Thursday, 16 June 2022

TAASISI YA IIA YAIPONGEZA SERIKALI KUIMARISHA VITENGO VYA UKAGUZI WA NDANI


Rais na Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Ukaguzi wa ndani Tanzania (IIA), CPA Zelia Njeza akizungumza.
Rais na Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Ukaguzi wa ndani Tanzania (IIA), CPA Zelia Njeza akizungumza.

Na Mwandishi Wetu

TAASISI ya Ukaguzi wa ndani nchini Tanzania (IIA) imeipongeza Serikali ya Tanzania dhidi ya mabadiliko makubwa iliyopanga kuyafanya kupitia Makadirio ya Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2022/23 ili kuimarisha vitengo vya ukaguzi wa ndani.


Akizungumza leo Jijini Dar es Salaam, Rais wa Taasisi ya Ukaguzi wa ndani, IIA, CPA Zelia Njeza amesema hatua hiyo ni kubwa kwa Serikali na inakwenda kuongeza ufanisi zaidi kwenye sekta ya ukaguzi wa ndani.


“…Kwanza tunaipongeza Serikali kwa kupeleka mapendekezo haya ya kutaka kufanya mabadiliko makubwa kwenye fani ya wakaguzi wa ndani, ambayo yanaanzia kufanywa kwa kukiboresha kitengo cha Mkaguzi Mkuu wa ndani, ‘Internal Auditor General (IAG)’,” alisema CPA, Njeza.


Aidha CPA, Njeza ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya IIA alibainisha kuwa taasisi hiyo inaamini endapo mapendekezo hayo yatapitishwa umma utarajie ufanisi mkubwa kuongezeka na pia kuboresha utawala bora pamoja na kupungua vitendo vya ubadhirifu wa fedha.


“Wananchi wategemee kuongezeka kwa ufanisi katika utendaji na utawa bora, hasa katika matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo eneo ambalo limekuwa na changamoto kidogo hapo awali.

Ametoa wito kwa wakaguzi wa ndani kujipanga katika utendaji ili kuiunga mkono Serikali dhidi ya mabadiliko makubwa ambayo imedhamiriya kuyafanya katika sekta hiyo.


Katika hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba (MB), akiwasilisha bungeni mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2022/23 bungeni Dodoma jana alibainisha kuwa, Serikali imepanga kuimarisha vitengo vya ukaguzi wa ndani kwa kuvijengea uwezo wa kitaaluma na kuongeza idadi ya watumishi katika fani mbalimbali kama vile TEHAMA, uhandisi, ukadiriaji majenzi, wakemia, wanasheria na fani nyingine ili kuondokana na dhana ya wakaguzi wa ndani kuwa na taaluma ya fedha pekee.


Waziri Dkt. Nchemba amesema, Serikali itafanya marekebisho ya Kanuni za Fedha za Umma kwa kuziwezesha Kamati za Ukaguzi kuwa na wajumbe wa nje watatu ikiwemo Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi ili kuongeza uhuru na ufanisi wa kamati za ukaguzi kupitia Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2022.


Pamoja na mambo mengine, ameongeza kuwa Serikali itafanya marekebisho ya Kanuni zitakazo itazitaka Kamati za Ukaguzi kuwasilisha taarifa za ukaguzi wa ndani kwa Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali kila robo mwaka, ikiwa ni pamoja na kutathmini muundo na majukumu ya Idara ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali ikiwemo kufanya stadi ya kujifunza kutoka nchi nyingine zenye Idara ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu Serikali kama Tanzania ili kuangalia muundo unaostahili na kukidhi mahitaji ya Idara hiyo kutekeleza majukumu yake kwa uhuru na ufanisi.


"...Vilevile napendekeza Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali kuwa na fungu lake (Independent Vote) pamoja na kuongeza idadi ya wakaguzi wa ndani ili kuimarisha na kuboresha ufanisi katika utendaji. Napendekeza kuanzia mwaka wa fedha 2022/23 taarifa za wakaguzi wa ndani zipelekwe moja kwa moja kwa Internal Auditor General (IAG) kama alivyoelekeza Mheshimiwa Rais wakati anapokea taarifa ya CAG," alisema Waziri Dkt. Nchemba katika hotuba yake bungeni mjini Dodoma.



Share:

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO ALHAMISI JUNI 16,2022



===





















Share:

Wednesday, 15 June 2022

Video Mpya : KISIMA MAJABALA - LUGULU... NGOMA KALI KINOMA


Malunde 1 blog inakualika kutazama Video Mpya ya Msanii wa Nyimbo za asili Kisima 'Nyanda Majabala' inaitwa Lugulu...Burudika mtu wangu
Tazama video
Share:

DKT. MAHERA AHIMIZA WATANZANIA KUHESABIWA

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Dkt.Wilson Mahera Charles

Na Mwandishi Wetu, DODOMA


Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Dkt.Wilson Mahera Charles amewataka watanzania kuwa tayari kushiriki kikamilifu zoezi la Sensa ya watu na makazi litakayofanyika Agosti 23, 2022, nchini kote.

Wito huo ameutoa leo ofisini kwake jijini Dodoma na kusema kuwa zoezi la Sensa ya watu na makazi ni muhimu kwa maendeleo ya nchi kwani hata Tume ya Taifa ya Uchaguzi hutegemea takwimu za sensa kukadiria idadi ya wapiga kura wapya watakaoandikishwa pamoja na waliopoteza sifa za kuandikishwa. 

“Kimsingi wapiga kura au shughuli za uchaguzi kwa ujumla zina uhusiano mkubwa na takwimu zitokanazo na sensa, kwani katika sensa ndipo Tume inaweza kubainisha idadi ya watu itakayowaandikisha katika daftari la kudumu la mpiga kura,”amesema Dkt. Mahera na kuongeza:

“Nawahimiza watanzania wote kujitokeza kuhesabiwa kwenye sensa ya watu na makazi mwaka huu na kila mmoja kumhamasisha mwenzake kuhesabiwa.”

Amesisitiza kuwa ili Tume huyo ifanye shughuli zake vizuri ni lazima ipate takwimu sahihi za watu, makazi na kutambua makundi maalum ambayo ni ya wanawake, wazee, vijana na watu wenye ulemavu.

Mkurugenzi wa Uchaguzi ameongeza kuwa ," kutokana na sensa ya mwaka huu kufanyika kwa kutumia teknolojia ya kisasa ambayo itawezesha kutambua idadi ya majengo ya umma na makazi ya watu, Tume tutatumia takwimu hizo, kuweka vituo vya uboreshaji wa daftari la kudumu la mpiga kura,"amefafanua na kuongeza;

Sensa ya mwaka huu itafanyika kidijiti na itaweza kubainisha idadi ya majengo ya umma ambayo sisi huyatumia kuweka vituo vya kujiandikisha, lakini pia itatusaidia pia kuweka vituo hivyo kwa mujibu wa anuani za makazi ambazo pia sensa inakwenda kuzitambua rasmi,” amesema Dkt Mahera.

Dkt Mahera pia amesema Tume imekua ikipanga mipango yake kwa takwimu kuanzia ngazi ya kata lakini sasa kwa kuwa sensa inakwenda kuweka kumbukumbu hadi ngazi ya kitongoji, itaweza kupanga mipango yake kwa urahisi zaidi na matumizi ya teknolojia katika uchaguzi yataongezeka.

Sensa ya watu na makazi hufanyika kila baada ya miaka 10 na mara ya mwisho Sensa hiyo ilifanyika mwaka 2012 ambapo watanzania milioni 44,929 walihesabiwa. 


Share:

AZUA GUMZO BAADA YA KUFANYA MAZISHI YA KUMKEJELI MKEWE ALIYE HAI


Mwanaume mmoja katika kijiji cha Emakhwale, kaunti ya Kakamega nchini Kenya amewaacha wakazi wa eneo hilo na mshangao baada ya kufanya mazishi ya kejeli ya mkewe waliyeachana naye.

Jack Shiundu, 32 na mkewe Lydia Masakwe, walinunua kipande cha ardhi mwaka mmoja uliopita na walikuwa wakiishi pamoja.

Shiundu anadaiwa kuchimba shimo na kufukia jeneza hilo dogo na kulifunika kwa nguo na picha za mkewe Masakwe ambaye bado yuko hai. 

Kulingana na TV47, jeneza hilo liligunduliwa na mkulima mmoja.

Alipoichimba, pia alipata kile kilichoonekana kama vipande vya nywele za binadamu ndani ya jeneza.

 Hata hivyo, familia ya Masakwe sasa imewataka polisi kumkamata mshukiwa mbaye ameingia mafichoni.

 Katika kisa cha awali  tuliliripoti kwamba polisi katika kaunti ya Embu wanachunguza kisa ambapo mzee wa miaka 70 anadaiwa kumdunga kisu mkewe hadi kufa baada ya kutofautiana kuhusu KSh 6000. Marehemu mwenye umri wa miaka 42, aliripotiwa kutoweka na pesa walizolipwa baada ya kuuza mbuzi.

Akithibitisha kisa hicho, kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Embu Mashariki Benjamin Muhia alisema baada ya kutoweka, mwanamke huyo alirejea nyumbani akiwa mlevi bila senti hata moja.

 Chifu wa kijiji cha Thau Daniel Ndwiga alisema alipata taarifa ya tukio hilo mwendo wa saa kumi na mbili jioni na alipofika eneo la tukio aliwakuta majirani waliokuwa na hasira wakipanga kumuua mshukiwa.

 Majirani wa wanandoa hao walisema walikuwa na mizozo ya nara kwa mara na hata wiki jana walikuwa na kesi katika fisi ya chifu.
Share:

TGNP YAWAKUTANISHA WADAU KUPITIA KIJIWE CHA KAHAWA KUFUATILIA BAJETI KUU YA SERIKALI 2022/2023


Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP,) Lilian Liundi akizungumza wakati wa mjadala wa bajeti ya fedha ya Taifa kwa mwaka 2022/2023 na kueleza kuwa jitihada zaidi zinahitajika katika sekta ya kilimo ambayo ushiriki wa wanawake ni mkubwa lakini ukuaji wake umekuwa mdogo, Juni 14,2022 jijini Dar es Salaam.


MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP,) umeendelea kuamini katika nguvu ya pamoja kwa kukutana na wadau na wanachama wa mtandao huo na kufuatilia mgawanyo wa rasilimali kwa kupitia bajeti kwa jicho la kijinsia.

Akizungumza wakati wa tafakari ya bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 kupitia jukwaa la Kijiwe cha Kahawa Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP,) Lilian Liundi amesema kuwa jukwaa hilo litawasaidia wanajamii na wadau wa maendeleo kutambua fursa na vipaumbele vilivyoainishwa katika bajeti pamoja na mapungufu ya kijinsia yaliyopo katika bajeti ya mwaka husika na kutoa mapendekezo kwa watunga sera na wahusika kuboresha zaidi ili kuwa na bajeti yenye kujenga uchumi na maendeleo endelevu kwa taifa.

Lilian amesema kuwa, bado kuna changamoto katika sekta za maji na kilimo katika bajeti ya mrengo wa kijinsia na takwimu zimekuwa zikiangalia changamoto hizo kwa maeneo ya mjini pekee na kuishauri Serikali kuu kwa kushirikiana na Serikali za mitaa kupitia Sensa ya watu na makazi inayokwenda kufanyika ilete takwimu sahihi ya wananchi, mahitaji yao pamoja na mgawanyo wa rasilimali kwa mrengo wa kijinsia.

Amesema katika sekta ya kilimo ambayo ina uhakika wa chakula na ushiriki wengi wa wanawake ukuaji wake ni kati ya asilimia 3 hadi 5 na bado uwekezaji wake hauna mkazo na kushauri maagizo na maelekezo yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan katika hotuba yake ya kwanza Bungeni juu ya kutumia malighafi za viwandani kutoka kwa wakulima wazawa litiliwe mkazo ili kujenga uchumi shindani kwa maendeleo endelevu.

Mwanamtandao wa TGNP kutoka Kishapu, Shinyanga Bi. Fredina Said katika kueleza changamoto wanazokumbana nazo akina Mama kujenga uchumi wa taifa kwa mrengo wa kijinsia amesema, upatikanaji wa maji safi na salama bado imeendelea kuwa kikwazo kwa wanawake katika kushiriki katika shughuli za kiuchumi katika Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.

Amesema kuwa Kata nyingi wilayani humo nyingi zimepitiwa na mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Viktoria ila bado hazijafikiwa na huduma hiyo kutokana na gharama ambazo wananchi hawawezi kuzimudu.

‘’Mimi natoka Kata ya Kiloleli kuna kata nyingi ambazo nyingine hazifanyi kazi na TGNP ila zina changamoto kubwa ya maji kuna Kata nyingi hazijapata huduma ya maji licha ya kupitiwa na mradi huo mkubwa…Gharama za kuunganishiwa maji zimefikia hadi shilingi laki mbili na themanini na unit moja inalipiwa shilingi elfu mbili kiasi ambacho mwanamke wa kijijini hawezi kukimudu’’,amesema.

Ameeleza kuwa katika harakati za kumtua Mama ndoo kichwani Serikali kupitia bajeti lazima iangalie namna bora ya kutatua changamoto za umbali na gharama ili wanawake ambao ndio wazalishaji wakubwa wajikite katika shughuli za uzalishaji mali.

‘’Baadhi ya Kata zinafuata maji kwa umbali wa Kilomita 15 na maji hayo sio salama na katika harakati hizo hukumbana na unyanyasaji wa kijinsia, mimba za mapema na hata kwa utoro kwa mabinti kutokana na hedhi na shuleni hakuna taulo wala maji ya kuwasitiri’’,amesema.

Raheli Misesi kutoka Kishapu, Shinyanga ameeleza katika sekta ya kilimo ambayo wanawake wanashiriki kwa asilimia 80 ni vyema Serikali ikaweka mkazo na juhudi mahususi katika kuboresha kilimo cha umwagiliaji hasa kwa wakulima wadogo vijijini.

‘’Kwa Wilaya ya Kishapu kwa mwaka huu kumekuwa na ukame hakuna mazao kwa sasa debe moja la mahindi linauzwa shilingi elfu kumi na nne hiki ni kiashiria kikubwa cha njaa ni vyema Serikali ikaweka juhudi kwa kuboresha kilimo cha umwagiliaji pamoja na teknolojia za kilimo ikiwemo matumizi ya trekta kwa wakulima wadogo na hiyo ni pamoja na kufanya tafiti kwa mbegu na mbolea za asili ambazo zinafanya vizuri katika ukuaji wa mazao.’’ Amesema.

Aidha amesema kuwa katika kuhakikisha bajeti inakuwa katika mrengo wa kijinsia wametembelea Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuzungumza na wanawake na akina baba vinara kuhusu changamoto hizo na kushauri namna ya kuongeza bajeti kama TGNP wanavyofanya.

Kuhusiana na sekta ya afya ameishukuru Serikali kwa jitihada za ujenzi wa vituo vya afya na kuiomba kuelekeza nguvu zaidi kwa kupeleka wahudumu wa kutosha pamoja na vifaa tiba.

Jukwaa hilo lililoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP,) limewakutanisha wananchi, wanajamii, wachambuzi, wanasiasa na wanachama wa mtandao huo na kusikiliza kwa pamoja uwasilishwaji wa bajeti ya Taifa na kutafakari na kujadili kwa mrengo wa kijinsia kwa namna ambavyo bajeti kuu imeakisi kupitia sauti za wanajamii.

Afisa Kiongozi wa Programu kutoka TGNP Bi. Joyce Mkina akiwasilisha mada katika jukwaa hilo.
Mtafiti wa masuala ya bajeti na mwanachama ya TGNP Edward Mhina akiwasilisha mada katika jukwaa hilo.
Mhandisi Wilhelma Malima kutoka shirika la Sanitation and Water Action (SAWA,) akichangia mada katika jukwaa la Kijiwe cha Kahawa maalumu kwa bajeti ya fedha ya mwaka 2022/2023.
Matukio mbalimbali wakati wa mjadala huo.
Share:

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMATANO JUNI 15,2022


Magazetini leo Jumatano June 15,2022














Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger