Saturday, 31 July 2021
BROTHERHOOD SURVEY SERVICES YATUMIA MAONESHO SHINYANGA KUTANGAZA MCHONGO WA VIWANJA IBADAKULI
Maelekezo 10 ya Waziri Ummy kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Ummy Mwalimu ametoa maelekezo 10 kwa Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya ya kuimarisha ukusanyaji mapato na upelekaji wa fedha za maendeleo kwenye miradi inayogusa wananchi.
Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu matumizi na mapato ya ndani ya Halmashuari hizo kwa mwaka 2020/21, Mhe.Waziri Ummy amezitaka Halmashauri ziendelee kubuni vyanzo vipya vya mapato ya ndani ambavyo haviitakuwa kero kwa wananchi ili kuongeza uwezo wa utoaji huduma kwa wananchi hususani huduma bora za Afya, Elimu na Miudombinu ya Barabara.
Pia, amesema Halmashauri ziimarishe usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ikiwa ni pamoja na matumizi ya mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji wa mapato ili kuondoa mianya ya uvujaji wa mapato na kusisitiza kila chanzo kikusanywe kwa kutumia POS machine ili kudhibiti upotevu huo.
BONYEZA HAPA KUJUA VITUO VITAKAVYOTOA CHANJO YA CORONA TANZANIA
“Halmashauri zihakikishe kuwa fedha za makusanyo ya ndani zinazokusanywa zinapelekwa benki ndani ya masaa 24 baada ya kuzikusanya. Ni marufuku na ni kosa la kisheria kwa Halmashauri kutumia fedha zilizokusanywa kabla ya kuzipeleka benki (fedha mbichi) kwa sababu yoyote ile,”amesema.
Amesisitiza Halmashauri zihakikishe zinapeleka na kutumia angalau asilimia 40 ya mapato yaliyokusanywa (kwa Halmashauri zinazokusanya chini ya Shilingi bilioni 5 kwa mwaka) na asilimia 60 (kwa Halmashauri zinazokusanya zaidi ya Shilingi bilioni 5 kwa mwaka) kwenye miradi ya maendeleo ili kutatua kero za wananchi hususan kuboresha huduma za Afya, Elimu na miundombinu ya barabara. Fedha hizi zitumike kwenye miradi yenye tija na inayogusa moja kwa moja wananchi na sio kugharamia semina, vikao, safari na mambo mengine yasiyogusa wanananchi moja kwa moja.
Aidha, amesema kwa Halmashauri zenye makusanyo kuanzia bilioni 5 na zaidi kwa mwaka, zihakikishe zinatumia angalau asilimia 10 ya sehemu ya fedha zao za maendeleo kwenye uboreshaji wa Miundombinu ya barabara kupitia TARURA.
“Ninazitaka Halmashauri kuhakikisha fedha za mapato ya ndani zinatumika kutekeleza na kukamilisha miradi kwa asilimia 100 ili wananchi waweze kuona faida za mapato ya ndani na hatimaye kuongeza mwamko wa ulipaji wa kodi na ushuru,”amesema.
Mhe. Waziri Ummy amesema Halmashauri zihakikishe zinapeleka asilimia 10 ya fedha za mikopo ya Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu kwenye shughuli zenye tija kama ilivyoelekezwa na Mh.Rais Samia Suluhu Hassan na katika hilo Halmashauri zihakikishe angalau asilimia 60 ya fedha za mikopo zinatolewa kwenye Vikundi hivyo.
“Halmashauri zihakikishe zinakamilisha miradi ambayo haijakamilika (viporo) kabla ya kuanzisha miradi mipya, Halmashauri zitumie sehemu ya fedha za matumizi ya kawaida kutoka kwenye mapato ya ndani ili kulipa madeni na hatimaye kuondoa malimbikizo ya madeni yasiyokuwa na msingi,”amesema.
Amehimiza Mabaraza ya Madiwani yahakikishe yanasimamia ipasavyo matumizi ya fedha za Halmashauri ili kupata thamani halisi ya fedha zinazotumika na kwamba yana wajibu wa kuhakisha fedha zinatumika kwenye miradi ya maendeleo yenye tija na manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi.
Kuhusu maelekezo kwa Mikoa, Mhe.Waziri huyo amesema Sekretarieti za Mikoa zifanye ufuatiliaji wa ukusanyaji wa mapato ya ndani na matumizi ya mapato hayo kwa Halmashauri zilizo ndani ya Mikoa yenu mara kwa mara ili kujiridhisha na ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri pamoja na matumizi yake na kuwasilisha taarifa za utekelezaji Ofisi ya Rais – TAMISEMI kila robo mwaka kabla ya tarehe 20 baad ya robo husika kuisha.
“Sekretarieti za Mikoa zifanye ufuatiliaji wa fedha za miradi inayotekelezwa kwa mapato ya ndani iliyopo kwenye Halmashauri zao ili kujiridhisha na ubora wa Miradi inayotekelezwa. Aidha Sekretariat zifanye ufuatiliaji wa kina wa miradi inayotekelezwa kwa fedha kutoka Serikali Kuu na wadau wengine,”amesema.