Sunday, 1 August 2021
Picha : BITEKO AFUNGA MAONESHO YA BIASHARA NA TEKNOLOJIA YA MADINI SHINYANGA....ATANGAZA KUZINGUA WALIOSHIKILIA LESENI ZA UCHIMBAJI
Vyombo Vya Ulinzi Na Usalama Na Mapambano Dhidi Ya Corona
Na Abubakari Akida, MOHA
Vyombo vya Ulinzi na Usalama nchini vimetakiwa kutokujiweka kando na mapambano dhidi ya ugonjwa wa Virusi vya Korona katika kipindi hiki ambacho nchi inapitia katika vita ya wimbi la tatu la ugonjwa huo.
Rai hiyo imetolewa leo mkoani Tabora na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo wakati akizungumza na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama mkoani hapo ambapo ameeleza mapambano ya ugonjwa huo ni suala linalotakiwa kushirikisha wizara zote zikiongozwa na wizara husika ya afya.
“Vyombo vya Ulinzi na Usalama mnayo nafasi kubwa katika mapambano dhidi ya maradhi ya Virusi vya Korona,mna mahabusu wako vituo vya polisi sehemu mbalimbali nchini,mna mahabusu wako katika magereza,tuna askari wetu wa usalama barabarani basi ili mradi kila sehemu mnahusiana na jamii moja kwa moja hivyo natoa wito kwa vyombo vyetu vyote vya ulinzi na usalama nchi nzima mhakikishe katika kazi zenu za kila siku mtoe elimu ya kujikinga na maradhi hayo” alisema Naibu Waziri Chilo
“lakini pia tahadhari hiyo ya kujikinga na maradhi hayo pia iende kugusa shughuli zenu za kila siku ikiwemo na nyie wenyewe kujikinga ili tusipoteze nguvu kazi ya taifa,Rais Samia Suluhu Hassani anawategemeeni sana katika kulinda amani na utulivu wan chi hii” aliongeza Naibu Waziri Chilo
BONYEZA HAPA KUJUA VITUO VITAKAVYOTOA CHANJO YA CORONA TANZANIA
“Mheshimiwa Naibu Waziri katika mkoa wetu kulikuwepo na matukio ya kihalifu ikiwemo mauaji,Watoto watukutu kujikusanya makundi na kufanya uhalifu katika sehemu mbalimbali ikiwemo uporaji lakini sasa hivi tumedhibiti hiyo hali na sasa mkoa uko salama ama kwa upande wa mauaji tulikua tunashuhudia mauaji ya watu watatu mpaka watano kwa wiki lakini sasa hivi matukio hayo yameisha kabisa huku jeshi likiendelea kuimarisha ulinzi kupitia doria tulizonazo” alisema ACP Sophia Jongo
Naibu Waziri yuko mkoani Tabora kwa ziara ya kikazi ambapo anatumia ziara hiyo pia kutembelea makazi ya wakimbizi ya Ulyankulu yaliyopo wilayani Kaliua ambayo yanatumiwa na wakimbizi waliokimbia machafuko ya kikabila nchini Burundi.
Wachimbaji Wadogo Kupokea Kifuta Jasho Cha Milioni 90 -Singida
Na. Steven Nyamiti – Mkalama Singida
Jumla ya Wachimbaji Wadogo wa Dhahabu 90 katika eneo la kijiji cha Tumuli wataanza kupokea kifuta jasho kuanzia tarehe 2 Agosti, 2021 baada ya utaratibu wa kupewa kifuta jasho kukamilika.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Madini Doto Biteko tarehe 31 Julai, 2021 katika kijiji cha Tumuli wilaya ya Mkalama Mkoani Singida wakati wa ziara ya kukagua na kutembelea shughuli za wachimbaji wadogo.
Ameeleza kuwa, wachimbaji watakaopokea kifuta jasho hicho ni wale walioandikishwa na ambao taarifa zao zipo kwenye Kanzidata kufuatia kuondolewa kuchimba kwenye eneo lenye leseni.
“Mgogoro huu una historia ndefu sana zaidi ya miaka 9, mwanzo walikua wachimbaji 26 wanaopaswa kupewa lakini sasa wameongezeka zaidi ya 100, lazima tutende haki kwa watu wote kuanzia mchimbaji hadi mwekezaji ili pande zote ziridhike,” amesema Biteko.
Aidha, Waziri Biteko ameagiza mgodi wa Chama cha Ushirika cha Uchimbaji Madini (Sekenke One Mining Cooperative Society) uliosimamishwa mwezi Disemba 2019, kutokana na zuio la kiusalama katika mgodi huo ufunguliwe mara moja ili shughuli za uchimbaji ziendelee.
Biteko amemuagiza Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Singida, Chone Lugangizya kuzungumza na kampuni ya Sekenke One ili wakubaliane waendelee kuchimba dhahabu kwa kuzingatia Sheria na Taratibu.
“Mimi ninachotaka kuona shughuli zinaendelea, utaratibu wa kufunga funga migodi huu huwa hautusaidii sana, tunaopoteza ni sisi, tunachotaka kuona wachimbaji wanarudi kwenye uchimbaji ili masoko haya yaweze kupanuka Zaidi,” amesisitiza Biteko.
Kuhusu utatuzi wa mgogoro baina ya Nabii Elia Makuli na kikundi cha Bathlomew Waziri Biteko amerejesha suala hilo kwenye ngazi ya Mkoa na Wilaya kwa ajili ya kulitatua ambapo Mkuu wa Wilaya ya Iramba Suleiman Mwenda amehaidi kufanyia kazi mgogoro huo kuanzia siku ya Jumatatu tarehe 2 Agosti.
Naye, Mkuu wa wilaya ya Mkalama Sophia Kizigo amethibitisha kuwa wilaya yake imepokea fedha hizo kutoka kampuni ya uchimbaji madini ya PuBo (PuBo Mining Limited) kiasi cha Shilingi Milioni 90 ambazo zimekabidhiwa kwenye ofisi ya TAKUKURU ili kifuta jambo hicho wapatiwe wananchi 90 waliopo kwenye kanzidata ambao watapokea kiasi cha Shilingi Milioni moja kila mmoja.
Kizigo ametoa onyo kwa wachimbaji wanaotaka kufanya udanganyifu ili kuongezea majina zaidi ya yale yanayotambulika.
“Wapo wananchi wananipigia simu wakitaja kuwa wao ni sehemu ya kupata kifuta jasho hicho, majina yao hayapo kati ya majina 90 ambayo tumeyapokea kutoka ofisi ya madini, nasisitiza tutafuata kanzidata ya Wizara ya Madini kama Waziri alivyoelekeza,” amesema Kizigo.
Waziri Biteko amehitimisha ziara ya siku mbili Mkoani ambapo ametembelea wachimbaji wadogo na kukagua Mgodi wa Kati wa Shanta, kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wachimbaji wadogo pamoja na kutoa elimu ya Sheria ya madini kwa wadau waliojitokeza. Katika ziara hiyo pia aliambatana na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahembe na Viongozi mbalimbali wa Serikali ya Vijiji na Halmashauri
Waziri Mkuu Mgeni Rasmi Uzinduzi Mafunzo Ya Uanagenzi Mbeya
Na. MWANDISHI WETU
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika Uzinduzi wa Programu ya Mafunzo ya Uanagenzi kwa Awamu ya Tatu tarehe 2 Agosti, 2021 katika Chuo kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST).
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alipokutana na Waandishi wa Habari kwenye Ukumbi wa Chuo cha MUST kwa lengo la kutoa taarifa kwa umma kuhusu tukio la uzinduzi huo na shughuli zitakazoambatana na uzinduzi.
Kaulimbiu katika uzinduzi huu ni “NGUVUKAZI YENYE UJUZI STAHIKI, MSINGI IMARA KATIKA MAENDELEO YA TAIFA”. Kaulimbiu hii inatokana na dhana nzima ya masuala ya ajira, inatoa fursa kwa kila mmoja kuweza kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi, ambapo anahitaji kuwa na ujuzi stahiki unaohitajika kufanya shughuli husika.
Akifafanua kuhusu programu hiyo, alieleza kuwa Ofisi yake imeendelea kuimarisha utekelezaji wa Programu ya Kukuza Ujuzi nchini kwa kuhakikisha inawafikia vijana wengi zaidi katika Mikoa yote nchini ambapo Programu hii ina vipengele vikuu vinne (4) ambavyo ni mafunzo uzoefu wa kazi kwa wahitimu (internship), urasimishaji wa ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa mafunzo (RPL), mafunzo ya uanagenzi (apprenticeship) na mafunzo ya kuhuisha ujuzi kwa wafanyakazi (skills upgrading).
Mafunzo ya Uanagenzi yanahusisha mhusika kutumia asilimia 40 ya muda wake kwa masomo ya nadharia darasani na asilimia 60 ya muda wake kwa masomo ya vitendo sehemu ya kazi. Mafunzo haya ni ya muda wa miezi sita na yalianza kutolewa Mwezi Juni, 2021 na yanatarajiwa kukamilika Mwezi Disemba, 2021 ambapo Serikali inayafadhili kwa asilimia 100 kulingana na kibali kilichotolewa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
“Tangu kuanzishwa kwa Programu ya kukuza ujuzi nchini, mafunzo ya uanagenzi yamefanyika awamu mbili ambazo jumla ya vijana 28,941 wamenufaika. Awamu hii ya tatu yanatolewa kwa vijana 14,440 na yanafanyika kupitia vyuo 72 katika Mikoa 26 ya Tanzania Bara”,alisisitiza Waziri Mhagama
Aliongezea kuwa mafunzo haya yanatolewa katika fani mbalimbali kama vile ufundi umeme wa majumbani na viwandani, umeme wa jua, useremala, ufundi magari, umeme wa magari, uchomeleaji na uungaji vyuma, utengenezaji wa vifaa vya aluminiam, upishi, uhudumu wa hoteli na vinywaji, ushonaji, uchenjuaji wa madini, ufundi bomba, ufundi uashi, uwekaji wa terazo na marumaru, ufundi viyoyozi na majokofu.
Aidha hadi Disemba, 2021 kutatarajia kuwa na jumla ya wanufaika wa kupitia programu zote nne kufikia 80,320. Kati ya hawa, vijana 43,381 ni kupitia mafunzo ya uanagenzi, vijana 20,334 kupitia mafunzo ya urasimishaji ujuzi, vijana 5,975 kupitia mafunzo ya uzoefu wa kazi (internship), vijana 9,080 (100 nchini Israel) kupitia mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa kutumia kitalu nyumba (green house), na vijana 1,550 kupitia mafunzo ya kukuza ujuzi wa waajiriwa (skills upgrading).
Sambamba na uzinduzi huo Mhe.Waziri Mkuu anatarajiwa kuwa na shughuli mbalimbali zitakazofanyika Mkoani Mbeya.
“Mhe. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atatembelea vyuo vinavyotoa mafunzo ya Uanagenzi Jijini Mbeya, atatembelea Kyela Polytechnic College, VETA Busokelo, VETA Mbeya, Chuo cha Ufundi cha Magereza Ruanda na Chuo cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) ili kuona na kukagua namna mafunzo yanavyotolewa, na kuweza kuzungumza na vijana wanaopata mafunzo husika”,alisema Waziri Mhagama.
Akihitimisha Waziri alitumia nafasi hiyo kuwaasa wananchi wote kuzingatia suala zima la afya hususan kipindi hiki ambapo tuna mlipuko wa COVID 19 nchini kwa kuchukua tahadhari zote huku wakizingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu wetu nchini.
“Ninapenda kutoa wito kwa wananchi watakaoshiriki kwenye tukio la uzinduzi huu kuchukua tahadhari zote ikiwemo kuvaa barakoa, kutumia vitakasa mikono na kunawa mikono kama inavyoelekezwa na wataalamu wa afya ili kujilinda na kulinda wengine”.
Rais Samia kufanya ziara ya kiserikali ya siku mbili nchini Rwanda
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara ya kiserikali ya siku mbili nchini Rwanda kuanzia Agosti 2, 2021 kwa mwaliko rasmi wa wa Rais wa nchi hiyo, Paul Kagame
Akiwa Rwanda, Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na mengine atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake, kisha atashuhudia utiaji saini hati za makubaliano na kuzungumza na vyombo vya habari
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu imeeleza kuwa ziara hiyo ya siku mbili inalenga kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano baina ya Rwanda na Tanzania.