Sunday, 27 October 2024

HOFU YATANDA MATUMIZI YA KEMIKALI YA ZEBAKI KWA WACHIMBAJI WADOGO WA DHAHABU, WACHENJUAJI NA WAMILIKI WA LESENI NZEGA

...
WACHIMBAJI Wadogo wa madini ya dhahabu, wachenjuaji na wamiliki wa leseni wilayani Nzega mkoani Tabora wameeleza hofu yao juu ya matumizi ya kemikali ya zebaki (Mercury)  kwenye shughuli zao na kuishauri Serikali kuzuia matumizi yake baada ya kubaini athari zake kiafya na kimazingira.


Baadhi ya wachimbaji, wachenjuaji na wamiliki wa leseni walisema hayo baada ya kufuatwa kwenye mgodi namba tano wa Lusu uliopo kitongoji cha Mkwajuni, Kata ya Lusu wilayani Nzega mkoani Tabora na wataalam kutoka Maabara ya mkemia mkuu wa Serikali, kanda ya kati.

Wadau hao walikuwa wakipewa elimu juu ya matumizi na utunzaji salama wa kemikali ya zebaki inayotajwa na shirika la afya duniani kuwa miongoni mwa vyanzo 10 hatarishi kwa afya za binadamu na mazingira.


Mmoja wa wachimbaji Aboubakar Nuru alisema baada ya kugundua madhara hayo makubwa ya Zebaki hawaoni haja matumizi yake kuendelea hata kama kuna tahadhari badala yake anashauri ni vyema ikapatikana na kuhamasishwa kemikali nyingi Mbadala ili kuwanusu wachimbaji na watu wanaowazunguka.


Aidha Salum Ngozani akasema bado ni ngumu kuiondoa haraka kemikali hiyo kabla ya kuweka namna bora ya kulinda kemikali nyingine mbadala aina ya Sodium cyanide ambayo ufungashaji wake huwa ni kwa kipimo kikubwa na kuwa rahisi kuwatamanisha wezi tofauti na ZEBAKI ambayo ni rahisi kufichika ambapo kiwango kidogo huweza kufanya kazi kubwa 


“Lakini kuna wanyonge hawawezi kumudu hii kemikali Mbadala, hawawezi kununua Wala kuilinda wakiwa migodini, Hawa watasaidiwaje?kuna watu wanaitwa manyani huku, wanaingia maduarani wakati wowote na hawawezi kuiacha, wataiba tu na ni miongoni mwa sisi, tutawezaje kuulinda?”Alisema Ngozani.

Aidha Mwenyekiti wa wachimbaji wadogo TABOREMA, wilayani Nzega na mjumbe wa mkutano mkuu wa FEMATA taifa, Joseph Mabondo, akaishukuru maabara ya mkemia mkuu wa Serikali kutoa elimu hiyo na kuwasihi kuendelea kuelimisha na wachimbaji  wa maeneo mengine ya wilaya hiyo juu ya matumizi mazuri na salama ya zebaki, namna ya kuiingiza katika maeneo yao, namna ya kuitumia, kujisajili kuuza kemikali na mambo mengine muhimu.
 
Mwenyekiti huyo akasema hata wao wameendelea kuelimisha wachimbaji wadogo juu ya madhara ya zebaki na wengine wamekubali kuachana nayo na kutumia kemikali Mbadala huku ambao bado wanatumia zebaki akitaka waendelee kuelimishwa.

 "Tumekuwa pia tukiwahimiza kujenga makaro ili kuzuia utiririshaji ovyo wa maji wanayotumia kuchenjua madini Ili wasisababishe athari kiafya na kimazingira" Alisema Mabondo.

Kwa upande wake Meneja wa mamlaka ya maabara ya mkemia mkuu wa Serikali kanda ya kati, inayohusisha mikoa ya Dodoma, Iringa, Singida, Tabora na Morogoro Bw Gerald Meliyo alisema kemikali ya zebaki sio salama kiafya na kimazingira ndio maana wanaendelea kutoa elimu ya kujikinga na athari zake wakati wa kuitumia.

Meliyo akasema kimataifa kemikali hiyo iko mbioni kuondolewa na baadhi ya maeneo ikiwemo hospitali na viwandani tayari wamesitisha matumizi yake huku mkakati wa Serikali ikiwa ni kuiondoa kabisa kemikali hiyo sokoni katika matumizi yake ndani ya miaka michache ijayo.

Akasema hawawezi kuzizuia kwa mara moja na ndio maana wanaendelea kutoa mafunzo ili wachimbaji watumie ila kwa tahadhari, "Ndio maana tunawahimiza kutumia vifaa kinga ili kujilinda na madhara yanayoweza kuwapata hata kama hayaonekani sasa, hata baadaye, huwa inaharibu mapafu, inakwenda kwenye ubongo, inafanya watu kutetemeka na hivyo kushindwa kufanya majukumu yao, lakini miaka michache ijayo huenda upatikanaji wake ukawa mgumu”Alisema Molel.

Akawahimiza wachimbaji hao kujiunga vikundi ili kutumia kemikali mbadala ya zebaki aina ya Sodium cyanide ambayo haina madhara makubwa tofauti na zebaki madhara yake ni makubwa kiafya na kimazingira.

Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Tabora Bi Fatuma Kyando akasema kama Serikali ama wasimamizi wa wachimbaji wadogo huwa wanaangalia zaidi afya ya watu wao kwa kutamani wachimbe kutafuta fedha huku wakiwa salama kiafya ili waweze kutumia fedha zao wanazotafuta hata baada ya kazi.

 
Akasema elimu hiyo kwa wachimbaji ni muhimu na itasaidia kwani inawagusa wahusika wenyewe moja kwa moja kwa kujua madhara na namna ya kuyaepuka wao na jamii inayowazunguka.
 
Katika hatua nyingine Baadhi ya wananchi wa kitongoji cha Mkwajuni kata ya Lusu yalipo machimbo hayo akiwemo Bi Dotto Ramadhani na Charles Patrick wameomba kuondolewa kwa migodi jirani na makazi na kudhibitiwa usafirishaji holela wa udongo utokanao na madini ili kunusuru afya za wakazi kwani wasafirishaji wamekuwa wakipeperusha ovyo mchanga bila kujali na kutengeneza njia katikati ya makazi na viwanja vya watu.

 "Mara vumbi, mara makemiko haya, Hawa wenye mialo (mashimo ya madini) inabidi wasogezwe waende mbali kabisa, kwanza hayo makrasha yenyewe ni kelele tupu, tunaomba Serikali itusaidie",alisema Charles Patrick.
Afisa madini mkazi mkoa wa Tabora Fatuma Kyando
Gerald Meliyo, meneja wa Maabara ya mkemia mkuu wa Serikali, Kanda ya kati

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger