuifanya iwe ya Rais wamekosea muelekeo wa kulifanya liende huko wanakotaka.
"Tumewagundua, tunawajua , tunajua njia wanazotumia na ndio maana tunaitwa Chama tawala nchini , tunaona kuna watu wamekaa kienyeji, wajifunze kwamba kuongoza nchi sio kazi lelemama , kupepeta mdomo ni kazi rahisi kutenda ni kazi ngumu, " amesema Chongolo.
Amesisitiza ushabiki, uzushi ni kazi rahisi lakini kazi ya kutenda ni kazi ngumu haina msalia mtume haina lele mama na kwamba yeye Katibu Mkuu na Mtendaji Mkuu wa Chama hicho toka jana na leo anarudia tena kuitaka Serikali iongeze kasi kwenye mchakato ili wafike mwisho na kupata matokeo yake na sio vinginevyo .
"Ukimuona adui yako anakupigia makofi unapofanya jambo achana nalo haraka kimbia tengeneza mkakati mpya wa kulitenda lakini ukimuona amenuna , anahangaika anapambana lisifanikiwe nyoosha mguu kanyaga mwendo hiyo ndio kwako faida.
" Na hili ninyi ni mashahidi angalieni sura zao, matamanio yao wote hawataki litokee , niwahakikishie litatokea tuko salama na tutafikia malengo na ndio kazi ya Chama kinachojitambua , chama chenye wajibu .Ni wahakikishie mambo yakitokea mapato yakiongezeka tunashindwaje kuongeza hata Newala kukawa na uwanja wa ndege mkubwa wa kisasa.
"Suala ni uwezo, ni wahakikishie na nisisitize tuko imara, tuko timamu wala hatuna habari ya kutumia muda mwingi , najua wana CCM mnajitambua mnajua dhamana yenu na wajibu wa kuisimamia Serikali itekeleze Ilani inavyotakiwa , tusome, tuelimishe wenzetu tusimamie hapo hapo, " amesema Chongolo.
MBUNGE UMMY MWALIMU ACHANGIA MILIONI SITA NA LAKI TATU (6,300,000) KUWEZESHA WAJASIRIAMALI NA VIJANA NGAMIANI KATI JIJINI TANGA









Mbunge wa Tanga Mjini, Mhe Ummy Mwalimu leo tarehe 16/07/2023 ametembelea Kata ya Ngamiani Kati ambapo pia amechangia kiasi cha shilingi milioni sita (6,000,000/-) kwa vikundi vitatu vya Wajasiriamali ambavyo ni Nguvu Kazi kilichopo barabara 12 Mnadani, Mtaa wa Makoko; Kikundi cha Kuonda Mai cha Wafanyabiashara wa kuku kilichopo Sokoni Ngamiani na Kikundi cha Wazee kilichopo mtaa wa Maua. Kila kikundi, kimepatiwa kiasi cha shilingi milioni 2.
Aidha, Mh Mbunge amechangia shilingi laki 3 kwa ajili ya kukarabati Sehemu ya kufanya mazoezi ya ngumi kwa vijana katika mtaa wa Karafuu.
Mhe Ummy ameeleza kuwa licha ys majukumu ya kitaifa aliyonayo ataendelea kutimiza wajibu wake kikamilifu wa kuwatumikia wananchi wa Tanga Mjini hususani kutatua kero za maendeleo ya wananchi kupitia fedha za Serikali Kuu, Fedha za Halmashauri pamoja na mshahara wake na posho.
Akizungumza baada ya kupokea mchango huo kwa niaba ya vikundi vingine, Ndugu Sadik Ali Mwenyekiti wa Kikundi cha Nguvukazi alimshukuru Mhe Mbunge kwa kuendelea kuwajali wananchi wake.
Katika ziara hii, Mhe Ummy aliongozana na Mhe Habibu Mpa, Diwani wa Kata ya Ngamiani Kati, Mhe Fatuma Kitogo, Diwani wa Viti Maalum pamoja na Viongozi wa CCM ngazi ya Kata na matawi.
Imetolewa na;-
Ofisi ya Mbunge, Jimbo la Tanga Mjini
16/07/2023
CHALAMILA AHIMIZA MAZOEZI KUJIKINGA NA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila aliwasihi wananchi kufanya mazoezi ili kuimarisha afya ya mwili hivyo kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza. Chalamila aliyasema hayo alipozindua maandalizi ya CRDB Bank Marathon inayotarajiwa kufanyika Agosti 13 jijini Dar es Salaam ikiwashirikisha wakimbiaji 7,000 kutoka kila pembe ya dunia.
“Mlio hapa naamini kabisa mnafahamu umuhimu wa mazoezi kwa afya zetu hasa katika kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza. Mimi binafsi nawasihi wana Dar es Salaam kufanya mazoezi kwa ajili ya afya zetu. Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan amekuwa akituasa sana juu ya umuhimu wa kufanya mazoezi. Nimefurahi leo kuwa hapa kwani nimepata wasaa wa kuchangamsha damu kidogo,” amesema Chalamila. 

Mkuu huyo wa mkoa amesema kwa muda mrefu amekuwa akizisikia mbio za CRDB Bank Marathon na baada ya kuja mjini sasa amepata nafasi ya kushiriki maandalizi ya msimu wa nne wa mbio hizo za hisani za kimataifa.
Zilipoanzishwa mwaka 2019, mbio hizo zilikusudia kufanikisha matibabu ya watoto 100 wenye matatizo ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na mwaka uliofuata fedha zilizopatikana zikijenga kituo cha huduma katika Taasisi ya Saratani Ocean Road kabla mwaka jana hazijawanufaisha wanawake wenye fistula na ujauzito hatarishi katika Hospitali ya CCBRT.
Kwenye mbio za mwaka huu, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema watafanikisha matibabu ya upasuaji wa moyo kwa Watoto, matibabu ya wanawake wenye ujauzito hatarishi na wale wenye fistula pamoja na kujenga kituo cha afya visiwani Zanzibar.“Haya ni makundi muhimu katika jamii yetu na wana uhitaji wa kuwa na afya njema, ni nguvukazi ya kutosha kushiriki ujenzi wa Taifa letu. Fedha zote zinazopatikana kutoka kwa washiriki wa CRDB Bank Marathon zitatumiwa kwa malengo haya yaliyotajwa hivyo kila mshiriki anachangia upatikanaji wa huduma bora za afya.
Nawasihi Watanzania wenzangu hasa kutoka Dar es Salaam na nchi nzima kwa ujumla kujisajili ili kushiriki mbio hizi huku kwani kwa kufanya hivyo tutakuwa tunaweka tofauti katika jamii na kuacha alama chanya,” amesema Nsekela.Kujiandikisha kwenye mbio hizi zitakazoishirikisha familia nzima zikiruhusu wakimbiaji wa kilomita tano, 10, 21 na 42, kwa mtu mmoja ni Sh45,000 tu lakini kwa kikundi cha kuanzia watu 30 ni Sh40,000 kila mmoja.
--









