Thursday, 22 October 2026

WAHITIMU MZUMBE WATAKIWA KUCHOCHEA MAFANIKIO YA DIRA YA TANZANIA 2050

...
Mgeni rasmi wa Mkutano wa 26 wa Baraza la Wahitimu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati), akimpongeza Mhitimu Bora wa Mwaka 2025/2026, Bw. Colins Mulema (kushoto), wakati wa mkutano huo uliofanyika katika Chuo Kikuu Mzumbe.

************

Chuo Kikuu Mzumbe kimewahimiza wahitimu wake kutumia maarifa, ujuzi na uzoefu walioupata chuoni kuchangia mafanikio ya Dira ya Tanzania ya 2050 kupitia ubunifu, ujasiriamali na uongozi wenye uwajibikaji.

Wito huo umetolewa katika Mkutano wa 26 wa Baraza la Wahitimu la Chuo Kikuu Mzumbe uliofanyika tarehe 21 Oktoba 2026 chuoni hapo, uliobeba kaulimbiu isemayo “Wahitimu kama Chachu ya Utekelezaji wa Dira ya Tanzania ya 2050 kupitia Ubunifu, Ujasiriamali na Uongozi Wenye Uwajibikaji.”

Akizungumza katika mkutano huo, Mgeni Rasmi, Prof. Elisante Ole Gabriel, Katibu Mkuu Mstaafu na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mstaafu, aliwahimiza wahitimu kutumia maarifa na uzoefu walioupata chuoni kuchochea ubunifu na ujasiriamali, akisisitiza kuwa mafanikio yao yanapaswa kuonekana pia kupitia mchango wao katika kutatua changamoto za jamii na kuleta maendeleo.

Prof. Gabriel pia alisisitiza umuhimu wa wahitimu kuchangia maendeleo ya Chuo Kikuu Mzumbe kupitia mawazo, uzoefu na rasilimali fedha. Alipendekeza kuimarishwa kwa mifumo endelevu ya uchangiaji kupitia Baraza la Wahitimu ili kuweka utaratibu wa kudumu wa kusaidia maendeleo ya chuo. Aidha, aliwahimiza kutumia fursa zilizopo katika soko la Afrika kuanzisha shughuli za ujasiriamali na ubunifu zenye tija kwa jamii.

Kwa upande wake, Kaimu Rais wa Baraza la Wahitimu, ambaye pia ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, alisema wahitimu ni mabalozi wa chuo hicho na wanapaswa kudumisha weledi na uadilifu katika majukumu yao.

Aliwataka kutumia nafasi zao katika sekta mbalimbali kutoa fursa za mafunzo kwa vitendo na ajira kwa wanafunzi, sambamba na kuimarisha ushirikiano wa kitaaluma na kitaasisi.

Prof. Mwegoha aliwahimiza pia wahitimu kuimarisha mitandao yao na kushiriki kikamilifu katika uongozi wa Baraza la Wahitimu ili kuimarisha shughuli zake na kutekeleza mipango iliyowekwa kwa mwaka 2026/2027.

Mkutano huo ulilenga kujadili maendeleo ya Baraza la Wahitimu, kuimarisha ushiriki wa wahitimu katika shughuli za chuo na kuweka mikakati ya utekelezaji wa shughuli za Baraza. Pia, ulisisitiza umuhimu wa kuendeleza uhusiano kati ya chuo na wahitimu kupitia kubadilishana uzoefu na kuwezesha wanafunzi kupata fursa za mafunzo na ajira.

Kupitia kaulimbiu hiyo, Mkutano wa 26 wa Baraza la Wahitimu la Chuo Kikuu Mzumbe umeweka wazi nafasi ya wahitimu katika kuijenga Tanzania yenye maendeleo endelevu, kwa kutumia maarifa na ujuzi wao kuibua bunifu, kukuza ujasiriamali na kutoa uongozi wenye uwajibikaji, hatua zinazotarajiwa kuchangia kufikiwa kwa malengo ya Dira ya Tanzania ya 2050.

Mgeni rasmi wa Mkutano wa 26 wa Baraza la Wahitimu la Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na wahitimu waliofanya vizuri kielimu kwa mwaka wa masomo 2025/2026.
Makamu mkuu wa chuo kikuu Mzumbe, Prof. William Mweghoha (kushoto), akizungumza na Meneja wa masoko yanayoibukia barani Afrika wa Taasisi ya Wahasibu wa Usimamizi (CIMA), Bw. Miley Rahman, alipowasili chuoni hapo kuhudhuria mkutano huo.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger