Na MWANDISHI WETU GEITA.
Maonesho ya Saba ya Teknolojia ya Madini yamefunguliwa rasmi na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ambapo Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) unatumia Maonesho hayo kuendelea kutoa elimu ya hifadhi ya jamii kwa sekta binafsi na sekta isiyo rasmi ikiwemo Sekta ya Madini.
Akizungumza na mamia ya wananchi waliojitokeza katika ufunguzi wa maonesho hayo, Mhe. Dkt. Biteko amesema maonesho yametoa fursa ya wananchi kupata elimu kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu uwekezaji kwenye sekta ya madini.
Aidha, amewataka wafanyabiashara wa madini kutumia mazingira rafiki yaliyowekwa na Serikali ya awamu ya sita katika kuboresha mazingira ya uwekezaji ili wafanye biashara zao kwa uhuru na kukuza uchumi.
Naye, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amesema mchango wa sekta ya madini unaendelea kukua siku hadi siku na kuwa wanatarajia hadi kufikia mwakani, sekta ya madini iwe inachangia katika pato la Taifa kwa asilimia kumi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martine Shigela amesema maonesho ya mwaka huu yameshirikisha zaidi ya washiriki 800 na yamechangia mafanikio ya mkoa huo.
Awali, akizungumza mbele ya Naibu Waziri Mkuu, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma, Bi. Lulu Mengele amesema NSSF inashiriki maonesho hayo kwa malengo ambapo katika mwaka wa fedha 2023/24, Mfuko kupitia Ofisi ya Mkoa wa Geita iliweza kukusanya shilingi bilioni 64 na kuwa asilimia 80 ya fedha hizo zilikusanywa kwenye makampuni mbalimbali ya madini.
Bi. Mengele amesema sekta ya madini ni wadau muhimu wa NSSF wakiwemo wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa ambao wote ni wanachama wa Mfuko na kuwa wamekuwa wakikusanya kiasi kikubwa cha fedha kutoka kwenye sekta ya madini.
Aidha, amesema NSSF imeendelea kuboresha huduma kupitia mifumo ya TEHAMA, ambapo kwa sasa wanachama wa NSSF wanaweza kufungua madai yao kidijitali huko huko waliko lengo ni kuondoa kero za wanachama na kusogeza huduma hukohuko waliko. Pia waajiri wanalipia michango ya wanachama wao wakiwa Ofisini bila ya kufika katika ofisi za NSSF.
Bi. Lulu amesema kupitia mifumo imechagiza mafanikio ya NSSF ambapo thamani imekua na kufikia trilioni 8.6. "Tunakushukuru sana mgeni rasmi hii ni kazi kubwa ya nyie viongozi mnayoifanya kutuongoza," amesema Bi.Lulu Mengele
0 comments:
Post a Comment