Sunday, 10 November 2019

Picha : WAKE WA VIONGOZI TANZANIA WAKABIDHI MADARASA,VYOO SHULE YA BUHANGIJA SHINYANGA...

Umoja wa wake wa viongozi nchini Tanzania ‘Ladies of New Millenium Women Group’ umekabidhi madarasa manne yenye thamani ya shilingi milioni 65.8 na matundu 1o ya vyoo yanayoendelea kujengwa katika shule ya Msingi Buhangija iliyopo katika Manispaa ya Shinyanga ambayo ni maalumu kwa watoto wenye mahitaji maalumu wakiwemo wenye ualbino,viziwi na wasioona.

Madarasa na matundu hayo ya vyoo yamekabidhiwa leo Jumapili Novemba 10,2019 na Mlezi wa Umoja wa wake wa viongozi,Maria Majaliwa kwa Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia,Profesa Joyce Ndalichako wakati wa ziara yake mkoani Shinyanga.

Akizungumza wakati wa kukabidhi madarasa hayo, Mlezi wa Umoja wa wake wa viongozi,Maria Majaliwa amesema umoja huo amesema madarasa hayo yataleta tija kwa wanafunzi katika kuhakikisha wanajifunza katika mazingira bora.

“Mheshimiwa Waziri nakukabidhi majengo mawili yenye madarasa mawili kila moja na matundu 10 ya vyoo yanayoendelea kujengwa na yapo mbioni kukamilika ikiwa ni sehemu ya kuunga juhudi zinazofanywa na Rais wa awamu ya tano Dkt. John Pombe Magufuli katika kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira bora,majengo haya yamejengwa kwa ubora wa hali ya juu kwa gharama nafuu”,amesema Mama Majaliwa ambaye ni Mke wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Kassim Majaliwa.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wake wa viongozi,Tunu Pinda amesema umoja huo pia utatoa shilingi milioni 3.6 kwa ajili ya kununua madawati yatakayowekwa kwenye vyumba hivyo vya madarasa huku akiwasisitiza wanafunzi kusoma kwa bidii ili waweze kutimiza ndoto zao za maisha.

Wakiwa katika shule ya Msingi Buhangija,wake wa viongozi waliopo madarakani na waliostaafu wametoa zawadi mbalimbali kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu wakiwemo wenye ualbino,viziwi,wasiosikia na wenye ulemavu wa ngozi,zawadi hizo ni pamoja na vifaa vya kujifunzia,vifaa vya kufanyia usafi,mafuta ya kupaka,kupikia,miswaki,taulo laini,dawa za meno,sukari na kadhalika vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni nne.

Wanawake hao pia wakiongozwa na Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia,Prof. Joyce Ndalichako wamegawa chakula na kula pamoja na wanafunzi wa shule ya msingi Buhangija huku wakiupongeza uongozi wa serikali ya mkoa wa Shinyanga kwa kuendelea kuwa karibu na shule hiyo maalumu.

Akizungumza, Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako aliwapongeza wake hao wa viongozi kwa kuguswa na hali iliyopo katika shule ya Buhangija na kuamua kusaidia kujenga madarasa ili wanafunzi wasome katika mazingira rafiki.

“Niwapongeze sana akina mama kwa kujitoa kusaidia watoto hawa,hakika mmekuwa mfano wa kuigwa.Niushukuru uongozi wa mkoa wa Shinyanga kwa kusimamia ujenzi huu ambapo majengo ni mazuri,yana kiwango kikubwa cha ubora ambapo kila jengo nimeambiwa limetumia shilingi milioni 16.4 hii ni gharama ndogo,hongereni sana”,amesema Prof. Ndalichako.

Katika hatua nyingine ameitoa wito kwa jamii kuachana na mila potofu kuhusu watu wenye ualbino huku akiwataka wazazi na walezi kuacha tabia ya kuficha watoto wenye ulemavu akisisitiza kuwa watoto wote ni sawa wanatakiwa kupewa haki yao ya elimu.

ANGALIA PICHA MATUKIO YALIYOJIRI
Muonekano wa majengo mawili yenye madarasa mawili kila moja yaliyojengwa na Umoja wa wake wa viongozi nchini Tanzania ‘Ladies of New Millenium Women Group’ katika shule ya Msingi Buhangija iliyopo katika Manispaa ya Shinyanga. Majengo hayo yamekabidhiwa leo Jumapili Novemba 10,2019 na uongozi wa Umoja wa wake wa viongozi kwa Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako . Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Viongozi mbalimbali wakiwa na Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako (wa pili kulia) wakiwa katika shule ya Msingi Buhangija wakati wa makabidhiano ya madarasa manne na matundu ya vyoo 10 katika shule hiyo.
Mlezi wa Umoja wa wake wa viongozi,Maria Majaliwa akisoma taarifa ya ujenzi wa madarasa manne yaliyojengwa na umoja huo katika shule ya msingi Buhangija. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack akifuatiwa na Mwenyekiti wa Umoja wa wake wa Viongozi,Tunu Pinda na Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Jasinta Mboneko.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack akizungumza wakati wa makabidhiano ya madarasa na matundu ya vyoo yaliyojengwa na Umoja wa wake wa viongozi nchini Tanzania.
Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akikata utepe wakati akipokea madarasa manne yaliyojengwa na Umoja wa wake wa viongozi nchini katika shule ya msingi Buhangija iliyopo katika Manispaa ya Shinyanga.

Ndani ya moja ya madarasa: Kulia ni Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga,Albert Msovela akimwelezea 
Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako kuhusu ujenzi wa madarasa hayo.
Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako na viongozi mbalimbali pamoja na wake wa viongozi wakitoka katika moja ya madarasa yaliyojengwa na Umoja wa wake wa viongozi nchini Tanzania.
Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako na viongozi mbalimbali,wake wa viongozi na wanafunzi wa shule ya msingi Buhangija wakipiga picha ya pamoja nje ya madarasa yaliyojengwa na Umoja wa wake wa viongozi.
Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako na viongozi mbalimbali,wake wa viongozi na wanafunzi wa shule ya msingi Buhangija wakipiga picha ya pamoja nje ya madarasa yaliyojengwa na Umoja wa wake wa viongozi.
Kulia ni Afisa Elimu mkoa wa Shinyanga,Mohammed Kahundi akifurahia na kucheza wakati viongozi wakiongozwa na Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia wakicheza muziki wakati wa makabidhiano ya madarasa manne.
Viongozi wakicheza muziki.
Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga,Albert Msovela akielezea kuhusu ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule ya msingi Buhangija. Vyoo hivyo vinajengwa na Umoja wa wake wa viongozi nchini Tanzania.
Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga,Albert Msovela akielezea kuhusu ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule ya msingi Buhangija. Vyoo hivyo vinajengwa na Umoja wa wake wa viongozi nchini Tanzania.
Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiwapongeza wake wa viongozi kujenga madarasa na vyoo katika shule ya msingi Buhangija.
Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako  akiwataka wazazi na walezi kutowabagua watoto wenye ulemavu.
Viongozi mbalimbali wa serikali na Chama Cha Mapinduzi wakimsikiliza  Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako  katika ukumbi wa Mikutano kwenye shule ya msingi Buhangija.
Wanafunzi wa shule ya msingi Buhangija wakitoa burudani ya wimbo mbele ya Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack akiwashukuru wake wa viongozi kwa kusaidia kujenga madarasa na vyoo katika shule ya msingi Buhangija.
Mwenyekiti wa Umoja wa wake wa viongozi, Tunu Pinda akizungumza katika ukumbi wa mikutano wa shule ya msingi Buhangija akielezea shughuli mbalimbali zinazofanywa na umoja huo katika kusaidia  jamii.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Jasinta Mboneko akizungumza katika ukumbi wa mikutano shule ya msingi Buhangija.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga,Mabala Mlolwa akiwapongeza wake wa viongozi kwa kutekeleza ilani ya CCM kwa vitendo upande wa sekta ya elimu kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.
Katibu Msaidizi wa Umoja wa wake wa viongozi,Naima Malima akielezea kuhusu Umoja wa wake wa viongozi ambao una wanachama 61 ambao ni wake wa viongozi waliopo madarakani na viongozi waliostaafu.
Mwalimu Mkuu shule ya msingi Buhangija Seleman Kipanya akitoa taarifa kuhusu shule hiyo.
Sehemu ya wake wa viongozi na madiwani wa Manispaa ya Shinyanga wakiwa ukumbini
Sehemu ya wake wa viongozi na madiwani wa Manispaa ya Shinyanga wakiwa ukumbini
Wanafunzi wakiwa ukumbini.
Wanafunzi wakiwa ukumbini.
Kulia ni Mwenyekiti wa Umoja wa wake wa viongozi, Tunu Pinda akikabidhi vifaaa vya kujifunzia wanafunzi kwa Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichakokwa ajili ya wanafunzi wa shule ya msingi Buhangija. 
 Mwenyekiti wa Umoja wa wake wa viongozi, Tunu Pinda akikabidhi vifaaa vya kujifunzia wanafunzi kwa Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako kwa ajili ya wanafunzi wa shule ya msingi Buhangija. 
 Mwenyekiti wa Umoja wa wake wa viongozi, Tunu Pinda akikabidhi sabuni kwa Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako kwa ajili ya wanafunzi wa shule ya msingi Buhangija. 
Sehemu ya vitu mbalimbali vilivyotolewa na Umoja wa wake wa viongozi kwa ajili ya wanafunzi wa shule ya msingi Buhangija.
Wake wa viongozi wakigawa vifaa mbalimbali vya shule kwa wanafunzi wa shule ya msingi Buhangija.
Katibu Msaidizi wa Umoja wa wake wa viongozi,Naima Malima akigawa taulo laini kwa wanafunzi wa shule ya msingi Buhangija.
Zoezi la kugawa vifaa vya shule likiendelea.
Zoezi la kugawa vifaa vya shule likiendelea.
Zoezi la kugawa vifaa vya shule likiendelea.
Wake wa viongozi wakicheza muziki na wanafunzi wa shule ya msingi Buhangija.
Wake wa viongozi wakicheza na wanafunzi wa shule ya msingi Buhangija.
Wake wa viongozi wakiongozwa na Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia,Prof. Joyce Ndalichako ( wa pili kushoto) wakigawa chakula kwa wanafunzi wa shule ya Msingi Buhangija.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack akiwapaka sabuni na kuwanawisha wanafunzi wa shule ya msingi Buhangija wakati wa kula chakula cha mchana.
Wake wa viongozi wakiendelea kugawa chakula kwa wanafunzi wa shule ya msingi Buhangija.
Zoezi la kugawa chakula likiendelea.
Picha ya kumbukumbu,Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko (kushoto) na wake wa viongozi nchini Tanzania.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde - Malunde 1 blog
Share:

Waziri Jafo Atengua Maamuzi Yote.......Kaagiza Wagombea Wote Waliongeliwa Uchaguzi Serikali za Mitaa Warudishwe

Waziri wa Nchi ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo ametangaza kuwaruhusu wagombea wote waliochukuwa fomu na kuzirejesha kwa ajili ya kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika nchini Tanzania Novemba 24, 2019 na amefuta maamuzi yote yaliyofanywa na wasimamizi wa uchaguzi Nchini kote ya kuwaengua wagombea wa vyama mbalimbali. 

Waziri Jafo ametoa uamuzi huu  leo November 10, 2019 jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na wanahabari leo

“Natoa Muongozo Wagombea wote waliochukuwa fomu na kuzirejesha waruhusiwe kushiriki uchaguzi huo, waingie ulingoni, hakuna kutafuta sababu, labda kama sio Raia wa Tanzania, hajajiandikisha Kwenye Mtaa husika, amejiandikisha mara mbili au hajadhaminiwa na Chama chake

“Wote waliochukua na kurejesha fomu wanaingia ulingoni na ratiba za kampeni zitaanza kupokelewa, hakuna kuweka mpira kwapani, hakuna kuruka kenchi,hakuna kukimbiana wote watashiriki Uchaguzi huu wa Serikali za Mitaa, hakuna kutafuta visingizio tena

“Kwahiyo nafuta maamuzi yaliyofanywa na Wasimamizi wa Uchaguzi Nchini kote ya kuwaengua Wagombea wa Vyama mbalimbali, tunafanya hivi Kwa busara, tusijiangalie sisi kama Viongozi wa Vyama mbalimbali, tuangalie watu ambao wapo kule chini wanataka kushiriki uchaguzi huu

“CHADEMA na ACT walitangaza kujiondoa, cha ajabu mpaka jana kuna Wanachama wa Vyama hivyo bado walikuwa wanaendelea kupeleka fomu, kwa hiyo licha ya utashi wa Viongozi, kule site hali ni tofauti watu wanataka kushiriki uchaguzi ndo maana nimetoa muongozo huu wa kuwaruhusu” Amesema Waziri Jafo


Share:

Chadema waitaka serikali kutotumia jina na nembo ya chama chao kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetaka Serikali kutotumia nembo na jina la chama hicho kwenye karatasi za kupigia kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 24, mwaka huu.

Naibu Katibu Mkuu (Bara), wa chama hicho, John Mnyika amesema amesema hayo leo Jumapili Novemba 10, jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema sababu ya uamuzi huo ni kutokana na wao kujiengua katika kinyang’anyiro hicho hivyo wagombea wao wasiwepo katika fomu hizo za kupigia kura.

“Kesho Novemba 11, tutamuandikia barua Waziri wa Tamisemi (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa), Suleiman Jaffo, kuacha kutumia jina nembo ya chama chetu.

“Pia tunamuomba Rais Dk. John Magufuli, kuingilia kati ukiukwaji wa sheria unaoendelea kwenye uchaguzi huo kama alivyohamasisha wakati wa uandikishaji,” amesema Mnyika.


Share:

Uteuzi Mpya Uliofanywa Na Rais Magufuli Mchana Huu




Share:

Ajali Yaua Watu Watatu Arusha

Jeshi la Polisi mkoani Arusha linamshikilia dereva wa gari ndogo aina ya Toyota Salon yenye namba za usajili T.213, Deogratius Thomas Kiwale, aliyesababisha vifo vya watu watatu na kujeruhi wawili baada ya gari lake kuacha njia na kugonga wafanyabiashara na watembea kwa miguu.

Taarifa hiyo imetolewa Novemba 9, 2019 na Kamanda wa Polisi mkoani humo ACP Jonathan Shanna, ambapo amesema kuwa ajali hiyo imetokea usiku wa kuamkia jana  majira ya saa 1:00 usiku, katika barabara ya Arusha Moshi maeneo ya Manchester, Kata ya Sekei Halmashauri ya Jiji la Arusha.

"Chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva kushindwa kulimudu gari lake hali iliyopelekea vifo na majeruhi, Dereva wa gari hilo amekamatwa na pindi upelelezi utakapokamilika atafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria" amesema ACP Shanna.

ACP Shanna ameyataja majina ya watu waliofariki na kupatwa na majeraha katika ajali hiyo kuwa ni Gudla Mashanga, mfanyabiashara na mkazi wa Sanawari, Honorina Zakaria, mfanyabiashara na mkazi wa Sanawari, Amina Hassan mkazi wa Moivo, ambapo majeruhi ni Rogath Minja, mfanyabiashara na mkazi wa Sanawari na Renatha Thadei ambaye pia ni mfanyabiashara na mkazi wa Sekei.

Kwa mujibu wa Kamanda Shanna, miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali ya Mount Meru, na majeruhi pia wamelazwa katika hospitali hiyo kwa ajili ya matibabu zaidi.


Share:

Rais Magufuli Abatilisha Ufutaji Shamba La Ekari 1000 Mvomero

Na Munir Shemweta, WANMM MVOMERO
Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli amebatilisha pendekezo la kufutwa shamba lenye ukubwa wa ekari 1000 lililopo Kidunda wilayani Mvomero mkoani Morogoro linalomilikiwa na Cecilia George Rusimbi.

Uamuzi wa Dkt Mafuli kubatilisha ufutaji shamba hilo unatokana na kubainika kuwa pendekezo lililowasilishwa la kufutwa shamba hilo kwa madai ya kutoendelezwa kutokuwa za kweli na ulilenga kumdhulumu mmiliki wake.

Akitangaza uamuzi huo wa Raisi jana wilayani Mvomero, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi alisema, baada ya kufuatilia mashamba yaliyopendekezwa kufutwa Dkt Magufuli alibaini taarifa alizopelekewa za kufuta shamba Cecilia hazikuwa sahihi na hivyo kuamua kubatilisha pendekezo lililowasilishwa kwake na kumpatia haki yake mmiliki.

Kufuatia hali hiyo Waziri Lukuvi aliwaonya Aaafisa ardhi nchini kuhakikisha wakati wa kufanya zoezi la ukaguzi/Upekuzi wa mashamba yasiyoendelezwa wanazingatia haki pamoja na kufuata sheria badala ya kufanya kazi hiyo kwa upendeleo au kumuonea mtu.

Hata hivyo, Waziri wa Ardhi alisema, utendaji kazi katika wilaya ya Mvomero umekuwa wa hovyo na usiozingatia maadili jambo linalopelekea wilaya hiyo kuongoza katika mkoa wa Morogoro kuwa na migogoro mingi ya ardhi sambamba na malalamiko mengi ya wananchi dhidi ya ofisi ya ardhi.

‘’Baadhi ya watumishi katika ofisi ya halmashauri ya wilaya ya Mvomero mnajifanya ni Maafisa ardhi au Wapima wakati hamkuajiriwa kwa nafasi hiyo, mnasaini nyaraka za ardhi na kuwaumiza wananchi’’ alisema Lukuvi

Kwa upande wake Cecilia George Rusimbi alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa uamuzi wake wa kubatilisha ufutaji sahamba lake na kuuelezea uamuzi huo kuwa  umezingatia haki na kusikia kilio chake ambapo alisema umempa faraja baada ya kuhangaika sana kuhusiana na shamba hilo.

‘’ Nimemiliki shamba tangu mwaka 1987 na kuhangaikia hati kwa muda mrefu na nimeshangazwa kuelezwa kuwa shamba langu liko katika mpango wa kufutwa kutokana na kutoendelezwa, hii imenifanya kuishi kwa wasiwasi’’ alisema Cecilia.

Waziri Lukuvi ameagiza shamba hilo la kilimo cha Michikichi, Mitiki na Bamboo  kupangwa upya na mmiliki wake kupatiwa hati kulingana na upimaji utakaofanywa na kumtaka kuliendeleza kwa mujibu wa sheria.

Sambamba na sakata la shamba la Cecilia, Lukuvi aliagiza kupunguzwa ukubwa wa Shamba Sangasanga na Lubango lililodaiwa kuwa na ukubwa wa ekari 1,103 wakati uhalisia wa shamba hilo ni ekari 500 na kuagiza mmiliki wake kurudisha hati ili apatiwe hati ilinayolingana na uhalisia wake na ekari 603.5 zilizoongezwa zitabaki kuwa ardhi ya akiba.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mwl Mohamed Utaly alieleza kuwa wilaya yake ina tatizo kubwa la migogoro ya ardhi pamoja na jitihada kubwa inayofanywa na ofisi yake kukabiliana na tatizo hilo na kuongeza kuwa mingine inachochewa na uhamasishaji unaowafanya wananchi kukata tamaa.

Katika hatua nyingine Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi alitembelea ofisi ya Ardhi katika halmashauri ya Mvomero na kubaini ‘madudu’ katika ofisi hiyo ambapo alibaini baadhi ya majalada ya wananchi waliomba kumilikishwa ardhi tangu mwaka 2012 katika halmashauri hiyo kushindwa kupatiwa hati huku.

Hali hiyo ilimfanya Waziri Lukuvi kumuagiza Kaimu Kamishana Msaidizi wa Ardhi Kanda Maalum ya Morogoro Erick Makundi kuhakikisha wale wote walioomba hati na kutumiza vigezo vya kupatiwa hati wanapatiwa kufikia mwezi ujao Desemba 2019. Pia ameagiza kufuatiliwa majalada 300 ambayo wamiliki wake wamekamilisha taratibu za kupatiwa hati lakini hawajapatiwa.

Sambamba na hilo Lukuvi aliagiza wafanyakazi wa ofisi ya ardhi katika halmashauri hiyo wanaojitolea kutosaini nyaraka zozote za ardhi kwa kuwa baadhi yao wamekuwa wakishiriki kutoza tozo kwa gharama za juu za shilingi 50,000 wakati gharama halisi ni 20,000.


Share:

WAZIRI MPINA AMTUMBUA MENEJA MKUU RANCHI ZA TAIFA ALIYEKUMBWA NA KASHFA YA RUSHWA MILIONI 12

Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa(NARCO), Profesa Philemon Wambura ambaye uteuzi wake umetenguliwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI  wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ametengua uteuzi wa Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Profesa Philemon Nyagi Wambura aliyefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa  makosa ya rushwa, matumizi mabaya ya madaraka, uhujumu uchumi na ubadhirifu wa mali za umma.
Kwa Mujibu wa Taarifa kwa Umma iliyotolewa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Edward Kondela imesema Waziri Mpina amefikia uamuzi huo kwa mamlaka aliyopewa kwa mujibu wa Sheria ya Makampuni Sura 212 na Sheria ya Mashirika ya Umma Na. 2 ya mwaka 1992.

Pia taarifa hiyo imebainisha kuwa uteuzi huo umetenguliwa kuanzia 08, Novemba 2019 na kwamba kuwa taratibu za kumpata Meneja Mkuu  mpya wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) zinaendelea.
Wiki iliyopita Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kagera, John Joseph aliwaambia waandishi wa habari mjini Bukoba kuwa Prof. Wambura aliomba na kupokea rushwa kiasi cha shilingi milioni 12 kutoka kwa mtu ambaye aliomba kupatiwa  kitalu kwenye moja ya Ranchi za Taifa zilizopo Missenyi Mkoani Kagera.
Alisema mnamo tarehe 23.09.2019 Takukuru ilipokea taarifa kwamba Profesa Wambura ambaye ni Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni za Ranchi za Taifa anajihusisha na vitendo dhidi ya rushwa  ambapo walianzisha uchunguzi mara moja.
Mkuu huyo wa Takukuru alisema kwenye uchunguzi huo walibaini kwamba mnamo Tarehe 3.1.2018, Profesa Wambura aliomba na kupokea rushwa ya shilingi milioni 12 kwa mtu ambaye aliomba kupewa kitalu lakini hakukubali kumpatia hadi apatiwe milioni 12 na mtu huyo ambaye kwa mujibu wa TAKUKURU jina lake limehifadhiwa aliweza kumpatia kiasi hicho cha fedha na ndipo alipofanikiwa kumpatia kitalu hicho.
Joseph alisema ni makosa kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kwa mtu yoyote kujihusisha na vitendo vya rushwa  ambapo tayari TAKUKURU imetoa onyo kali kwa watu wote kutojihusisha na vitendo vya rushwa kwani TAKUKURU iko macho wakati wote na itanawasa na kuwafikisha kwenye vyombo vya dola.
Share:

Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Sisty Nyahoza Asema Wapinzani Wanatakiwa Kujilaumu Wenyewe kwa Kutofuata Sheria za Uchaguzi

Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Sisty Nyahoza amesema malalamiko yanayotolewa na vyama vya siasa kuhusu kuenguliwa wagombea wao katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa yamesababishwa na wao wenyewe.

Miongoni mwa malalamiko ambayo yalitolewa na vyama hivyo, ni pamoja na wagombea wao kuenguliwa au kuwekewa pingamizi kwa sababu ya kukosa sifa kutokana na kukosea kujaza fomu zao.

Mengine ni wagombea kuenguliwa kwa sababu ya kujaza jina la chama kwa kifupi mfano, Chadema badala ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo au ACT Wazalendo  badala ya Alliance for Change and Transparency.

Nyahoza amesema matatizo na malalamiko mengi yanayovikumba vyama vya upinzani katika uchaguzi huu, yanatokana na kutozingatia sheria na kanuni zilizowekwa.

“Hivi vyama mara kwa mara tunaongea nao kuhusu kuzingatia sheria na kanuni, sasa kama watakuwa hawazisomi na kuzifuata watakuwa wanalalamika mara kwa mara,” alisema Nyahoza.

Kuhusu fomu inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ya mgombea mmoja ambaye amekatwa baada ya kuandika kwa kifupi ACT Wazalendo na kuelezwa na msimamizi wa uchaguzi huo kwamba chama hicho hakipo kwenye orodha ya msajili, alisema chama hicho kimesajiliwa kwa jina la Alliance for Change and Transparency (ACT Wazalendo) na sio ACT Wazalendo, hivyo hilo ni kosa.

“Hiyo wanayosema ni kifupi ni kama ilivyo CCM kwa Chama Cha Mapinduzi, lakini huwezi kuandika CCM tu kwani inaweza ikawa inamaanisha kitu kingine.

“Sisi kama walezi siku zote tumekuwa tukiwasisitiza kuzisoma na kuzingatia sheria, lakini kama baba unasema na mtoto hafuati matokeo yake ndiyo hayo,” alisema Nyahoza.

Alisema kuwa vyama vyote vya siasa vina wanasheria na watu waliobobea kwenye mambo hayo, ambao wana uwezo wa kuwaongoza wanachama wao katika mambo hayo muhimu.

Credit: Mtanzania


Share:

Waziri Wa Kilimo Aagiza Viongozi Wa Saccos Ya Kurugenzi Jijini Arusha Wakamatwe

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Arusha
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameliagiza jeshi la Polisi Mkoani Arusha kwa kushirikiana na Mkuu wa Upelelezi, na Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) kuwakamata viongozi mbalimbali wa Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo cha Arusha Kurugenzi kutokana na ubadhilifu wa fedha za wanachama.
 
Waziri Hasunga ametoa maagizo hayo jana tarehe 9 Novemba 2019 mara baada ya kusikiliza malalamiko ya wanachama wa chama hicho wakati wa kikao kazi kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha na kuhudhuriwa pia na Mkuu wa Mkoa huo Mhe Mrisho Gambo.
 
Amesema kuwa watuhumiwa hao wanapaswa kukamatwa haraka iwezekanavyo kuanzia waliokuwa viongozi mwaka 2004 mpaka 2015 ili kurudisha fedha zote walizozizihujumu za wanachama na walizokopa.
 
Wengine alioagiza wakamatwe ni pamoja na wajumbe wote wa kamati za mikopo, Kamati ya usimamizi wa SACCOS iliyokuwepo kipindi chote hicho, Wajumbe wote wa Bodi ya SACCOS iliyokuwepo awali kabla ya Bodi iliyopo sasa. 

“Tunachotaka sisi fedha zote za wanachama zirudi na hata leo wakirudisha fedha hizo hatutaendelea na kesi” Alisema
 
Pia ameagiza mwanachama wa SACCOS hiyo Bi Zainab Nassor aliyeanzisha vikundi hewa 14 akamtwe, huku wengine ni aliyekuwa Mwenyekiti wa SACCOS Dkt Freedom Makiago,  Makamu Mwenyekiti Gasto Gasper, Meneja Christina Sumaye, na wajumbe Andrea Sekidio, Joseph Kuhamwa na Mwanahamisi Gembe.
 
Katika hatua nyingine Mhe Hasunga ameagiza kukamatwa kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa kamati ya Usimamizi Bi Mwanahawa Kombo, na wajumbe Samwel Mushy, Estomin Chang’ah. Huku akiagiza pia karani wa SACCOS hiyo Edith Malley kukamatwa.
 
Katika hatua nyingine ameagiza viongozi wote walioandikwa kwenye vikundi vya mikopo kukamatwa haraka iwezekanavyo na kuchukuliwa hatua za haraka ikiwemo kurudisha fedha za wanachama.
 
Mhe Hasunga amesema kuwa lengo la kunzishwa vyama vya ushirika ilikuwa ni kuwanufaisha wananchi kupitia umoja huo muhimu kwani mafanikio yanahusisha nguvu ya pamoja.
 
Hata hivyo ameagiza Bodi iliyopo madarakani kubainisha taarifa za kumbukumbu zote za chama hicho kwa kuonyesha idadi ya wanachama na akiba walizonazo katika chama, idadi ya hisa na kiasi cha fedha zinazodaiwa na kila mwanachama.
 
Kwa sasa chama kinadaiwa fedha kiasi cha shilingi 2,486,365.68 zilizotokana na mikopo kutoka Taasisi mbalimbali za kifedha, Amana, Akiba na Hisa za wanachama hususani wastaafu ambazo zilichukuliwa kwa kutumiwa na wahusika hao bila utaratibu na kwa malengo yao binafsi.
 
Wanachama wastaafu wanadai zaidi ya shilingi 831,764,924.87 zitokanazo na fedha za Amana walizoweka katika chama kutumia viinua mgongo vyao baada ya kustaafu utumishi, Akiba na Hisa walizowekeza tangu wajiunge na chama hicho.
 
Wanachama wanaoendelea na chama na waliojitoa wanadai zaidi ya shilingi 770,181,745.56 zitokanazo na Amana, Akiba na Hisa walizowekeza tangu wajiunge na chama hicho.
 
Kadhalika, Taasisi za kifedha zinazodai ni pamoja na (CRDB, NSSF na TUMAINI SACCOS) wanaodai zaidi ya shilingi 874,575,517.25 bakaa ya mikopo iliyotolewa bila kuzingatia utaratibu wa kifedha na kwa kutumia taarifa za udanganyifu.
 
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga yupo Mkoani Arusha kwa ziara ya kikazi ya siku 2 kwa mualikowa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe Mrisho Gambo ambapo pamoja na mambo mengine atashuhudia shughuli za sekta ya kilimo.


Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger