Monday, 3 June 2019

Wizara Ya Fedha Na Mipango Yaomba Kuidhinishiwa Bajeti Ya Shilingi Trilioni 11.94 Mwa 2019/2020


UTANGULIZI


1.            Mheshimiwa Spika, kutokana na    taarifa iliyowasilishwa ndani ya Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, naomba kutoa hoja kwamba, sasa Bunge lako lipokee na kujadili mapitio ya utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka 2018/19 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2019/20. Aidha, naomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango na Taasisi zilizo chini yake pamoja na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kwa mwaka 2019/20.

2.           Mheshimiwa Spika, awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kutujalia uhai na afya njema na kutuwezesha kukutana tena kushiriki mkutano huu wa Bunge unaojadili Bajeti ya mwaka 2019/20, ambayo ni ya Nne tangu Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani.

3.           Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee, napenda nitumie fursa hii kuwapongeza kwa dhati kabisa Viongozi Wakuu wa Serikali, nikianza na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mhe. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Kassim M. Majaliwa (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa miongozo yao iliyojaa hekima na uzalendo. Ni dhahiri kwamba, katika kipindi cha takriban miaka mitatu na nusu ya uongozi wao, tumepata mafanikio mengi ambayo kila mmoja wetu anapaswa kujivunia. Naomba Mwenyezi Mungu aendelee kuwajalia afya njema ili dhamira zao za dhati za kuwaletea watanzania maendeleo ziendelee kuleta manufaa kwetu na kwa vizazi vijavyo.

4.           Mheshimiwa Spika, napenda pia nitumie fursa hii, kuwapongeza sana Mhe. Balozi Dkt. Augustine Philip Mahiga (Mb.), kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, pamoja na Mhe. Prof. Palamagamba John Aidan Kabudi (Mb.), kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Nawaahidi ushirikiano wa hali ya juukatika kutekeleza majukumu yetu ya kumsaidia Mhe. Rais ili shughuli za Serikali ziendelee kufanyika kwa ufanisi zaidi.

5.           Mheshimiwa Spika, napenda kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika na Wenyeviti wote wa Bunge kwa kuendesha vizuri majadiliano ya Bajeti za Wizara mbalimbali. Aidha, napenda kumpongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Mhe. George Boniface Simbachawene (Mb) na Makamu Mwenyekiti Mhe. Mashimba Mashauri Ndaki (Mb) kwa kuongoza vizuri majadiliano ya Kamati. Vilevile, nawashukuru wajumbe wote wa Kamati ya Bajeti kwa michango yao mizuri ambayo inatusaidia sana katika kutekeleza majukumu ya Wizara kwa ufanisi. Aidha, Wizara inaahidi kuendelea kuzingatia maoni na ushauri kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge wote wakati wa kujadili taarifa hii ya utekelezaji wa Bajeti ya Wizara yangu kwa mwaka 2018/19 na Mpango na Bajeti ya mwaka 2019/20.

6.           Mheshimiwa Spika, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji (Mb), Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, kwa msaada mkubwa na ushirikiano anaonipatia katika kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Wizara.  Aidha, nawashukuru Bw. Doto M. James, Katibu Mkuu HAZINA na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Naibu Makatibu Wakuu Bi. Amina Kh. Shaaban, Dkt. Khatibu M. Kazungu na Bw. Adolf H. Ndunguru kwa kusimamia shughuli za kiutendaji za Wizara kwa ufanisi. Vilevile, nawashukuru Makamishna, Wakurugenzi, Wakuu wa Taasisi zilizoko chini ya Wizara ya Fedha na Mipango, Wakuu wa Vitengo   na wafanyakazi wote wa Wizara, kwa kutimiza wajibu wao wa kuwatumikia Watanzania.

7.           Mheshimiwa Spika, baada ya maneno haya ya shukrani, naomba nijielekeze katika hoja yangu yenye maeneo makuu mawili ambayo ni: mapitio ya utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara kwa mwaka 2018/19 na Mpango na Bajeti kwa mwaka 2019/20.

8.           Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2018/19, bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango inatekelezwa katika mafungu nane ya kibajeti ambayo ni: - Fungu 50 - Wizara ya Fedha na Mipango; Fungu 21 - HAZINA; Fungu 22 - Deni la Taifa; Fungu 23 - Mhasibu Mkuu wa Serikali; Fungu 7 - Ofisi ya Msajili wa HAZINA; Fungu 10 - Tume ya Pamoja ya Fedha; Fungu 13 - Kitengo cha Udhibiti wa Fedha Haramu; na Fungu 45 – Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi.

Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara kwa Mwaka 2018/19


9.           Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga uchumi wa viwanda na kuwaletea Watanzania maendeleo inafikiwa, Wizara iliandaa Mpango na Bajeti ya mwaka 2018/19 kwa kuzingatia miongozo mbalimbali ya kitaifa, kikanda na kimataifa ambayo ni pamoja na: Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17- 2020/21, Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti 2018/19, Sheria ya Bajeti Na.11 ya Mwaka 2015, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi 2015, Agenda ya Kamisheni ya Umoja wa Afrika 2063 na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2030. Aidha, Mpango na Bajeti ulizingatia ahadi na maelekezo yaliyotolewa na Mheshimiwa Rais katika hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ushauri na maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti pamoja na Sera mbalimbali za Serikali.

Mapatona Matumizi ya Wizara kwa Mwaka 2018/19


10.        Mheshimiwa Spika, Muhtasari wa mapato na matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2018/19 ni kama inavyooneshwa kwenye kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 6 hadi ukurasa wa 9.

UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU


11.        Mheshimiwa Spika, napenda sasa nitumie fursa hii kulieleza Bunge lako tukufu kuhusu majukumu yaliyotekelezwa na Wizara pamoja na taasisi zilizo chini yake kwa kipindi cha kuanzia Julai 2018 hadi kufikia Aprili 2019 ambayo yameainishwa katika hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 9 hadi ukurasa wa 124.


Kubuni na Kusimamia Utekelezaji wa Sera za Uchumi Jumla


12.        Mheshimiwa Spika, malengo ya uchumi jumla kwa mwaka 2018/19 yalikuwa: kuhakikisha Pato la Taifa linakua kwa asilimia 7.2 mwaka 2018; mfumuko wa bei unabaki katika wigo wa tarakimu moja; mapato ya ndani yanafikia asilimia 15.8 ya pato la Taifa; na mapato ya kodi yanafikia asilimia 13.6 ya Pato la Taifa na nakisi ya bajeti inafikia asilimia 3.2.

13.        Mheshimiwa Spika, uchumi wa nchi yetu umeendelea kuimarika ambapo mwaka 2018, Pato la Taifa kwa kutumia bei ya kizio ya mwaka 2015 lilikua kwa asilimia 7.0 ikilinganishwa na asilimia 6.8 mwaka 2017. Sekta zilizokua kwa kasi kubwa ni pamoja na Sanaa na Burudani (asilimia 13.7), ujenzi (asilimia 12.9), usafirishaji na uhifadhi mizigo (asilimia 11.8) na habari na mawasiliano (asilimia 9.1). Ukuaji huu wa uchumi umeenda sambamba na utolewaji wa huduma bora kwa wananchi zikiwemo maji, afya, umeme, elimu na ujenzi wa miundombinu ya reli, bandari, viwanja vya ndege, madaraja na barabara pamoja na kuimarisha usafiri wa anga.
                                      
14.        Mheshimiwa Spika, mfumuko wa bei umeendelea kushuka na kubakia katika kiwango cha tarakimu moja. Kwa mwezi Aprili 2019, mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 3.2 ikilinganishwa na asilimia 3.8 kwa kipindi kama hicho mwaka 2018. Hali hii imetokana na kuimarika kwa upatikanaji wa chakula katika masoko ya ndani na nchi jirani, kutengamaa kwa bei za mafuta katika soko la dunia, usimamizi madhubuti wa Sera za bajeti na fedha na utulivu wa thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya sarafu nyingine. Utulivu huu wa bei umesaidia wazalishaji, wanunuzi na walaji kuweka mipango na mikakati ya muda mrefu bila kuhofia mabadiliko ya mara kwa mara ya bei ya malighafi na bidhaa.

Uandaaji na Ufuatiliaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa


15.        Mheshimiwa Spika, Wizara imefanikiwa kufuatilia utekelezaji wa miradi 102 ya maendeleo kati ya 179. Miradi iliyofuatiliwa ilijumuisha sekta za Viwanda, Maji, Kilimo, Nishati, Uvuvi, Afya, Elimu, Madini, Sheria, Ujenzi na Uchukuzi. Ufuatiliaji huo umesaidia kurekebisha upungufu uliojitokeza katika utekelezaji na kuainisha hatua za kuzingatiwa katika kutayarisha mpango wa mwaka 2019/20.

Kusimamia Ukusanyaji wa Mapato ya Serikali


Mapato ya Kodi na Yasiyo ya Kodi

16.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Wizara ilipanga kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani yakijumuisha mapato ya Halmashauri ya jumla ya shilingi trilioni 20.89. Kati ya hizo, mapato ya kodi yalikuwa shilingi trilioni 18.0, Halmashauri shilingi bilioni 735.6 na mapato yasiyo ya kodi shilingi trilioni 2.16. Hadi kufikia Aprili 2019, mapato ya ndani yakijumuisha mapato ya Halmashauri yalifikia shilingi trilioni 15.46. Kati ya kiasi hicho, mapato ya kodi yalikuwa shilingi trilioni 12.9, sawa na asilimia 87.4, mapato yasiyo ya kodi shilingi trilioni 2.04, sawa na asilimia 122 na mapato ya Halmashauri shilingi bilioni 529.25, sawa na asilimia 72 ya lengo la kipindi hicho.

17.        Mheshimiwa Spika, kati ya mapato yasiyo ya kodi ya kiasi cha shilingi trilioni 2.04 yaliyopatikana hadi kufikia Aprili 2019, jumla ya shilingi bilioni 600.45 zimekusanywa na Wizara ya fedha na Mipango, sawa na asilimia 100.44 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 597.81. Mafanikio haya yametokana na kuimarishwa kwa ufuatiliaji na usimamizi wa mashirika, kampuni na taasisi za umma ambazo Serikali imewekeza.

18.        Mheshimiwa Spika, ili kuendelea kuleta uwazi na ufanisi katika ukusanyaji wa mapato, Wizara  ilipanga kuunganisha Wizara, Idara na Taasisi za Serikali 300 kwenye Mfumo wa Serikali wa Kielektroniki wa ukusanyaji na usimamizi wa maduhuli (Government e- Payment Gateway - GePG). Hadi kufikia Aprili 2019, jumla ya Taasisi 210 zimeunganishwa kwenye mfumo wa GePG ikiwa ni asilimia 70 ya lengo. Aidha, hadi sasa jumla ya taasisi 410    kati ya taasisi 667 zimeunganishwa na zinakusanya mapato kupitia mfumo huu.  Mfumo huu unaiwezesha Serikali kuona moja kwa moja miamala ya ukusanyaji wa mapato na kujua kiwango cha mapato kinachokusanywa kwa siku.

Misaada na Mikopo kutoka kwa Washirika wa Maendeleo

19.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Wizara ilipanga kuratibu upatikanaji wa misaada na mikopo nafuu ya kiasi cha shilingi trilioni 2.67 kutoka kwa washirika wa Maendeleo ili kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo. Hadi kufikia mwezi Aprili 2019, misaada na mikopo ilifikia shilingi trilioni 1.70, sawa na asilimia 86 ya lengo la kipindi hicho.




Mikopo ya Ndani na Nje yenye Masharti ya Kibiashara

20.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Wizara ilitarajia kuratibu upatikanaji wa mikopo ya ndani na nje yenye masharti ya kibiashara ya jumla ya shilingi trilioni 8.90. Kati ya hizo, shilingi trilioni 3.11 ni mikopo ya nje, shilingi trilioni 1.19 ni mikopo ya ndani na shilingi trilioni 4.60 ni mikopo ya ndani ya kulipia hatifungani zilizoiva (rollover). Hadi kufikia Aprili, 2019 kiasi cha shilingi bilioni 692.30 kilikopwa kutoka nje na shilingi trilioni 3.3 zilikopwa kutoka soko la ndani zikijumuisha malipo ya dhamana za Serikali zilizoiva (rollover).

Usimamizi wa Deni la Serikali



22.         Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kufanya tathmini ya Deni la Taifa kila mwaka ili kupima uhimilivu wake. Matokeo ya tathmini iliyofanyika Desemba, 2018 inaonesha kuwa, Deni la Taifa ni himilivu katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu. Tathmini hiyo ilionesha kuwa: uwiano wa thamani ya sasa ya Deni la Taifa (Present Value of Total Public Debt) kwa Pato la Taifa ni asilimia 27.2 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 70; thamani ya sasa ya Deni la nje pekee (Present Value of External Debt)  kwa Pato la Taifa ni asilimia 22.2 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 55; thamani ya sasa ya  deni la nje kwa mauzo ya nje ni asilimia 157.3 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 240; na ulipaji wa deni la nje kwa kutumia mauzo ya bidhaa nje ni asilimia 15.2 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 23.

23.        Mheshimiwa Spika, Serikali ilitenga kiasi cha shilingi trilioni 1.41 kwa ajili ya kulipa riba ya deni la ndani. Hadi kufikia Aprili, 2019 kiasi cha shilingi trilioni 1.06 kimelipwa sawa na asilimia 75.18 ya lengo. Aidha, Serikali ilitenga shilingi bilioni 689.67 kwa ajili ya kulipa riba ya deni la nje. Hadi kufikia Aprili, 2019 shilingi bilioni 588.30 zimelipwa sawa na asilimia 85.30 ya lengo. Vilevile, Serikali ilitenga shilingi trilioni 1.66 kwa ajili ya kulipia mtaji wa deni la nje, ambapo hadi kufikia Aprili, 2019 shilingi trilioni 1.23 zimelipwa sawa na asilimia 74.10 ya lengo. Wizara itaendelea kusimamia Deni la Serikali kwa kuzingatia Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada SURA 134 pamoja na Mkakati wa Muda wa kati wa Kusimamia Madeni.

Malipo ya Pensheni na Michango ya Mwajiri kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii


24.        Mheshimiwa Spika, Serikali ilitenga kiasi cha shilingi trilioni 1.19 kwa ajili ya kulipia mchango wa mwajiri kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.  Hadi kufikiaAprili, 2019 kiasi cha shilingi bilioni 797.29 sawa na asilimia 67.0 ya lengo kililipwa ikiwa ni uwasilishaji wa michango ya mwajiri kwa watumishi wote wa Umma walio kwenye “Payroll” ya Serikali na kwa wakati.  

25.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Serikali ilitenga kiasi cha shilingi bilioni 424.74 kwa ajili ya kulipa mafao ya Kustaafu na mirathi kwa wastaafu wanaolipwa na HAZINA. Hadi kufikia Aprili 2019, kiasi cha shilingi bilioni 314.92 sawa na asilimia 74.14 kilitumika kulipa Wastaafu 4,016, Mirathi ililipwa kwa Warithi 854 na Pensheni kwa kila mwezi kwa Wastaafu 57,055. Katika kurahisisha ulipaji wa mafao ya wastaafu, Serikali imetengeneza mfumo wa ukokotoaji wa Mafao, uhifadhi wa kumbukumbu pamoja na utoaji wa Vitambulisho vya kielektroniki kwa kutumia mfumo wa TPPS (Treasury Pensioners Payment System).

Kubuni na Kusimamia Mifumo ya Taarifa za Fedha


26.        Mheshimiwa Spika, Wizara imefanikiwa kubuni mfumo wa ufuatiliaji wa Mali za Serikali ujulikanao kama Government Asset Management Information System-GAMIS kwa ajili ya  kurahisisha usimamizi na udhibiti wa Mali za Serikali. Aidha, Wizara imebuni na kuanza kutengeneza mfumo wa usimamizi wa fedha za miradi ya Maendeleo kutoka kwa washirika wa maendeleo zinazopelekwa moja kwa moja kwa watekelezaji (Direct to Projects Funds) ambao unatarajiwa kuanza kutumika Julai, 2019. Lengo ni kutambua miradi yote na kuweka uwazi kuhusu fedha zinazotolewa na Washirika wa Maendeleo bila kupitia Mfuko Mkuu wa Serikali.

27.        Mheshimiwa Spika, majukumu mengine yaliyotekelezwa chini ya usimamizi wa mifumo ya taarifa za fedha ni kama inavyooneshwa kwenye kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 24 hadi ukurasa wa 28.

    

Kuandaa na kufuatilia utekelezaji wa Bajeti ya Serikali


28.        Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha Mamlaka za Serikali za Mitaa zinatoa huduma bora kwa Wananchi, Wizara imeendelea kuzijengea uwezo kwa kuzipatia fedha za kutekeleza miradi ya kimkakati ili ziweze kujitegemea kimapato na kupunguza utegemezi wa ruzuku ya Serikali Kuu. Katika mwaka 2018/19, Wizara imefanya uchambuzi wa Miradi ya Kimkakati 111 yenye thamani ya shilingi bilioni 749.63 kutoka kwenye Halmashauri 67 kwa ajili ya kuzingatiwa katika bajeti ya 2019/20. Matokeo ya uchambuzi huo ni kuwa jumla ya miradi 15 yenye thamani ya shilingi bilioni 137.38 kutoka kwenye Halmashauri 12 ilikidhi vigezo na mikataba kusainiwa. Orodha ya Halmashauri na idadi ya Miradi ni kama ifuatavyo: Halmashauri ya Jiji la Tanga mradi mmoja na Halmashauri ya Jiji la Mwanza miradi miwili; Halmashauri za Manispaa ya Kinondoni miradi miwili, Kigamboni mradi mmoja, Iringa mradi mmoja, Ilemela miradi miwili; Halmashauri ya Mji wa Tarime mradi mmoja; Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo mradi mmoja, Biharamuro mradi mmoja, Kibaha mradi mmoja na Hanang mradi mmoja.

29.        Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu kuandaa na kufuatilia utekelezaji wa Bajeti ya Serikali ni kama inavyooneshwa kwenye kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 28 hadi ukurasa wa 32.

Usimamizi na Udhibiti wa Matumizi ya Fedha za Umma


30.        Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali, imefanya uhakiki wa madeni ya malimbikizo ya mishahara katika Wizara, Idara zinazojitegemea na Wakala wa Serikali 142; Sekretarieti za Mikoa 24 na Mamlaka ya Serikali za Mitaa 185.  Aidha, Wizara imeendelea kuhakikisha usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za Umma zinazotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kufanya ukaguzi maalum katika Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili Kampasi ya Mloganzila, ambapo mapendekezo ya ukaguzi yaliwasilishwa kwa taasisi husika kwa ajili ya kuyafanyia kazi ili kuleta ufanisi katika utekelezaji wa miradi.

31.        Mheshimiwa Spika, majukumu mengine yaliyotekelezwa katika kusimamia na kudhibiti Matumizi ya Fedha za Umma ni kama inavyooneshwa kwenye kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 33 hadi ukurasa wa 35.

Usimamizi wa Mali za Serikali


32.        Mheshimiwa Spika, Wizara ilifanya uhakiki wa mali na madeni katika taasisi zilizounganishwa ambazo ni Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (PSPF, GEPF, PPF na LAPF) na mamlaka za maji Dar es Salaam (DAWASA na DAWASCO). Baada ya utambuzi wa mali na madeni ya taasisi hizo, Serikali itahakikisha kuwa inachukua hatua stahiki kulingana na matokeo ya uhakiki. Wizara pia imefanya uhakiki wa majengo yaliyobaki wazi Jijini Dar es Salaam baada ya Serikali kuhamishia shughuli zake Jijini Dodoma kwa lengo la kuandaa utaratibu wa kugawa majengo hayo kwa baadhi ya Taasisi za Serikali ambazo zina uhitaji wa majengo hayo.

33.        Mheshimiwa Spika, majukumu mengine yaliyotekelezwa katika Usimamizi wa Mali za Serikali ni kama inavyooneshwa kwenye kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 35 hadi ukurasa wa 37.

Udhibiti wa Utakasishaji wa Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi


34.        Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Kitengo cha Udhibiti wa Fedha Haramu (FIU) imeendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria za Udhibiti wa Fedha Haramu kwa kutekeleza majukumu mbalimbali ikiwa ni pamoja na:  kupokea na kuchambua taarifa 1,305 za miamala shuku kutoka kwa watoa taarifa na kuwasilisha taarifa fiche 32 kwenye vyombo vinavyosimamia utekelezaji wa sheria kwa ajili ya uchunguzi; kupokea taarifa 5,536 zinazohusu usafirishaji fedha taslimu na hati za malipo mipakani; kuratibu na kusimamia zoezi linaloendeshwa na ESAAMLG la tathmini ya mifumo ya udhibiti wa fedha haramu (AML/CFT Mutual Evaluation); kuimarisha ushirikiano na  FIU za nchi za Djibouti, Sudan, Ethiopia, Somalia, China (Taiwan) na Mauritius na pia kufanya majadiliano ya kuingia katika makubaliano ya ushirikiano na FIU za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Jamaica, Japan, Trinidad and Tobago, Botswana, Canada, Jamhuri ya Kongo na Kazakhstan. Aidha, Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu imekagua benki nne ili kujiridhisha na utekelezaji wa Sheria za Udhibiti wa Fedha Haramu.

35.        Mheshimiwa Spika, majukumu mengine yaliyotekelezwa katika Udhibiti wa Utakasishaji wa Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi ni kama inavyooneshwa kwenye kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 37 hadi ukurasa wa 39.

Tume ya Pamoja ya Fedha 


36.        Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa majukumu ya Tume ya Pamoja ya Fedha umeoneshwa kuanzia ukurasa wa 39 hadi ukurasa wa 40.

Usimamizi wa Mashirika na Taasisi za Umma


37.        Mheshimiwa Spika,      katika mwaka 2018/19, Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kushirikiana na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali imefanya Ukaguzi Maalum katika Kampuni 34 ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache. Aidha, Ofisi ya Msajili wa Hazina imeandaa Mpango Kazi wa kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa katika ripoti ya ukaguzi na utekelezaji unaendelea. Utekelezaji wa Mpango Kazi unajumuisha kupitia mikataba ya ubia, uendeshaji na utaalam kwa kampuni husika. Lengo kuu la zoezi hili ni kubaini sababu za Serikali kupata kiwango kidogo cha gawio au kutopata kabisa na kuchukua hatua stahiki ili kuongeza mapato ya Serikali. Aidha, ufuatiliaji wa madeni kwa wawekezaji waliobainika kutomaliza kulipa bei ya ununuzi wa kampuni hizo unaendelea.

38.        Mheshimiwa Spika, majukumu mengine yaliyotekelezwa katika Usimamizi wa Mashirika na Taasisi za Umma ni kama inavyooneshwa kwenye kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 40 hadi ukurasa wa 47.

Uratibu wa Mikakati ya Kupunguza Umaskini


39.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Wizara imefanya uchambuzi wa awali wa Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi 2017/18 ambao, unaonesha kuwa umaskini wa mahitaji ya msingi umepungua kutoka asilimia 28.2 mwaka 2011/12 hadi asilimia 26.4 mwaka 2017/18. Kiwango cha umaskini wa chakula kimepungua kutoka asilimia 9.7 mwaka 2011/12 na kufikia asilimia 8.0 mwaka 2017/18.

40.        Mheshimiwa Spika, tathmini ya viashiria vya umaskini usio wa kipato inaonesha tumefanya vizuri katika kuboresha hali ya makazi, umeme, huduma ya maji safi na salama, vyoo, umiliki wa vyombo vya usafiri na mawasiliano. Viashiria vinaonesha kuwa makazi yaliyojengwa kwa kutumia zege, mawe, saruji na vyuma yameongezeka. Vilevile, kaya zinazoishi katika nyumba zenye paa la kisasa zimeongezeka kutoka asilimia 68.0 mwaka 2011/12 hadi asilimia 84.1 mwaka 2017/18. Aidha, asilimia 78.8 ya kaya zinaishi kwenye nyumba zilizojengwa kwa kuta imara mwaka 2017/18 ikilinganishwa na asilimia 46.0 mwaka 2011/12.   Vilevile, asilimia 50.1 ya kaya zinaishi kwenye nyumba zilizojengwa kwa sakafu imara mwaka 2017/18 ikilinganishwa na asilimia 40.0 mwaka 2011/12.

41.        Mheshimiwa Spika, majukumu mengine yaliyotekelezwa katika kuratibu  Mikakati ya Kupunguza Umaskini ni kama inavyooneshwa kwenye kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 48 hadi ukurasa wa 52.

Ununuzi wa Umma


42.        Mheshimiwa Spika, Wizara imefanikiwa kufanya marekebisho ya Kanuni ya 164 ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ili kumpa mzabuni haki ya kupata taarifa ya ukamilishwaji wa mchakato wa ununuzi. Aidha, Kanuni ya 226 ilirekebishwa kumpa mamlaka Mlipaji Mkuu wa Serikali kutoa idhini kwa Maafisa Masuuli kuongeza idadi ya wajumbe wa timu za majadiliano kwenye miradi mikubwa yenye maslahi kwa Taifa. Marekebisho hayo yamezingatia maoni ya wadau juu ya changamoto za utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma Sura 410.

43.        Mheshimiwa Spika, majukumu mengine yaliyotekelezwa katika kusimamia Ununuzi wa Umma ni kama inavyooneshwa kwenye kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 52 hadi ukurasa wa 60

Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi - PPP


44.        Mheshimiwa Spika, Wizara imepokea mapendekezo ya miradi ya ubia ipatayo 33, kati ya hiyo miradi sita imekidhi vigezo na kufanyiwa kazi. Miradi hiyo ni: Mradi wa Uboreshaji wa Huduma ya Usafiri jijini Dar es Salaam Awamu ya kwanza (Dar- Rapid Transit Project- Phase1); Mradi wa Viwanda Vitatu vya Uzalishaji wa Dawa muhimu na Vifaa Tiba; mradi wa Usambazaji wa Gesi asilia katika Jiji la Dar es Salaam, Lindi na Mtwara; Mradi ya Ujenzi ya Hoteli ya Nyota Nne; Kituo cha Biashara katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere; na Mradi wa ujenzi wa hosteli ya wanafunzi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE). Aidha, Wizara imekamilisha uchambuzi wa mawasilisho ya awali ya miradi 22 ya Mamlaka za Serikali za Mitaa na wahusika watajulishwa kuhusu maeneo ya kufanyia kazi kwa mujibu wa Sheria, mwongozo na taratibu za PPP.

45.        Mheshimiwa Spika, majukumu mengine yaliyotekelezwa katika eneo la Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi ni kama inavyooneshwa kwenye kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 60 hadi ukurasa wa 65.

Utekelezaji wa Majukumu ya Mashirika na Taasisi za Umma


46.        Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa majukumu ya Taasisi na Mashirika yaliyo chini ya Wizara kwa mwaka 2018/19 ni kama inavyooneshwa kwenye kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 65 hadi ukurasa wa 114.

          Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi

47.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali imefanya ukaguzi wa hesabu za: Wizara na Idara za Serikali 65; Vyama vya Siasa 14; Sekretariati za Mikoa 26; Wakala za Serikali 33; Mifuko Maalum 16; Taasisi nyingine za Serikali 42; na Balozi za Tanzania 41. Aidha, ukaguzi ulifanyika kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa 185 na Mashirika ya Umma 176. Vilevile, Ofisi imefanya ukaguzi maalum  kwenye taasisi zifuatazo: Shirika la Usafiri Dar-es-Salaam (UDA); Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF); Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA); Taasisi ya Elimu Tanzania; Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC); Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA); Jeshi la Polisi; na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege.

48.        Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi pia ilifanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo 469 na ripoti za ukaguzi zimetolewa. Aidha, katika ukaguzi wa ufanisi, jumla ya taarifa 10 zimetolewa katika kipindi kilichoishia Machi, 2019. Vilevile, hadi kufikia Aprili, 2019 Ofisi imetoa ripoti kuu tano. Taarifa hizo ni muhtasari wa jumla ya taarifa 1,042 za ukaguzi zilizotolewa kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2017/18.

          Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo

49.        Mheshimiwa Spika, maelezo ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyo chini ya Wizara kwa mwaka 2018/19 ni kama inavyooneshwa kwenye kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 117 hadi ukurasa wa 121.

CHANGAMOTO NA MIKAKATI YA KUKABILIANA NAZO


Changamoto


50.        Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa bajeti ya Wizara, changamoto zifuatazo zilijitokeza katika mwaka huu wa fedha ambazo ni:

(i)          Masharti yasiyo rafiki ya mikopo kwenye masoko ya fedha duniani;
(ii)         Kupungua na kutopatikana kwa wakati kwa fedha kutoka kwa Washirika wa Maendeleo katika kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo; na
(iii)        Mwamko mdogo wa kulipa kodi kwa hiari, kudai au kutoa risiti za kielektroniki.



Mikakati ya Kukabiliana na Changamoto


51.        Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto za utekelezaji wa bajeti kama zilivyobainishwa hapo juu, Wizara inaendelea kuchukua hatua mbalimbali zikiwemo:

(i)          Kuhakikisha kuwa Wizara na Taasisi zote za umma zinatumia Mfumo wa Serikali wa Kielektroniki wa ukusanyaji na usimamizi wa maduhuli (Government e- Payment Gateway - GePG);
(ii)         Kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa lengo la kupunguza utegemezi;
(iii)        Kuboresha mfumo wa usimamizi wa mashine za kielektroniki za kutolea risiti ili ziweze kutumika kwa kila muamala unaofanywa. Uboreshaji huu utaondoa uwezekano wa kughushi risiti na kupunguza mianya ya ukwepaji wa kodi;
(iv)       Kudhibiti biashara ya magendo kupitia bahari, maziwa, mipaka, na njia zisizo rasmi kwa kushirikiana na Taasisi nyingine za Serikali kama TANROADS, Mamlaka ya Bandari, Jeshi la Polisi, Jeshi la Wanamaji na Usalama wa Taifa;
(v)         Kuongeza jitihada za ukusanyaji wa kodi za majengo kwa kushirikisha wadau muhimu wakiwemo Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, OR-TAMISEMI, Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa, na Ofisi ya Taifa ya Takwimu;
(vi)       Kuendelea kusimamia utekelezaji wa bajeti kwa kuzingatia Sheria ya Bajeti Na. 11 ya Mwaka 2015;
(vii)      Kuendelea kuimarisha ushirikiano na Washirika wa Maendeleo kwa kutekeleza Mwongozo wa Ushirikiano (DCF) ili kuhakikisha fedha zilizoahidiwa zinatolewa kwa wakati; na
(viii)     Kuendelea na majadiliano na taasisi za fedha za kimataifa ili kuhakikisha kuwa fedha zinazotokana na mikopo ya kibiashara zinapatikana kwa kipindi kilichobaki.

MALENGO YA MPANGO NA BAJETI KWA MWAKA 2019/20


52.        Mheshimiwa Spika, naomba sasa nieleze kuhusu malengo ya mpango na bajeti ya Wizara na Taasisi zake kwa mwaka 2019/20;

MPANGO WA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA WIZARA


53.        Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2019/20, Wizara itaendelea kusimamia majukumu mbalimbali ikiwa ni pamoja na yafuatayo:


(ii)         Kuratibu uandaaji na ufuatiliaji wa mipango ya maendeleo ya Taifa;

(iii)        Kusimamia hatua mbalimbali za ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuwezesha utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa ufanisi;

(iv)       Kuratibu upatikanaji wa Misaada na Mikopo kutoka kwa Washirika wa Maendeleo na kuhakikisha kuwa inaendelea kutolewa kama ilivyoahidiwa na kwa wakati ili kugharamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo;

 

(v)         Kusimamia Deni la Serikali kwa kuhakikisha inakopa kwenye vyanzo vyenye riba nafuu;

(vi)       Kufanya ufuatiliaji na tathmini ya mikopo iliyodhaminiwa na Serikali ili kuhakikisha wadaiwa wanalipa madeni husika kwa wakati kuepusha uwezekano wa kuongeza mzigo kwa Serikali wa kulipa mikopo hiyo;

(vii)      Kusimamia mfumo wa udhibiti wa matumizi ya fedha za umma ikiwa ni pamoja na kufanya maboresho ya mfumo wa Akaunti Jumuifu ya Hazina (Treasury Single Account) kwa lengo la kuboresha mfumo wa matumizi ya umma ili kuiongezea Serikali uwezo wa kugharamia shughuli zake kwa wakati;


(ix)        Kusimamia na kudhibiti matumizi ya fedha za umma ili kupata thamani halisi ya fedha katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo;

(x)         Kuratibu zoezi la uthamini wa mali katika taasisi za Serikali ili kuwa na taarifa sahihi za mali pamoja na kuendelea kuondosha mali chakavu, sinzia (dormant) na zilizokwisha muda wake;  

(xi)        Kusimamia utekelezaji wa Sheria za Udhibiti wa Fedha Haramu kwa kupokea na kuchambua taarifa za miamala shuku zinazohusu utakasishaji wa fedha haramu na ufadhili wa ugaidi;

(xii)      Kusimamia zoezi linaloendelea la tathmini ya kitaifa ya mifumo ya kudhibiti utakasishaji fedha haramu na ufadhili wa ugaidi (Mutual evaluation). Tathmini hiyo itaijengea nchi sifa na uwezo wa kushirikiana na nchi nyingine duniani kwa kubadilishana taarifa zinazohusu udhibiti wa utakasishaji wa fedha haramu na ufadhili wa vitendo vya kigaidi;

(xiii)     Kusimamia Mashirika na Taasisi za Umma kwa kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli kutoka katika Taasisi na Mashirika ya Umma na Kampuni ambazo Serikali ina hisa, kuhakikisha viwanda vilivyobinafsishwa vinafanya kazi kwa ufanisi, kurejesha viwanda vilivyoshindwa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa makubaliano na kuwapatia wawekezaji wengine wenye uwezo na nia ya kuviendeleza;

(xiv)     Kuratibu Mikakati ya Kupunguza Umaskini;


(xvi)     Kuratibu shughuli za PPP nchini; na


54.        Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu Mpango wa Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara ni kama inavyooneshwa kwenye kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 125 hadi ukurasa wa 145.

Usimamizi na Uratibu wa Taasisi na Mashirika ya Umma Chini ya  Wizara

 

55.        Mheshimiwa Spika, mipango kwa mwaka 2019/20 kwa upande wa Mashirika na Taasisi za Umma zilizo chini ya Wizara ni kama inavyooneshwa kwenye kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 147 hadi ukurasa wa 167.

Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi


56.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/20, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi imepanga kutekeleza vipaumbele nane ikiwa ni pamoja na: kufanya ukaguzi wa mafungu ya Bajeti ya Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea, Wakala na Taasisi za Serikali, Sekretariati za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa katika Mikoa yote nchini, Mashirika ya Umma; kufanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na Wahisani; kufanya kaguzi za kiufundi katika maeneo yenye uwekezaji mkubwa wa rasilimali za Umma kama vile ujenzi wa barabara na viwanja vya ndege, reli za  kisasa, na Miradi ya umeme; kufanya maboresho ya mfumo wa ukaguzi kwa kutumia TEHAMA; na kukagua ukusanyaji wa mapato ya kodi na yasiyo ya kodi; ukaguzi wa ufanisi, kaguzi maalum, na kaguzi za kiuchunguzi (forensic audits) katika maeneo yatakayoainishwa; na kuwajengea Wakaguzi uwezo wa kufanya ukaguzi katika maeneo mapya ya ukaguzi pamoja na ukaguzi katika uhalifu wa kifedha kwa kutumia mtandao (financial crimes auditing).

MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2019/20


Makadirio ya Mapato


57.        Mheshimwa Spika, katika mwaka 2019/20, Wizara inakadiria kukusanya maduhuli kiasi cha shilingi 967,042,379,000 (bilioni 967.04) kutoka katika vyanzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na gawio, kodi za pango, marejesho ya mikopo, michango kutoka katika taasisi na mashirika ya umma, mauzo ya leseni za udalali na mauzo ya nyaraka za zabuni. Mchanganuo wa maduhuli yanayokadiriwa kukusanywa kwa mafungu ni kama inavyoonekana kwenye Jedwali Na. 6 ukurasa wa 181 wa kitabu cha Hotuba yangu.

Makadirio ya Matumizi kwa Mwaka 2019/20


58.        Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2019/20 Wizara ya Fedha na Mipango, Taasisi zake pamoja na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi inakadiria kutumia kiasi cha shilingi 11,942,986,578,719 (trilioni 11.94). Kati ya fedha hizo, shilingi 11,212,404,636,988 (trilioni 11.21) ni kwa ajili matumizi ya kawaida na shilingi 730,581,941,731 (bilioni 730.58) ni matumizi ya maendeleo. Matumizi ya kawaida yanajumuisha shilingi 608,371,517,988 (bilioni 608.37) kwa ajili ya mishahara na shilingi 10,604,033,119,000 (trilioni 10.60) kwa ajili ya matumizi mengineyo. Aidha, matumizi ya maendeleo yanajumuisha shilingi 677,000,000,000 (bilioni 677.00) fedha za ndani na shilingi 53,581,941,731 (bilioni 53.58) ni fedha za nje.

MAOMBI YA FEDHA KWA MAFUNGU


Fungu 50 – Wizara ya Fedha na Mipango


59.        Mheshimiwa Spika, katika Fungu hili kwa mwaka 2019/20, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:
(a) Matumizi ya kawaida - shilingi 65,713,430,000 (bilioni 65.71). Kati ya hizo:

(i)        Mishahara - shilingi 37,920,916,000 (bilioni 37.92); na
(ii)       Matumizi mengineyo – shilingi 27,792,514,000 (bilioni 27.79).

(b) Miradi ya Maendeleo – shilingi 34,763,757,000 (bilioni 34.76). Kati ya hizo:

(i)      Fedha za Ndani – shilingi 13,000,000,000 (bilioni 13.00); na
(ii)     Fedha za Nje - shilingi 21,763,757,000 (bilioni 21.76).

 

Fungu 21 – HAZINA


60.        Mheshimiwa Spika, katika Fungu hili kwa mwaka 2019/20, Wizara inaombakuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:

(a)Matumizi ya Kawaida – shilingi 1,272,801,249,988  (trilioni 1.27). Kati ya hizo:

(i)          Mishahara - shilingi 536,520,631,988 (bilioni 536.52); na
(ii)         Matumizi mengineyo – shilingi 736,280,618,000 (bilioni 736.28) ambazo ni kwa ajili ya matumizi ya idara, taasisi zilizo chini ya Fungu hili, pamoja na matumizi maalum.

(b) Miradi ya maendeleo – shilingi 683,717,888,733 (bilioni 683.71). Kati ya hizo:

(i)          Fedha za Ndani - shilingi 656,000,000,000(bilioni 656.00); na

(ii)         Fedha za Nje - shilingi 27,717,888,733 (bilioni 27.71).

Fungu 22- Deni la Taifa


61.        Mheshimiwa Spika, katika Fungu hili kwa mwaka 2019/20, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:

Matumizi ya kawaida – shilingi 9,730,012,708,000 (trilioni 9.73). Kati ya hizo:

(i)          Mishahara - shilingi 8,885,708,000 (bilioni 8.88); na

(ii)         Matumizi mengineyo - shilingi 9,721,127,000,000 (trilioni 9.72)

Fungu  23 – Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali


62.        Mheshimiwa Spika, katika Fungu hili kwa mwaka 2019/20, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:

(a)Matumizi ya kawaida - shilingi 44,066,048,000 (bilioni 44.07). Kati ya hizo:

(i)          Mishahara – shilingi 7,029,314,000 (bilioni 7.03); na
(ii)         Matumizi mengineyo - shilingi 37,036,734,000 (bilioni 37.04).

(b)Miradi ya Maendeleo – shilingi 3,300,000,000 (bilioni 3.30). Kati ya hizo:

(i)          Fedha za ndani – shilingi 2,000,000,000 (bilioni 2.00);na
(ii)         Fedha za Nje  - shilingi 1,300,000,000 (bilioni 1.30)

Fungu 7 – Ofisi ya Msajili wa HAZINA


63.        Mheshimiwa Spika, katika Fungu hili kwa mwaka 2019/20, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:

(a)     Matumizi ya kawaida – shilingi 40,510,802,000 (bilioni 40.51). Kati ya hizo:

(i)       Mishahara – shilingi 3,281,016,000(bilioni 3.28); na
(ii)      Matumizi mengineyo – shilingi 37,229,786,000 (bilioni 37.23).

(b)         Miradi ya Maendeleo – shilingi 2,300,000,000 (bilioni 2.30). Kati ya hizo:

(i)       Fedha za ndani – shilingi 1,000,000,000 (bilioni 1.00); na
(ii)      Fedha za Nje  - shilingi 1,300,000,000 (bilioni 1.30).

Fungu 10 – Tume ya Pamoja ya Fedha


64.        Mheshimiwa Spika, katika Fungu hili kwa mwaka 2019/20, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:
Matumizi ya Kawaida - shilingi 2,207,935,000 (bilioni 2.20)
Kati ya hizo:

(i)    Mishahara - shilingi 649,793,000 (milioni 649.79); na
(ii)   Matumizi mengineyo - shilingi 1,558,142,000 (bilioni 1.55).

 

Fungu 13 – Kitengo cha Udhibiti wa Fedha Haramu


65.        Mheshimiwa Spika, katika Fungu hili kwa mwaka 2019/20, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:

(i)    Matumizi ya mengineyo - shilingi 2,015,586,000 (bilioni 2.01); na

(ii)   Matumizi ya Maendeleo – shilingi 200,295,998 (milioni 200.29)  ambazo ni fedha za nje.

Fungu 45 – Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi


66.        Mheshimiwa Spika, katika Fungu hili kwa mwaka 2019/20, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:

(a)Matumizi ya kawaida – shilingi 55,076,878,000 (bilioni 55.07). Kati ya hizo:

(iii)    Mishahara – shilingi 14,084,139,000(bilioni 14.08); na
(iv)    Matumizi mengineyo – shilingi 40,992,739,000 (bilioni 40.99)

(b)Miradi ya Maendeleo – shilingi 6,300,000,000 (bilioni 6.30). Kati ya hizo:

(iii)    Fedha za ndani – shilingi 5,000,000,000 (bilioni 5.00); na
(iv)    Fedha za Nje  - shilingi 1,300,000,000 (bilioni 1.30).

SHUKRANI


67.        Mheshimiwa Spika, napenda nirudie tena kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwasilisha hotuba hii mbele ya Bunge lako Tukufu. Aidha, kwa namna ya pekee kabisa naomba nitumie fursa hii kuwashukuru Washirika wa Maendeleo wote wakiwemo nchi na mashirika ya kimataifa ambao wamekuwa wakisaidia kwa namna mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara. Vilevile, napenda kuwashukuru Watanzania wote wenye mapenzi mema na uzalendo kwa nchi yao ambao wamekuwa wakilipa kodi stahiki na kwa hiari. Naomba nitumie fursa hii kuwaambia kuwa, mchango wao katika ujenzi wa Taifa letu unathaminiwa sana na utaendelea kukumbukwa hata kwa vizazi vijavyo.

68.        Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, napenda nikushukuru tena wewe binafsi, kwa kunipa nafasi ya kuwasilisha hoja hii  pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunisikiliza. Hotuba hii inapatikana katika tovuti ya Wizara kwa anuani ya www.mof.go.tz

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

 



Share:

Ufahamu Ugonjwa Wa Ngiri Na Tiba Yake

Tatizo la Ngiri Linavyosababisha Upungufu wa Nguvu za Kiume na Maumbile Kusinyaa.
 
Ngiri au Hernia ni aina ya ugonjwa ambao unampata mtu baada ya misuli au kuta za tishu mwilini zinazoshikiria au kubeba viungo (organs) fulani mwilini kupoteza uimara wake au kuwa na uwazi (Opening) na hivyo kusababisha viungo hivyo kutoshikiriwa ipasavyo katika sehemu vinapostahili kuwepo.

Katika mwili wa binadamu, maeneo ambayo tatizo hili hutokea mara kwa mara ni maeneo ya tumboni, katika eneo la kinena, eneo la paja kwa juu na pia ngiri inaweza kutokea katika eneo ambalo mtu alifanyiwa upasuaji (operesheni).

Dalili za Ngiri
Tumbo kuunguruma, kiuno kuuma, kupata choo kama cha mbuzi, kushindwa kufanya tendo la ndoa, mishipa ya uume kulegea, kutokuwa na hamu ya kurudia tendo la ndoa, korondani moja kuvimba, mgongo kuuma.

Dalili zingine za ugojwa wa ngiri ni pamoja na;

Uvimbe unaoteremka kuingia ndani ya korodani unaojulikana kitaalamu kama Direct Scoratal inguinal Hernia.
Uvimbe unaojitokeza tumboni na kuteremka hadi ndani ya korodani, uvimbe huu hauumi na unaweza kurudishwa kwa urahisi iwapo mgonjwa atalala chali na kusukuma kwa vidole, uvimbe huu.
Na pindi ukikubali kurudi ndani ndipo unapoitwa Reduible direct scrotal inguinal hernia.
Na pia endapo utashindikana kurudi tumboni ndipo unapoitwa Irreduible direct scrotal inguinal hernia.

Tiba ya Ngiri
Tiba yake ni kufanyiwa upasuaji , ama kutumia dawa za asili ili kupona kabisa tatizo hilo. Wasiliana Nami Kwa Ushauri zaidi wa Tatizo hili au tatizo  sugu la Vidonda ya Tumbo, Busha .


 Simu: 0714006521


Share:

Nape Ammwagia Pongezi Waziri Makamba

Mbunge wa Jimbo la Mtama,Nape Nnauye ametoa pongezi kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira kwa kusimamia suala la katazo la mifuko ya Plastiki.

Katika ukurasa wake wa Twitter leo asubuhi Jumatatu Juni 3, 2019 Nape ameandika ujumbe akisema kazi iliyofanywa na Makamaba ni mfano wa kiongozi na siyo mtawala .

Akiwa ameambatanisha picha yake (Nape) na Makamba wakiwa wamevalia masharti ya rangi ya kijana inayotumiwa na CCM, Nape amendika, “Namna wewe na wenzako mlivyosimamia swala la mifuko ya plastiki ni mfano tosha wa utofauti kati ya kuongoza na kutawala.. Hongera sana!.”

Waziri Makamba ameongoza kampeni hiyo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alilotoa bungeni miezi kadhaa iliyopita akisema kuanzia Juni mosi, 2019, itakuwa ni marufuku kutengeneza, kuingiza, kuuza na kutumia mifuko ya plastiki kwa ajili ya kubebea bidhaa za aina yoyote na matumizi yake yatakoma Mei 31, 2019.



Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger