Thursday, 10 March 2022

HOSPITALI YA WAJAWAZITO YAPIGWA MAKOMBORA UKRAINE

...


Hospitali ya wanawake wajawazito katika Mji wa Mariupol nchini Ukraine, Jumatano ya Machi 9, 2022 imepigwa makombora na majeshi ya Urusi ambapo inaelezwa kwamba watoto wachanga kadhaa wamefukiwa na kifusi.

Hayo yamesemwa na Rais wa Ukraine, Volodymir Zelensky kupitia akaunti yake ya mtandao wa Twitter na kueleza kuwa huo ni ukatili wa kupitiliza unaofanywa na majeshi ya Urusi nchini humo, ambapo ameposti video inayoonesha baadhi ya majengo katika hospitali hiyo yakiwa yameharibiwa vibaya kutokana na shambulio hilo.

Video nyingine zinaonesha wagonjwa wakiwa wanajaribu kukimbia eneo hilo, wengi wakiwa wamejeruhiwa ambapo magari kadhaa pia yanaonekana yakiwa yamefukiwa na kifusi.

“Shambulio la moja kwa moja la majeshi ya Urusi katika hospitali ya wanawake wajawazito. Dunia itaendelea kuunga mkono ugaidi mpaka lini? Fungeni anga sasa hivi! Zuieni mauaji! Mnazo nguvu za kufanya hivyo lakini mnaonekana kupoteza utu,” ulisomeka ujumbe wa Rais Zelensky kupitia Twitter.

Mamlaka katika hospitali hiyo, zimesema imepata madhara makubwa ingawa hazikueleza ni watu wangapi waliouawa na waliojeruhiwa.

Mji wa Mauripol umekuwa ukishambuliwa mfululizo na majeshi ya Urusi kwa muda wa wiki nzima ambapo huduma muhimu za kijamii kama chakula, maji na umeme, hazipatikani kwa siku kadhaa sasa.

Muda mfupi kabla ya shambulio hilo la hospitalini, Waziri wa mambo ya Kigeni wa Ukraine, Dmytro Kuleba alitoa taarifa kwamba zaidi ya watoto wachanga 3,000, hawakuwa na chakula wala madawa na kuomba mashirika ya kibinadamu ya kimataifa, kusaidia kutengeneza njia ya kuwaondoa watoto hao nchini Ukraine ili kuokoa maisha yao.


Majeshi ya Urusi yalitangaza kwamba Jumatano ya Machi 9, yataachia njia ya kuwaondoa raia kutoka katika mji huo lakini kwa mara nyingine tena, yameshindwa kutekeleza ahadi zake.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger