Sunday, 1 August 2021

Vyombo Vya Ulinzi Na Usalama Na Mapambano Dhidi Ya Corona

...

 Na Abubakari Akida, MOHA
Vyombo vya Ulinzi na Usalama nchini vimetakiwa kutokujiweka kando na mapambano dhidi ya ugonjwa wa Virusi vya Korona katika kipindi hiki ambacho nchi inapitia katika vita ya wimbi la tatu la ugonjwa huo.

Rai hiyo imetolewa leo mkoani Tabora na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo wakati akizungumza na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama mkoani hapo ambapo ameeleza mapambano ya ugonjwa huo ni suala linalotakiwa kushirikisha wizara zote zikiongozwa na wizara husika ya afya.

“Vyombo vya Ulinzi na Usalama mnayo nafasi kubwa katika mapambano dhidi ya maradhi ya Virusi vya Korona,mna mahabusu wako vituo vya polisi sehemu mbalimbali nchini,mna mahabusu wako katika magereza,tuna askari wetu wa usalama barabarani basi ili mradi kila sehemu mnahusiana na jamii moja kwa moja hivyo natoa wito kwa vyombo vyetu vyote vya ulinzi na usalama nchi nzima mhakikishe katika kazi zenu za kila siku mtoe elimu ya kujikinga na maradhi hayo” alisema Naibu Waziri Chilo

“lakini pia tahadhari hiyo ya kujikinga na maradhi hayo pia iende kugusa shughuli zenu za kila siku ikiwemo na  nyie wenyewe kujikinga ili tusipoteze nguvu kazi ya taifa,Rais Samia Suluhu Hassani anawategemeeni sana katika kulinda amani na utulivu wan chi hii” aliongeza  Naibu Waziri Chilo

BONYEZA HAPA KUJUA VITUO VITAKAVYOTOA CHANJO YA CORONA TANZANIA


Awali akisoma taarifa ya hali ya ulinzi na usalama ya mkoa huo,Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora,Kamishna Msaidizi wa Polisi Sophia Jongo amesema kumekuwepo na kupungua kwa matukio ya uhalifu katika mkoa huo huku jeshi la polisi likiendelea na operesheni mbalimbali katika kuhakikisha matendo ya uhalifu yanapungua.

“Mheshimiwa Naibu Waziri katika mkoa wetu kulikuwepo na matukio ya kihalifu ikiwemo mauaji,Watoto watukutu kujikusanya makundi na kufanya uhalifu katika sehemu mbalimbali ikiwemo uporaji lakini sasa hivi tumedhibiti hiyo hali na sasa mkoa uko salama ama kwa upande wa mauaji tulikua tunashuhudia mauaji ya watu watatu mpaka watano kwa wiki lakini sasa hivi matukio hayo yameisha kabisa huku jeshi likiendelea kuimarisha ulinzi kupitia doria tulizonazo” alisema ACP Sophia Jongo

Naibu Waziri yuko mkoani Tabora kwa ziara ya kikazi ambapo anatumia ziara hiyo pia kutembelea makazi ya wakimbizi ya Ulyankulu yaliyopo wilayani Kaliua ambayo yanatumiwa na wakimbizi waliokimbia machafuko ya kikabila nchini Burundi.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger